Unapimaje Mafanikio Ya Kweli Katika Maisha Yako?

Unapimaje Mafanikio Ya Kweli Katika Maisha Yako?

Mafanikio ni neno ambalo linafahamika na kuzoeleka sana katika jamii yetu, lakini maana yake hasa ni nini? Ni kwa namna gani unaweza kupima mafanikio katika maisha? Je, mafanikio kuwa na utajiri, mamlaka na cheo, au kuna jambo jingine zaidi ya hayo?
Katika makala ya leo, nitaelezea maana ya mafanikio na kudadavua ni kwa jinsi gani unaweza kupima mafanikio ya kweli kwenye maisha yako. Nitaelezea vigezo vya ndani na vya nje ambayo vinachangia mafanikio na ni kwa jinsi gani unaweza kuvitumia kupima mafanikio yako.

Mafanikio ni nini?

Mafanikio yanaweza kutafsiriwa kama kufikia malengo au ndoto za maisha yako. Ni jinsi unavyoweza kutumia uwezo ulio ndani yako (your potential) kuweza kuishi maisha ya furaha na uliyoyakusudia (fulfilling and meaningful life). Kimsingi, mafanikio siyo tu kufikia malengo uliyojiwekea, lakini pia ni kufikia viwango vya maisha ya furaha (fulfilling life).

Mafanikio yanaweza kuwa na maana tofauti kwa watu tofauti pia, hii ndiyo sababu ni lazima kuwa makini kusema “mtu fulani amefanikiwa”. Jambo la msingi hapa ni kuwa, kama unahisi kuwa umefanikiwa, ni lazima uwe na furaha ya maisha baada ya kufikia malengo uliyojiwekea.

Umuhimu wa kupima mafanikio.

Kupima mafanikio ni jambo la muhimu sana. Linakuwezesha kufahamu wapi ulipo na hivyo kukupatia hamasa (motivation) ya kuendelea mbele kufikia malengo uliyojiwekea. Bila kupima mafanikio, unaweza kupoteza mwelekeo wa malengo yako. Kupima mafanikio pia kunakuwezesha pia kufurahia malengo uliyoyafikia, kujifunza kutokana na makosa na kufanya maboresho yanayohitajika.
Katika makala hii pia nitaelezea jinsi ya kupima mafanikio yako kwa kuwianisha vigezo vya ndani (internal factors) na vya nje (external factors).

Vigezo vya ndani (Internal Factors ) vya kupima mafanikio ya kweli

Unapimaje Mafanikio Ya Kweli Katika Maisha Yako?

Vigezo vya ndani ni mambo katika maisha yako ambayo yako ndani ya uwezo wako. Vigezo vya ndani ni hivi vifuatavyo:

1. Kuwa na furaha katika maisha yako (Happiness And Fulfillment)

Miongoni mwa vigezo vya muhimu sana vya kuzingatia unapopima mafanikio ni kuangalia kama una furaha ya maisha. Kigezo hiki kinajumuisha:

i. Kufanya kitu au kazi unayoipenda (passion).

ii. Kuwa na mahusiano bora (positive relationship).

iii. Kujua kusudi la maisha yako (Your life purpose) na kufanya vitu vinavyochangia kutimiza kusudi la maisha yako. Sasa hebu tuangalie kila kipengele kwa undani.

i. Kufanya kitu au kazi unayoipenda (passion)

Kufanya kitu kinachoendana na passion yako inamaanisha kufanya kazi unayoipenda na hivyo kufurahia kazi yako, haijalishi unalipwa mshahara kiasi gani au unapata kipato kiasi gani. Inamaanisha kuwa, unaamka kila siku na kuwa na shauku ya kazi yako. Unapokuwa unafanya kazi ambayo ni passion yako, kazi inabadilika kuwa siyo kazi bali inakuwa ni kitu unachokifurahia.

ii. Kuwa na mahusiano bora (positive relationship)

Kuwa na mahusiano bora ni jambo la muhimu sana ili kuwa na furaha katika maisha. Hii inajumuisha mahusiano bora na familia yako, marafiki zako na jamii yako. Ili kuimarisha mahusiano hayo, tenga muda wa kuwa na familia yako, marafiki zako na jamii yako.

iii. Kujua kusudi la maisha yako (Your life Purpose) na kufanya vitu vinavyochangia kutimiza kusudi la maisha yako.

Kufanya jambo linaloendana na kusudi la maisha yako inachangia kufanya uwe na furaha. Inakupatia hamasa na hivyo kukuwezesha kutotoka nje ya malengo yako.

2. Maendeleo binafsi (Personal Growth)

Kigezo cha pili cha ndani cha kuangalia unapopima mafanikio ya kweli ni maendeleo binafsi (personal growth). Katika kuangalia maendeleo binafsi katika maisha inajumuisha
i. kuweka na kutimiza malengo (setting and achieving clear, measurable goals),
ii. kujifunza kutokana na na makosa ( learning from your mistakes) na
iii. Kujitambua (self-awareness and self-improvement).

i. Kuweka na kutimiza malengo (setting and achieving clear, measurable goals)

Ni jambo la muhimu sana kuweka malengo kwa sababu ndiyo yanayokupatia ramani ya maisha yako. Unapofahamu wapi unakwenda, Inakupatia hamasa ya kufanya kazi kwa bidii na bila kutoka nje ya ramani. Pia inakuwezesha kupima mafanikio kwa kila hatua ndogo unayopiga kuelekea kwenye kutimiza malengo yako makubwa ya maisha.

ii. Kujifunza kutokana na makosa (Learning from your mistakes)

Kujifunza kutokana na makosa ni sehemu nyingine ya muhimu sana kwenye maendeleo yako binafsi (Personal growth). Unapokuwa umefanya makosa, chukulia makosa hayo kuwa ni fursa kwako kwa ajili ya kujifunza, kupata uzoefu na kuboresha pale ambapo ulikuwa na udhaifu. Kwa kuangalia makosa uliyoyafanya, itakusaidia kutokurudia makosa hayo na hivyo kukuwezesha kufanikiwa kwenye kazi zako.

iii. Kujitambua (Self-awareness and self-improvement)

Hili ni jambo la msingi sana kwenye maendeleo yako (Personal growth). Maana ya kujitambua ni kufahamu ubora wako (your strengths) na madhaifu yako (your weaknesses) na kuchukua hatua ya kuboresha mapungufu yako ili uwe mtu bora zaidi na hivyo kuweza kutimiza malengo yako katika ubora wa hali ya juu.

3. Afya ya kimwili na kiakili (Mental And Physical Health)

Kuwa na afya bora kimwili na kiakili ni kigezo cha muhimu sana cha ndani kinachopima mafanikio yako. Hii inajumuisha kufanya kila kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako kuweza:
i. Kuboresha afya yako ya mwili.
ii. Kuhimili misongo (stress) na changamoto (challenges) za maisha.
iii. Kuweka uwiano mzuri wa kazi na maisha yako (good work -life balance).

i. Kuboresha afya yako ya mwili.

Hii inajumuisha kula mlo kamili (healthy diet), kufanya mazoezi na kupata usingizi wa kutosha. Unapokuwa na afya bora, mwili wako unakuwa na nguvu ya kuweza kutimiza malengo yako ya maisha na hivyo kuchangia kwenye mafanikio yako.

ii. Kuhimili misongo na changamoto (Coping with stress and challenges).

Hili ni jambo la muhimu sana kwenye afya yako ya mwili na akili. Maisha yamejaa milima na mabonde, hivyo ni muhimu kuweza Kuhimili changamoto na misongo inayojitokeza kwenye maisha yako.

iii. Kuweka uwiano mzuri wa kazi na maisha yako (good work -life balance)

Kuweka uwiano mzuri kati ya kazi zako na maisha yako mengine ni jambo la muhimu sana. Hii itakuwezesha kufanikiwa kwenye kazi zako wakati huohuo ukiwa na muda mzuri wa kufurahia na familia yako, marafiki zako na jamii yako kwa ujumla.

Vigezo vya nje (External Factors ) vya kupima mafanikio ya kweli.

Unapimaje Mafanikio Ya Kweli Katika Maisha Yako?

Pamoja na vigezo vya ndani nikivyoelezea hapo juu, pia kuna vigezo vya nje vinavyotumika kupima mafanikio yako. Vigezo hivyo ni hivi vifuatavyo:

1. Utajiri au kuwa na uchumi imara (Financial Stability And Wealth)

Kigezo cha kwanza kabisa cha nje ni kuwa tajiri au kuwa na uchumi imara. Watu wenye pesa nyingi, nyumba nzuri au gari huwa wanaonekana kuwa wamefanikiwa. Watu hawa huwa wamefanya kazi kwa bidii kuweza kutimiza malengo yao. Hivyo, ili uweze kuwa na uhuru wa kifedha, ni lazima uzingatie mambo yafuatayo:
i. Kuepukana na madeni
ii. Kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa muda mrefu.

i. Kuepukana na madeni.

Ili uweze kuepukana na madeni, ni sharti ujifunze kuweka bajeti. Kwa kufanya hivyo, utaweza kutumia kipato chako bila kuingia kwenye madeni na kubakiza kiasi cha pesa ambacho utaweka akiba, kuwekeza na kuwa na uchumi imara.

ii. Kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa muda mrefu.

Kigezo hiki, kina uhusiano wa moja Kwa moja na kigezo cha kwanza. Kama utaweza kuishi chini ya kipato chako, utapata pesa ya ziada ambayo utaiwekeza kwenye biashara, kununua hisa, hati fungani na kadhalika. Unapoiwekeza pesa yako, itaongezeka na hivyo kufanya uwe na mafanikio kwenye maisha yako. Jambo la msingi hapa ni kuwekeza pesa yako mahali ambapo itaongezeka thamani.

2. Kufanikiwa kwenye kazi kipaji au taaluma Yako (Professional Accomplishments)

Kigezo kingine cha kupima mafanikio ya nje ni kufanikiwa kwenye taaluma, kipaji au kazi yako. Hii inajumuisha kufikia malengo uliyojiwekea. Kufanya mambo makubwa kwenye kazi yako ambayo yataleta mchango chanya kwenye eneo lako la kazi.

3. Kuwa na mchango kwenye jamii yako (Contribution To Society)

Kigezo cha mwisho kwenye kupima mafanikio yako ni kwa kuangalia ni mchango gani unaotoa kwenye jamii yako. Jamii yako lazima ihisi uwepo wako. Taaluma yako, kipaji chako au kazi yako ni lazima itatue matatizo yaliyopo kwenye jamii yako. Kwa kufanya hivyo, jamii itakupenda na kukuheshimu kwa sababu utakuwa unasaidia kutatua changamoto zinazoikabili.
Mafanikio ya kweli ni lazima yawe na uwiano wa vigezo vya ndani na vya nje.
Hivyo, ili uweze kuhitimisha kuwa na mafanikio ya kweli ni lazima kuwe na uwiano kati ya vigezo vya ndani na vya nje.

Swali la leo.

Katika maisha yako, unafikiri ni vigezo gani vya mafanikio haujavifikia na unatamani kuvifanyia kazi ili uweze kuwa na mafanikio ya kweli?

Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika hapa chini kwenye box la maoni.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp