Tiba 7 Za Umaskini Na Sheria 5 Za Jinsi Ya Kuwa Tajiri.

Tiba 7 Za Umaskini Na Sheria 5 Za Jinsi Ya Kuwa Tajiri.

George Samuel Clason ni mwandishi aliyeishi mwanzoni mwa karne ya 20 ambaye alibadilisha kabisa mtizamo wa watu katika mambo yote yanayohusu ushauri wa kifedha. Baada ya kuhudumu katika Vita vya Uhispania na Amerika, George alianza kuandika vipeperushi vya jinsi ya kupata mafanikio ya kifedha. The Richest Man In Babylon (Mtu Tajiri Zaidi katika Babeli ) ni mkusanyiko wa machapisho yake maarufu zaidi alivyowahi kuandika. George anasifiwa kwa kubuni neno ‘Jilipe kwanza’ yaani ‘pay yourself first.’ kitabu hiki kinaelezea kanuni za jinsi ya kuwa tajiri.

The Richest Man In Babylon (Mtu Tajiri Zaidi katika Babeli) ni kitabu ambacho kimedumu kwa karibu miaka 100. Pamoja na kuwa kitabu cha zamani, kitabu hiki bado kinatumika leo kama kilivyokuwa kinatumika wakati kinachapishwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1926. Kitabu hiki kinaelezea ushauri wa kifedha kupitia mkusanyiko wa mifano. Mifano hii imetoka Babeli ya kale. Mhusika mkuu wa kitabu hiki ni Arkadi. Arkadi ni mwandishi maskini ambaye alikuja kuwa ‘mtu tajiri zaidi Babeli.

Babeli lilikuwa jiji tajiri zaidi ulimwenguni wakati huo kwa sababu watu wake walithamini thamani ya pesa. Kitabu hiki ni mojawapo ya vitabu vya kitamaduni vyenye ushawishi mkubwa vinavyotoa ushauri wa kifedha. Mwishoni mwa muhtasari wa kitabu hiki, utakuwa na ufahamu mkubwa kuhusiana na fedha kupitia ushauri wa kifedha wa Arkad. Hapa, utajifunza tiba saba za umaskini na sheria tano za dhahabu. Hizi zitakusaidia kuzalisha pesa, kuzilinda na kuziwekeza na hivyo kuwa tajiri.

Tiba Saba za Arkad.


1.Jilipe Kwanza

Unapaswa kuangalia kila wakati jinsi ambavyo unaweza kuokoa pesa unazopata kwa kupunguza matumizi kadiri unavyoweza. Clason anapendekeza kuokoa angalau 10% ya mapato yako. Ikiwa unaweza kuokoa sehemu kubwa kuliko hii, basi hiyo ni nzuri zaidi. Pesa hizi unapaswa kuziwekeza Ili zizae na kuongezeka. Ikiwa una deni, unapaswa kuishi kwa 70% ya kile unachopata. Okoa 10% kwa ajili ya kuwekeza na utumie 20% iliyobaki kulipa deni lako. Unapaswa kuweka kando hii pesa kabla ya kufanya matumizi yoyote mengine ya pesa zako. Hivyo, mwandishi anasisitiza kujilipa kwanza kwenye kila kipato unachokipata kabla ya kuanza matumizi mengine.

2.Dhibiti Gharama Zako Za Maisha.
Unatakiwa kudhibiti gharama zako. Ili kuokoa angalau 10% ya mapato yako, itabidi upunguze matumizi yako. Unahitajika kutumia 90% au chini ya mapato yako. Kwa hiyo, unapaswa kujifunza kuishi chini ya kipato chako kwa kuzuia gharama zisizo za lazima. Kama gharama zako zitakua sawa na mapato yako, basi hutapata pesa inayobaki ambayo utaiwekeza. Kaa chini na utafakari ni matumizi gani ambayo unaweza kuyapunguza. Kama utashindwa kupunguza matumizi yako yaani mapato yako yakiwa sawa na matumizi, basi utakuwa ukiokoa 0% ya mapato yako kila mwezi. Mfano kamili wa hili ni wakati watu wanapopata nyongeza ya mshahara. Badala ya kutumia hii kama fursa ya kuokoa pesa zaidi, watu huanza kutumia zaidi na hivyo kushindwa kuweka akiba. Unaweza kuokoa pesa kwa kudhibiti hamu yako ya kununua vitu visivyo vya lazima na kudumisha tabia hii maisha yako yote.

Huwezi kuwa tajiri bila kudhibiti gharama zako za maisha. Ili uweze kudhibiti gharama zako za maisha ni lazima uwe na bajeti. Ili kupanga bajeti kwa ufanisi unahitajika kugawanya gharama zako katika makundi mawili: mahitaji ya lazima na mahitaji yasiyo ya lazima. Tenga takriban 50% ya bajeti yako kwa mahitaji ya lazima kama vile kodi ya nyumba, chakula na kadhalika. Kisha unapaswa kutenga salio kwa ajili ya matumizi yasiyo ya lazima.

3.Ifanye Pesa Ikufanyie Kazi.
Kuokoa pesa na kutotumia pesa bila mpangilio, haitoshi kukufanya uwe tajiri. Unapaswa kuwekeza pesa zako. Tiba mbili za kwanza yaani kuokoa pesa kwa kuweka akiba na kudhibiti gharama za maisha, zitakusaidia katika tiba hii ya tatu. Tiba mbili za kwanza zitakupatia pesa za kuwekeza.

Kila senti ya akiba yako inapaswa kuwekezwa. Kila unapopata faida ya pesa uliyowekeza, unapaswa kuiwekeza pia faida hiyo. Ukifanya hivi, utajiri wako utaongezeka polepole. Utakuwa unaunda jeshi la wafanyakazi ambao watakuwa wanakufanyia kazi.

Baadhi ya maeneo bora ya kuwekeza akiba yako ni kwenye hisa, hati fungani au mali isiyohamishika. Ikiwa utafanya uwekezaji mzuri, pesa zako ulizowekeza zitaongezeka sana. Kwa hiyo, usiruhusu fursa kubwa zikupite. Ikiwa fursa nzuri ya uwekezaji itatokea, hakikisha umeielewa vizuri kabla ya kuwekeza pesa zako. Hivyo, ili uwe na pesa nyingi kwa ajili ya kuwekeza, unapaswa kupunguza matumizi yako zaidi.

Jambo la muhimu hapa unalopaswa kuzingatia ni kuwa, hakikisha unawekeza pesa zako katika maeneo ambayo una ujuzi. Au, ikiwa kuna fursa ambayo huna ujuzi nayo, huenda ukahitaji kujifunza zaidi, watu bora wa kujifunza kutoka kwao ni washauri wa kifedha.

4.Linda Utajiri Wako
Kuna hatari zinazohusiana na kujaribu kuwa tajiri Kwa haraka. Ni rahisi kupoteza pesa kwa kufanya uwekezaji duni. Hivyo, ili kupunguza hatari ya kupoteza pesa zako, njia moja ya kufanya ni kujifunza kutoka kwa wale ambao wamefanikiwa kujenga utajiri katika eneo unalotaka kuwekeza.

5.Miliki Nyumba Yako

Kumiliki nyumba humpa mtu kujiamini zaidi.

Kukodisha nyumba ni njia rahisi ya kupoteza pesa. Unakuwa unampa pesa zako tu mwenye nyumba. Ni bora kuchukua mkopo na kununua au kujenga nyumba. Wakati utakapokuwa umemaliza kulipa mkopo, utakuwa unamiliki nyumba yako. Baada ya kuwa umemiliki nyumba yako, unaweza kuitumia vyovyote utakavyopenda. Unaweza kuipangisha na ikawa ni uwekezaji unaokuletea pesa. Lakini, mwandishi anashauri kuwa, njia bora zaidi ni kununua nyumba bila mkopo.

6.Jiandae kwa maisha yako ya uzeeni au kipindi ambacho hutakuwa tena na nguvu za kufanya kazi.
Maisha ya kila mtu huanzia utotoni hadi uzeeni. Hii ndiyo njia ya maisha na hakuna mtu anayeweza kukwepa kupita kwenye njia hiyo. Kwa hiyo, unapaswa kufanya maandalizi kwa kuwa na kipato kwa ajili ya siku zijazo kwako wewe pamoja na familia yako. Hali ya kifedha inaweza kubadilika ghafla. Kwa hiyo, unahitajika kuwa na mpango madhubuti ili hali ikiwa mbaya uweze kujikwamua na kuendeleza maisha yako. Kwa mfano, unaweza kuugua na hivyo usiweze kufanya kazi au kupoteza kazi yako. Unatakiwa kuwa na vitega uchumi mahali ambavyo vinakuletea kipato .

7.Wekeza Ndani Yako
Mali yako ya thamani kuliko zote ni akili yako. Kwa hivyo, ili kuongeza uwezo wako wa kupata utajiri, lazima uwekeze ndani yako. Unahitajika kuboresha uwezo wako wa kuongeza kipato chako. Unaweza kufanya hivyo kwa kupata ujuzi na maarifa mapya muhimu kwa ajili ya kupata utajiri katika kipindi hicho. Fikiria jinsi unavyoweza kupata pesa zaidi. Kisha, fikiria ni mabadiliko gani unayohitaji kujifanyia mwenyewe ili kupata utajiri huo unaoutamani. Wekeza katika kufanya mabadiliko hayo.

Pamoja na kujifunza ujuzi mpya, kuwekeza ndani yako kunaweza kumaanisha kukuza tabia mpya nzuri zitakazokusaidia kufikia malengo yako ya kifedha. Mifano ya tabia nzuri ni kufanya mazoezi kila siku, kusoma vitabu vya elimu ya fedha kabla ya kulala na kuacha tabia ya matumizi mabaya ya fedha.

Sheria Tano za Dhahabu.

Uhuru wa kifedha

Katika kitabu hiki, Clason pia anatoa muhtasari wa jinsi ya kuwa na mafanikio ya kifedha. Anatupatia sheria tano za jinsi ya kuwa tajiri. Sheria hizi anaziita sheria Tano za dhahabu. Ametumia neno dhahabu kwa sababu dhahabu ilitumika kupima kiasi cha utajiri kipindi cha Babeli ya zamani. Hivyo kwa sasa unaweza

kutumia neno pesa badala ya dhahabu.
Zifuatazo ni sheria tano za jinsi ya kuwa tajiri kama zilivyoelezwa kwenye kitabu hiki cha The Richest Man In Babylon:

1. Dhahabu huja kwa urahisi kwa wale wanaookoa angalau 10% ya mapato yao.

2. Dhahabu huongezeka kwa wale watu ambao wataiwekeza Ili iendelee kuwazalishia faida.

3. Dhahabu inashikamana na watu wanaowekeza dhahabu zao kwa watu wenye busara.

4. Dhahabu hukimbia kutoka kwa watu wanaoiwekeza kwenye biashara au uwekezaji ambao hawana elimu ya kutosha au taarifa za kutosha.

5. Dhahabu hukimbia kutoka kwa watu wanaolazimisha dhahabu kuzalisha utajiri wa haraka isivyowezekana.

Siri ya kutengeneza utajiri ni kuwa na matumizi kidogo iwezekanavyo, kuokoa pesa ili uweze kuwekeza. Pia kuwekeza kwako mwenyewe ili uweze kuwa na maarifa ya kutosha kukamata fursa za kifedha zinapojitokeza.

Ili uweze kuwa tajiri, lazima ufikirie juu ya pesa zako kama mti. Mti hukua polepole kutoka kwenye mbegu, na unahitaji maji na mwanga ili uweze kusitawi. Tiba hizi saba ni chakula cha mti wako wa pesa. Kwa kuzingatia tiba hizi saba huku ukifanya kazi kwa bidii, utaweza kufikia uhuru wa kifedha na kuwa tajiri.

Ni matumaini yangu umepata maarifa ya kutosha ya tiba saba za Umaskini na sheria tano za jinsi ya kuwa tajiri kama zilivyoelezwa kwenye kitabu hiki cha The Richest Man In Babylon. Kama una maoni au swali lolote, usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

6 Replies to “Tiba 7 Za Umaskini Na Sheria 5 Za Jinsi Ya Kuwa Tajiri.”

  1. Nashukuru sana ndugu yangu angalau umenifunguavsana katika eneo hili la fedha
    Nutayatebdea kazi kwa kweli

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp