
Aristotle aliwahi kusema maneno yafuatayo:
“95% of everything you do is the result of your habit.”
Kwa tafsiri ya kiswahili maana yake ni kuwa, asilimia 95 ya kila kitu unachokifanya inatokana na tabia yako.
Hapa inamaanisha kuwa, ukitaka kuwa na mafanikio ni lazima ujenge tabia za mafanikio. Fanya vitu vinavyochangia kwenye mafanikio yako na ujitahidi kuvifanyia mazoezi mpaka vigeuke kuwa ndiyo tabia yako na ujizuie kufanya vitu ambavyo havina mchango wowote kwenye mafanikio yako. Katika makala ya leo nitakushirikisha tabia 6 za watu waliofanikiwa.
Ninawezaje kujenga tabia?
Tabia yoyote iwe nzuri au mbaya inajengwa kwa kurudiarudia (repetition). Hivyo kama unahitaji kujenga tabia njema za mafaniko ni sharti uwe tayari kuzirudiarudia kila siku. Baada ya muda utazoea kuzifanya na hivyo zitabadilika na kuwa ndiyo tabia yako. Katika makala hii tutaangalia tabia za watu waliofanikiwa.
Tabia 6 za watu waliofanikiwa.
1. Wanaweka malengo ya siku (daily goal setting)
Watu waliofanikiwa huwa wanaweka malengo ya siku. Hivyo ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na tabia ya kuweka malengo yako ya siku. Unapoenda kulala, hakikisha umeweka malengo yako ya siku inayofuata. Unapoamka unapaswa kufanya kazi zako kwa bidii ili uweze kutimiza malengo ya siku uliyojiwekea. Umuhimu wa kuweka malengo ya siku ni kuwa, unapoweka malengo na unayafikiria muda wote, utaweza kuyatimiza kwani utakuwa na hamasa ya kuyatimiza. Hivyo, watu waliofanikiwa huwa wanafikiria juu ya malengo yao muda wote.
2. Huwa ni watu wanaolenga kupata matokeo (result oriented)
Watu waliofanikiwa huwa wanafikiria kiwango cha matokeo watakayopata kwenye malengo waliyojiwekea. Hivyo, ili uweze kufanikiwa, kuweka malengo pekee haitoshi, ni lazima uwe na kipimo kitakachokusaidia kuona kama malengo yako yamefanikiwa au la. Kwa mfano, umeweka lengo la kusoma kitabu kila siku. Hili ni lengo ambalo liko kwa ujumla sana. Ili uweze kupima matokeo ni sharti lengo lako uliweke katika mfumo huu: Nitakuwa nikisoma kurasa 10 za kitabu kila siku. Hivyo, hata katika malengo yako mengine hakikisha unakuwa mtu wa kupima matokeo. Je, ni orodha ya mambo gani uliyoiweka leo? Weka vipaumbele vya mambo yako na vipimo vitakavyokusaidia kuangalia mafanikio.
3. Wanajali sana mahitaji ya watu (people oriented)
Watu waliofanikiwa huwa wanajali sana ni kwa jinsi gani wanaweza kusaidia watu wengine kutatua changamoto zao. Hivyo ili uweze kufanikiwa ni lazima ufikirie unawezaje kutatua changamoto za watu. Iwe kwenye kazi yako au biashara yako, jambo la kwanza kufikiria ni kuwa, biashara yangu au kazi yangu inatatua changamoto gani katika jamii. Kama ni kwenye kazi yako, jali sana watu unaowahudumia. Kama ni kwenye biashara yako, wajali wateja wako kwa kuwapa huduma bora. Jali changamoto za watu na uzitatue nawe utafanikiwa sana kwenye kazi au biashara yako.
4. Wanajali sana afya zao.
Watu waliofanikiwa huwa wanajali sana afya zao. Hii ni kwa sababu wanafahamu kuwa mafanikio yao yanategemea sana kama afya zao zitakuwa bora. Hivyo, ili uweze kufanikiwa, ni lazima mwili wako uwe na afya njema. Jali afya yako kwa kula vizuri, kufanya mazoezi pamoja na kupumzika.
5. Huwa ni waminifu
Waswahili wanasema kuwa, uaminifu ni mtaji. Watu wote waliofanikiwa ni waminifu kwenye kazi zao. Hivyo, ili uweze kufanikiwa, unapaswa kuwa mwaminifu kwenye maisha yako. Unapokuwa mwaminifu kwenye maisha yako, utavuta fursa nyingi sana kuja kwako. Kupitia uaminifu wako, utavutia watu kukupatia mtaji, kazi, masoko na fursa nyingine nyingi.
6. Huwa na nidhamu binafsi (self-discipline)
Nidhamu ndio msingi wa mafanikio yote katika maisha. Maana ya nidhamu ni:
Uwezo wa wewe mwenyewe kufanya kile unachotakiwa kufanya katika muda muafaka bila kujali unajisikia kufanya au la.
Watu waliofanikiwa huwa na nidhamu kubwa sana kwenye maisha yao. Hata wewe ili uweze kufanikiwa, hakikisha unakuwa na nidhamu kwenye maisha yako. Unapokuwa umeweka malengo, hakikisha kuwa unakuwa na nidhamu ya kuyakamilisha kwa muda muafaka. Kwa kufanya hivyo, utafanikiwa sana.
Swali la leo.
Je, ni tabia zipi za mafanikio ambazo unazijenga kwa sasa?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika kwenye sanduku la maoni hapa chini.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024
I have to thank you for the efforts youve put in writing this blog. Im hoping to check out the same high-grade blog posts by you later on as well. In fact, your creative writing abilities has encouraged me to get my own website now 😉