
Katika maisha, ili uweze kufanikiwa kuna kanuni ambazo unapaswa kuzifahamu na kuzifanyia kazi. Kanuni hizi ni za msingi sana kwa mtu yeyote anayetaka kufanikiwa. Hivyo, katika makala hii nitakushirikisha kanuni au sheria sita za mafanikio.
Sheria 6 Za Mafanikio
1.Sheria Ya Sababu Na Matokeo (The Law of Cause and Effect)
Sheria ya Sababu na Matokeo inasema kuwa, kwa kila tukio linalotokea katika maisha yako kuna sababu maalum. Inasema kuwa kila kitu huwa kinatokea kwa sababu, iwe unaijua sababu hiyo au la. Hakuna ajali.
Sheria ya Sababu na Matokeo inamaanisha kuwa, kuna sababu maalum za mafanikio na kuna sababu maalum za kushindwa. Kuna sababu maalum za afya na za ugonjwa. Kuna sababu maalum za furaha na za huzuni. Ikiwa kuna jambo katika maisha yako unalotaka kulifanikisha, unahitajika tu kufuatilia sababu zake na kuzirejea. Ikiwa kuna tukio katika maisha yako usilolifurahia, unahitajika kufuatilia sababu zake na kuziacha.
Sheria hii ni rahisi kiasi kwamba inawachanganya watu wengi. Wanaendelea kufanya, au kuto kufanya, mambo yanayosababisha wao kuwa na huzuni na kuchanganyikiwa, na kisha wanawalaumu wengine, au jamii, kwa matatizo yao.
Uendawazimu umefafanuliwa kama “kufanya mambo yale yale kwa njia ile ile na kutarajia kupata matokeo tofauti.” Hivyo, ili uweze kupata matokeo ya tofauti, unahitajika kufanya mambo yako kwa namna tofauti.
Kuna methali ya Kiskoti inayosema, “Ni bora kuwasha mshumaa mdogo kuliko kulaani giza.” Ni bora zaidi kukaa chini na kuchambua kwa makini sababu za shida zako kuliko kukasirika na kuzilalamikia.
Katika kitabu cha Wagalati 6:7 Biblia inasema, “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.”
Sheria ya Sababu na Matokeo linaitwa Sheria ya Kupanda na Kuvuna. Inasema kuwa chochote unachopanda, ndicho utakachovuna. Pia inasema kuwa chochote unachovuna leo ni matokeo ya kile ulichopanda hapo awali. Ikiwa unataka kuvuna mavuno tofauti katika eneo lolote la maisha yako katika siku zijazo, unahitajika kupanda mbegu tofauti leo, na bila shaka, hii inahusu zaidi mbegu za akili.
Matumizi muhimu zaidi ya Sheria ya Sababu na Matokeo, au kupanda na kuvuna, ni hii: “Mawazo ni sababu na hali ni matokeo.”
Mawazo yako ndio sababu kuu ya hali ya maisha yako. Kila kitu katika uzoefu wako kimeanza na wazo la aina fulani, lako au la mtu mwingine.
Jinsi ulivyo au utakavyokuwa, ni matokeo ya jinsi unavyofikiria. Ikiwa utabadilisha ubora wa mawazo yako, utabadilisha ubora wa maisha yako. Mabadiliko katika uzoefu wako wa nje yatatokana na mabadiliko katika uzoefu wako wa ndani. Utavuna kile unachopanda.
Uzuri wa sheria hii isiyobadilika ni kwamba kwa kuikubali, unachukua udhibiti kamili wa mawazo yako, hisia zako na matokeo yako.
Kila kipengele cha mafanikio au kushindwa kwenye biashara kinaweza kuelezewa na sheria hii ya msingi. Ikiwa unapanda sababu sahihi, utavuna matokeo unayotarajia. Ikiwa unazalisha bidhaa au huduma zenye ubora ambazo wateja wanazihitaji na wako tayari kuzilipia, na kisha kuzitangaza kwa nguvu, utafanikiwa katika kuuza. Ikiwa haufanyi hivyo, hautafanikiwa.
Ikiwa unafanya kazi ya ubora wa hali ya juu na kufikia matokeo ambayo kampuni yako inayahitaji ili kukua na kustawi, utafanikiwa na utakuwa na furaha katika kazi yako. Ikiwa unawatendea wengine vizuri, watakutendea vizuri pia.
2.Sheria Ya Imani (The Law of Belief)
Sheria ya Imani inasema kuwa chochote unachokiamini, kwa hisia, kinakuwa ukweli wako. Kadri unavyoamini kwa nguvu kuwa kitu hiki ni cha kweli, ndivyo kinavyokuwa cha kweli zaidi kwako. Ikiwa unaamini kitu kwa dhati, huwezi kukifikiria kwa njia tofauti. Imani yako ko inakupa aina ya mtazamo wa maisha yako. inahariri au kukufanya kupuuza taarifa zinazoingia ambazo hazilingani na kile ulichoamua kuamini.
William James wa Harvard alisema, “Imani huunda ukweli halisi.” Katika Biblia, inasema, “Kwa kadiri ya imani yako [imani] itafanyika kwako.” Kwa maneno mengine, hauamini kile unachokiona bali unaona kile unachoamini.
Kwa mfano, ikiwa unaamini kabisa kuwa unastahili kuwa na mafanikio makubwa maishani, basi bila kujali kinachotokea, utaendelea kusonga mbele kuelekea malengo yako. Hakuna kitu kitakachokukwamisha.
Kwa upande mwingine, ikiwa unaamini kuwa mafanikio ni suala la bahati au ajali, basi utakatishwa tamaa kwa urahisi na kuvunjika moyo wakati mambo yanapokuwa hayaendi sawa kwako. Imani yako inakuandaa kwa ajili ya mafanikio au kushindwa.
Watu kwa ujumla wana mitizamo miwili ya kuangalia dunia. Mtizamo wa kwanza ni mtazamo chanya wa dunia. Ikiwa una mtazamo chanya wa dunia, kwa ujumla unaamini kuwa dunia ni mahali pazuri pa kuishi. Hivyo unakuwa na mwelekeo wa kuona mazuri kwa watu na hali, na kuamini kuwa kuna fursa nyingi karibu nawe na unaweza kuzitumia. Unaamini kuwa ingawa huenda wewe si mkamilifu, wewe ni mtu mzuri kwa ujumla. Kimsingi, wewe ni mtu mwenye matumaini.
Njia ya pili ya kuangalia dunia ni kwa mtazamo hasi wa dunia. Ikiwa una mtazamo hasi wa dunia unakuwa na mwelekeo wa kukata tamaa juu yako mwenyewe na maisha yako. Kwa ujumla unakuwa unaamini kuwa “Hauwezi kupambana na hali ya maisha yako,” na kwamba “Wenye nacho huendelea kuwa na nacho na wasio nacho huendelea kuwa maskini,” na pia unaamini kuwa, haijalishi anavyofanya kazi kwa bidii, hauwezi kufanikiwa kwa sababu mambo yamepangwa kinyume na wewe.
Watu wenye mtazamo hasi huona ukosefu wa haki, ukandamizaji na bahati mbaya kila mahali. Wakati mambo yanapokwenda vibaya kwao, kama inavyotokea mara nyingi, wanalaumu bahati mbaya au watu wabaya. Wanajiona kama wahanga. Kwa sababu ya mtazamo huu, hawajipendi wala kujiheshimu.
Hivyo, vizuizi vikubwa vya kiakili ambavyo utahitajika kuvishinda ni vile vilivyomo katika imani yako vinavyokuzuia kuchukua hatua kuhusu maisha yako. Vizuizi hivi vinakurudisha nyuma kwa kukuzuia hata kujaribu. Mara nyingi vinakufanya kuona vitu ambavyo si vya kweli kabisa.
3.Sheria Ya Matarajio (The Law of Expectations)

Sheria ya Matarajio inasema kuwa, chochote unachotarajia kwa kujiamini kinakuwa ni unabii wako mwenyewe. Kwa maneno mengine, kile unachopata sio lazima kile unachotaka maishani, bali ni kile unachotarajia. Matarajio yako yana athari kubwa na isiyoonekana ambayo inasababisha kufanikiwa au kushindwa.
Kwa njia fulani, kila mara unakuwa kama mtabiri wa maisha yako. Watu waliofanikiwa wana mtazamo wa matarajio ya kujiamini na chanya. Wanatarajia kuwa na mafanikio, wanatarajia kupendwa, wanatarajia kuwa na furaha, na mara chache wanavunjika moyo.
Watu wasiofanikiwa wana mtazamo wa matarajio hasi, wa ukosoaji na wa kukata tamaa ambao kwa namna fulani unafanya hali kutokea kama walivyotarajia.
Katika kitabu cha “Pygmalion in the Classroom,” Dkt. Robert Rosenthal wa Chuo Kikuu cha Harvard anaelezea jinsi matarajio ya walimu yanavyokuwa na athari kubwa kwenye utendaji wa wanafunzi wao. Aligundua kuwa ikiwa wanafunzi wanahisi kuwa wanatarajiwa kufanya vizuri, huwa wanajitahidi kufanya vizuri zaidi kuliko ambavyo wangekuwa bila matarajio hayo.
Kwa hiyo, ni muhimu kuhakikisha kwamba matarajio yako yanakubaliana na kile unachotaka kuona kinatokea maishani mwako. Kuwa na matarajio mazuri kwako mwenyewe, na matarajio hayo yatakuwa na nguvu ya kubadilisha utu wako na maisha yako kwa ujumla.
4.Sheria ya Mvuto (The Law of Attraction)
Sheria ya Mvuto inasema kwamba wewe ni sumaku hai. Unavuta bila kukosea katika maisha yako watu na hali zinazolingana na mawazo yako yanayokutawala. Ndiyo maana waswahili wanasema kuwa, ” ndege wa aina moja huruka pamoja.” Kila kitu katika maisha yako umekivuta mwenyewe kutokana na mawazo yako.
Marafiki zako, familia yako, mahusiano yako, kazi yako, matatizo yako, na fursa zako vyote vimevutwa kwako kutokana na njia yako ya kawaida ya kufikiri katika kila eneo.
Unapoangalia kila kipengele cha maisha yako, chanya au hasi, utaona kwamba ulimwengu wako wote umeutengeneza mwenyewe. Na kadiri unavyoweka hisia zaidi kwenye wazo, ndivyo kasi ya mtetemo itakuwa kubwa zaidi na ndivyo utakavyovuta watu na hali zinazolingana na wazo hilo katika maisha yako kwa haraka zaidi.
Utaona kuwa, sheria hii huwa inafanya kazi kila wakati katika maisha yako. Kwa mfano, Unamfikiria rafiki yako na mara hiyo hiyo anakupigia simu. Unaamua kufanya jambo fulani na mara tu baada ya hapo unaanza kupata mawazo na msaada kuhusiana na jinsi utakavyofanikisha jambo hilo. Unakuwa kama sumaku inayovuta vipande vya chuma.
Watu wengi wanajizuia wenyewe kufanikiwa kwa sababu hawajui jinsi ya kutoka walipo hadi wanapotaka kwenda. Lakini kwa sababu ya Sheria ya Mvuto, si lazima uwe na majibu yote kabla hujaanza. Mradi tu unaelewa vizuri unachotaka na aina ya watu unaotaka kuwa nao, utawavuta katika maisha yako.
Watu wenye furaha wanaonekana kuvutia watu wengine wenye furaha katika maisha. Mtu aliye na ufahamu wa ustawi anaonekana kuvutia mawazo na fursa za kutengeneza pesa. Wauzaji wanaoaminika na wenye msisimko huvutia wateja wakubwa na bora zaidi. Wafanyabiashara chanya huvutia rasilimali, wateja, wasambazaji na mabenki wanayohitaji kujenga biashara zenye mafanikio. Sheria ya Mvuto inafanya kazi kila mahali na wakati wote.
5.Sheria ya Uwiano (The Law of Correspondence).

Sheria ya Uwiano ni mojawapo ya sheria muhimu zaidi, na kwa namna nyingi ni sheria ya muhtasari inayofafanua sheria nyingine nyingi. Inasema kuwa, “Jinsi ulivyo ndani, ndivyo ulivyo nje.” Sheria hii inamaanisha kwamba, ulimwengu wako wa nje ni taswira ya ulimwengu wako wa ndani. Sheria hii inafafanua kuwa, unaweza kujua kinachoendelea ndani yako kwa kuangalia kinachoendelea kukuzunguka wewe.
Katika Biblia, kanuni hii inaelezwa kwa maneno haya, “Kwa matunda yao, mtawatambua.” Kila kitu katika maisha yako ni kutoka ndani kwenda nje. Ulimwengu wako wa nje ni udhihirisho unaolingana na ulimwengu wako wa ndani wa mawazo na hisia.
Ulimwengu wako wa nje wa mahusiano unaendana na mtu uliye ndani, utu wako wa kweli wa ndani. Ulimwengu wako wa nje wa afya unaendana na mitazamo yako ya ndani ya akili. Ulimwengu wako wa nje wa mapato na mafanikio ya kifedha unaendana na ulimwengu wako wa ndani wa mawazo na maandalizi. Jinsi ambavyo watu wanakuitikia na kuingiliana na wewe inaakisi mitazamo na tabia yako kwao.
Mwanafalsafa Mjerumani Goethe alisema, “Lazima uwe kitu ili uweze kufanya kitu.” Lazima ubadilike wewe mwenyewe. Lazima uwe mtu tofauti ndani kabla ya kuona matokeo tofauti nje.
6.Sheria ya Usawa wa Akili (The Law of Mental Equivalency)
Sheria ya Usawa wa Akili inajulikana pia kama Sheria ya Akili na inaweza kufikiriwa kama ufafanuzi wa sheria zilizotangulia. Kimsingi, inasema kwamba, Mawazo yako, unayoyafikiria kwa undani na kuyarudia yakiwa na hisia, baadaye huwa yanakuwa ukweli wako. Karibu kila kitu ulicho nacho katika maisha yako kimeundwa na mawazo yako mwenyewe, kwa ubora au ubaya.
Kwa maneno mengine, mawazo ni vitu. Yanachukua maisha yako mwenyewe. Kwanza unakuwa nayo, kisha yanakumiliki. Unatenda kwa namna inayolingana na kile unachofikiria mara nyingi zaidi. Hatimaye, unakuwa kile unachofikiria. Na ukibadilisha mawazo yako, unabadilisha maisha yako.
Kila kitu kinachotokea katika maisha yako kwanza huanza kutokea katika namna ya wazo. Hii ndio sababu tafakari ni sifa muhimu ya wanaume na wanawake waliofanikiwa.
Nguvu ya Kufikiri Chanya
Unapoanza kufikiri kwa njia chanya na kwa kujiamini kuhusu vipengele vikuu vya maisha yako, unachukua udhibiti wa kile kinachotokea kwako. Unaleta maisha yako katika maelewano na sababu na athari. Unapanda sababu chanya na kuvuna athari chanya. Unaanza kuamini zaidi katika nafsi yako na uwezo wako. Unatarajia matokeo chanya zaidi. Unavuta watu na hali chanya, na hivi karibuni maisha yako ya nje ya matokeo yataanza kulingana na ulimwengu wako wa ndani wa mawazo ya kujenga.
Mabadiliko haya yote yanaanza na mawazo yako. Badilisha mawazo yako na maisha yako yatabadilika.
Nimatumaini yangu kuwa umenufaika na makala hii ya sheria 6 za mafanikio. Kama una maoni au swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024