
Ili uweze kufanikiwa katika maisha, ni lazima ufahamu jinsi ya kuitumia siku yako vizuri. Kila mtu amepewa sawa siku yenye masaa 24. Tofauti ya watu wenye mafanikio na ambao hawajafanikiwa inatokana na jinsi wanavyotumia masaa ya siku. Unaopanza asubuhi siku yako vizuri, unafungua milango ya mafanikio. Hii ndiyo sababu waswahili wanasema kuwa, nyota njema huonekana asubuhi. Saa chache za kwanza za siku ni muhimu sana kuliko saa nyingine zozote za siku. Mmoja wa wanafikra wakuu alisema kwamba saa ya kwanza ni usukani wa siku. Katika makala ya hii nitakushirikisha ratiba za asubuhi za watu wenye mafanikio.
Umuhimu wa Saa za Asubuhi
Saa za asubuhi, unapamka tu, zinaweka mwelekeo wa siku yako yote, zikiathiri mawazo yako na uzalishaji wako katika masaa yote yanayofuata. Umuhimu wa saa hizi za asubuhi ndio sababu baadhi ya watu wenye mafanikio makubwa duniani huweka kwa umakini taratibu za asubuhi ambazo zinalenga kuwasaidia kuanza siku vizuri na kutumia masaa yanayofuata kwa ufanisi mkubwa.
Jinsi ya Kuanza Siku Vizuri.
1.Panga Siku Yako Usiku Mmoja Kabla.
Ikiwa ungependa kuanza kila siku kwa njia bora zaidi iwezekanavyo, zingatia kutekeleza baadhi ya taratibu hizi zilizothibitishwa za asubuhi kwenye ratiba yako ya asubuhi. Kwanza, panga siku yako usiku mmoja kabla. Kuandaa siku yako usiku mmoja kabla inaweza kuwa si sehemu ya taratibu za asubuhi, lakini ni njia nzuri ya kuanza siku yako vizuri.
Kwa kupanga kile unachotaka kukamilisha usiku kabla, unaweza kuanza kila siku ukiwa na mpango kichwani badala ya kuamka bila kujua unachotaka kufanya. Panga ratiba yako ya asubuhi pamoja na kile unachotaka kufanya. Kisha, amka asubuhi inayofuata na uweke mpango huo kwenye vitendo.
2.Weka Malengo ya Siku Kila Asubuhi
Pili, weka malengo ya siku kila asubuhi. Panga siku yako usiku kabla, lakini weka malengo yako asubuhi. Kwa mfano, unaweza kupanga kufanya kazi kwenye mradi siku nzima. Kisha, asubuhi weka lengo la ni kiasi gani cha mradi huo unataka kukamilisha. Hivyo ndivyo watu wenye mafanikio hufanya.
Kuweka malengo asubuhi ni mkakati mzuri kwa kuwa watu wengi huwa na nia ya kufanikiwa wanapoanza siku yao. Ikiwa utaweka malengo makubwa asubuhi, utahisi kulazimika zaidi na kujituma zaidi kuyatimiza kadri siku inavyoendelea.
3.Epuka Kuangalia Simu Yako au Vifaa Vingine vya Kielektroniki
Tatu, epuka kuangalia simu yako au barua pepe mara tu unapoamka. Hii ni kwa sababu inaweza kuleta usumbufu ambao unaweza kuingilia kati ratiba yako ya asubuhi. Pia unaweza kupata habari za kukatisha tamaa ambazo zinaweza kuua motisha yako wakati ambapo unahitaji kuichochea.
Subiri mpaka ratiba yako ya asubuhi itakapokamilika ndio uangalie simu yako. Julie Morgenstein, mtaalamu wa usimamizi wa muda, aliandika kitabu kinachoitwa Don’t Check Your Email in the Morning. Subiri mpaka saa 11:00 asubuhi na fanya kazi kwa masaa matatu mfululizo kabla ya kuangalia barua pepe zako, kisha fanya kazi tena kwa masaa matatu kabla ya kuziangalia tena, na ziangalie mara mbili au tatu tu kwa siku, na katikati ya wakati huo uzime na uache kuzitazama.
4.Fanya Mazoezi na Kunyosha Mwili Wako.
Nne, fanya mazoezi. Tafiti zimeonyesha kwamba watu wanaofanya mazoezi asubuhi wana uwezekano mkubwa wa kufuata ratiba ya mazoezi kuliko wale wanaofanya mazoezi mchana. Sababu ni kwamba unapamka asubuhi, unakuwa umepumzika na umejaa nishati. Mchana, baada ya siku ndefu ya kazi, unaweza kuwa hauna nishati au hamasa ya kufanya mazoezi.
Kunyoosha na kufanya mazoezi asubuhi pia kunakufanya damu yako izunguke na kukupa mlipuko wa nishati na adrenalin ambayo itakusaidia kuanza siku vizuri.
5.Soma
Tano, soma. Tafiti zinaonyesha kuwa watu wenye mafanikio, mamilionea waliojitengenezea mafanikio wote wanasoma kwa saa moja au zaidi kila asubuhi. Kama vile kufanya mazoezi asubuhi kunavyoufanya mwili wako kuwa tayari, kusoma asubuhi kunaifanya akili yako pia kuwa tayari.
Saa za asubuhi ni wakati mzuri wa kusoma kidogo kabla ya kwenda kazini. Ninapendelea kusoma kitu cha kielimu au cha kuhamasisha au cha kutia moyo ambacho kinanipa hamasa kidogo.
6.Tafakari
Sita, tafakari. Tafakari ni njia bora ya kusafisha akili yako, kuondoa msongo wa mawazo na kusaidia kuzingatia kazi iliyopo. Tumia dakika chache kukaa kimya na kuacha akili yako itulie.
Si tu kwamba tafakari ya asubuhi itakusaidia kufurahia faida zote za kiafya zinazohusiana na tafakari, lakini pia itakuruhusu kuanza siku na mwelekeo mpya na safi.
7.Tumia Muda na Familia Yako
Saba, tumia muda na familia yako. Asubuhi inaweza isiwe na muda mwingi wa kutumia na familia yako kabla hawajaondoka, lakini unapaswa kutumia vyema muda unaoupata. Kaa chini na ule kifungua kinywa nao kama hiyo ni chaguo. Ikiwa si chaguo, angalau chukua muda kuzungumza nao kidogo kabla hamjaenda kila mmoja kwenye majukumu yake.
Hakika hakuna motisha bora kwa siku kuliko kutumia muda kidogo na wale unaowapenda zaidi. Zaidi ya yote, itakuwa motisha nzuri kwao pia wanapoanza siku yao.
Kabla sijahitimisha makala hii ya ratiba za asubuhi za watu wenye mafanikio, ningependa kukuachia wazo la kushiriki na marafiki zako. Akili yako ni kama misuli. Kadri unavyoitumia, ndivyo inavyokuwa na nguvu zaidi.
Sasa, ningependa kusikia kutoka kwako, swali langu la leo ni, je, unafanya mambo sahihi asubuhi? Acha maoni hapa chini nami nitahakikisha ninakufuatilia.
Ikiwa umeifurahia makala hii na kuhisi ilikuwa ya thamani katika kukufundisha kuhusu taratibu za asubuhi za watu wenye mafanikio, washirikishe na marafiki zako. Pia kama una swali au maoni yoyote usisite kuandika hapa chini. Unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024