Faida 10 Usizozijua Za Kuanzisha Blog Yako.

Faida 10 za Kuanzisha blog


Kwa nini unapaswa kuanzisha blog? Kama limekuwa ni swali ambalo umekuwa ukijiuliza kwa muda mrefu, basi nikuhakikishie kuwa, makala hii ni kwa ajili yako. Katika makala hii, nitakushirikisha faida 10 usizozifahamu za kuanzisha blog yako.
Kabla ya kuendelea kwenye faida za kuanzisha blog, hebu kwanza nizungumzie maana ya blog pamoja na aina zake.
Maana ya blog.
Kwa tafsiri rahisi, blog ni aina ya tovuti. Aina hii ya tovuti inakuwa na vitu vifuatavyo:
i. Makala: Blog inakuwa na makala ambazo zinaandikwa mara kwa mara. Kila makala moja inapoandikwa inakuwa juu ya makala ya zamani. Kwa mfano, kama uliandika makala juzi na jana, makala ya juzi itakuwa chini ya makala ya jana. Mfano mzuri wa blog ni hii uliyopo kwa sasa.
ii. Sehemu ya kuweka maoni: Kila makala inapowekwa kwenye blog, kwa chini yake huwa kunakuwa na sehemu ya kuweka maoni. Hivyo, kama msomaji atakuwa amepata swali au maoni yoyote kuhusiana na makala husika, ataweza kuweka maoni yake kwenye sehemu ya kuwekea maoni.
iii. Maktaba: Hii ni sehemu ambayo makala zote za blog zilizowahi kuandikwa huhifadhiwa.
Aina za Blog.
Kuna aina nyingi sana za blog na nitakutajia aina chache tu kama ifuatavyo:
i. Blog binafsi (Personal blog)
Hizi ni blog ambazo huanzishwa na watu binafsi ili kuelezea mambo yao binafsi ya ki-maisha.
ii. Blog za biashara.
Hizi ni blog ambazo huanzishwa na watu au wafanyabiashara ili kutangaza bidhaa au huduma zao na kuweza kuwasiliana na wateja wao.
iii. Blog za kitaalamu.
Hizi ni blog ambazo huanzishwa na watu ambao ni wataalamu wa fani fulani ili kuweza kutoa elimu kutokana na utaalamu wao. Kwa mfano, kuna blog za kilimo, afya, elimu, mapambo, mapishi, mitindo na kadhalika.
iv. Blog za habari.
Hizi ni blog zinazotoa habari na matukio yanayotokea kila siku. Mfano blog ya Milladayo.
v. Blog za Burudani.
Hizi ni blog zinazoandika habari za michezo na burudani. Mfano blog ya Salehe Jembe.
Faida 10 Za kuanzisha Blog.
Kuna faida nyingi sana za wewe kuanzisha blog. Miongoni mwa faida hizo ni hizi zifuatazo:
1. Blog itakujengea ujasiri na kufahamika.
Ukiwa na blog utaweza kufahamina na watu wengi na hivyo kukuza jina lako. Kutokana na kukuza jina lako, utakuwa na followers wengi. Hivyo, ukihitaji kuuza bidhaa au huduma, tayari utakuwa na mtaji wa watu wengi wanaokufahamu.
2. Kupata watembeleaji wengi (Traffic) kwenye bidhaa au huduma unayotoa.
Kama utakuwa unauza bidhaa au unatoa huduma mtandaoni, unapokuwa na blog na ukawa unaandika makala mbalimbali za kuelimisha, utapata watembeleaji wengi kwenye blog yako na hivyo utaweza kuwauzia bidhaa au huduma unayotoa.
3. Kuongeza wigo wa marafiki (Network)
Unapokuwa na blog, utaweza kufahamiana na watu wengi kutokana na makala unazoandika na hivyo kuweza kukuza mtandao wa marafiki.
4. Kuongeza Mauzo (Sales)
Pamoja na kufahamiana na kuongeza mtandao wa marafiki, makala unazoandika zitakufanya uaminike (Trust) na kukujengea heshima (credibility) mambo ambayo ni ya msingi katika kuongeza mauzo ya bidhaa au huduma unayotoa.
5. Kujifunza zaidi.
Ili uweze kuandika makala mara kwa mara, utatakiwa kujifunza zaidi. Hivyo, kwa kuwa na blog, itakufanya uweze kujifunza kila siku mambo mapya kutokana na mada unayoandikia kwenye blog yako.
6. Kuibadilisha jamii kwa kufanya vitu vya tofauti.
Kama una maarifa ambayo ufikiria ukiyatoa kwa jamii yako yataleta mabadiliko, basi, kwa kutumia blog utaweza kuielimisha jamii yako na jamii itakupenda na kukuheshimu.
7. Utaweza kuwasaidia watu.
Kama una ujuzi wowote ambao inawezekana ni wa kujifunza au umesoma chuoni, kwa nini usiwashirikishe watu ujuzi ulionao? Kwa kutumia blog, utaweza kuwashirikisha watu ujuzi wako nao watakupenda na kukuheshimu.
8. Utaweza kutangaza biashara yako.
Kama una bidhaa au huduma yoyote, blog ni sehemu nzuri sana ya kuweza kutangaza biashara yako.
9. Jamii itakutambua kuwa wewe ni mtaalamu (Expart)
Unapokuwa na blog, utaweza kuelimisha jamii ujuzi ulionao. Hivyo, jamii itakueshimu na kukutambua kuwa wewe ni mtaalamu wa fani au ujuzi huo.
10. Utatengeneza pesa.
Unapokuwa na blog na blog yako ikawa na watembeleaji wengi, utaweza kutengeneza pesa. Katika kutengeneza pesa, kuna njia nyingi ambazo unaweza kuzitumia. Njia hizo zimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni:
i. Njia za moja kwa moja (Direct methods)
ii. Njia zisizo za moja kwa moja (Indirect method)
i. Njia za moja kwa moja ni (Direct methods)
Njia za moja kwa moja ni njia ambazo utapata kipato moja kwa moja kutoka kwenye blog yako. Ingawa njia hizi sikupendekezei uzitumie kwenye blog yako kwani ili uweze kupata kipato kupitia njia hizi, ni lazima blog yako iwe na watembeleaji wengi. Mojawapo ya njia hizo ni:
-Kuweka matangazo ya biashara kwenye blog yako (Advertisements)
-Kupata makampuni yatakayodhamini blog yako.
Undani wa njia hizi nimeuelezea kwenye makala yangu ya njia za kutengeneza kipato kupitia blog.
ii. Njia zisizokuwa za moja kwa moja (Indirect methods)
Hizi ndio njia ambazo ninakushauri uzitumie, kwani zitakupatia kipato kikubwa hata kama blog yako itakuwa na watembeleaji wachache. Njia hizo ni pamoja na:
Kuandika na kuuza vitabu pepe (ebooks) kutokana na makala unazoandika.
Kuandaa kozi za mtandaoni kutokana na mada unazoandika na kuziuza kwa wasomaji wako.
-Kutoa huduma za kitaalamu za kulipia kwa wasomaji wako.
-Kuuza bidhaa zako zingine kwa wasomaji wa blog yako.
Njia hizi zote, nimezielezea kwa kina kwenye makala yangu ya njia za kutengeneza kipato kupitia blog.
Pia kama unahitaji kujifunza kutengeneza blog yako wewe mwenyewe, unaweza kupitia makala yangu ya jinsi ya kuanzisha blog, ambapo nimeelezea kwa kina na kwa lugha rahisi, jinsi ambavyo utaweza kuanzisha blog yako wewe mwenyewe. Lakini pia kama utahitaji huduma ya kutengenezewa blog, basi unaweza ukawasiliana nami kwa simu no. 0752 081669.
Ni matumaini yangu, kuwa umepata maarifa ya kutosha kuhusiana na faida za kuanzisha blog yako. Kama una swali au maoni, usisite kuandika hapo chini. Pia unaweza kuwasiliana nami moja kwa moja kwa kutumia na. 0752 081669. Asante na karibu tena kwenye makala zijazo.

Mambo 3 Ya Kufanya Kila Siku Ili Kufanikiwa.

Mambo 3 Ya Kufanya Kila Siku Ili Kufanikiwa.

Mafanikio Katika maisha yanategemea na jinsi unavyoitumia siku moja uliyopewa ya kuishi. Pia mafanikio ya siku yanategemea ni kwa namna gani umetumia vizuri masaa na dakika kwa siku hiyo. Kumbuka kuwa, muda ni rasilimali ya muhimu sana ambayo kila mtu amepewa kwa usawa. Hivyo, mafanikio yoyote Katika maisha yanategemea kwa kiwango kikubwa na jinsi unavyotumia muda wako. Kumbuka kuwa, haitoshi kuweka malengo ya mwaka, malengo hayo hayataweza kufanikiwa kama hautajua namna ya kuitumia vyema kila siku inayokuja na kupita.
Maana ya mafanikio.
Mafanikio ni neno pana sana na tafsiri yake inatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Kwa ujumla, mafanikio ni kuweza kufikia malengo uliyokusudia katika maisha yako kama vile: kuhitimu masomo, Kuanzisha biashara, kujenga nyumba, kuongeza kipato chako, kuwa na maisha mazuri na kadhalika. Hivyo, Kila mmoja anaweza kutafsiri neno mafanikio kwa kuhusianisha na malengo aliyojiwekea. Katika makala ya leo, nitakushirikisha mambo 3 muhimu ya kufanya Kila siku Ili uweze kufanikiwa.
Mambo 3 ya kufanya Kila siku ili uweze kufanikiwa.

1.Weka orodha ya mambo unayopaswa kuyakamilisha.
Ili uweze kufanikiwa Katika maisha, ni lazima uwe na orodha ya mambo unayopaswa kuyakamilisha ndani ya siku husika. Orodha hii unatakiwa kuiandika siku moja kabla ili unapoamka asubuhi uwe na ufahamu wa mambo unayopaswa kuyafanya. Hii itakusaidia kutokupoteza muda wako kwenye mambo ambayo si ya msingi. Pia itakusaidia kutokufanya mambo ambayo haukuwa umeyapanga.

2.Tumia Kanuni ya 80/20
Kanuni ya 80/20 ni Kanuni maarufu sana ya mafanikio ambayo Kwa jina jingine inaitwa ‘Pareto Principle‘. Hii ni Kanuni ya muhimu sana ambayo itakusaidia kufanikiwa katika maisha. Kanuni hii inasema kuwa:
“20 percent of your activities will account for 80 percent of your results”.
Maana ya kanuni hii Kwa lugha ya kiswahili ni kuwa: asilimia 20 ya mambo unayoyafanya ndiyo yanayochangia asilimia 80 ya mafanikio yako. Halafu, asilimia 80 ya mambo unayoyafanya yanachangia asilimia 20 tu kwenye mafanikio. Maana yake ni kuwa, ili uweze kufanikiwa ni lazima ufahamu kuwa, kuna mambo machache ya muhimu ambayo ukiyafanya, ndiyo yanayochangia kwa kiwango kikubwa kwenye mafanikio yako. Halafu, mambo mengine yaliyobaki yanachangia sehemu ndogo ya mafanikio yako.
Kwa mujibu wa kanuni hii,unapokuwa umeweka orodha ya mambo ambayo utayafanya Kwa siku, hakikisha unaanza na mambo muhimu yanayochangia kwa kiwango kikubwa kwenye mafanikio yako. Weka nguvu na akili zako zote kwenye kutimiza mambo hayo ya muhimu sana halafu ndio umalizie na mambo ambayo yanachangia Kwa kiwango kidogo kwenye mafanikio yako.

3. Anza na mambo magumu.
Katika orodha ya mambo ya kufanya uliyoweka, unapoamka na kuanza kutekeleza, anza na mambo ambayo ni magumu. Hii ina faida kubwa sana kwani itakusaidia kuweza kuyafanya ukiwa na nguvu na hivyo kufanya Kwa ufanisi. Baada ya kuwa umemaliza kufanya mambo magumu ambayo yanahitaji umakini wa hali ya juu, basi hapo ndio utaweza kuhamia kwenye mambo rahisi.
Kwa leo niishie hapo. Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa kuhusiana na mambo matatu muhimu unayopaswa kuyafanya kila siku ili uweze kufanikiwa. Kama una swali au maoni yoyote kuhusiana na mada hii, usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami moja Kwa moja Kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu tena katika makala ijayo.

Kanuni Ya Kupata Mafanikio: “The Equal Odds Rule”

Kanuni ya kupata mafanikio

Keith Simonton, mwanasaikolojia aliyehitimu masomo yake Chuo Kikuu cha Havard, mwaka 1977 alikuja na kanuni ya mafanikio inayojulikana kwa jina la The Equal Odds Rule. Kanuni hii aliiandika kwenye chapisho la “Creative productivity, age and stress: a biographical time-series analysis of 10 classical composers la mwaka 1977.
Kanuni ya The Equal Odds Rule inasema hivi:
“The average publication of any particular scientist does not have any statistically different chance of having more of an impact than any other scientist’s average publication.”
Kwa tafsiri rahisi ni kuwa, chapisho lolote la mwanasayansi yoyote haliwezi kuleta matokeo makubwa na ya tofauti kuliko chapisho la mwanasayansi mwingine.
Maana yake ni kuwa, ili mwanasayansi aweze kuleta matokeo makubwa na ya tofauti itategemea ni mara ngapi mwanasayansi huyo amerudia kufanya utafiti wa kile kitu kuliko wanasayansi wengine.
Hivyo ndivyo kanuni hii ya The Equal Odds Rule inavyoelezea jinsi ya kupata mafanikio kwenye jambo lolote. Ili uweze kupata mafanikio, nitakushirikisha mambo matatu ambayo unapaswa uyazingatie na kuyafanyia kazi kwa mujibu wa kanuni hii.
1. Amua unataka kuwa nani.
Hili ni jambo la muhimu sana na la kwanza kabisa unapotaka kupata mafanikio kwenye jambo lolote. Amua unataka kuwa nani au unataka kubobea kwenye kazi gani kwenye maisha yako. Je unataka kuwa mkulima, mfanyabiashara, mwanamichezo, mwajiriwa au uliyejiajiri? Hii itakusaidia kutambua ni kwenye eneo gani utawekeza nguvu zako na akili zako zote ili uweze kupata mafanikio. Kumbuka kuwa unapokuwa umechagua eneo ambalo utabobea kwenye maisha, utaifanya akili yako iongeze ubunifu Zaidi.
2. Amua huduma au bidhaa utakazokuwa unazalisha
Baada ya kuwa umeamua unataka kuwa nani, hatua ya pili ni kuchagua huduma utakazokuwa unatoa au bidhaa ambazo utakuwa unazalisha kwenye eneo ulilochagua. Kwa mfano umeamua kuwa mkulima. Kumbuka kuwa, kilimo ni eneo pana sana, hivyo unaweza kuchagua huduma au bidhaa ambazo utakuwa unazalisha. Kwa mfano, unaweza kuchagua kuzalisha mazao, kusindika, kusafirisha na kadhalika. Kama umejiajiri, chagua bidhaa au huduma ambayo watu watakutambua kuwa unatoa kwa viwango vya juu. Chagua huduma au bidhaa ambazo utakuwa unazalisha, usitake kufanya kila kitu kwani hautafanya kwa ufanisi hivyo utashindwa. Chagua eneo moja au maeneo machache ya kutoa huduma ambayo utajikita zaidi na hivyo kubobea.
3. Toa huduma au zalisha bidhaa mara nyingi na kwa muda mrefu bila kuacha.
Hapa ndio kwenye kiini cha kanuni hii ya The Equal Odds Rule. Katika kanuni hii inasema, mafanikio yatapatikana kama utaamua kufanya jambo moja na kulifuatilia kwa muda mrefu bila kuacha. Unapokuwa umechagua kufanya kazi fulani kwenye maisha yako, fanya kwa muda mrefu bila kuacha, haijalishi utapata vikwazo na kushindwa mara nyingi kiasi gani. Kumbuka kuwa, unapokuwa unarudia kufanya kile kitu mara nyingi na bila kuacha, hata kama utakuwa unapitia changamoto za kushindwa, kushindwa huko kutakupatia uzoefu mkubwa wa kufanikiwa baadaye kama hautakata tamaa.Mara nyingi watu wanashindwa kupata matokeo makubwa kwenye kazi wanazofanya kwa sababu wanafanya kidogo tu halafu wanakata tamaa na kuacha. Kama unataka kufanikiwa, fanya shughuli uliyoichagua kwa muda mrefu bila kukata tamaa.
Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ya jinsi ya kupata mafanikio kwa kutumia kanuni hii ya The equal odds rule. Kama una maoni yoyote kuhusiana na mada hii, ninatamani sana uweke maoni yako hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu no. 0752 081669. Asante na karibu kwenye Makala ijayo.

Kanuni Ya Mafanikio ‘Choma Meli Zako Zote’

Kanuni ya Mafanikio

Hernan Cortes, kamanda wa Hispania alikuja na Kanuni ya Mafanikio moja inayojulikana kama “Choma Meli Zako Zote'”. Kanuni hii inatokana na kazi aliyopewa ya kwenda kuvamia kisiwa kilichokuwa kinajulikana Kwa jina la Veracruz nchini Mexico mwaka 1519.

Kitu alichokifanya ni kuwa, alichukua makamanda 500 pamoja na Meli 11 za kivita na akawapandisha kwenda kuvamia kwenye kile kisiwa. Alipofika kwenye kile kisiwa, akaamuru makamanda pamoja na mabaharia wote washuke. Baada ya wote kuwa wameshuka, akaagiza Meli Zote zichomwe moto. Wakati Meli zilipokuwa zinaungua, akawauliza makamanda pamoja na mabaharia ” mnaona nini?” wakamjibu “Tunaona moto pamoja na moshi, meli zetu zinaungua”. Akawaambia ” Hivyo basi, hatuna uchaguzi zaidi kwenye vita hii. Ni lazima tuchague moja kati ya mambo haya mawili: Moja, tuamue kufa tushindwe vita, au pili, tupigane tushinde vita ambayo tumeianza.”

Unajua nini kilitokea? Ingawa walikuwa ni wachache ukilinganisha na jeshi ambalo walilikuta pale kisiwani, walishinda ile vita. Hapa ndipo tunapata Kanuni ya kuchoma meli zako zote. Kanuni ya kuchoma meli zako zote inamaanisha, ili uweze kufanikiwa kwenye malengo yako uliyojiwekea, jitahidi kufanya jambo na kulifuatilia kwa kutoa kila kitu ulichonacho. Hata Biblia inasema:
“Lolote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako, kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe” Mhubiri 9:10.
Maana yake ni kuwa, Katika maisha, ili uweze kufanikiwa kwenye jambo lolote ni lazima uwekeze nguvu zako zote na kila kitu ulichonacho. Kutokana na kanuni hii ya ‘choma meli zako zote’, kuna mambo matatu ambayo lazima uyazingatie:

  1. Lazima uamue kuhusu hatma ya maisha yako (Your future)

Lazima uamue kuhusu hatma ya maisha yako (your future). Usiruhusu maisha yako yaendeshwe na hali zinazokuzunguka au na matokeo ambayo yanaambatana na maisha yako. Hivyo, lazima uamue kuhusiana na kazi uliyonayo, kama ni mahusiano yako hauyafurahii, amua leo kuboresha mahusiano yako. Hivyo, haupaswi kuona kuwa, hali yako uliyonayo hauna mamlaka nayo na kwamba hauwezi kufanya kitu chochote kuboresha hali yako. Hivyo, jambo la kwanza kwenye Kanuni hii ya kuchoma meli zako zote ni , amua kuhusiana na kesho yako.

2. Achilia na usahau mambo yaliyopita.

Moja ya vitu ambavyo vinawafanya watu wengi washindwe kufanikiwa Katika maisha yao ni Kwa sababu wameruhusu mambo yao yaliyopita yaendeshwe maisha yao. Pengine kuna mambo ya kukatisha tamaa uliyopitia huko nyuma, pengine kuna maumivu uliyoyapata kutokana na mahusiano yako au uzoefu fulani unaoumiza ulioupitia. Mambo haya yote yamekusababisha mpaka sasa ukijiangalia unajiona kuwa ni mtu ambaye hauwezi kusonga mbele au kuchukua hatua na kufikia kule unakotaka kwenda. Hivyo, jambo la pili, usiruhusu mambo yaliyopita yaendelee kutembea na wewe. Hesabu mambo yaliyopita kuwa yalikuwa ni mambo ya kukufundisha, kukukomaza na kufanya uwe bora zaidi leo.

3. Tumia Kila kitu ulichonacho kufuatilia ndoto ambayo umechagua.

Kama alivyofanya Hernan Cortes ni kwamba, angeachia zile meli, angekuwa ameachia upenyo wa yeye kurudi atakapokuwa amezidiwa na maadui. Lakini Kwa sababu alichoma meli zote, kilichotokea ni kwamba, alihakikisha kwamba hakuna upenyo wa kukimbia. Hivyo, Ili ufanikiwe, toa kila kitu ulichonacho kupigania ndoto zako. Kama uko kwenye biashara, fanya kazi Kwa bidii, tumia nguvu zako, tumia akili zako zote. Kama uko kazini umeajiriwa na ndicho ulichokichagua, hakikisha unatumia kila kitu ulichonacho kufanya ambacho umekichagua. Tatizo la watu wengi ni kwamba, hawaweki kila kitu walichonacho Ili kufanikiwa.
Nimatumaini yangu kuwa umejifunza hizi hatua tatu kwenye kanuni ya mafanikio ya kuchoma meli zako zote kuweza kufikia ndoto zako. Kumbuka kuwa, siku zote hauwezi kufanikiwa kama ulichoamua kufanya haukifanyi Kwa nguvu zako zote. Je, wewe una ndoto gani? Nitafurahi sana kama utaniandikia hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami Kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala ijayo.

Tabia 8 Zinazozuia Fursa Za Mafanikio Maishani.

Tabia 10 Zinazozuia Fursa Za Mafanikio Maishani

Katika Maisha, ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na uwezo wa kuchangamkia fursa zinazokuja mbele yako. Watu waliofanikiwa ni wale waliotumia kwa usahihi fursa ambazo walizipata. Ninapozungumzia fursa, ninamaanisha jambo lolote ambalo ukilipata litakufanya ufanikiwe Katika maisha. Mfano wa fursa ni kama vile kupata ajira, kupata mtaji wa biashara, kupata wateja kwenye biashara yako na kadhalika. Kimsingi, fursa hazitafutwi bali zinavutiwa. Kuna tabia ambazo mtu akiwa nazo zinamfanya aweze kuvutia fursa nyingi kwake. Lakini pia kuna tabia ambazo ukiwa nazo zinafukuza fursa. Unabaki unalalamika tu kuwa huna bahati ya mafanikio, kumbe mafanikio umeyazuia kutokana na tabia ulizonazo. Katika makala ya leo nitakushirikisha tabia nane zinazozuia fursa za Mafanikio kwenye maisha yako.
Tabia 8 zinazozuia fursa za Mafanikio kwenye maisha yako.

  1. Mawazo hasi (negative thought)
    Mawazo hasi ni tabia inayoweza kuzuia fursa za Mafanikio. Mtu mwenye mawazo hasi ni mtu ambaye haamini kuwa anaweza kufanikiwa. Haamini kuwa vitu vinawezekana. Hawezi kuthubutu kufanya jambo ambalo linaweza kumletea Mafanikio. Hivyo, ukiwa na mawazo hasi watu watashindwa kukushirikisha fursa ambazo zingeweza kukufaa Katika maisha yako wakijua kuwa utazitilia mashaka na hivyo hautathubutu kuzifanyia kazi.
  2. Malalamiko au kutoa lawama.
    Malalamiko ni tabia nyingine ambayo inaweza kuzuia fursa za Mafanikio kwenye maisha yako. Mtu mwenye malalamiko ni mtu ambaye haridhiki na chochote atakachopata. Ni mtu ambaye analalamikia watu changamoto alizonazo badala ya kutafuta njia ya kuzitatua. Kimsingi, watu hawapendi mtu mwenye kulalamika muda wote kwani huwa wanahisi kuwa analalamika Ili awatwike matatizo yake. Mtu mwenye malalamiko hata kama akipata fursa, hataridhika bali ataitafutia kasoro na kulalamika. Hivyo ukiwa mtu mlalamishi, watu hawatakushirikisha fursa, kwani wanafahamu kuwa hautaridhika nayo.
  3. Kutokujali muda na kutokuwa na ratiba
    Kutokujali muda ni tabia nyingine ambayo inaweza kuzuia fursa za mafanikio kwenye maisha yako. Watu wanajali sana muda, hivyo wakiona kuwa wewe haujali muda, watakukwepa na hawatakushirikisha fursa. Jitahidi kujali sana muda Kwa kuwa na ratiba Katika maisha yako. Usikubali muda Wako kupotea bila sababu ya msingi kwani muda ni rasilimali ambayo ikipotea hauwezi kuirudisha.
  4. Kutokuwa mwaminifu
    Kuna msemo wa kiswahili unaosema ‘uaminifu ni mtaji’. Ukiwa mwaminifu Katika mambo Yako yote, watu watakuamini na watatamani kufanya na wewe kazi. Kama umeajiriwa fanya kazi zako Kwa uaminifu, watu watakupenda na utapata fursa nyingine nyingi kupitia uaminifu Wako. Kama umejiajiri, kuwa mwaminifu kwenye kazi unazoletewa. Zifanye Kwa ubora wa hali ya juu, watu watakupenda na utapata fursa nyingi zaidi. Hivyo, kutokuwa mwaminifu ni tabia inayoweza kuzuia fursa za Mafanikio kwenye maisha yako.
  5. Kudharau mwanzo mdogo
    Watu wengi wameshindwa kuanzisha biashara au kazi zao Kwa kuhofia kuanzia na mwanzo mdogo. Ili uweze kufanikiwa. Kubali kuanzia chini Ili upate msingi wa kukupeleka kwenye mafanikio unayoyahitaji. Ukianzia chini na ukafanya Kwa uaminifu, unajiwekea nafasi ya kupata fursa kubwa zaidi.
  6. Kushindwa kujifunza kwa haraka
    Katika Dunia ya leo mambo yanabadilika Kwa haraka sana. Hii ni kuanzia mfumo wa maisha, jinsi tunavyofanya kazi, jinsi tunavyofanya biashara na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hivyo Ili uweze kuendana na mabadiliko haya, unapaswa kuwa mwepesi kujifunza. Ukishindwa kujifunza kwa haraka utaachwa nyuma na utakosa fursa za mafanikio kwenye maisha yako. Kama unafanya biashara, jifunze Kila siku Ili uboreshe biashara yako. Kama unafanya kazi usiache kuboresha ujuzi Wako ili uweze kutoa huduma Bora zaidi. Kumbuka kuwa unapotoa huduma bora, unajiweka kwenye nafasi ya kupata fursa nyingi zaidi za mafanikio.
  7. Kujifanya mjuaji
    Ujuaji ni tabia mbaya sana inayoweza kukukosesha fursa. Mtu mjuaji ni mtu ambaye anahisi kuwa anajua Kila kitu hivyo hahitaji kujifunza zaidi. Ni mtu ambaye hashauriki. Watu hawapendi mtu mjuaji hivyo hawawezi kumshirikisha fursa kwani wanajua kuwa ataharibu.
  8. Kuwa na hasira za haraka Mtu mwenye hasira za haraka ni mtu asiyetabirika. Anaweza kukasirika muda wote akafanya maamuzi ya ajabu ambayo yanaweza kuleta hasira kubwa kazini au kwenye biashara. Hivyo, ukiwa na hasira za haraka, watu watashindwa kukushirikisha fursa ambazo zingeweza kukufaa Katika maisha yako. Ni matumaini yangu kuwa umepata maarifa ambayo yatakusaidia kwenye safari yako ya mafanikio. Kama una swali au maoni yoyote kuhusiana na mada hii usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana name moja kwa moja kwa simu namba 0752081669. Asante na karibu kwenye makala ijayo.

Hatua 4 Za Kupitia Kabla Wazo Lako Halijafanikiwa

Hatua 4 Za Kupitia Kabla Wazo Lako Halijafanikiwa

Kwenye maisha, ili uweze kuweka malengo ambayo yatakupa matokeo makubwa katika maisha yako ni lazima utaanzia katika wazo. Mambo yote makubwa unayoyaona hapa duniani yalianzia kwenye wazo. Mtu alikaa akawaza na akaamua kuchukua hatua. Ili wazo liweze kufanikiwa, ni lazima lipitie mchakato wa hatua mbalimbali. Watu wengi huwa wanaishia njiani kwenye mchakato huo na ndio maana mawazo yao huishia njiani na hivyo kushindwa kufikia malengo waliyokusudia. Katika Makala ya leo nitakushirikisha na kukupitisha kwenye hatua hizi nne muhimu ambazo ni lazima upitie kabla wazo lako halijafanikiwa.
Hatua 4 ambazo utapitia kabla wazo lako halijafanikiwa.
1. Conception stage

Katika hatua hii, unakuwa umepata wazo ambalo unafikiria linaweza kukutoa kimaisha. Ni hatua ambayo unakuwa na hamasa kubwa ya kufanya. Katika hatua hii hauoni vikwazo vyovyote ambavyo vinaweza kusababisha wazo lako lisiweze kufanikiwa. Unakuwa na hamu ya kumshirikisha kila mtu wazo lako. Hii ni hatua ya mwanzo kabisa.
2. Rejection stage
Baada ya conception stage, hatua inayofuata ni rejection stage. Katika hatua hii, wazo lako linaanza kupata upinzani. Unaanza kupata ukosoaji kutoka kwa marafiki, ndugu na jamaa wa karibu yako ambao mwanzoni uliamini kuwa wanaweza kukusaidia. Katika hatua hii watu wako wa karibu wanageuka na kuwa wakosoaji wakubwa. Ni hatua ambayo watu wanakuwa wanakueleza mapungufu tu ya wazo ulilowashirikisha na hawakupi mazuri ambayo yapo kwenye wazo lako. Ili uweze kuvuka kwenye hatua hii ni lazima uwe na uvumilivu wa kukabiliana na wakosoaji wote na usonge mbele ili uweze kupata mafanikio.
3. Implementation stage
Baada ya kuwa umevuka vikwazo vya wakosoaji wote, hatua inayofuata kuelekea mafanikio ya wazo lako ni implementation stage. Hapa unaanza kufanya kile ambacho ulikuwa umekipanga. Katika hatua hii unapaswa kufanya kwa bidii bila kuacha. Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu walipofikia kwenye hatua hii walifanya kidogo halafu wakaacha na kuhamia kwenye wazo lingine jipya. Kwa lugha nyingine wanaacha kufanyia kazi mawazo yao wanaanzisha wazo jipya na hivyo kurudi kwenye hatua ya mwanzo ambayo ni conception stage. Ili uweze kufanikiwa, fanyia kazi wazo lako bila kuacha na kwa muda mrefu. Komaa na wazo lako na mafanikio utayaona.
4. Celebration stage
Hatua ya nne ni celebration stage. Hii ni hatua ambayo, mafanikio yameanza kuonekana. Hata wale waliokuwa wanakukosoa na kukupinga wanapoona umeanza kufanikiwa wanarudi kuungana na wewe na kujisifia kuwa na wao walikuwa ni sehemu ya mafanikio yako. Ni hatua nzuri ambayo unatakiwa kuendelea kufanyia kazi wazo lako.
Hivyo, mafanikio yoyote huwa hayaji kirahisi. Kila aliyefanikiwa alianza na wazo. Baada ya kuwa amepata wazo na kuanza kulifanyia kazi, alipitia vikwazo vingi vya wakosoaji na hatimaye baada ya kushinda vikwazo hivyo, mafanikio yalipatikana. Hivyo, kama una wazo na unafikiria kuwa linaweza kukutoa kimaisha, usihofu kufanya. Utapitia katika hatua hizi nilizozizungumzia kwenye somo hili, ukiweza kuvuka hatua tatu za mwanzo, mafanikio utayaona.
Kwa leo niishie hapo. Ni matumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kutosha ambayo yatakusaidia kushinda vikwazo vyote ili uweze kufanikiwa. Kama una swali au maoni yoyote, usisite kuandika hapo chini. Pia unaweza kuwasiliana name moja kwa moja kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye Makala zinazofuata.

Aina 4 Za Elimu Unazohitaji Ili Uweze Kufanikiwa.

Aina 4 za Elimu Unazohitaji Ili uweze Kufanikiwa

Ili uweze kufanikiwa katika maisha unahitajika kuwa na aina nyingi mbalimbali za elimu na maarifa. Maarifa hayo unapokuwa umejifunza kwa pamoja na kuyafanyia kazi yatakusaidia kutimiza malengo uliyojiwekea. Katika mfumo wetu wa elimu tumekuwa tukijifunza aina mbili tu za elimu ambazo kwa uhalisia hazitoshi kutufanya tufanikiwe kwa viwango vya juu. Aina hizo za elimu ni elimu ya kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu (scholastic education) na elimu inayofundisha ujuzi (professional) education. Aina hizi za elimu ni muhimu lakini bila kuongeza na aina nyingine mbili za elimu ambazo nitakushirikisha katika Makala hii hazitoshi kukufanya uweze kufanikiwa. Hivyo, katika Makala ya leo nitakushirikisha aina nne za elimu unazohitaji ili uweze kufanikiwa.
Zifahamu aina 4 za elimu unazohitaji ili uweze kufanikiwa.
Aina hizi za elimu zimegawanyika katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza ni
1. elimu inayofundishwa darasani.
2. Elimu ambayo haifundishwi darasani.
1. Elimu inayofundiswa darasani.
Katika kundi hili la elimu kuna elimu za aina mbili ambazo ni:
a. Elimu ya kujua kusoma kuandika na kuhesabu (scholastic education).
Hii ni elimu inayokusaidia kufahamu kujua kusoma, kuandika na kuhesabu. Katika elimu hii, mtu anasoma elimu kuondoa ujinga. Hivyo mtu anaposema kuwa amesoma, huwa anamaanisha aina hii ya elimu. Aina hii ya elimu pekee haiwezi kukufanya uweze kufanikiwa.
b. Elimu inayofundisha utaalamu (professional education)
Hii ni elimu inayofundishwa kwenye vyuo mbalimbali. Kazi ya hii elimu ni kufundisha utaalamu kwenye fani mbalimbali. Elimu hii ndiyo inayozalisha wataalamu kama vile madaktari, wahandisi, walimu na kadhalika. Hii ni elimu ambayo inazalisha wataalamu ambao wanaingiza kipato kwa kuuza utaalamu wao. Wanaweza kuwa wameajiriwa au kujiajiri. Hivyo ili waweze kutengeneza kipato, ni lazima wauze utaalamu wao. Aina hii ya elimu itakuwezesha kuwa na kipato cha kati (middle income). Haiwezi kukufanya uweze kufanikiwa kwa kiwango cha juu na kuwa na uhuru wa kifedha. Hii ni kwa sababu haiwezi kukufanya uwe na kipato endelevu (passive income).
2. Elimu ambayo haifundishwi darasani.
Katika kundi hili la elimu kuna aina mbili za elimu ambazo ni:
a. Elimu ya msingi kuhusu fedha (financial education)
Hii ni elimu ya muhimu sana kwani inakufundisha jinsi kutengeneza kipato chako, jinsi ya kutumia kipato chako na ni jinsi gani utawekeza pesa zako ili ziweze kuongezeka thamani na hivyo kukufanya utajirike na kuwa na uhuru wa kifedha (financial freedom), jinsi ya kuweka bajeti na kadhalika. Elimu hii ndiyo inawatofautisha watu matajiri na masikini. Elimu hii haifundishwi darasani. Unaipata kupitia kusoma vitabu mbalimbali. Hivyo wekeza sana kwenye aina hii ya elimu ili uweze kufanikiwa.
b. Elimu ya maendeleo binafsi (self development)
Hii ni elimu inayokusaidia kuweza kutumia vipawa, vipaji na uwezo ulionao ili uweze kufanikiwa. Aina hii ya elimu ni muhimu sana kwani unapofahamu jinsi ya kutumia vipawa na vipaji ulivyonavyo utaweza kufanikiwa kwa viwango vya juu sana. Ndiyo maana kuna watu ambao hawakuwahi kuingia darasani lakini wana mafanikio makubwa sana katika maisha yao. Elimu hii pia unaipata kupitia kusoma vitabu. Hivyo wekeza muda wako kusoma vitabu ili uweze kufanikiwa katika maisha.
Swali la msingi ni hili, je elimu mbili za kwanza sio muhimu?
Jibu ni hapana. Elimu zote ni muhimu, hivyo ili uweze kufanikiwa, kama ukiwa na elimu ya darasani halafu ukaongezea kwenye aina hizi mbili za elimu ambazo hazifundishwi darasani basi mafanikio yako yatakuwa makubwa sana. Hivyo basi kama umebahatika kusoma, basi wekeza pia na kwenye aina hizi mbili za elimu ili uweze kufanikiwa. Lakini pia, kama haukubahatika kusoma, wekeza kwenye aina hizi mbili za elimu ambazo hazifundishwi darasani, utafanikiwa kwani kuna watu ambao hawakubahatika kuingia darasani, lakini kwa sasa ni matajiri wakubwa.
Kwa leo niishie hapo, nimatumaini yangu umepata maarifa ya kutosha ambayo yatakufanya uweze kufanikiwa katika maisha yako. Kama una maoni au swali lolote usisite kuweka maoni yako hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana name moja kwa moja kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu tena katika Makala zinazofuata.

Mbinu 2 Za Kukusaidia Kutunza Muda Wako.

Mbinu 2 Za Kukusaidia Kutunza Muda Wako.

Katika maisha ili uweze kufanikiwa, unahitaji rasilimali. Kati ya rasilimali zote ambazo Mungu ametubariki, Muda ndiyo rasilimali ya muhimu sana kuliko rasilimali zote na inapaswa kutunzwa kwa umakini wa hali ya juu. Hii ni kwa sababu, muda ukipotea hauwezi kuurudishwa (non- renewable resource). Muda ni wa thamani kuliko pesa kwani ukipoteza pesa, unaweza kutafuta nyingine ukapata na maisha yakaendelea. Lakini ukipoteza muda hauwezi kuurudisha. Hivyo, ili uweze kufanikiwa ni lazima uweze kufahamu jinsi ya kutunza muda wako. Katika Makala ya leo, nitakushirikisha mbinu mbili ambazo zitakusaidia kutunza muda wako ili uweze kufanikiwa.
Mbinu 2 za kukusaidia kutunza muda wako uweze kufanikiwa.
1. Panga vitu vyako katika mpangilio maalumu (systematic arrangement).
Jambo la kwanza kabisa ambalo litakusaidia kutunza muda wako ni kupanga vitu vyako katika mpangilio maalumu. Kama ni nyumbani weka mpangilio maalumu unaoonesha vitu vyako vitakaaje. Kwa mfano, nguo za kazini mahali zinapokaa, funguo za nyumba, ufunguo wa gari, vitabu na kadhalika. Mpangilio huu utakusaidia kufahamu kila kitu mahali kinapokuwa na hivyo kukusaidia kuokoa muda ambao ungeweza kuupoteza kwa kutafuta vitu. Kama ni ofisini, fanya mpangilio mzuri wa aina za faili. Mfano weka sections mbalimbali zinazotofautisha aina ya faili zilizopo ofisini kwako. Mfano unaweza kutofautisha aina za faili kama vile: Faili za barua, faili za nyaraka, faili za mikataba, faili za mambo ya fedha na kadhalika. Hii itakusaidia kutumia muda mfupi sana kutafuta faili zako. Pia unaweza kuweka mpangilio wa vitu vingine vilivyopo ofisini kwako kama vile vitabu, daftari, peni, mihuri na kadhalika. Kwa kufanya hivyo, utaonkoa muda mwingi sana ambao utautumia kufanya shughuli zingine.
2. Panga vitu vyako siku moja kabla.
Jambo la pili ambalo unaweza kulitumia kutunza muda wako ni kupanga vitu vyako siku moja kabla. Hapa kama unaenda kazini, unaweza kupanga nguo ambazo utavaa na unazitenga kabisa. Pia unatenga vitu vingine ambavyo utakwenda navyo kazini, kama vile vitabu, notebook, laptop na kadhalika. Hii itakusaidia unapoamka kesho, usipoteze muda muda kuanza kutafuta vitu ambavyo unapaswa kuenda navyo kazini. Kwa kufanya hivyo, utaokoa muda mwingi sana ambao utautumia kwa kuwahi kwenye eneo lako la kazi na hivyo kuongeza ubora wa kazi yako.
Kwa leo niishie hapo, nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kutosha ambayo yatakusaidia kutunza muda wako vizuri ili uweze kufanikiwa kwenye maisha yako. Kumbuka kuwa muda ndio rasilimali ambayo ikipotea hauwezi kuirudisha. Kama una maoni au swali lolote, usisite kuandika hapo chini. Pia kama una swali lolote kuhusiana na mada ya leo, usisite kuwasiliana name moja kwa moja kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu kwenye Makala zinazokuja.

Rasilimali 3 Unazohitaji Kutimiza Malengo Yako

Rasilimali 3 Muhimu Unazohitaji Uweze Kutimiza Malengo Yako

Watu wengi huwa wanaweka malengo makubwa katika maisha yao lakini wanaofanikiwa kutimiza malengo yao ni wachache sana. Hata wewe unaweza kujiuliza, mwaka uliopita ulikuwa umeweka malengo, je umeweza kutimiza malengo yako kwa kiwango gani? Jibu unalo. Lakini pia mwaka huu inawezekana una malengo ambayo tayari umeyaweka. Ili uweze kutimiza malengo yako, kuna rasilimali ambazo lazima uwekeze. Kila lengo unalopanga litahitaji rasilimali hizi. Katika Makala ya leo nitakushirikisha rasilimali tatu muhimu unazohitajika kuwa nazo ili uweze kutimiza malengo yako.
Rasilimali 3 muhimu unazohitaji uweze kutimiza malengo yako
1. Muda

Muda ndio rasilimali ya kwanza na muhimu sana katika maisha ambayo unahitaji kuweza kufikia malengo yako. Ni rasilimali ambayo inapaswa kulindwa na kutumika kwa uangalifu mkubwa sana. Hii ni kwa sababu muda ukipotea hauwezi kurudishwa (non-renewable resource). Hivyo ili uweze kutimiza malengo yako unapaswa kutumia vizuri muda wako kwenye kile tu ulichojiwekea malengo. Usiruhusu muda wako kupote ovyo. Kumbuka kuwa unaweza kupotesa pesa na ukatafuta nyingine ukaipata. Lakini hauwezi kuurudisha muda uliopotea. Mara nyingi huwa ninaona watu wapo kijiweni, na ukiwasalimia wanasema tupo hapa tunapoteza muda! Wanapoteza rasilimali ya thamani ambayo hawawezi kuirudisha. Hivyo, muda ni rasilimali ya thamani sana kwenye mafanikio yako.
2. Watu
Rasilimali nyingine ambayo utahitaji kuweza kufanikisha malengo yako ni watu. Utahitaji watu wa kukushika mkono, utahitaji watu wa kukusaidia kwenye kazi yako na utahitaji watu kwenye kila unachokifanya.
3. Fedha
Fedha pia ni rasilimali nyingine ambayo ni ya muhimu ili uweze kutimiza malengo yako. Fedha inahitajika katika kuendesha mradi au biashara uliyoianzisha.
Swali la msingi ni hili, kwa nini watu wengi huwa wanashindwa kutimiza malengo yao?
Jibu ni kuwa, watu wengi wanashindwa kutimiza malengo yao kwa sababu huwa wanatapanya rasilimali zao kwenye malengo mengi. Unakuta mtu ameanza biashara ya duka, mara akasikia kilimo cha matikiti kinalipa akaamua kulima matikiti, baadaye akasikia kuwa biashara ya mtandao inalipa akaamua pia kufanya biashara hiyo. Kumbuka kuwa kila lengo linahitaji rasilimali hizi muhimu tatu kama nilivyozielezea hapo juu yaani muda, watu na fedha. Hivyo ukiwa na malengo mengi utashindwa kufanikiwa kwa sababu utakuwa unarashia kwenye kila lengo. Hivyo, ili uweze kufanikiwa kutimiza malengo yako, ni lazima uwekeze nguvu kwenye lengo moja. Nguvu zako zote na rasilimali zako zote ni sharti uziwekeze kwenye lengo moja, hapo mafanikio utayaona. Kumbuka kuwa mafanikio hayaji kwa kufanya vitu vingi, bali yanakuja kwa kufanya kitu kimoja kwa weredi wa hali ya juu. Weredi huu unapatikana pale tu ambapo utakuwa umewekeza rasilimali zako zote kwenye lengo lako yaani pesa zako zote, muda wako wote na watu wa kukusaidia kufikia lengo lako.
Kuna neno la kingereza linalosema FOCUS. Maana ya neno focus ni kuzingatia na kufanya kile ulichokipanga na kukataa kila vishawishi ambavyo vitakuhamisha kwenye kile unachokifanya. Hivyo ili uweze kutimiza malengo yako ni lazima uwe na Focus, fanya kitu kimoja na usiruhusu upepo wowote ambao unaweza kuja kutaka kukuhamisha kwenye kile unachokifanya.
Kwa leo niishie hapo. Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kutosha ambayo yatakusaidia kuweza kufanikisha malengo yako. Kama una maoni au swali, usisite kuandika hapo chini. Pia kwa ushauri wowote, usisite kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye Makala zinazofuata.

Jinsi Ya Kutambua Kusudi La Maisha Yako

Jinsi kugundua Kusudi la Maisha Yako

Katika maisha, Mungu amemuumba kila mwanadamu na kumleta duniani kwa kusudi maalumu. Hivyo Mungu amempatia kila mwanadamu uwezo mkubwa ndani yake, kila mtu kwa aina yake ili aweze kutimiza kusudi lake la kuwa duniani. Hata wewe, Mungu ameruhusu uwepo duniani kwa kusudi maalumu. Ukigundua kusudi la maisha yako, utaweza kufanya mambo makubwa sana. Kwa bahati mbaya sana, watu wengi wanazaliwa mpaka wanakufa bila kutambua kusudi la maisha yao na hivyo kushindwa kutumia uwezo mkubwa ambao Mungu ameuweka ndani yao ambao kama wangeutumia wangeweza kufanya mambo makubwa sana Duniani na wangekuwa mbaraka mkubwa kwa watu wengine. Katika Makala ya leo nitakushirikisha jinsi ya kutambua kusudi la maisha yako ili uweze kufanikiwa kufanya mambo makubwa.
Jinsi ya kutambua kusudi la maisha yako uweze kufanikiwa.
1. Chunguza nguvu (umahili) wako.
Ili uweze kugundua kusudi la maisha yako, njia ya kwanza ni kuchunguza kwenye uwezo wako wa ndani. Hebu jichunguze, ni vitu gani ambavyo ukivifanya, unavifanya kwa ubora wa hali ya juu. Kwa mfano inawezekana ukawa una uwezo wa kuongea vizuri mbele za watu, kuimba, kucheza mpira, kuandika na kadhalika. Kutambua uwezo ulio nao ni hatua kubwa sana ya kutambua kusudi ambalo Mungu amekuleta Duniani. Hii itakusaidia kuwekeza nguvu kubwa kwenye eneo ambalo una umahili wa kutosha na kukufanya uweze kufanya mambo makubwa na ya kushangaza. Kumbuka kuwa kila uwezo au umahili ulionao una uwezo kabisa wa kuubadilisha na ukawa ni chanzo cha kuuingizia kipato.
2. Ongea na watu wa karibu wakuambie uwezo wako upo kwenye maeneo gani.
Njia nyingine ya kutambua kusudi la maisha yako ni kuongea na watu wako wa karibu. Hawa wanaweza kuwa ni wale watu unaowaamini kuwa watakuambia ukweli wa jinsi ulivyo. Mfano: marafiki wako wa karibu, mke au mme wako, wazazi na kadhalika. Waulize maswali wakuambie ni kitu gani unapokuwa unakifanya, unaonekana umekifanya vizuri sana na watu huwa wanakifurahia. Kusanya majibu ambayo watakuwa wamekupatia. Majibu uliyoyapata, yatakusaidia kugundua uwezo wako na hivyo kuweza kufahamu kusudi la maisha yako.
3. Fikiria ni vitu gani ulivyowahi kuvifanya na watu wakavifurahia (Past experience).
Njia nyingine ambayo unaweza kugundua kusudi la maisha yako ni kwa kuangalia uzoefu wako wa nyuma (past experience). Hapa unaangalia mambo yote ambayo uliwahi kuyafanya na ukayafurahia na pia watu wakakupongeza kuwa umefanya vizuri. Mfano, inawezekana kuna siku uliwahi kusimama mbele ya watu na ukaongea vizuri, baada ya kumaliza kuongea watu wakakupongeza sana kuwa umeongea vizuri sana. Hii ni dalili nzuri kuwa una uwezo mkubwa wa kuongea mbele ya watu kwa sababu si kila mtu anaweza kusimama na akaongea mbele za watu vizuri. Huo ulikuwa ni mfano tu, sasa unaweza kufikiria mambo yote uliyowahi kuyafanya na watu wakakupongeza.
Baada ya kutumia njia nilizokuelezea hapo juu, sasa unaweza kujua ni mambo gani una uwezo kubwa wa kuyafanya. Kwa kuangalia mambo hayo, sasa unaweza kufikiria ni kazi au shughuli gani unaweza kuifanya ambayo inahusiana na uwezo ulio nao. Kazi utakayoifanya ndilo litakuwa ni kusudi lako la maisha kwa sababu itakuwa ni kazi ambayo utakuwa unaifurahia na ni kazi ambayo inakuwezesha kutumia uwezo wote ambao Mungu ameuweka ndani yako. Hivyo, utafanya kazi kwa viwango vya juu na Kufanikiwa sana.
Kwa leo niishie hapo. Kama una maoni yoyote kuhusiana na mada ya leo, usisite kuweka maoni au swali lolote, usisite kuweka hapo chini. Pia kama unahitaji ushauri wowote, usisite kuwasiliana name moja kwa moja kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu tena katika Makala zinazokuja.

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp