Njia 7 za Kupata Subscribers Wengi Kwenye Chaneli Yako.

Njia 7 za Kupata Subscribers Wengi Kwenye Chaneli Yako.

Mafanikio kwenye chaneli ya YouTube yanatokana na kuwa na subscribers wengi. Hivyo mojawapo ya vipimo muhimu vya kupima mafanikio kwenye chaneli yako ya YouTube ni kupitia idadi ya watu wanaofuatilia Chaneli yako (subscribers). Ukiwa na subscribers wengi maana yake ni kuwa, video zako zitakuwa na watazamaji wengi. Kuweka video mara kwa mara huwa na athari kubwa kwenye idadi ya watu wanaofuatilia chaneli yako kwa sababu, kadiri unavyoweka video, ndivyo watu wanavyozitazama na kuzishea kwa marafiki zao. Hivyo, unapokuwa na video nyingi ambazo watu watazitazama na kuwashirikisha marafiki zao, utaweza kuongeza idadi ya wafuasi (subscribers). Hata hivyo, kupata subscribers kwenye YouTube hutokana na sababu nyingi zaidi ya kuweka video tu. Katika makala ya leo nitakushirikisha vidokezo 7 vya kusisimua vya jinsi ya kuongeza wanaofuatilia chaneli yako.

Kidokezo #1: Andaa video zenye maudhui yanayovutia na kuelimisha
Ikiwa unataka watu watazame video zako, unahitajika kuwa na maudhui yanayovutia na yenye kuelimisha. Hapa kuna baadhi ya njia ambazo zitakusaidia kuandaa maudhui bora zaidi:

Andaa maudhui ya video zako kwa kulenga kundi fulani la jamii.
Hakikisha kwamba unaandaa maelezo ya video yako (script) kabla ya kuanza kurekodi video yako ili kuepuka kuwajaza watazamaji taarifa zisizo za lazima. Iwapo unahisi kuwa kuna maelezo mengi katika video moja, yagawanye katika video kadhaa.
Watazamaji wanapenda unapotumia mfano kila baada ya muda fulani. Tumia mifano kadiri uwezavyo na uhakikishe kuwa inatoka kwenye tovuti au vyanzo vya habari vinavyoaminika na vyenye ubora wa hali ya juu.

Weka vivutio kwenye video zako ili watazamaji wawe na hamu ya kuangalia.
Anza video zako kwa kitu kinachogusa changamoto ya watazamaji. Kitu hicho kitakuwa ni ndoano (hook) ya kuvutia ambayo itawafanya watu watake kuendelea kutazama video yako mpaka mwisho.

Kidokezo #2: Andaa na Uweke Video Mara Kwa Mara
Hakuna shaka kwamba kuandaa na kuweka video mara kwa mara husaidia kuongeza wanaofuatilia kwenye chaneli yako. Kinyume chake, ikiwa hutaweka video kwa muda mrefu, watu hawatataka kujisajili kwenye chaneli yako.
Kulingana na utafiti uliofanyika, chaneli za YouTube zinazoweka video zaidi ya mara moja kwa wiki hufanya vyema zaidi kuliko zile ambazo haziweki video mara kwa mara. Mtu anapojisajili kweye chaneli yako, huwa anapata taarifa kwenye barua pepe yake kila unapopakia video mpya. Mtu akipata taarifa ya barua pepe mara moja kwa wiki, kuna uwezekano mkubwa kwamba atashiriki video yako, hasa ikiwa maudhui yake yanavutia na yanaelimisha. Hivyo, ikiwa unaweka zaidi ya video moja kwa wiki, kuna uwezekano mkubwa wa kupata subscribers wengi zaidi.

Kidokezo #3: Boresha Video Zako
Kuboresha video zako husaidia maudhui yako kuwa ya hali ya juu kwenye YouTube. Ili kuhakikisha kuwa video zako zinafikia hadhira inayofaa, unaweza kuboresha idadi ya vipengele vya video zako kama vile kichwa cha habari, maelezo, video na meta tagi zingine.

Kichwa cha habari.
Kutumia neno kuu la msingi katika kichwa chako cha video kunaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa video yako kutazamwa zaidi.

Maelezo.
Unapoandika maelezo ya video yako, hakikisha kuwa unatoa taarifa zote muhimu zinazohusiana na malengo ya video yako.

Weka tagi kwenye video zako.
Tagi ni maneno muhimu ambayo watu wakitafuta mtandaoni, wataiona video yako. Hivyo, ukiweka tagi kweye video zako, utawezesha video zako kuonekana kwa urahisi mtandaoni na hivyo kupata watazamaji wengi.

Kidokezo #4: Boresha chaneli yako ya YouTube
Ili kupata wafuatiliaji zaidi kwenye YouTube, unahitaji kuboresha sio tu video zako lakini pia hata Mwonekano wa chaneli yako. Hapa kuna baadhi ya njia rahisi zaidi za kufanya:

1.Weka video ya kionjo (trailer) inayoelezea kwa ufupi lengo la chaneli yako.
Kionjo huwapa hadhira yako muhtasari wa kile chaneli yako inatoa. Kupitia trela yako, unaweza kuwapa hadhira yako wazo kuhusu:
aina ya video unazoweka
ratiba yako ya kuweka video na kadhalika.

2.Tengeneza Mwonekano wa Kuvutia wa Chaneli yako
Ili chaneli yako ivutie, weka maelezo yanayoitambulisha kwa watazamaji wako. Tumia maneno ya msingi na yanayoendana na maudhui unayotoa kwenye chaneli yako. Kwa kufanya hivyo, utaiwezesha chaneli yako kuonekana kwa urahisi mtandaoni.

Kidokezo #5: Andaa Video za Ubora wa hali ya Juu
Jambo jingine linalochangia kuongeza wanaofuatilia chaneli yako ni kuweka video za ubora wa juu! Watu hawapendi kutazama video ambazo hazina sauti na video duni. Ikiwa unaweka video bora, watu watakuchukulia kwa uzito wa hali ya juu na kujihusisha na video zako.

Kidokezo #6: Shirikiana na hadhira yako kwa kujibu maswali na maoni yao.
Unapotangamana na watazamaji wako, unawapa hisia ya kuridhika kuwa unawajali na kuwapenda. Hii husababisha uwezekano mkubwa wa watu wengine kutamani kujisajili kwenye chaneli yako. Pia wahimize watazamaji wako kujisajiri kwenye chaneli yako.

Kidokezo #7: Tangaza Video Zako Kwenye Majukwaa Mengine Na Mitandao Ya Kijamii.
Ikiwa utapenda video zako zifikie watu nje ya YouTube, ni wazo zuri kutangaza video zako kwenye majukwaa mengine na mitandao ya kijamii.

Ni matumaini yangu kuwa makala hii ya “jinsi ya Kupata Wafuasi (Subscribers) Wengi Kwenye Chaneli Yako Ya YouTube” itakusaidia kufikia malengo yako ya YouTube. Ili kujitambulisha kama mtaalamu kwenye YouTube, unahitaji kupata idadi kubwa ya subscribers. Njia pekee ya kufanya hivyo ni kwa kutoa maudhui mazuri, kuboresha maeneo muhimu ya chaneli yako pamoja na kuandaa video zenye ubora wa hali ya juu.

Kama una swali au maoni yoyote, usisite kuandika maoni yako hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Makosa 4 Ya Kuepuka Kwenye Chaneli Yako Ya YouTube

Makosa 4 Ya Kuepuka Kwenye Chaneli Yako Ya YouTube

Unapoanzisha chaneli yako mpya ya YouTube, pengine tayari una mambo machache unayohitaji kuyafanya ili uweze kufanikiwa. Lakini, kama ilivyo muhimu kujua mambo unayopaswa kufanya, ni muhimu pia kujua ni makosa gani ya kuepuka. Katika makala ya leo nitakushirikisha makosa manne ambayo unapaswa kuyaepuka unapoanzisha chaneli yako ya YouTube.

Kosa #1 – Kupuuzia kujibu maoni na maswali ya watazamaji wako.
Watazamaji wako ndiyo sababu pekee inayokufanya uwe na chaneli ya YouTube. Bila wao, huwezi kupata mafanikio. Ikiwa watazamaji wako watakuuliza maswali au kukuachia maoni katika sehemu ya maoni ya video zako, basi unahitajika kuwajibu mapema iwezekanavyo. Unahitajika kuhakikisha kuwa unajibu kwa ufasaha majibu yanayoendana na swali lililoulizwa. Kadiri unavyojihusisha na watazamaji wako, ndivyo watakavyohisi wameunganishwa zaidi na biashara yako.

Kosa #2 – Kutoboresha Vichwa vya habari vya Video Zako
Ikiwa hutajumuisha maneno muhimu yanayoendana na maudhui ya video zako kwenye vichwa vya habari vya video zako, watazamaji wako hawataweza kukupata kwa urahisi katika matokeo ya utafutaji wanapokuwa wametafuta video zako mtandaoni. Unatakiwa kuhakikisha kuwa, unaandaa video za kipekee na zinazovutia ambazo zinajumuisha kwenye vichwa vya habari maneno muhimu ili video zako ziweze kuonekana juu zaidi katika viwango vya utafutaji.

Kosa #3 – Kutotangaza video zako.
Ukishindwa kutangaza video zako, inakuwa vigumu zaidi kwa watazamaji wako kutambua video ambazo umetayarisha. Ili uweze kupata watazamaji wengi kwenye video zako, unahitajika kushea video zako kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, telegram na kadhalika. Pia unaweza kushare video zako kwenye blog au tovuti yako kama utakuwa nayo. Pia katika kila video unayoweka kwenye chaneli yako, hakikisha unaweka logo inayowakilisha utambulisho wako (brand). Usipoweka utambulisho (brand) kwenye video zako, itakuwa ni vigumu kukuza jina la chaneli yako pamoja na biashara au huduma unayotoa.

Kosa #4 – Kutokuweka picha (thumbnail) kwenye video zako.
YouTube huruhusu kuweka picha inayotambulisha maudhui ya video yako (thumbnail). Picha hii ndiyo itaayoonekana karibu na kichwa cha habari cha video yako katika matokeo ya utafutaji. Usipochagua picha yako mwenyewe, YouTube itaipa video yako picha ambayo haitaendana na maudhui uliyoyakusudia ya video yako. Hivyo, ili kuwashirikisha watazamaji wako vyema zaidi, unahitajika kuhakikisha kuwa unaweka picha yako maalum ambayo inawakilisha vyema maudhui ya video yako.

Unapoanzisha chaneli yako ya YouTube, haya ni mambo manne ambayo unapaswa kuyaepuka. Kwa kuzingatia mambo haya niliyoyaeleza katika makala hii utakuwa kwenye njia nzuri ya kukuza chaneli yako ya YouTube na kupata mafanikio makubwa kwenye biashara yako.

Kwa leo niishie hapo. Ni matumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kukusaidia kuwa na chaneli ya YouTube yenye mafanikio. Kama una maoni au swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa kupiga au WhatsApp 0752 081669. Karibu tena kwenye makala zinazokuja.

Maswali 5 Ya Kujiuliza Kabla ya Kuanzisha Channel Ya YouTube

Channel ya YouTube

Katika makala zangu zilizopita nilielezea njia mbalimbali za kuanzisha biashara mtandaoni na kutengeneza kipato. Miongoni mwa njia hizo ni kuanzisha na kumiliki channel ya YouTube.Ikiwa umekuwa ukifikiria kuanzisha channel ya YouTube Kwa ajili ya biashara yako na hivyo kutengeneza kipato, kabla ya kuchukua hatua hiyo ni muhimu kujiuliza maswali kadhaa. Katika makala ya leo nitakushirikisha maswali matano muhimu Unayopaswa kujiuliza kabla ya kuanzisha channel ya YouTube ili uweze kupata mafanikio kwenye channel yako.

Maswali 5 Unayopaswa Kujiuliza Kabla ya Kuanzisha Channel Ya YouTube.

1.Kwa nini Unataka Kuanzisha Channel Ya YouTube?
Huenda hili ndilo swali muhimu zaidi unalohitaji kujiuliza kabla ya kuanzisha channel ya YouTube. Je, unahitaji kuanzisha channel ya YouTube kwa ajili ya kupeleka watembeleaji wengi kwenye tovuti ya kampuni yako? Je, unahitaji kuanzisha channel ili kujitangaza watu wafahamu biashara au huduma unayotoa ? Je, una maarifa au ujuzi na hivyo una shauku ya kuwashirikisha watu maarifa yako? Je, unaona kuna tatizo fulani katika jamii na unahisi unaweza kulitatua kupitia kuelimisha kwa kurekodi video? Je, una kipaji fulani na hivyo unahitaji kukionyesha ili watu wakutambue? Hizi zote ni sababu nzuri za kutaka kuanzisha channeli ya YouTube. Hata hivyo, ikiwa unataka kuanzisha channel kwa lengo tu la kutengezeza pesa nyingi, basi unahitaji kufikiria upya kabla ya kufanya uamuzi wako. Kumbuka kuwa kupata pesa kinatakiwa kiwe kipaumbe chako cha mwisho. Kumbuka kuwa, pesa ni matokeo ya kutatua changamoto katika jamii. Hivyo channel yako inapaswa kujikita katika kutatua changamoto fulani katika jamii. Hivyo, ukiweza kutatua changamoto fulani kupitia channel yako, pesa zitakuja tu.

2.Je, nitakuwa ninaweka video zinazotangaza biashara na huduma zangu?
Watu wengi huwa wanaingia YouTube kwa sababu wanataka kuburudishwa, kufahamishwa na kuelimishwa, si kutazama matangazo ya biashara. Ili uweze kuwa na mafanikio kwenye channel ya YouTube ni sharti uwe unatengeneza video zenye manufaa na taarifa zinazoboresha taswira ya kampuni yako bila kutangaza sana. Kuandaa video za ” jinsi ya kufanya”, kunaweza kukusaidia kujenga uaminifu (trust) na kukubalika ( authority) kwa kwa wateja wako na wafuasi wako bila kulazimika kuuza bidhaa kwenye video zako.

3.Je, Nielezeje Video Zangu za YouTube?
Maelezo ya video zako yanapaswa kuwa mafupi na yanapaswa kujumuisha URL ya tovuti ya kampuni yako katika sentensi ya kwanza ya maelezo ili kuwahimiza watazamaji wako kutembelea tovuti yako. Pia hakikisha unajumuisha maneno ya msingi (keywords) kwenye maelezo yako ambayo yanawiana na malengo ya video zako pamoja na channel yako kwa ujumla. Hii itasaidia kuzifanya video zako zionekane kwa urahisi watu wanapozitafuta mtandaoni.

4.Je, Nitayarishe Video Zangu Mimi Mwenyewe?
Unaweza kuchagua kutayarisha video zako wewe mwenyewe au kuajiri mtu au kampuni ya utayarishaji. Hii itategemea ni pesa kiasi ngapi na wakati unaotaka kuwekeza. Ikiwa una rasilimali chache, unaweza kupiga video na smartphone yako au kamera ya HD. Hata hivyo unaporekodi video, unatakiwa kuhakikisha kuwa unapakia video mpya mara kwa mara. Ukiweza kurekodi video mpya na ya kusisimua kila wiki, utaweza kukuza idadi ya watu wanaofuatilia channel yako haraka.

5.Je, Niruhusu Maoni kwenye Video Zangu?
Kuruhusu watu kutoa maoni na kuuliza maswali kwenye video zako za YouTube kutawahimiza kushiriki uzoefu wao na kampuni yako na itaonyesha kuwa uko tayari kupokea maoni yao. Unaweza kufanya maoni yaonyeshwe kiotomatiki, au tu baada ya kuwa umeyaidhinisha.

Kuanzisha Channel ya YouTube kwa ajili ya biashara yako ni njia nzuri ya kukuza brand yako na biashara yako kwa ujumla. Hivyo, kujiuliza maswali haya kabla ya kuanzisha channel yako kunaweza kukuweka kwenye njia ya mafanikio.

Nimatumaini yangu umepata maarifa ya kutosha ambayo yatakusaidia kupata mafanikio unapokuwa umeanzisha channel yako ya YouTube. Kama una maoni au swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami moja kwa moja kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Hatua 7 Za Kufuata Ili Uweze Kufikia Uhuru Wa Kifedha.

Uhuru wa kifedha

Katika maisha lengo moja ambalo sote tunalo sawa ni kwamba, sote tunataka kuwa na kipato zaidi ili tuweze kuwa na uhuru wa kifedha. Hata hivyo, ni asilimia ndogo tu kati yetu tunapata uhuru wa kifedha tunaotamani. Sote tunataka kuwa na pesa za kutosha ili tuwe na maisha bora. Swali pekee ni, “Je, uko tayari kuwa na uhuru wa kifedha?” Habari njema ni kwamba kuna watu wengi zaidi wanaopata uhuru wa kifedha haraka zaidi kuliko hapo awali. Kupitia mipango sahihi ya kifedha pamoja na utekelezaji makini unaweza kuboresha kipato chako na kuwa miongoni mwa watu wenye uhuru wa kifedha . Katika makala ya leo nitakushirikisha hatua saba za kufuata ili uweze kukuza kipato chako na kuwa na uhuru wa kifedha.

Kanuni ya kuwa na Uhuru wa Kifedha
Uhuru wa kifedha unamaanisha kuwa una uwezo wa kuishi maisha yako bila kuwa na wasiwasi wa kupungukiwa au kuishiwa na fedha. Ikiwa uko tayari kupata uhuru wa kifedha, hapa kuna Kanuni yenye vipengele saba unayoweza kutumia ili kukusaidia kukusanya mali, kuwa na furaha zaidi, na kupata uhuru wa kifedha katika miaka ijayo.

1.Anza Kuwa na mtizamo chanya Kuhusu fedha.
Hatua ya kwanza ya kuwa tajiri na kupata uhuru wa kifedha inahusisha kuwa na mtizamo chanya kuhusu fedha. Kufikiria vibaya kuhusu fedha ni kikwazo cha kihisia ambacho lazima ukiondoe ili uweze kufikia uhuru wa kifedha. Lazima uondoe mawazo kwamba, kuwa na pesa nyingi husababisha uovu au kwamba, pesa haiwezi kununua furaha. Unapoanza kuwa na mtizamo chanya kuhusu pesa, utavutia fursa na kufungua milango zaidi ya kutengeneza kipato.

2.Andika Upya Malengo Yako Makuu ya Uhuru wa Kifedha
Jiwekee malengo ya kifedha. Andika upya na uhakiki malengo yako kwenye karatasi kila siku na ufikirie jinsi unavyoweza kuyatimiza. Hii itakuchukua kati ya dakika tano mpaka kumi. Kitendo cha kuandika upya malengo yako, na kuyafikiria kila asubuhi kabla ya kuanza ratiba yako ya siku nzima, kutaongeza nafasi zako za kuyatimiza.

3.Panga Ratiba Yako Ya Siku.
Panga ratiba yako ya siku mapema. Wakati mzuri wa kufanya hivyo ni usiku uliopita. Kitendo chenyewe cha kupanga kila siku, kila wiki, na kila mwezi mapema mambo ambayo utayafanya, kitakufanya uwe na hamasa zaidi na makini zaidi katika kila kitu unachofanya.Unapoweka mambo utakayofanya kwenye orodha, utaweza kujidhibiti ili ufanye tu mambo ambayo umeyakusudia kwa muda husika. Unapopanga kila siku mapema utaweza kudhibiti na kufuatilia tabia zako za matumizi pia. Panga kiasi unachopaswa kutumia kwa wiki, mwezi, au mwaka na uamue ni kiasi gani utaweza kuweka akiba.
Kwenye pesa yako uliyoitenga Kwa ajili ya akiba, weka sehemu ya pesa hivyo kwenye akaunti ya akiba, nyingine kwenye hazina ya dharura, nyingine kwa ajili ya kulipia madeni Pia unaweza kufikiria kutenga sehemu yako ya akiba kwa ajili ya kuwekeza kwenye soko la hisa na mifuko ya pamoja ya uwekezaji.

4.Kanuni ya Kuzingatia
Zingatia kwa nia moja, kila saa ya kila siku, inatumika vyema kwa ajili ya malengo uliyojiwekea. Kanuni ya umakini ni muhimu kabisa kufikia uhuru wa kifedha. Hakikisha kuwa kila kitu unachokifanya katika suala la kuweka malengo na mipango ya kifedha, kinalenga kukuwezesha kuamua jambo moja au mawili ambayo unapaswa kuzingatia zaidi kuliko kitu kingine chochote. Mambo unayozingatia zaidi na kutumia muda mwingi kufanya yanapaswa kuwa katika upatanishi wa moja kwa moja na malengo yako ya kifedha.Tumia muda wako kuzingatia kile kitakachokutengenezea pesa nyingi zaidi.

5.Wekeza Ndani Yako
Sikiliza programu za sauti za mafunzo mbalimbali kuhusu fedha kwenye gari lako. Kwa kugeuza gari lako kuwa chuo kikuu cha magurudumu, unaweza kuwa mmoja wa watu wenye ujuzi zaidi katika taaluma yako.
Nunua kozi za usimamizi wa fedha, soma vitabu kuhusu maendeleo binafsi ya kifedha na utafute makala mtandaoni kuhusu fedha. Unaweza hata kuwekeza kwako mwenyewe kwa kupata ushauri kutoka kwa mshauri wa kifedha. Baada ya muda utakuwa na maarifa mengi katika eneo la fedha kiasi kwamba watu watakuja kwako kutaka ushauri.

Jiulize Maswali Haya Ya Ajabu.
Jiulize “Maswali ya ajabu” mawili baada ya kila tukio muhimu maishani mwako.
Swali la kwanza ni, “Nilifanya nini Kwa usahihi?”

Na swali la pili ni, “Nitafanya nini Kwa namna tofauti, wakati ujao?”

Kwa kukagua utendaji wako mara baada ya kila tukio muhimu maishani mwako kama vile, mkutano, simu ya mauzo, na uwasilishaji, utakuwa bora haraka kuliko unavyoweza kufikiria. Majibu ya maswali haya yote mawili ni chanya. Kwa kukagua ulichofanya vizuri na kile ambacho ungefanya kwa njia tofauti wakati ujao, unapanga akilini mwako mwelekeo wa kuwa bora zaidi wakati ujao. Ikiwa utachukua dakika chache na kuandika kila kitu ulichofanya kwa usahihi na kila kitu ambacho ungefanya kwa njia tofauti mara tu baada ya tukio muhimu kama vile, simu au wasilisho, utajifunza kukua na kuboresha kazi yako kwa haraka zaidi. Unapojitathimini na kufanya maboresho kwenye kazi yako, kwa kweli, kutaboresha pia pesa ambazo utakuwa unapata.

7.Kuwa Mkarimu kwa Wengine
Jambo la mwisho ni kumtendea kila mtu unayekutana naye kama mteja wa mamilioni. Mtendee kila mtu, nyumbani na kazini, kana kwamba ndiye mtu muhimu zaidi ulimwenguni. Kwa kuwa kila mtu anaamini kwamba yeye ndiye mtu muhimu zaidi ulimwenguni, unapomtendea kana kwamba ndiye mtu wa thamani na muhimu kuliko wote, atathamini kwa jinsi ulivyomtambua na kumthamini na hivyo atakupenda na huduma yako au bidhaa yako pia ataipenda. Ni ukweli uliothibitishwa kwamba kuwa mtu mkarimu zaidi kutakusaidia kuvutia utajiri zaidi na kuwa mtu mwenye furaha zaidi.

Jinsi ya Kuokoa Pesa na Kupata Uhuru wa Kifedha.

Uhuru wa kifedha

Katika jambo hili, ninapendekeza mchakato wa polepole wa kujifunza kuokoa pesa. Kwa kuanzia, anza na 1% ya mapato yako na kuishi kwa 99% nyingine.
Kwa mfano, ikiwa unapata Tsh.200,000 kwa mwezi, fanya uamuzi leo wa kuokoa Tsh.2000 kwa mwezi. Kisha unaweza kuishi kwa kutumia Tsh.198, 000 nyingine. Okoa pesa kwa muda mrefu kwa kufungua akaunti tofauti ya benki, akaunti yako ya “uhuru wa kifedha”.
Mara tu unapoweka pesa kwenye akaunti hii ya akiba/uwekezaji, hutazitoa au kuzitumia kwa sababu yoyote ile.

Mara tu unapokuwa na maisha mazuri kwa 99% ya mapato yako, ongeza kiwango chako cha akiba cha kila mwezi hadi 2% na kuendelea.
Ndani ya mwaka mmoja, utajikuta unaishi kwa raha kabisa kwa 98% ya mapato yako ya sasa.

Endelea na mchakato huu hadi uokoe 15% na kisha 20% ya mapato yako. Hutaona hata tofauti katika kiwango chako cha maisha kwa sababu badiliko litakuwa ni la taratibu sana. Lakini tofauti katika maisha yako ya kifedha itakuwa ya kushangaza kabisa.

Kwa leo niishie hapo. Ni matumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kukusaidia kupiga hatua kuelekea kwenye uhuru wa kifedha. Kama una swali au maoni yoyote, usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami moja kwa moja kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Hatua 10 Za Kuwa Na Mafanikio Na Kuwa Tajiri

Hatua 10 Za Kuwa Na Mafanikio Na Kuwa Tajiri

Napoleon Hill alikuwa ni mwandishi wa vitabu vya mafanikio, raia wa Marekani. Vitabu vyake vililenga zaidi kwenye kanuni za mafanikio na kuwa tajiri katika maisha na kifedha. Alianza kazi yake kama mwandishi wa habari kabla ya kuwa mshauri wa rais wa Marekani wa kipindi kile aliyejulikana kwa jina la Franklin D. Roosevelt.
Ni wakati alipofanya mahojiano na Andrew Carnegie ndipo alipopata hamasa ya kuanza kazi yake ya kuhamasisha watu juu ya mafanikio. Alitumia maarifa aliyoyapata kwenye mahojiano hayo kuandika vitabu vya mafanikio katika biashara na kutengeneza kipato. Vitabu vyake vingi vimeendelea kuwa maarufu mpaka sasa kama vile vilivyokuwa kabla ya kifo chake mwaka 1970.

Hatua 10 Za Kuwa Na Mafanikio Na KuwaTajiri.
Kitabu Cha Think and Grow Rich kinaelezea nguvu iliyopo kwenye kuwa na fikra chanya kwenye maisha. Kitabu hiki kinaelezea umuhimu wa kuwa na fikra chanya za mafanikio. Watu waliofanikiwa toka zamani walikuwa na mawazo chanya kuwa watafanikiwa wakiwa na uvumilivu pamoja na elimu ya kile walichokuwa wanafanya. Pia walikuwa wamezingukwa na watu waliokuwa wana mawazo yanayoendana ya mafanikio kwenye kile walichokuwa wanafanya.
Kila mmoja anaweza kushindwa katika malengo aliyojiwekea ya maisha, lakini, kwa wale ambao wataendelea kujaribu bila kukata tamaa watafanikiwa.
Mambo ya msingi ya kujifunza kutoka kwenye kitabu cha Think and grow rich.

1: Mafanikio yanahitaji kuwa na malengo pamoja na mipango iliyoainishwa vizuri.
“Set your mind on a definite goal and observe how quickly the world stands aside to let you pass.” — Napoleon Hill.

Maana yake ni kuwa, jiwekee malengo, hapo ndipo utaona jinsi utakavyowapita wengine kimafanikio kwa haraka.

Jambo la muhimu kabisa katika mafanikio ni kujua nini hasa unachohitaji kufanikiwa. Bila kuwa na malengo yaliyo bayana, hatuwezi kuanza safari ya mafanikio. Hivyo, andika malengo yako kwa lugha rahisi iwezekanavyo. Kama unataka kuwa tajiri, unatakiwa ubainishe ni kiasi gani cha pesa unataka kumiliki utakapokuwa umefikisha umri fulani. Malengo yatakusaidia kufahamu ni kwa kiwango gani unapaswa kuwekeza ili uweze kufikia lengo kuu uliloliweka.

Baada ya kuwa umefahamu hitaji lako kuu na umejiwekea muda wa kuwa umelitimiza, jambo linalofuata ni kuweka mikakati ya hatua kwa hatua jinsi ya kutimiza lengo lako kuu. Baada ya kuwa umeweka hizo hatua, anza kufanyia kazi mara moja bila kukawia.
Kuweka malengo kutakupatia hamasa ya kufanya bidii kwenye kazi zako na hivyo kuweza kufanikiwa.

2: Kuwa na shauku ya kutimiza malengo yako. (Desire is the Starting Point of All Achievement)
Unaweza kupata chochote unachokitafuta katika maisha kama utakuwa na shauku (desire) ya kukipata.
Hii haimaanishi kuwa na shauku tu ya kupata kile unachokitamani. Kwa mfano unatamani kuwa na pesa na hivyo kwa kuwa na shauku tu pesa itashuka kwa muujiza, hapana. Badala yake ni kuwa, unapokuwa na shauku ya kufikia lengo kubwa katika maisha, utahamasika kuweka mipango madhubuti ya kufikia mafanikio.

Hatua zifuatazo zitakusaidia kuweka malengo yako ya kufanikiwa na kuwa tajiri (becoming wealthy):

i. Amua ni kiasi gani cha pesa unahitaji kukipata.

ii. Amua ni kitu gani utatoa au utawekeza ili uweze kupata kiasi cha pesa unachokihitaji.

iii. Weka tarehe ambayo umeamua kuwa utakuwa umepata kiasi hicho cha pesa.

iii. Weka mipango ya hatua kwa hatua ya jinsi utakavyofikia lengo lako. Pia angalia ni kitu gani utaanza kukifanyia kazi sasa bila kuchelewa.
Mambo yote hapo juu yaandike kwa sentensi fupi.
Jambo la mwisho, hakikisha kuwa unasoma sentensi hiyo mara mbili kwa siku.

3: Watu waliofanikiwa huwa wana imani na uwezo wao (successful People Have Faith in Their Abilities)
Imani isiyoyumba ndiyo rasilimali ya muhimu sana na ya ajabu sana kwenye mafanikio yako. Watu walio na imani watafanya kila kitu kwa nguvu, na kwa akili zao zote ili waweze kutimiza malengo yao. Hii ni kwa sababu, hautaweza kutimiza malengo yako kama haujiamini.

Mahatma Gandhi ni mfano mzuri sana wa nguvu ya imani na kujiamini. Gandhi hakuwa na nguvu yoyote ya kifedha au kijeshi. Badala yake alikuwa na imani isiyoyumba kuwa angeweza kuongoza taifa lake la India kupata uhuru. Imani Hii ilimuwezesha kuwashawishi wananchi wenzake kuanza kupigania uhuru wao.

Hata sisi, hatuna tofauti na Gandhi. Ikiwa tutakuwa na imani, ikiwa tutajiamini sisi wenyewe na uwezo tulionao, tutaweza kupata chochote tunachokihitaji.

4: Hauwezi kuwa na imani wakati huohuo ukiwa na hofu na mashaka.
Imani haiwezi kuwepo mahali palipo na hofu. Hivyo, wakati tutakapokuwa tumeshinda hofu zinazotukatisha tamaa, tutakuwa na imani isiyoyumba kutimiza malengo yetu na kupata utajiri.

Kuna aina sita za hofu:
i. Hofu ya umasikini ambayo husababisha kujiona kuwa haufai na kuwa na mashaka.

ii. Hofu ya kukosolewa. Hii ni hofu ambayo humfanya mtu asichukue hatua kwa kuogopa kuwa watu watamdharau na kumkosoa.

iii. Hofu inayosababishwa na hali ya kiafya. Kama mtu afya yake haiko sawa, anaweza kuogopa kuchukua hatua kutimiza malengo yake.

iv. Hofu ya kupoteza marafiki. Wakati mwingine unaweza kuogopa kuchukua hatua kwa kuogopa kupoteza marafiki.

v. Hofu inayotokana na uzee. Umri unavyozidi kwenda kuelekea kwenye uzee uwezo wa kufanya mambo huwa unapungua na kumfanya mtu awe na uoga wa kufanya mambo makubwa ambayo yatabadilisha maisha yake.

vi. Hofu ya kifo. Hofu ya kifo huwa inatufanya tuwaze zaidi kufa badala ya kuwaza ni kwa namna tunaweza kuishi tukiwa na maisha bora.
Mawazo yote ya hofu, hayawezi kukupatia mafanikio ya kifedha. Hivyo, tunapaswa kuepuka hofu ili tuweze kutimiza malengo yetu.

5: Pata elimu ya kitu unachotaka kufanya.
Elimu ni miongoni mwa vitu vya msingi sana katika kufikia malengo yako ya maisha. Kuwa na elimu haimaanishi kuwa na Diploma au Shahada.

Henry Ford ni mfano mzuri wa mtu ambaye hakubahatika kusoma lakini alikuwa na maarifa ya msingi ya kumsaidia kuweza kutimiza malengo yake.

Kuwa na mafanikio haihitaji kuwa na vitu vingi unavyovifahamu, badala yake, unahitajika kuwa kuwa na elimu na na uzoefu sahihi wa kile unachotaka kufanikiwa.

Ni rahisi kuridhika kuwa unafahamu vya kutosha kile unachokifanya katika maisha yako. Lakini, wale ambao wanaendelea kujifunza zaidi na kubobea kwenye ujuzi wa kazi wanazozifanya huwa wanafanikiwa sana. Hivyo, unaweza kujiendeleza zaidi kwa kusoma chuoni au kusoma kozi mtandaoni zinazoendana na kile unachokifanya ili uweze kukifanya kwa ufanisi na hivyo kufanikiwa kwenye maisha yako.

Pia, ili uweze kupata maarifa ya kutosha, mara zote unapaswa kujenga mahusiano na kuwa karibu na watu wenye uzoefu na elimu ya kile unachokifanya.

6: Kuwa na ndoto kubwa na uwe na hisia ya kuwa lazima utafanikiwa.
Kila mtu aliyefanikiwa, alianza kuwa na ndoto. Baada ya kuwa na ndoto, akajenga hisia kuwa lazima atafanikiwa. Hisia hizi zikanasa kwenye ubongo. Hivyo ili uweze kupata mafanikio, ni lazima uwe na ndoto pamoja na na hisia kali za kufanikiwa kwenye ndoto yako. Unapokuwa na hisia za mafanikio, hapo ndipo utapata njia na mipango ya kuwekeza kutimiza ndoto zako.

7: Tambua uwezo wako pamoja na mapungufu yako.
Kama unatambua udhaifu wako, utajipa changamoto ya kuzuia udhaifu wako usiweze kuzuia kutimiza malengo yako. Miongoni mwa mapungufu ambayo watu wengi wanayo ni pamoja na kukosa hamasa ya kufanya mambo (lack of ambition), kughairisha mambo (procrastination) na kuwa na malengo yasiyopimika (vague goals).

Ingawa unaweza kufahamu uwezo wako na udhaifu wako, unaweza kufahamu kwa ufasaha uwezo na mapungufu yako kwa kuandaa maswali ya kukuongoza kama ifuatavyo:

Je, nimetimiza malengo yangu ya mwaka?
Je, huwa ninakuwa na ushirikiano na wenzangu? Na kadhalika.

8: Kuwa na mtizamo chanya.
Unapokuwa ukifanya kazi kutimiza malengo yako, kuwa na mtizamo chanya kuwa utafanikiwa haijalishi utapitia changamoto kubwa kiasi gani. Jenga urafiki na mahusiano na watu walio na mtizamo chanya wa maendeleo kwani ukiwa umezungukwa na watu wenye mtizamo hasi, watakukatisha tamaa.

9: Watu waliofanikiwa ni wavumilivu kwenye changamoto.
Jizatiti kwenye malengo yako.

Watu huwa wanaferi katika malengo yao kutokana na kukosa uvumilivu. Katika malengo yako utapitia kushindwa lakini kumbuka kuwa mvumilivu. Kila unapopata changamoto, ichukulie kuwa ni sehemu ya kujifunza na kukufanya uwe bora zaidi. Watu waliofanikiwa huwa hawatoki nje ya malengo yao haijalishi wanapitia changamoto kubwa kiasi gani.

Jinsi ya kujenga uvumilivu na ustahimilivu kwenye malengo.
Ili uweze kuwa na uvumilivu pamoja na ustahimilivu kwenye kutimiza malengo yako, kanuni hizi zifuatazo zitakusaidia:

i. Andaa lengo katika maisha yako kutokana na kitu unachokipenda (Passion)

ii. Gawa lengo lako kwenye sehemu ndogondogo za utekelezaji na uweke mpango wa kutimiza lengo lako kwa kila sehemu ndogo uliyoiainisha.

iii. Usiruhusu mawazo hasi kuathiri utekelezaji wa malengo yako.
iv. Jenga mahusiano bora na watu wote ambao watakushika mkono katika nyakati ngumu.

10: Jiunge na kundi lenye shauku ya mafanikio ambalo mtabadilishana uzoefu (Mastermind group).
Kutengeneza kipato kunahitaji nguvu. Bila kuwa na nguvu hautaweza kuweka mipango yako katika utendaji. Kundi lako litaundwa na watu wenye shauku ya kufanikiwa na litakuwa na watu wenye ujuzi wa aina mbalimbali ambao mtabadilishana uzoefu na kupeana hamasa ya kuweza kufikia mafanikio. Tumia ujuzi ambao utakuwa unaupata kwenye kundi lako kutimiza malengo yako.

Kwa ufupi, kitabu cha Think And Grow Rich kinaelezea njia rahisi na zilizothibitishwa ambazo zitakusaidia kuwa tajiri. Kanuni hizi zimeelezwa kwa lugha rahisi na pia ni rahisi kuzifuata.

Kuwa na mtizamo chanya na kuweka mipango inayotekelezeka ni njia zitakazokusaidia kufikia malengo yako na kuwa tajiri. Pia unatakiwa kuambatana na watu sahihi ambao watakupa hamasa ya kufanyia kazi malengo yako.
Kanuni hizi ni za msingi, na hivyo jinsi utakavyozitumia itategemea na malengo yako. Hata hivyo, kitabu hiki kinatoa ushauri bora sana kwa mtu yeyote mwenye ndoto kubwa maishani ya kufanikiwa na kuwa tajiri.

Kama una maoni au swali lolote usisite kuandika hapa. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Sababu 3 Zinazozuia Usifanikishe Malengo Yako.

Sababu 3  Zinazozuia Usifanikishe Malengo Yako.

Katika maisha, kuna sababu nyingi sana ambazo huwa zinasababisha watu washindwe kutimiza malengo yao. Lakini kuna sababu tatu kubwa ambazo zimesababisha watu wengi washindwe kufikia mafanikio kwenye malengo yao. Kimsingi sababu hizi ukiweza kuzikabili, utaweza kutimiza malengo yako kwa haraka sana. Katika makala ya leo nitakushirikisha sababu 3 Zinazozuia usifanikishe malengo yako.

Sababu 3 Zinazozuia usifanikishe malengo yako.

1.Kushindwa kufanya maamuzi.
Watu wengi wameshindwa kufanikiwa kwenye malengo yao na katika maisha yao kwa ujumla kwa sababu walishindwa kufanya maamuzi. Hata wewe inawezekana bado hujafanikiwa kutimiza malengo yako kwa sababu umeshindwa kufanya maamuzi ambayo yangebadilisha maisha yako. Sababu kubwa zinazofanya watu washindwe kufanya maamuzi ni pamoja na hizi zifuatazo:

i. Wanaogopa kujihatarisha (taking risk)
Watu wanaogopa kufanya maamuzi kwa kuogopa kujihatarisha. Wanaogopa kuwa itakuwaje. Hata wewe inawezekana ulitakiwa ufanye maamuzi fulani ambayo yangebadilisha maisha yako, lakini umekuwa ukiogopa itakuwaje ukishindwa kufanikiwa. Kumbuka kuwa, hata usipofanya maamuzi, bado utakuwa unajihatarisha. Unajihatarisha kwa sababu hautafanikiwa.

ii. Wanaogopa watu watawaonaje.
Watu wengi huwa wanashindwa kufanya maamuzi sahihi yakayotimiza malengo yao kwa kuogopa watu watawaonaje. Hata wewe inawezekana unahitajika kufanya kazi fulani, biashara fulani au unahitaji kujiendeleza kielimu, lakini unahofia watu watakusemaje. Kumbuka kuwa, hata usipofanya maamuzi, bado utasemwa tu. Hivyo, ni bora ufanye maamuzi kwani hatma ya maisha yako ipo mkononi mwako.

iii. Wanaamini maisha ni majaaliwa.
Watu wengi ambao huwa wanashindwa kufanya maamuzi wanaamini ipo siku watafanikiwa kwani mafanikio ni majaaliwa. Hivyo hawako tayari kupambania maisha. Hivyo, kama unataka kufanikiwa katika maisha yako, hakikisha unafanya maamuzi bila kuchelewa.

2.Kutokukamilisha mambo.
Hili ni tatizo kubwa sana linalozuia usifanikishe malengo yako. Watu wengi wamekuwa na tabia ya kuanzisha mambo lakini wanashindwa kuyakamilisha. Hata wewe inawezekana ulianza biashara fulani au kazi fulani lakini ukaishia njiani. Inawezekana ulianza kusoma kitabu lakini umeishia njiani na kadhalika. Kumbuka kuwa hauwezi kufanikiwa kwa kuanzisha mambo, bali utafanikiwa kama utakuwa unakamilisha mambo uliyoyaanzisha. Hivyo ninakukumbusha kuwa, ili uweze kufanikisha malengo yako, hakikisha mambo unayoyaanzisha unayakamilisha.

3.Kufanya mambo na kuacha.
Hili ni tatizo kubwa sana linalozuia mafanikio ya watu wengi. Unakuta mtu leo anaanzisha biashara hii baada ya muda mfupi anaona haimlipi anahamia kwenye biashara nyingine. Baadaye anaona nayo haimlipi anahamia kufanya kitu kingine. Unakuta kila kitu anachokifanya kinakuwa hakina mwendelezo. Kumbuka kuwa, ili uweze kufanikiwa, ni lazima ufanye kitu kimoja kwa muda mrefu. Hata kama utakiona hakikulipi lakini baada ya muda kitakuletea mafanikio makubwa.

Swali la leo:
Ni kitu gani ambacho ulianza kukifanya halafu ukaishia njiani?

Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika hapa chini kwenye sanduku la maoni nami nitakurudia ili tupeane ushauri zaidi. Pia kama una swali lolote usisite kuandika swali lako au kwa kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Jinsi Ya Kupanga Bajeti Ili Uwe Na Mafanikio.

Jinsi Ya Kupanga Bajeti Ili Uwe Na Mafanikio.

Moja ya jambo la muhimu sana katika mafanikio yako ya kifedha ni kuwa na bajeti. Watu wengi wamekuwa wakipata pesa nyingi lakini wameshindwa kupiga hatua kwa kuwa huwa wanashindwa kutambua pesa zao huwa zinapotelea wapi. Hata wewe hebu jiulize, ni pesa nyingi kiasi gani zilizowahi kupita mkononi mwako? Halafu tafakari ni mambo gani uliyoyafanya. Katika makala ya leo nitakushirikisha njia rahisi na yenye mafanikio ya jinsi ya kupanga bajeti ya matumizi yako.

Jambo la kuzingatia kabla ya kuanza kupanga bajeti yako: Mkumbuke Mungu kwa kurudisha Zaka na Kutoa Sadaka.
Ili uweze kupata mafanikio na mibaraka, kumbuka kuanza kutenga asilimia 10 ya kipato chako kwa ajili ya Zaka ya Mungu na kiasi fulani kwa ajili ya Sadaka. Baada ya hapo, pesa yako iliyobaki, igawanye kwa kutumia bajeti ambayo nitaielezea kwenye makala hii ya leo. Kumbuka ya kuwa, Mungu ndiye mtoa uhai, afya na mibaraka yote.
Malaki 3:10
Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.

Jinsi ya kupanga bajeti ili uwe na mafanikio.

Kanuni ya 50/30/20.
Kanuni ya 50/30/20 ilitolewa na Senator wa Marekani Elizabeth Warren ambaye aliandika kitabu chake kinachoitwa Ultimate Lifetime: Money Plan. Katika kanuni hii alisema kuwa, unapokuwa umepata kipato chochote, unapaswa kukigawa katika mafungu matatu kama ifuatavyo:

Asilimia 50 : Matumizi ya lazima.
Haya ni matumizi ambayo ni ya lazima katika maisha yako. Matumizi ambayo ni lazima yaendelee katika maisha. Kwa mfano chakula, malazi na matumizi mengine ambayo unaona kabisa lazima yafanyike ili maisha yako yaendelee. Hivyo, chukua pesa yako uliyopata na uzidishe kwa asilimia 50, utapata pesa ambayo unapaswa kuitumia kwenye matumizi yako ya lazima. Pesa ya matumizi yako ya lazima isizidi asilimia 50.

Asilimia 30: Matumizi yasiyo ya lazima.
Haya ni matumizi ambayo siyo ya lazima, lakini unaweza kuyafanya kama unapesa ya kutosha. Ni matumizi ambayo hata kama utaamua kutoyafanya, maisha yako yataendelea. Hivyo, matumizi yako yasiyo ya lazima, yasizidi asilimia 30. Mfano wa matumizi yasiyo ya lazima ni kama vile, kwenda kujiburudisha mwisho wa juma, kununua fasheni mbalimbali za nguo, kutokupitwa na simu za kisasa na kadhalika.

Asilimia 20: Akiba, Uwekezaji na kulipa madeni.
Katika asilimia hii ishirini, utaitumia kwenye kuweka akiba, kuwekeza na kulipa madeni. Unaweza kuongeza hii asilimia 20 kwa kupunguza kiwango cha matumizi yasiyo ya lazima ili uweze kupata pesa nyingi zaidi kwa ajili ya kuwekeza na hivyo kuharakisha mafanikio yako.

Nimatumaini yangu umepata maarifa ya kutosha ambayo yatakusaidia jinsi ya kupanga bajeti ili uweze kuwa na mafanikio. Kama una swali au maoni, usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Kanuni 3 Za Fedha Zinazoleta Mafanikio Na Utajiri.

Kanuni 3 Za Fedha Zinazoleta Mafanikio Na Utajiri

Mafanikio yoyote ya kifedha yanaongozwa na kanuni. Kanuni hizi ndiyo huwa zinasababisha mtu apate fedha nyingi au awe masikini. Watu wengi wameshindwa kupata mafanikio ya kifedha kwa sababu wamekuwa wakitumia fedha bila kufahamu kuwa kuna kanuni zinazotawala matumizi ya fedha ili mtu aweze kufanikiwa. Katika makala ya leo, nitakushirikisha kanuni 3 za fedha zinazoleta mafanikio na utajiri. Kanuni ambazo ukizifahamu na ukazifanyia kazi utaweza kuitumia pesa yako vizuri, ukaizalisha na hivyo kuwa na mafanikio. Lakini pia, kwa kushindwa kufuata kanuni hizi, pesa zitakukimbia.

Kanuni 3 za fedha zinazoleta mafanikio na utajiri.

1.Kufanya kitu unachokipenda (Passion)- Mike Phillips 1977.
Kanuni ya kwanza iliandikwa na Mike Phillips mwaka 1977. Mike Phillips ni mtaalamu wa masuala ya fedha katika benki nchini Marekani. Mwaka 1977 aliandika kanuni hii kwenye kitabu chake kinachoitwa Kanuni Saba Za fedha (Seven laws of money). Katika kanuni hii anaeleza kuwa, hauwezi kufanikiwa kama kitu unachokifanya haukipendi. Hivyo ili uweze kupata mafanikio makubwa ya kifedha, ni sharti ufanye kazi au kitu ambacho unakipenda kwa dhati kutoka moyoni. Kitu ambacho utakifanya hata kama hakikupi matokeo unayoyatarajia kwa sasa. Kitu ambacho utakuwa tayari kukifanya hata kama hakikulipi kwa sasa. Unapokuwa unafanya kitu unachokipenda na kwa muda mrefu, baadaye kitu hicho kitakulipa na kukupatia mafanikio makubwa.

2.Jilipe asilimia 10 ya kila kipato chako- George Clason (1926)
Kanuni ya pili ni kanuni iliyoandikwa na George Clason mwaka 1926 kwenye kitabu chake maarufu kinachoitwa The Richest Man in Babylon. Katika kanuni hii anaeleza kuwa, ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe unatenga asilimia kumi ya kila pato lako kwa ajili ya kuweka akiba. Akiba hii unatakiwa uwekeze kwenye kitu kinachozalisha ili iweze kuongezeka. Hii haijalishi unapata pesa kiasi gani. Mafanikio yako yatatokana tu ni kwa kiwango gani unawekeza pesa yako. Ukiona kwenye maisha yako pesa yote unayopata inatumika kwenye matumizi ya kawaida, basi tambua kuwa hautaweza kupata mafanikio. Hivyo, ili uweze kupata mafanikio, hakikisha kila unapopata kipato, kabla ya matumizi, anza kwa kutenga asilimia 10 kwa ajili ya kuwekeza.

3.Kabiliana na kanuni ya Parkinson (Parkinson Law).
Kanuni hii inatokana na na Mwingereza anayeitwa Northcote Parkinson. Kanuni hii inasema hivi:
“Kiwango cha matumizi huwa kinaongezeka kadiri kipato kinavyoongezeka”.

Maana yake ni kuwa, ili uweze kufanikiwa kifedha, ni sharti uvunje kanuni hii. Kadiri kipato chako kinavyoongezeka ni lazima matumizi yako yabaki vilevile au yaongezeke kwa kiwango kidogo kuliko ongezeko la kipato.

Swali la leo:
Ni kanuni ipi kati ya kanuni hizo 3 umekuwa hauizingatii? Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika hapa chini kwenye sanduku la maoni. Nami nitakurudia ili tupeane ushauri zaidi.
Pia kama una swali au maoni, usisite kuandika hapa chini. Asante sana na karibu katika makala zijazo.

Jinsi Ya Kutumia Muda Vizuri: Parkinson Law

Jinsi Ya Kutumia Muda Vizuri: Parkinson Law

Kila mmoja amepewa masaa 24 katika siku moja. Lakini, jinsi tunavyotumia masaa tuliyopewa ndiyo itaashiria kiwango cha mafanikio yetu. Watu waliofanikiwa huwa wanatumia vizuri sana masaa ndani ya siku ili waweze kutimiza malengo yao na kufanikiwa katika maisha yao. Sasa, ni kwa jinsi gani watu waliofanikiwa hutumia muda wao? Wengi wao wanafahamu kanuni ya Parkinson na hivyo huwa wanatumia kupanga muda wao. Katika makala ya leo nitakushirikisha jinsi ya kutumia muda wako vizuri.

Kanuni ya Parkinson inasema hivi:
“Work expands to fill the time available for completion.”
Kwa lugha ya kiswahili ni kuwa, kazi huwa inachukua muda wote ulioutenga wa kuikamilisha
.

Hii ina maanisha kuwa, haijalishi ni muda mrefu kiasi gani ulioutenga kwa ajili ya kufanya kazi fulani, kwa muda ulioutenga, kazi yako itakamilika kwa muda huohuo. Kama umetenga muda mfupi, na kazi yako itakamilika ndani ya muda mfupi. Kwa mfano, kama umetenga dakika ishirini za kufanya kazi fulani, utatumia dakika hizo hizo ishirini kukamilisha kazi hiyo. Sasa anza kutumia kanuni ya Parkinson kwa faida kwa kufuata hatua hizi 5.

1.Weka malengo na vipaumbele.
Hatua ya kwanza ya kutumia kanuni ya Parkinson ni kuandika malengo yako na vipaumbele. Elezea kwa nini kazi hii uipe kipaumbele cha kwanza na endelea kuainisha kazi zako zote za siku kwa vipaumbele vyake na kila kazi uipatie muda wa kuikamilisha.

2. Ainisha vikwazo na changamoto ambazo unahisi zinaweza kujitokeza.
Weka orodha ya vikwazo au changamoto ambazo unahisi zinaweza kujitokeza unapokuwa ukitekeleza kazi zako. Hii ni hatua ya muhimu sana, usiiruke. Unapokuwa umefikiria mapema vikwazo au changamoto ambazo zinaweza kujitokeza, utaweza kuziepuka au kuzifanyia kazi mapema hivyo kuokoa muda na kufanya kwa ubora.

3. Weka muda wa kutimiza kila kazi.
Baada ya kukamilisha hatua za mwanzo, basi unatakiwa kugawa muda kwa kila kazi. Kama kazi zako zitakuwa na sehemu ndogondogo, unaweza pia kila kazi ndogo ukaigawia muda wake. Lengo ni kuhakikisha muda wako haupotei. Hii itakusaidia kuwa na picha kamili kuwa kazi zako zote za siku zitatumia muda kiasi gani.

4. Tambua na uondoe vitu vyote ambavyo huwa vinapoteza muda (time wasters)
Hii ni hatua ya muhimu sana ambayo itakusaidia kutunza vizuri muda wako. Unapokuwa umemaliza kazi moja, kuwa makini sana na uepukane na vitu vingine ambavyo vitakuchukulia muda wako ambavyo haviendani na kazi zako. Miongoni mwa vitu hivyo vinaweza kuwa, kujibu barua pepe ambazo hazina umuhimu, kuingia kwenye mitandao ya kijamii, kupoteza muda Whatsapp kwa vitu ambavyo siyo vya msingi na kadhalika.

Katika makala ya leo tumeangalia jinsi ya kutumia muda vizuri ili kuwa na mafanikio. Kwa kutumia kanuni hii ya Parkinson, utaweza kutumia muda wako vizuri na kufanya mambo makubwa ndani ya siku.

Swali la leo:
Tayari umejifunza kuhusu kanuni ya Parkinson, utaitumiaje kutunza muda wako vizuri?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika hapa chini kwenye box la maoni. Pia kama una maoni yoyote au swali, usisite kuandika hapa chini. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Kanuni 3 Za Kuwa Na Maisha Yenye Furaha.

Kanuni 3 Za Kuwa Na Maisha Yenye Furaha

Hivi umeshawahi kupitia kipindi ambacho umekuwa ukijihisi hauna furaha katika maisha yako? Kila kitu unachokifanya unaona kabisa kinakuletea furaha ya muda mfupi tu na baadaye furaha yako inatoweka. Tatizo ni kuwa, umekuwa ukitafuta furaha bila kuwa na kanuni madhubuti ambazo zitakuletea furaha ya kudumu katika maisha yako. Hivyo, ili uweze kuwa na furaha katika maisha yako, unaohitajika kuwa na muda wa kuweka kanuni ambazo zitakuletea furaha katika maisha yako. Katika makala ya leo nitakushirikisha kanuni 3 za kuwa na maisha yenye furaha.

Kanuni 3 za kuwa na maisha yenye furaha.

1.Kuwa mtu mwenye malengo.
Miongoni mwa kanuni ya muhimu sana ya kuwa na maisha yenye furaha ni kuwa mtu mwenye malengo. Ili uweze kuwa na furaha, unahitajika kuweka malengo ambayo yataendana na kusudi la maisha yako na kuyafanyia kazi kila siku. Hii itakupa ramani halisi ya mwelekeo wa maisha yako na jinsi ambavyo utaitumia kila siku kuweza kutimiza malengo yako. Kwa kufanya hivyo utakuwa ukisogelea mafanikio yako na hivyo furaha yako kuongezeka. Kwa kufanyia kazi malengo uliyoyaandika, utajihisi furaha unapokuwa ukipiga hatua kwa kukamilisha lengo moja baada ya lingine kwa siku hiyo. Siku inapokuwa imeisha na ukaangalia nyuma mambo uliyoyatimiza, utajiona mwenye furaha kwani utakuwa unapiga hatua kuelekea kwenye mafanikio yako.

2.Kuwa mtu unayetaka matokeo.
Unapokuwa umeandika malengo yako, utaweza kupima maendeleo yako kwa kuweka vigezo vya mafanikio. Vigezo hivi vitakuwezesha kufahamu mafanikio yako hatua kwa hatua. Utaweza kufahamu ni hatua gani uliyofikia na ni hatua gani zaidi zinahitajika kuweza kufikia matokeo uliyoyakusudia. Unapokuwa unapima hatua za mafanikio yako, utaweza pia kujifunza muda ulioutumia na hivyo kukujengea tabia ya kutunza muda. Kadiri unavyokuwa unapiga hatua kwenye mafanikio uliyojiwekea kwa kutumia vigezo vya mafanikio ulivyoviweka, ndivyo utakavyokuwa na furaha zaidi katika maisha yako.

3.Endelea kuchukua hatua bila kuacha.
Kwa kuwa kuweka malengo ni jambo la muhimu sana ambalo litakupa hamasa ya kufanya kazi, ni muhimu kuendelea kuchukua hatua bila kuacha. Kumbuka, kuwa na malengo yaliyoandikwa bado haitoshi. Unahitajika kuchukua hatua kufanyia kazi malengo yako bila kuacha. Unapokuwa unapiga hatua haijalishi ni kubwa au ni ndogo kiasi gani, furaha yako itaongezeka.

Swali la leo.
Ni kanuni gani kati ya hizi tatu za kuwa na maisha yenye furaha utaanza kuitumia leo?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika kwenye sanduku la maoni hapa chini. Pia kama una swali au maoni yoyote, usisite kuandika hapa chini. Asante na karibu tena katika makala ijayo.

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp