Njia 7 za Kupata Subscribers Wengi Kwenye Chaneli Yako.

Njia 7 za Kupata Subscribers Wengi Kwenye Chaneli Yako.

Mafanikio kwenye chaneli ya YouTube yanatokana na kuwa na subscribers wengi. Hivyo mojawapo ya vipimo muhimu vya kupima mafanikio kwenye chaneli yako ya YouTube ni kupitia idadi ya watu wanaofuatilia Chaneli yako (subscribers). Ukiwa na subscribers wengi maana yake ni kuwa, video zako zitakuwa na watazamaji wengi. Kuweka video mara kwa mara huwa na athari kubwa kwenye idadi ya watu wanaofuatilia chaneli yako kwa sababu, kadiri unavyoweka video, ndivyo watu wanavyozitazama na kuzishea kwa marafiki zao. Hivyo, unapokuwa na video nyingi ambazo watu watazitazama na kuwashirikisha marafiki zao, utaweza kuongeza idadi ya wafuasi (subscribers). Hata hivyo, kupata subscribers kwenye YouTube hutokana na sababu nyingi zaidi ya kuweka video tu. Katika makala ya leo nitakushirikisha vidokezo 7 vya kusisimua vya jinsi ya kuongeza wanaofuatilia chaneli yako.

Kidokezo #1: Andaa video zenye maudhui yanayovutia na kuelimisha
Ikiwa unataka watu watazame video zako, unahitajika kuwa na maudhui yanayovutia na yenye kuelimisha. Hapa kuna baadhi ya njia ambazo zitakusaidia kuandaa maudhui bora zaidi:

Andaa maudhui ya video zako kwa kulenga kundi fulani la jamii.
Hakikisha kwamba unaandaa maelezo ya video yako (script) kabla ya kuanza kurekodi video yako ili kuepuka kuwajaza watazamaji taarifa zisizo za lazima. Iwapo unahisi kuwa kuna maelezo mengi katika video moja, yagawanye katika video kadhaa.
Watazamaji wanapenda unapotumia mfano kila baada ya muda fulani. Tumia mifano kadiri uwezavyo na uhakikishe kuwa inatoka kwenye tovuti au vyanzo vya habari vinavyoaminika na vyenye ubora wa hali ya juu.

Weka vivutio kwenye video zako ili watazamaji wawe na hamu ya kuangalia.
Anza video zako kwa kitu kinachogusa changamoto ya watazamaji. Kitu hicho kitakuwa ni ndoano (hook) ya kuvutia ambayo itawafanya watu watake kuendelea kutazama video yako mpaka mwisho.

Kidokezo #2: Andaa na Uweke Video Mara Kwa Mara
Hakuna shaka kwamba kuandaa na kuweka video mara kwa mara husaidia kuongeza wanaofuatilia kwenye chaneli yako. Kinyume chake, ikiwa hutaweka video kwa muda mrefu, watu hawatataka kujisajili kwenye chaneli yako.
Kulingana na utafiti uliofanyika, chaneli za YouTube zinazoweka video zaidi ya mara moja kwa wiki hufanya vyema zaidi kuliko zile ambazo haziweki video mara kwa mara. Mtu anapojisajili kweye chaneli yako, huwa anapata taarifa kwenye barua pepe yake kila unapopakia video mpya. Mtu akipata taarifa ya barua pepe mara moja kwa wiki, kuna uwezekano mkubwa kwamba atashiriki video yako, hasa ikiwa maudhui yake yanavutia na yanaelimisha. Hivyo, ikiwa unaweka zaidi ya video moja kwa wiki, kuna uwezekano mkubwa wa kupata subscribers wengi zaidi.

Kidokezo #3: Boresha Video Zako
Kuboresha video zako husaidia maudhui yako kuwa ya hali ya juu kwenye YouTube. Ili kuhakikisha kuwa video zako zinafikia hadhira inayofaa, unaweza kuboresha idadi ya vipengele vya video zako kama vile kichwa cha habari, maelezo, video na meta tagi zingine.

Kichwa cha habari.
Kutumia neno kuu la msingi katika kichwa chako cha video kunaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa video yako kutazamwa zaidi.

Maelezo.
Unapoandika maelezo ya video yako, hakikisha kuwa unatoa taarifa zote muhimu zinazohusiana na malengo ya video yako.

Weka tagi kwenye video zako.
Tagi ni maneno muhimu ambayo watu wakitafuta mtandaoni, wataiona video yako. Hivyo, ukiweka tagi kweye video zako, utawezesha video zako kuonekana kwa urahisi mtandaoni na hivyo kupata watazamaji wengi.

Kidokezo #4: Boresha chaneli yako ya YouTube
Ili kupata wafuatiliaji zaidi kwenye YouTube, unahitaji kuboresha sio tu video zako lakini pia hata Mwonekano wa chaneli yako. Hapa kuna baadhi ya njia rahisi zaidi za kufanya:

1.Weka video ya kionjo (trailer) inayoelezea kwa ufupi lengo la chaneli yako.
Kionjo huwapa hadhira yako muhtasari wa kile chaneli yako inatoa. Kupitia trela yako, unaweza kuwapa hadhira yako wazo kuhusu:
aina ya video unazoweka
ratiba yako ya kuweka video na kadhalika.

2.Tengeneza Mwonekano wa Kuvutia wa Chaneli yako
Ili chaneli yako ivutie, weka maelezo yanayoitambulisha kwa watazamaji wako. Tumia maneno ya msingi na yanayoendana na maudhui unayotoa kwenye chaneli yako. Kwa kufanya hivyo, utaiwezesha chaneli yako kuonekana kwa urahisi mtandaoni.

Kidokezo #5: Andaa Video za Ubora wa hali ya Juu
Jambo jingine linalochangia kuongeza wanaofuatilia chaneli yako ni kuweka video za ubora wa juu! Watu hawapendi kutazama video ambazo hazina sauti na video duni. Ikiwa unaweka video bora, watu watakuchukulia kwa uzito wa hali ya juu na kujihusisha na video zako.

Kidokezo #6: Shirikiana na hadhira yako kwa kujibu maswali na maoni yao.
Unapotangamana na watazamaji wako, unawapa hisia ya kuridhika kuwa unawajali na kuwapenda. Hii husababisha uwezekano mkubwa wa watu wengine kutamani kujisajili kwenye chaneli yako. Pia wahimize watazamaji wako kujisajiri kwenye chaneli yako.

Kidokezo #7: Tangaza Video Zako Kwenye Majukwaa Mengine Na Mitandao Ya Kijamii.
Ikiwa utapenda video zako zifikie watu nje ya YouTube, ni wazo zuri kutangaza video zako kwenye majukwaa mengine na mitandao ya kijamii.

Ni matumaini yangu kuwa makala hii ya “jinsi ya Kupata Wafuasi (Subscribers) Wengi Kwenye Chaneli Yako Ya YouTube” itakusaidia kufikia malengo yako ya YouTube. Ili kujitambulisha kama mtaalamu kwenye YouTube, unahitaji kupata idadi kubwa ya subscribers. Njia pekee ya kufanya hivyo ni kwa kutoa maudhui mazuri, kuboresha maeneo muhimu ya chaneli yako pamoja na kuandaa video zenye ubora wa hali ya juu.

Kama una swali au maoni yoyote, usisite kuandika maoni yako hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp