
Ndugu mpendwa, nimatumaini yangu kuwa unafuatilia Makala hii kwa makini kwa sababu unahitaji kutengeneza pesa mtandaoni. Hivyo, nikuhakikishie kuwa uko mahali sahihi. Baada ya kusoma Makala hii mpaka mwisho utakuwa umepata maarifa ya kina ambayo yatakuwezesha kutengeneza pesa bila kuathiri muda wako wa kazi.
Soma:Jinsi ya kutengeneza pesa (kipato) kupitia Blog:Njia 9 unazoweza kuzitumia.
Katika Makala hii nitakushirikisha kila kitu kutokana na uzoefu nilionao katika mtandao wa intaneti.
Njia 10 za kutengeneza pesa mtandaoni bila kuathiri muda wako wa kazi
Mpendwa, inawezekana kabisa kujiajiri na kutengeneza pesa mtandaoni. Hata hivyo unatakiwa ufanye kazi kwa bidii sana na wakati mwingine unaweza ukapitia kushindwa kwa namna moja au nyingine. Sikufundishi njia za kupata utajiri wa haraka, bali ninakufundisha jinsi ya kujenga biashara yako taratibu kupitia mtandao wa internet.
Inawezekana kwa sasa unafahamu mojawapo ya njia nzuri sana ya kutengeneza pesa kupitia intaneti ni kupitia kuanzisha na kumiliki blog yako mwenyewe. Hata hivyo kuna njia nyingi tu ambazo unaweza kuzitumia kuweza kujiajiri na kutengeneza pesa kupitia mtandao wa internet. Katika Makala hii nitakuelezea njia 10 ambazo unaweza kujiajiri mtandaoni na ukajipatia kipato.
Katika miaka yangu mingi ya uzoefu wa kutumia mtandao wa intaneti, nimegundua na kujifunza njia hizi ninazokuletea katika Makala hii. Njia hizi zinahitaji ujitoe hasa na ufanye kazi kwa bidi sana mwanzoni, lakini baadae zinakuwa ni chanzo kikubwa sana cha kipato endelevu.
Kitu cha msingi ambacho tutakizingatia katika kila njia ambayo utaamua kuitumia kutengeneza pesa mtandaoni ni kulenga kundi Fulani la watu unaotaka uwapatie huduma yako au kuwauzia bidhaa yako, kwa kiingereza inajulikana kama “niche” .Tafsiri nyingine ya niche ni mada (topic) unayoitolea huduma au kuuzia bidhaa.
Sasa hebu tuanze kuangalia njia hizi ambazo utazitumia kutengeneza pesa mtandaoni.
1. Tengeneza pesa mtandaoni kwa kuanzisha Blog inayohusiana na mada Fulani (Niche Blog).

Kama una mada Fulani unayoipenda unaweza kuanzisha blog kufundisha mada hiyo. Kwa mfano, kama unapenda kupika anzisha blog ambayo utakuwa unafundisha watu mapishi. Kama wewe ni mwalimu anzisha blog na ufundishe masomo uliyosomea. Kama wewe umesomea biashara, anzisha blog na ufundishe biashara na ujasiriamali. Kwa kweli kila ujuzi ulionao ambao sijautaja hapa unaweza kuutumia kuanzisha blog na ukafundisha watu ujuzi huo. Kupitia kufundisha watu ujuzi ulionao utapata kundi kubwa la watu ambao watakuwa wakikuamini na ambao watakuwa wakifuatilia blog yako.
Sasa swali ambalo unaweza kujiuliza ni kuwa, unawezaje kutengeneza pesa mtandaoni kupitia blog?
Jibu ni hili; Kwa sababu utakuwa tayari una kundi la watu wanaofuatilia Makala zako na ambao watakuwa wamependa kile unachofundisha, unaweza kukusanya Makala zako na ukaziboresha na ukaandaa vitabu pepe (ebooks) ambavyo utaviuza kwa wafuatiliaji wa blog yako. Nakuhakikishia kuwa kama watu wamependa kile unachofundisha nina uhakika kuwa watakuwa tayari kununua vitabu vyako. Pia unaweza ukaandaa kozi mbalimbali kutokana na kile unachofundisha na ukauza kwa wasomaji wako. Unaweza pia kuuza bidhaa yoyote inayoendana na kile unachofundisha na watu wakanunua.
Swali jingine ni kuwa, kama mimi sina bidhaa, nitauza nini?
Kama una watu wanaofuatilia blog yako unahitaji kuwauzia bidhaa ili uweze kujipatia kipato lakini huna bidhaa, unaweza kuuza bidhaa za watu wengine na ukapata gawio (commissions). Aina hii ya biashara inaitwa affiliate marketing. Katika Makala zinazofuata nitazungumzia biashara hii jinsi inavyofanya kazi mtandaoni.
Jambo la kupendeza ni kuwa kumiliki blog gharama yake ni ndogo sana kupitia kwenye wordpress na pia ni bure kabisa kupitia blogger. Nakushauri kama unahitaji kuanzisha blog yako kibiashara tumia wordpress kwani inakupa uhuru wa kuweka vitu vingi kwenye blog yako.
Kwa mfano:
unaweza kuweka mfumo wa malipo na watu wakanunua bidhaa zako moja kwa moja kwenye blog yako,
unaweza kufungua duka lako la mtandaoni,
unaweza ukawa na jukwaa (forum) kwenye blog yako,
unaweza kuandaa kozi mbalimbali na ukaziuza na mambo mengine mengi kitu ambacho huwezi kufanya kwenye blogger.
Hatua za kufuata unapotaka kuanzisha blog:
1. Chagua jina la blog yako na ununue anuani yako ya mtandaoni (domain name) .Hakikisha anuani inaendana na mada (niche) ya kile unachotaka kufundisha. Kwa mfano kama wewe una utaalamu wa Kilimo, basi unaweza ukawa na anuani kwa mfano kilimobora.com, kama unahitaji kufundisha mapishi unaweza kuwa na anwani ya mapishiyetu.com n.k. Unaweza kununua domain kupitia kwenye kampuni ya Namecheap. Kuna makampuni mengi yanayouza domain lakini nakupendekezea namecheap kwa sababu wanauza kwa bei ya chini kuliko makampuni mengine.
2. Baada ya kuwa umepata anuani yako, hatua inayofuata ni kutafuta mahali ambapo blog yako itahifadhiwa (hosting). Kuna makampuni mengi yanayotoa huduma hii, lakini nakupendekezea pia Namecheap kwa sababu wanahost kwa gharama ndogo kuliko makampuni mengine.
3. Baada ya kuwa umelipia gharama za hosting, Utatakiwa kuchagua application ambayo utaitumia kutengenezea blog yako. Utachagua WordPress kwani ni application nzuri ambayo ni rahisi kuitumia na unaweza kutengeneza blog wewe mwenyewe hata kama huna utaalamu wa lugha ya computer (coding).
4. Hatua inayofuata ni kuweka muonekano (Theme) kwenye blog yako. Unaweza kuchagua Hello Theme au Astra ambazo zote ni za bure kabisa.
5. Baada ya hapo blog yako itakuwa tayari na unaweza kuanza kuandika Makala kwenye blog yako. Pia kama unahitaji kuwa serious na kazi yako ya blog, unaweza kuwekeza Zaidi kwenye elimu kupitia vitabu mbalimbali vinavyofundisha namna ya kuanzisha blog, au kusoma kwenye kozi zingine mbalimbali.
2. Tengeneza na uuze application za Simu.

Kutokana na mapinduzi ya simu za mkononi, matumizi ya application yanaendelea kuwa makubwa na hivyo unaweza ukawekeza muda wako kutengeneza application mbalimbali za simu na ukatengeneza pesa kwa muda wako wa ziada bila kuathiri muda wako wa kazi. Iwe ni application inayotatua tatizo Fulani katika jamii au application ya burudani kama vile kuchezea game unaweza kutengeneza pesa.
Najua sasa utakuwa unafikiria application mbalimbali ambazo unazitumia kila siku ambazo zipo google play store au Apple store na unashangaa ni nani aliyezitengeneza. Utashangaa kuwa application nyingi zimetengenezwa na watu binafsi pamoja na wafanyabiashara wadogo. Kwa takwimu zilizopo ni kuwa watengenezaji binafsi wa application walitengeneza kiasi cha dola za kimarekani billioni ishirini kwenye Apple store kwa mwaka 2016 pekee.
Jinsi unavyoweza kutengeneza pesa mtandaoni kwa kutengeneza application za simu.
Kuna njia mbili ambazo unaweza kuzitumia:
1. Unaweza kuwa na wazo la kutengeneza application ambayo unafikiri itatatua tatizo kwenye jamii na watu wataipenda lakini hauna ujuzi wa jinsi ya kuitengeneza,tafuta mtaalamu wa kutengeneza app na umlipe akutengenezee na kuiweka google play pamoja na Apple store. Kama app yako itakuwa imetengenezwa vizuri na ikakubaliwa na google play store pamoja na Apple store utaweza kutengeneza pesa kila mtu anapopakua app yako.
2. Njia ya pili rahisi ni pale ambapo wewe mwenyewe una ujuzi wa kutengeneza app. Unaweza kutengeneza na kuiweka app yako playstore na apple store na ukatengeneza pesa kadiri watu wanavyopakua app yako. Pia unaweza ukawa unatengeneza app na kuziuza kwa watu wengine na ukatengeneza pesa.Kama unahitaji kujifunza kutengeneza App bora unaweza kujiunga na tovuti kama
Treehouse, CodeAcademy, na Skillcrush ili kupata ujuzi unaohitaji.
3. Anzisha duka la mtandaoni na uuze bidhaa kupitia mtandao wa Internet.

Kama utafikiria bidhaa nzuri ambazo zitatatua matatizo ya watu unaweza kuanzisha duka la mtandaoni na ukauza bidhaa zako. Zamani haikuwa rahisi kuanzisha duka la mtandaoni na maduka yalikuwa machache mno. Lakini kwa sasa ni rahisi mno kuanzisha duka la mtandaoni. Kwa kutumia wordpress, unaweza kuanzisha duka lako la mtandaoni hata kama hauna ujuzi wowote wa lugha za computer (codes).
Kuna njia mbili ambazo unaweza kuzitumia kuanzisha duka lako la mtandaoni.
1.unaweza kuuza bidhaa ambazo umetengeneza wewe mwenyewe kulingana na kundi la watu unaolenga kutatua matatizo yao.
2.unaweza kununua bidhaa kwa bei ndogo kwenye masoko ya mtandaoni yanayouza bidhaa kwa bei ndogo. Nakupendekezea soko la Aliexpress. Ni soko ambalo linauza bidhaa kwa bei ndogo kuliko masoko yote duniani. Na habari njema ni kuwa unaweza kuagiza bidhaa hata moja moja na bidhaa zikakufikia popote ulipo kupitia posta . Ukichangamkia fursa hii utatengeneza pesa nyingi na kwa muda mfupi kwani utashangaa bidhaa inayouzwa Tanzania kwa shilingi 25,000/=, Aliexpress unaweza ukakuta inauzwa kwa sh. 6000/=. Katika njia hii utaagiza bidhaa na ukiisha kuzipokea utaziweka kwenye duka lako la mtandaoni na kuziuza. Pia unaweza kuwauzia majirani zako.
4. Toa huduma kutokana na ujuzi ulionao utengeneze pesa mtandaoni.

Kama una ujuzi wowote kama vile uandishi, ubunifu (designing), utengenezaji wa tovuti na software (web development), masoko, uandishi na usimamizi wa miradi au ujuzi mwingine wowote ulionao , unaweza kufungua tovuti na ukajitangaza na watu wenye uhitaji wa huduma yako wakakutafuta. Fanya utafiti wa huduma unayotaka kuitoa, fungua tovuti na ujitangaze. Watu wanaohitaji huduma yako watakutafuta na utatengeneza pesa kwa muda wako wa ziada bila kuathiri kazi yako.
5. Fundisha mtandaoni na uuze ujuzi wako(Online coaching)

Kama ilivyo katika kutoa huduma kutokana ujuzi ulionao, unaweza ukaanza kufundisha na kutoa ushauri katika eneo ulilobobea. Kwa mfano, kama wewe umesomea masuala ya Biashara, unaweza kuwa unafundisha mada mbalimbali za biashara na pia ukatoa ushauri wa kibiashara kwa wateja wako kwa malipo.
6. Andaa kozi mbalimbali kutokana na ujuzi wako na uziuze mtandaoni.

Kama una ujuzi wa kutosha kutokana mada Fulani inawezekana kutokana na kazi unayofanya kwa sasa, au kutokana na kitu ambacho umejifunza na kukifahamu vizuri au kutokana na elimu uliyoipata chuoni, unaweza kuandaa vizuri ujuzi wako na ukaupangilia vizuri na ukaandaa kozi ambayo utawauzia watu ujuzi wako na kutengeneza pesa. Uzuri wa kuandaa kozi ni kuwa unaweza kuiuza kwa miaka mingi na ikawa ni chanzo chako kizuri cha kukuingizia kipato. Uandaaji wa kozi unahitaji kujitoa kwa nguvu zako zote na kutenga muda wa kutosha. Lakini baada ya kozi kukamilika inakuwa ni chanzo cha kudumu cha kutengeneza pesa. Kozi pamoja na bidhaa nyingine za mtandaoni kama vile vitabu pepe (ebooks) vinaitwa mifereji ya Kipato endelevu au kwa kiingereza “passive income streams”.Hii ni kwa sababu, baada tu ya kukamilisha kuandaa kozi au kitabu pepe na ukaviweka mtandaoni, vitakuingizia pesa mtandaoni hata ukiwa umelala kwa miezi na miaka.

Njia nyingine ya kuweza kutengeneza kipato (Pesa) kupitia mtandao wa intanet ni kuanzisha Channel ya Youtube. Ukianzisha channel ukawa unafundisha mada ambayo unaifahamu vizuri na itakayopendwa na watu, unaweza kutengeneza pesa nzuri. Ili uweze kutengeneza pesa kupitia matangazo ya youtube (Google adsence) , unatakiwa channel yako ifikishe subscribes kuanzia 1000 na masaa ya watu kuangalia video zako yafikie 4000 ndani ya mwaka mmoja.Jambo zuri ni kuwa mtandao wa Youtube ni wa pili kwa kuwa na watembeleaji wengi baada ya Google . Pia tofauti na matangazo ya google adscence, unaweza kutumia video zako kutangaza biashara au huduma zako zingine na ukafikia watu wengi.
Ili uweze kuanzisha Youtube channel, unapaswa kuchagua ni video za aina gani ambazo utakuwa unaweka. Channel nyingi zilizofanikiwa zimegawanyika katika makundi yafuatayo:
Channel zinazotoa elimu: Kimsingi watu mara nyingi hutafuta njia ya haraka na nyepesi ya kujifunza mambo mbalimbali. Hivyo ukifungua Youtube channel inayoelimisha jamii kuhusu kufanya jambo Fulani unalolifahamu au kuwa na uzoefu nalo unaweza kupata wafuasi wengi na ukatengeneza pesa nzuri.
Channel zinazoburudisha: Kundi lingine la channel ni zile zinazoburudisha. Kama una uwezo wa kuandaa video mbalimbali zinazoburudisha watu, unaweza kupata wafuasi wengi na hivyo ukatengeneza pesa.
Baada ya kuanzisha channel yako, itangaze kupitia mitandao ya kijamii kama vile facebook, Instagram, whatsap, twitter na mingine mingi ili iweze kufahamika na kuwa na waangaliaji wengi.
8. Andika na uuze vitabu pepe.

Watu wengi wanatamani kujifunza jinsi ya kuandika kitabu pepe (ebook) lakini wanashindwa waanzie wapi. Bila kujali kitu gani, nina uhakika hata wewe unaweza kuandika kitabu kutokana na maarifa na ujuzi ulionao.Kama utakusanya maarifa uliyonayo na kuyaweza kwenye kitabu pepe ambacho watu wanaweza kupakua (download) ambacho watu wanaweza kuongeza ujuzi, kuboresha kazi zao, kuanzisha biashara n.k unaweza kubadilisha maisha ya mtu Fulani na wakati huohuo ukatengeneza pesa.
Unaweza kuuza kitabu chako wewe mwenyewe kwenye blog au tovuti yako.
9. Anzisha huduma ya Graphic Design kwa makampuni au wafanya biashara wanaokuzunguka.

Ukiangalia mazingira yanayokuzunguka , utaona kuwa kuna wafanyabiashara wengi na ofisi binafsi nyingi ambazo zinahitaji huduma ya graphics, mfano kutengenezewa logo, promotional materials na mengine mengi.Ukiwa na ujuzi wa kutumia software kama Adobe Illustrator, Venngage, Stencil, and Visme unaweza kuwa designer mzuri sana na ukatengeneza pesa kwa muda wako wa ziada.
10. Kuwa mshauri wa Biashara
Kama wewe umesomea na una ujuzi katika masuala ya biashara unaweza ukawa mshauri wa biashara kwa watu wanaohitaji kuanzisha biashara au wafanyabiashara wanaohitaji kukuza biashara zao na wakakulipa kwa huduma unayotoa.
Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ya namna unavyoweza kuanzisha biashara na kutengeneza pesa mtandaoni. Kama unahitaji ushauri, usisite kuwasiliana nami kwa simu namba 0752081669. Kama utahitaji huduma yoyote inayohusu jinsi ya kuanzisha biashara mtandaoni, unaweza kutembelea ukurasa wa huduma zetu kupata huduma unayohitaji. Pia ninaomba uwashirikishe na marafiki zako Makala hii kwa kushare kwenye mitandao yako ya kijamii.
Asante na karibu kwenye Makala zijazo.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024

Nimekuelewa sana ndugu.
Asante na karibu sana mpendwa.
asante kwa ujumbe
Asante na karibu sana.
Asante Sana kwa ujumbe
Asante na karibu sana.