Mambo 4 Ya Kufanya Unapoamka Asubuhi

Mambo 4 ya kufanya unapoamka asubuhi

Jinsi unavyoianza siku yako kila unapoamka asubuhi ina mchango mkubwa sana katika mafanikio yako. Watu wengi huwa wanakosea jinsi wanavyoanza siku asubuhi na hivyo kushindwa kupata mafanikio. Kisaikolojia, ukishindwa kuanza siku yako vizuri, utakuwa umeharibu siku nzima kwani utashindwa kupata matokeo makubwa uliyokuwa unayakusudia. Katika Makala ya leo nitakushirikisha mambo manne muhimu unayopaswa kuyafanya kila unapoamka asubuhi ili uweze kupata mafanikio makubwa katika maisha yako.
Mambo 4 muhimu ya kufanya kila unapoamka asubuhi.
1. Anza na Mungu.
Mungu ndiye muweza wa kila kitu. Ndiye anayetupa uhai, uwezo na nguvu za kufanya kazi zetu. Hivyo jambo la kwanza kabisa, uanpoamka asubuhi, anza na maombi. Muombe Mungu akusaidie katika kazi zako zote unazoenda kuzifanya. Hii itakusaidia kujenga mahusiano mazuri na Mungu na hivyo kukuwezesha kufanikiwa kwenye kazi zako. Pia unapoanza na Mungu, unapata utulivu wa akili kwa kuwa utakuwa umekabidhi mipango, na kazi zako zote kwake.
2. Angalia malengo yako ya muda mrefu.
Jambo la pili la kufanya kila unapoamka asubuhi ni kupitia malengo yako ya muda mrefu. Hapa utaangalia kama kazi unazoenda kuzifanya ndani ya siku ya leo zinatimiza malengo yako ya muda mrefu au la. Hii itakusaidia kutokuhama kwenye malengo yako uliyojiwekea ya muda mrefu. Kumbuka kuwa, ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na malengo makubwa uliyojiwekea. Kwa mfano , kwa mwaka huu umeweka malengo ya kuandika kitabu. Hivyo, unapoanza siku yako angalia kazi unazoenda kuzifanya zisikuhamishe kwenye lengo lako la muda mrefu.
3. Soma, angalia au sikiliza kitu kinachokutia nguvu na kukupa hamasa.
Kila unapoamka asubuhi, jambo la tatu unalopaswa kulifanya ni kusoma kitabu ambacho kitakupa hamasa (inspirational book). Lakini pia kama huna kitabu unaweza kuangalia video ambayo ina mada zinazohamasisha. Hii itakupa nguvu na hamasa kufanya kazi kwa bidi kutimiza malengo yako. Usianze siku yako kwa kuangalia udaku au kuangalia taarifa. Kumbuka kuwa unapoangalia taarifa, utapata taarifa nyingi ambazo nyingine ni za kusikitisha. Ukifanya hivyo utakuwa umeharibu hamasa ya kufanya kazi kwa siku nzima. Kumbuka kuwa jinsi unavyoianza siku yako asubuhi, ndio itaashiria jinsi siku nzima itakavyokuwa. Kama utaichosha akili yako kwa kusoma udaku asubuhi, utakuwa umeharibu utendaji wako wa siku nzima.
4.Hakikisha unaorodhesha vitu ambavyo utavifanya kwa siku nzima.
Baada ya kuwa umefanya mambo matatu kama nilivyoelezea hapo juu, jambo linalofuata ni kuorodhesha mambo yote ambayo utayafanya kwa siku nzima. Kuna faida kubwa sana kuorodhesha mambo unayoenda kuyafanya. Faida ya kwanza ni kutokupoteza muda kwani utakuwa unafahamu mambo unayopaswa kuyafanya, lipi linaanza na lipi linafuata. Faida ya pili ni kuhakikisha kuwa unafanya mambo yale tu ambayo umeyapanga yafanyike kwa siku hiyo hivyo kukusaidika kutimiza malengo yako ya muda mrefu uliyojiwekea.
Kwa leo niishie hapo. Ni matumaini yangu umepata maarifa ya kutosha kuhusiana na mambo unayopaswa kuyafanya kila unapoamka asubuhi. Jambo la msingi ni kuchukua hatua. Kumbuka kuwa, mafanikio makubwa yanajengwa na vitu vidogo vidogo tunavyovifanya kila siku. Kama una maoni au swali lolote, usisite kuweka maoni yako hapa chini. Pia kwa ushauri wowote, usisite kuwasiliana nami moja kwa moja kwa simu no. 0752 081669. Asante na karibu tena katika Makala zinazokuja.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

2 Replies to “Mambo 4 Ya Kufanya Unapoamka Asubuhi”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp