
Watu wengi wamekuwa wakijiuliza na kushindwa kupambanua tofauti iliyopo kati ya blog na tovuti. Inawezekana hata wewe ni miongoni mwao. Katika makala ya leo nitakushirikisha tofauti iliyopo kati ya blog na tovuti na kipi uchague kama unataka kuanzisha biashara mtandaoni na kutengeneza kipato.
Blog ni nini?
Blog ni tovuti inayowekewa makala mara kwa mara kwa lengo la kuvuta wasomaji na hivyo kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.Katika kila makala kunakuwa na sehemu ambapo msomaji anaweza kuandika maoni yake kuhusiana na makala hiyo au kuuliza swali.
Umekuwa ukisoma blog nyingi bila wewe kujua na hata sasa uko kwenye blog yangu. Inawezekana umewahi kusikia maneno blog na tovuti. Je unajua tofauti yake?
Katika Makala hii tutaangalia maana ya blog, tofauti iliyopo kati ya blog na tovuti na kipi unapaswa kuchagua kati ya blog na tovuti.
Kimsingi blog zote ni tovuti , lakini sio tovuti zote ni blog.
Tofauti iliyopo kati ya Blog na Tovuti.
Kabla hatujaangalia tofauti iliyopo kati ya blog na tovuti, hebu tuangalie kwanza historia fupi ya blog jinsi ilivyoanza mpaka sasa.
Historia fupi ya Blog
Blog zimekuwepo toka miaka ya 1993 na kwa sasa zina miongo miwili na nusu. Japokuwa kumekuwa na mjadala kuwa ni nani hasa mwandishi wa kwanza wa blog, kuna mtu mmoja anaweza kuwa ndiye mwandishi wa kwanza wa blog.
Mwaka 1993 Rob Palmer alianza kufanya kazi kwenye kampuni moja mjini London ambapo alikuwa akiandika makala za robo mwaka za kampuni na kuziweka kwenye tovuti ya kampuni.
Wakati Palmer alipokuwa akiandika makala kwa ajili ya kampuni yake, karibia mwaka mmoja baadaye blog nyingine ilianzishwa na Justin Hall. Blog yake ilikuwa na links na hivyo, watu wengine pamoja na makampuni wakagundua umuhimu wa kuwa na aina hiyo ya tovuti kwa ajili ya kubadilishana taarifa.
Wakati wa kipindi hicho blog zilijulikana kama “online journal” na “online diaries”. Mwaka 1997 mwandishi wa blog Mmarekani Jorn Barger aliziita blog kama “weblog,” ambapo kwa haraka sana zilibadilika jina kutoka “online diaries na online journals “ na kuwa “blog” kama tunavyolitumia leo.
Watengenezaji wa mifumo ya internet (Web developers ) kwa haraka waligundua kuwa watu walipendelea zaidi blog kuliko kitu kingine mtandaoni na hivyo wakaamua kutafuta suluhisho la kuboresha blog.
Mwaka 1998, Open Diary ilianzishwa. Hili lilikuwa ni jukwaa (platform) la watu kuandika makala zao na kubadilishana uzoefu wakati huohuo likiwa na sehemu ya watu kutoa maoni (comments). Platform zingine za blog zilianzishwa zikiwemo LiveJournal, Blogger, Tumblr na Xanga.
Ilipofika mwaka 2003, shughuli za blog zilibadilika kabisa pale ambapo wanachuo wawili walipotengeneza WordPress, mfumo bora kabisa (content management system (CMS)) ambao unachukua karibia mbili ya tatu ya tovuti zote zilizopo kwenye mtandao wa internet duniani leo.
Mwaka 2007, mifumo mingine ya blog (micro-blogging) ilianzishwa. Miongoni mwa mifumo iliyoanzishwa ilikuwa ni Twitter kwa lengo la watu kuandika makala fupifupi zenye maneno kati ya 300-400.
Mwaka 2016, WordPress ilianzisha mfumo kwa ajili ya blog ( .blog domain extension), hali ambayo ilizifanya blog kuendelea kuongeza umaarufu. Kwa sasa kunakadiriwa kuwa na makala mpya millioni 70 zinazoandikwa na kuwekwa kwenye blog za WordPress kila mwezi.
Kuna tofauti gani kati ya Blog na Tovuti?

Tofauti kubwa iliyopo kati ya blog na tovuti ni kuwa, blog inawekewa makala mpya(dynamic) mara kwa mara wakati tovuti haiwekewi makala mpya mara kwa mara (static).
Na kama tulivyoona kabla, blog zote ni tovuti lakini si tovuti zote ni blog.
Tofauti nyingine kubwa ni kuwa tovuti huwa inakuwa na kurasa za msingi kama vile:
Mwanzo au Nyumbani (home),
Huduma zetu (service page) na
Wasiliana Nasi (Contact page).
Pia tovuti inaweza kuwa hata yenye ukurasa mmoja.
Kwa upande mwingine, blog ina kurasa kama zile zilizopo kwenye tovuti pamoja na sehemu ya kuweka makala mbalimbali ambayo kila mara makala mpya huwa zinawekwa.Kila makala huwa na sehemu ambayo wasomaji wanaweza kuuliza maswali au kutoa maoni yao.
Kila unapoweka makala mpya , makala mpya huoneana juu ya makala zingine za zamani. Hivyo wasomaji wako watakuwa wakiona makala mpya kwanza.
Kipi bora, kuwa na Tovuti au Blog?
Kumbuka nilisema hapo awali kuwa tovuti imeundwa na kurasa za msingi tu kwa mfano:
Masaa yako ya kazi,anuani au Menu.
Bidhaa unazouza.
Huduma unazotoa.
Hivyo hata ukurasa mmoja unaweza kutosha kuunda tovuti.
Lakini Blog huwa ina hizo kurasa zote ambazo tovuti inazo pamoja na ukurasa wa kuweka makala mpya (Post page).
Hivyo kama unahitaji kuwa unaweka makala mbalimbali ili kuwasiliana na wateja wako, nakushauri uwe na blog badala ya tovuti.
Blog ni njia nzuri sio tu ya kuwasiliana na wateja wako bali pia kuvutia wateja wapya kuja kwenye biashara au huduma unayotoa.
Kuna tofauti gani kati ya kurasa za msingi na kurasa za Makala (Post pages)?
Kurasa za Makala(Post pages):
1. Huwa zinawekewa makala mara kwa mara.
2. Kila makala huwa na kichwa cha habari na wakati mwingine vichwa vidogo vya habari.
3. Makala huwa zimepangiliwa kulingana na mwezi na mwaka zilipowekwa.
4. Makala huwa zimepangiliwa kulingana na makundi (categories).
5. Kila makala ina sehemu ya kuweka maoni (comments)
6. Kila makala ina jina la mwandishi na tarehe iliyowekwa.
7. Unaweza kuwa na makala zisizokuwa na idadi.
Kurasa za Msingi (pages):
1. Huwa na taarifa za msingi ambazo hazibadiliki mara kwa mara.
2. Taarifa hizi hazionyeshi kuwa ziliwekwa lini.
3. Kurasa hizi zimeandikwa si kwa lengo la kushare taarifa zake kwenye mitandao ya kijamii.
4. Hazina sehemu ya kuweka maoni (comments).
5. Hazina taarifa za mwandishi wala tarehe ya kuandikwa.
Idadi ya kurasa za msingi huwa ni ndogo.
Kurasa za msingi ambazo kila blog na tovuti zinapaswa kuwa nazo.
Hata kama blog yako ni kwa ajili tu ya kuandika makala mbalimbali, kurasa hizi zifuatazo unapaswa kuwa nazo.
1.Sisi Ni Nani (About page)
Ukurasa wa Sisi Ni Nani (The About Us Page) hutumika kuelezea kuwa Blog yako au Tovuti yako inahusika na nini.
Ukurasa huu unasaidia kuwaelezea watembeleaji wa blog au tovuti yako huduma unayotoa na hivyo kuwawezesha kufanya maamuzi kama huduma unayoitoa wanaihitaji au la. Katika ukurasa huu unaweza pia kuelezea kampuni yako, malengo na njozi za kampuni yako kuhusiana na huduma unayotoa.
Kama wewe ni mwandishi wa blog, unaweza kutumia ukurasa huu kuweka link za mitandao yako ya kijamii, kuwaomba wasomaji wako waungane na wewe (follow) kwenye mitandao ya kijamii, kuwasimulia wasifu wako kwa ufupi na kuwaelekeza makala muhumu kwao kuzisoma.
2. Wasiliana Nasi (Contact page)
Huu ni ukurasa ambao unaweza kuweka form ambayo watu wataweza kuwasiliana na wewe na kupata huduma unayoitoa.Pia unaweza kutumia ukurasa huu kuuza bidhaa au huduma unayotoa. Hii ni sehemu ambapo utaweka anuani yako ya barua pepe (email), Anuani yako na namba ya simu. Uwe ni mwandishi wa blog au mfanyabiashara ,unatakiwa kuweka mawasiliano yako wazi kupitia ukurasa huu ili watu waweze kukupata kwa urahisi.
3. Privacy policy page
Unapaswa kuwaambia watembeleaji wa blog yako kuwa unakusanya taarifa zao kwa mfano, email au hata kupitia kifaa cha Google Analytics ambacho huwa kinatoa takwimu za watembeleaji wa blog yako.
4. Vigezo na masharti (Terms of Service)
Ukurasa huu ni wa muhimu kama unauza bidhaa kwenye blog yako au unatangaza bidhaa za makampuni mengine kwa kulipwa gawio (commission). Ukurasa huu unaelezea jinsi ambavyo mteja pamoja na wewe mtoa huduma haki zenu zinalindwa kwenye biashara hiyo.
Hizi ndio kurasa nne ambazo kila tovuti inapaswa kuwa nazo.
Pamoja na kuwa na kurasa hizi, ninasisitiza tena kwa nguvu zote kuwa na blog kwenye tovuti yako.
Kwanini kila Tovuti inapaswa kuwa na Blog?

Kama tovuti yako imetengenezwa kwa kutumia WordPress au platform zingine, inawezekana kabisa kuweka blog kwenye tovuti yako!
Hii ni kwa sababu: Unapokuwa na blog kwenye tovuti yako unakuwa na uwezo wa kuvutia watembeleaji wengi kwenye tovuti yako. Hii ni kwa sababu, kwenye blog utaweza kuandika makala nyingi zenye kuelimisha na hivyo kujenga mahusiano na wateja wako. Pia unapoandika makala nyingi kupitia blog, tovuti yako itaonekana zaidi watu wanapoitafuta kwenye Google na hivyo utapata watembeleaji wengi.
Kwa nini Unapaswa kuanzisha blog (Badala ya Tovuti)?
Tovuti ni nzuri kwa watu ambao tayari wana biashara na hivyo wanahitaji tu kutangaza biashara zao. Lakini hata na wao pia wanaweza kuweka blog kwenye tovuti zao ili wapate mahali ambapo watakuwa wakiandika makala mbalimbali na hivyo kuzifanya tovuti zao ziweze kuonekana kwa urahisi kwenye Google search engine.
Tovuti sio nzuri kwa mtu ambaye ndio anaanza na hana bidhaa yoyote wala huduma anayotoa.
Kwa mfano, kama wewe una duka la nguo, unaweza kuanzisha tovuti badala ya blog. Unaweza kuweka kurasa ambazo utawaelezea wateja wako huduma unazotoa, muda wa kazi , mawasiliano yako n.k.
Hata hivyo, kama huna bidhaa au huduma yoyote unayotoa, unaweza kuanzisha blog ukielimisha watu kutokana na ujuzi ulionao na baadaye utakapokuwa umepata wasomaji wengi wanaofuatilia blog yako ndio unaweza kuamua kuuza bidhaa au huduma kutokana na kile unachofundisha.
Jinsi Blog ilivyo na njia nyingi za kutengeneza pesa kuliko Tovuti.
Sasa hebu tulinganishe jinsi blog ilivyo na njia nyingi za kutengeneza pesa kuliko Tovuti.
Kama una tovuti (Isiyo kuwa na blog) una njia chache tu ambazo unaweza kuzitumia kutengeneza kipato kupitia tovuti yako.
Njia moja iliyozoeleka ni ile ya kuuza bidhaa au huduma kutoka kwa wateja ambao tayari unao. Pia wateja wengine wanaweza kukupata kwa kukutafuta kwenye search engine kama vile Google, kwa wewe kulipia matangazo Google au kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram n.k.
Kwa upande wa Blog, kuna njia nyingi sana za kutengeneza kipato. Uzuri wa blog ni kuwa unakuwa unatengeneza kipato huku ukielimisha jamii na kukuza jina (Brand) ya blog yako na wewe mwenyewe. Miongoni mwa njia hizo ni hizi zifuatazo:
1. Kuuza huduma mbalimbali unazotoa
2. Kutangaza na Kuuza bidhaa za makampuni mbalimbali kwa lengo la kupata gawio (commissions)
3. Kuuza bidhaa mbalimbali (Physical and Digital products)
1.Kuuza huduma mbalimbali unazotoa.
Kupitia makala ambazo utakuwa unaziandika na kuelimisha jamii, watu watakuamini na kukuona kuwa wewe ni mtaalamu wa mada unayofundisha ambaye unaweza kutatua changamoto zao. Hivyo unaweza kutoa huduma mbalimbali kwa malipo kutokana na utaalamu ulionao.
2.Kutangaza na Kuuza bidhaa za makampuni mbalimbali kwa lengo la kupata gawio (commissions)
Njia nyingine unayoweza kuitumia kujipatia kipato kwenye blog yako ni ile ya kutangaza na kuuza bidhaa za makampuni mbalimbali kwa lengo la kupata gawio (commissions) . Njia hii inajulikana kwa kiingereza kama Affiliate marketing. Kuna makampuni mengi yanayotoa huduma hii ambayo unaweza kujiunga na wakakupa link ambayo utaiweka kwenye blog yako. Kila msomaji atakayebofya link hiyo ataelekezwa kwenye tovuti ya kampuni husika ambapo kuna bidhaa au huduma inayouzwa. Iwapo mteja atanunua bidhaa au huduma hiyo, wewe unapata gawio. Miongoni mwa makampuni yaliyo na program hii ni amazon, Aliexpress na kwa Tanzania kuna getvalue n.k
3.Kuuza bidhaa mbalimbali (Physical and Digital products)
Kuuza bidhaa pia ni njia unayoweza kuitumia kujipatia kipato kupitia blog yako. Unaweza kuuza bidhaa zinazoshikika (Physical Products) au bidhaa pepe (Digital products).
Bidhaa pepe (Digital products) ni rahisi sana kutengeneza kwani unaweza kukusanya makala ambazo umekuwa ukiandika na kuziweka kwenye vitabu na ukauza vitabu pepe (ebooks) . Pia unaweza kutumia makala ulizoandika kuandaa kozi na kuiuza kwenye blog yako.
Kwa ufupi:
Katika Makala hii tumeangalia tofauti ya blog na tovuti . Swali langu kwako ni kuwa baada ya kusoma Makala hii, utachagua kipi kati ya blog na tovuti?
Je una biashara na unataka iwafikie watu wengi zaidi au unahitaji kujiajiri kupitia mtandao wa internet kwa kutoa maarifa yako kwa jamii huku ukijipatia kipato?
Vyovyote vile kati ya mambo hayo mawili Blog itakuwezesha kuyatimiza kikamilifu.
Je una maoni yoyote? Usisite kudondosha maoni yako hapa chini.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024