Kanuni za Kujiwekea Malengo

Kanuni za Kujiwekea Malengo

Ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na malengo. Kujiwekea malengo kunaweza kuwa na uzoefu wenye nguvu wa kubadilisha maisha yako ikiwa utafanya kwa usahihi. Katika makala hii nitakushirikisha kanuni tano za msingi za kujiwekea malengo ambazo ni muhimu kwa mafanikio yako makubwa.

Kanuni ya Kwanza: Ulinganifu

Ili uweze kufanya vizuri zaidi katika maisha yako, malengo yako na maadili yako lazima yaendane. Maadili yako yanawakilisha imani yako ya kina kuhusu kile unachoona kuwa ni chema na chenye manufaa na kile unachoona kuwa ni kibaya kwako. Utendaji wako wa juu na mafanikio yako yatategemea tu pale ambapo malengo yako na maadili yako yapo katika upatanifu kamili.

Kanuni ya Pili: Eneo la Ubora

Kila mtu ana uwezo na ni bora katika kitu fulani, na pengine vitu kadhaa. Unaweza kufikia mafanikio makubwa tu kwa kupata eneo lako la ubora na kisha kuweka moyo wako wote katika kukuza vipaji vyako katika eneo hilo. Kwa lugha nyingine eneo la ubora ni kitu kimoja ambacho una uwezo wa kipekee wa kukifanya kwa ubora. Ni jukumu lako kukibaini kitu hicho, ikiwa bado hujakibaini.

Eneo lako la ubora linaweza kubadilika kadri taaluma yako inavyokua, lakini watu wote waliofanikiwa kwa kweli ni wale ambao wamegundua na kuwekeza nguvu zao zote kwenye maeneo yao ya ubora. Eneo lako la ubora mara zote ni kufanya kile unachokifurahia zaidi na kukifanya vizuri. Hivyo, kanuni ya pili ya kujiwekea malengo ni kwa kutambua eneo lako la ubora.

Kanuni ya Tatu: Kanuni ya Shamba la Almasi

Kanuni ya Shamba la Almasi inatokana na jina la hotuba iliyotolewa na mhubiri aitwaye Russell Conwell. Hotuba hiyo ilipendwa sana.

Katika hotuba hiyo alielezea hadithi ya mkulima mmoja mzee wa kiafrika ambaye alifurahia sana siku moja aliposikia kutoka kwa mfanyabiashara aliyesafiri kwenda Afrika kugundua migodi ya almasi na kuwa tajiri sana. Hivyo na yeye aliamua kuuza shamba lake, kuandaa safari, na kuelekea ndani ya Afrika ili kutafuta almasi kwa lengo la kuwa tajiri mkubwa.

Kwa miaka mingi, alisafiri sehemu kubwa ya bara la Afrika akitafuta almasi. Hatimaye, aliishiwa pesa. Mwishoni kabisa, akiwa peke yake, katika hali ya kukata tamaa, alijitupa baharini na kuzama.

Wakati huo huo, ndani ya shamba alilouza, siku moja mkulima mpya alikuwa akinywesha punda katika kijito kilichokatisha shamba hilo. Alipata jiwe la ajabu lililotoa mwanga kwa namna ya kushangaza. Alilipeleka nyumbani kwake na hakuwa anafahamu lolote kuhusiana na jiwe hilo. Baadaye, mfanyabiashara yule yule alipita kwenye shamba lile na yule mkulima mpya akamwonyesha lile jiwe. Mfanyabiashara alifurahi sana na akauliza kama yule mkulima mzee alikuwa amerudi hatimaye. Hapana, aliambiwa. Mkulima mzee hakuwa ameonekana tena tangu aondoke.

Mfanyabiashara alichukua jiwe hilo na kusema, “Hii ni almasi ya thamani kubwa.” Mkulima mpya alikuwa na shaka, lakini mfanyabiashara alisisitiza na akaomba aonyeshwe wapi alipata almasi hiyo. Wakaenda kwenye shamba ambalo mkulima alikuwa akinywesha punda, na walipozunguka, walipata almasi nyingine, na nyingine, na nyingine. Ikabainika kwamba shamba lote lilikuwa limejaa madini ya almasi. Mkulima mzee alikuwa ameenda Afrika kutafuta almasi bila ya kutazama chini ya miguu yake mwenyewe.

Hadithi hii inafundisha kwamba mkulima mzee hakuweza kutambua kwamba almasi hazionekani kama almasi katika hali yake ya asili. Huonekana kama mawe kwa macho yasiyo na elimu. Almasi inapaswa kukatwa, kupigwa msasa, na kung’arishwa kabla haijawa kama ile inayouzwa kwenye maduka ya vito.

Vivyo hivyo, mashamba yako ya almasi pengine yapo chini ya miguu yako mwenyewe. Lakini mara nyingi yamejificha yanahitaji juhudi kuweza kuyagundua. Mashamba yako ya almasi pengine yapo kwenye vipaji vyako, elimu yako, uzoefu wako, tasnia yako, mji wako, mawasiliano yako na kadhalika. Mashamba yako ya almasi yapo chini ya miguu yako mwenyewe na unachotakiwa kufanya ni kuchukua muda kuyatambua na kisha kuyafanyia kazi.

Theodore Roosevelt aliwahi kusema, “Fanya kile unachoweza, kwa kile ulicho nacho, hapo hapo ulipo.” Huna haja ya kuhamia nchi nyingine au kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yako. Mara nyingi, kile unachokitafuta kiko karibu sana na wewe. Lakini hakionekani kama fursa kwa sababu hujatumia muda wako kuchunguza na kufanyia kazi kwa bidii uwezo ulionao.

Kanuni ya Nne: Uwiano

Kanuni ya uwiano inasema kwamba, unahitaji malengo mbalimbali katika maeneo sita muhimu ya maisha ili uweze kufanya vizuri zaidi. Kama vile gurudumu la gari linavyopaswa kuwa na uwiano ili liweze kuzunguka kwa urahisi, unapaswa kuwa na malengo yenye uwiano ili maisha yako yaweze kwenda vizuri.

Unahitajika kuweka malengo katika maeneo yafuatayo:
malengo ya kifamilia
malengo ya kimwili kiafya.
malengo ya kielimu na maendeleo binafsi (self development).
malengo ya kazi na taaluma.
malengo ya kifedha na mali.
Hatimaye, unahitaji malengo ya kiroho,

Ili kudumisha uwiano mzuri, unahitajika kuwa na malengo mawili au matatu katika kila eneo, jumla ya malengo kumi na mawili hadi kumi na nane. Aina hii ya uwiano itakuwezesha kuwa unafanya kazi kila wakati juu ya kitu muhimu kwako. Unapokuwa haufanyi kazi kwenye ajira yako, unaweza kufuatilia malengo ya kifamilia. Unapokuwa haufanyi kazi juu ya afya ya mwili, unaweza kufanya kazi juu ya maendeleo binafsi na kadhalika.Lengo ni kutokupoteza muda wako kwa kufanya vitu ambavyo havipo kwenye malengo yako.

Kanuni ya Tano: Kusudi Kuu la Maisha

Kanuni ya tano ya kujiwekea malengo ni uamuzi wa kusudi kuu la maisha yako. Kusudi lako kuu ni lengo lako nambari moja, lengo ambalo ni muhimu zaidi kwako kuliko lengo lingine lolote kwa wakati huu. Unaweza kuwa na malengo mbalimbali lakini unaweza kuwa na kusudi kuu moja tu. Kukosa kwa mtu kuchagua lengo au kusudi kuu ni sababu kuu ya kutawanya juhudi, kupoteza muda na kushindwa kupiga hatua.

Jinsi ya kuchagua lengo kuu ni kwa kuchanganua malengo yako yote na kujiuliza, “Ni lengo gani, nikilifikia, litanisaidia zaidi katika kufanikisha malengo yangu mengine yote?”

Kwa kawaida, linaweza kuwa ni lengo la kifedha au kibiashara, lakini wakati mwingine linaweza kuwa lengo ni la afya au mahusiano. Uchaguzi wa kusudi lako kuu ndio mwanzo wa mafanikio yako makubwa. Lengo hili linakuwa ndiyo”dhamira” yako na kanuni ya kupanga shughuli zako zingine zote. Unapokuwa na msisimko au hamasa kuhusu kufanikisha lengo kuu lililo wazi, unaanza kusonga mbele haraka licha ya vikwazo na vizingiti vyote ambavyo utakutana navyo.

Kwa kutumia kanuni hizi tano za kujiwekea malengo, unaweza kufanikisha mambo makubwa na kuwa na mabadiliko ya kweli katika maisha yako. Ulinganifu kati ya malengo na maadili yako, kutambua eneo lako la ubora, kugundua mashamba yako ya almasi, kudumisha uwiano katika malengo yako yote, na kuchagua kusudi lako kuu la maisha, ni mambo muhimu yatakayokupeleka kwenye viwango vya juu vya mafanikio. Kumbuka, fursa yako kubwa inaweza kuwa karibu zaidi kuliko unavyofikiria, na mara nyingi inahitaji kazi ngumu na kujitolea ili uweze kuitambua na kuifanikisha.

Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa yatakayo kusaidia kuwa na kanuni za kujiwekea malengo. Kama una maoni au swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp