
Keith Simonton, mwanasaikolojia aliyehitimu masomo yake Chuo Kikuu cha Havard, mwaka 1977 alikuja na kanuni ya mafanikio inayojulikana kwa jina la The Equal Odds Rule. Kanuni hii aliiandika kwenye chapisho la “Creative productivity, age and stress: a biographical time-series analysis of 10 classical composers la mwaka 1977.
Kanuni ya The Equal Odds Rule inasema hivi:
“The average publication of any particular scientist does not have any statistically different chance of having more of an impact than any other scientist’s average publication.”
Kwa tafsiri rahisi ni kuwa, chapisho lolote la mwanasayansi yoyote haliwezi kuleta matokeo makubwa na ya tofauti kuliko chapisho la mwanasayansi mwingine.
Maana yake ni kuwa, ili mwanasayansi aweze kuleta matokeo makubwa na ya tofauti itategemea ni mara ngapi mwanasayansi huyo amerudia kufanya utafiti wa kile kitu kuliko wanasayansi wengine.
Hivyo ndivyo kanuni hii ya The Equal Odds Rule inavyoelezea jinsi ya kupata mafanikio kwenye jambo lolote. Ili uweze kupata mafanikio, nitakushirikisha mambo matatu ambayo unapaswa uyazingatie na kuyafanyia kazi kwa mujibu wa kanuni hii.
1. Amua unataka kuwa nani.
Hili ni jambo la muhimu sana na la kwanza kabisa unapotaka kupata mafanikio kwenye jambo lolote. Amua unataka kuwa nani au unataka kubobea kwenye kazi gani kwenye maisha yako. Je unataka kuwa mkulima, mfanyabiashara, mwanamichezo, mwajiriwa au uliyejiajiri? Hii itakusaidia kutambua ni kwenye eneo gani utawekeza nguvu zako na akili zako zote ili uweze kupata mafanikio. Kumbuka kuwa unapokuwa umechagua eneo ambalo utabobea kwenye maisha, utaifanya akili yako iongeze ubunifu Zaidi.
2. Amua huduma au bidhaa utakazokuwa unazalisha
Baada ya kuwa umeamua unataka kuwa nani, hatua ya pili ni kuchagua huduma utakazokuwa unatoa au bidhaa ambazo utakuwa unazalisha kwenye eneo ulilochagua. Kwa mfano umeamua kuwa mkulima. Kumbuka kuwa, kilimo ni eneo pana sana, hivyo unaweza kuchagua huduma au bidhaa ambazo utakuwa unazalisha. Kwa mfano, unaweza kuchagua kuzalisha mazao, kusindika, kusafirisha na kadhalika. Kama umejiajiri, chagua bidhaa au huduma ambayo watu watakutambua kuwa unatoa kwa viwango vya juu. Chagua huduma au bidhaa ambazo utakuwa unazalisha, usitake kufanya kila kitu kwani hautafanya kwa ufanisi hivyo utashindwa. Chagua eneo moja au maeneo machache ya kutoa huduma ambayo utajikita zaidi na hivyo kubobea.
3. Toa huduma au zalisha bidhaa mara nyingi na kwa muda mrefu bila kuacha.
Hapa ndio kwenye kiini cha kanuni hii ya The Equal Odds Rule. Katika kanuni hii inasema, mafanikio yatapatikana kama utaamua kufanya jambo moja na kulifuatilia kwa muda mrefu bila kuacha. Unapokuwa umechagua kufanya kazi fulani kwenye maisha yako, fanya kwa muda mrefu bila kuacha, haijalishi utapata vikwazo na kushindwa mara nyingi kiasi gani. Kumbuka kuwa, unapokuwa unarudia kufanya kile kitu mara nyingi na bila kuacha, hata kama utakuwa unapitia changamoto za kushindwa, kushindwa huko kutakupatia uzoefu mkubwa wa kufanikiwa baadaye kama hautakata tamaa.Mara nyingi watu wanashindwa kupata matokeo makubwa kwenye kazi wanazofanya kwa sababu wanafanya kidogo tu halafu wanakata tamaa na kuacha. Kama unataka kufanikiwa, fanya shughuli uliyoichagua kwa muda mrefu bila kukata tamaa.
Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ya jinsi ya kupata mafanikio kwa kutumia kanuni hii ya The equal odds rule. Kama una maoni yoyote kuhusiana na mada hii, ninatamani sana uweke maoni yako hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu no. 0752 081669. Asante na karibu kwenye Makala ijayo.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024
2 Replies to “Kanuni Ya Kupata Mafanikio: “The Equal Odds Rule””