
Mafanikio yoyote ya kifedha yanaongozwa na kanuni. Kanuni hizi ndiyo huwa zinasababisha mtu apate fedha nyingi au awe masikini. Watu wengi wameshindwa kupata mafanikio ya kifedha kwa sababu wamekuwa wakitumia fedha bila kufahamu kuwa kuna kanuni zinazotawala matumizi ya fedha ili mtu aweze kufanikiwa. Katika makala ya leo, nitakushirikisha kanuni 3 za fedha zinazoleta mafanikio na utajiri. Kanuni ambazo ukizifahamu na ukazifanyia kazi utaweza kuitumia pesa yako vizuri, ukaizalisha na hivyo kuwa na mafanikio. Lakini pia, kwa kushindwa kufuata kanuni hizi, pesa zitakukimbia.
Kanuni 3 za fedha zinazoleta mafanikio na utajiri.
1.Kufanya kitu unachokipenda (Passion)- Mike Phillips 1977.
Kanuni ya kwanza iliandikwa na Mike Phillips mwaka 1977. Mike Phillips ni mtaalamu wa masuala ya fedha katika benki nchini Marekani. Mwaka 1977 aliandika kanuni hii kwenye kitabu chake kinachoitwa Kanuni Saba Za fedha (Seven laws of money). Katika kanuni hii anaeleza kuwa, hauwezi kufanikiwa kama kitu unachokifanya haukipendi. Hivyo ili uweze kupata mafanikio makubwa ya kifedha, ni sharti ufanye kazi au kitu ambacho unakipenda kwa dhati kutoka moyoni. Kitu ambacho utakifanya hata kama hakikupi matokeo unayoyatarajia kwa sasa. Kitu ambacho utakuwa tayari kukifanya hata kama hakikulipi kwa sasa. Unapokuwa unafanya kitu unachokipenda na kwa muda mrefu, baadaye kitu hicho kitakulipa na kukupatia mafanikio makubwa.
2.Jilipe asilimia 10 ya kila kipato chako- George Clason (1926)
Kanuni ya pili ni kanuni iliyoandikwa na George Clason mwaka 1926 kwenye kitabu chake maarufu kinachoitwa The Richest Man in Babylon. Katika kanuni hii anaeleza kuwa, ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe unatenga asilimia kumi ya kila pato lako kwa ajili ya kuweka akiba. Akiba hii unatakiwa uwekeze kwenye kitu kinachozalisha ili iweze kuongezeka. Hii haijalishi unapata pesa kiasi gani. Mafanikio yako yatatokana tu ni kwa kiwango gani unawekeza pesa yako. Ukiona kwenye maisha yako pesa yote unayopata inatumika kwenye matumizi ya kawaida, basi tambua kuwa hautaweza kupata mafanikio. Hivyo, ili uweze kupata mafanikio, hakikisha kila unapopata kipato, kabla ya matumizi, anza kwa kutenga asilimia 10 kwa ajili ya kuwekeza.
3.Kabiliana na kanuni ya Parkinson (Parkinson Law).
Kanuni hii inatokana na na Mwingereza anayeitwa Northcote Parkinson. Kanuni hii inasema hivi:
“Kiwango cha matumizi huwa kinaongezeka kadiri kipato kinavyoongezeka”.
Maana yake ni kuwa, ili uweze kufanikiwa kifedha, ni sharti uvunje kanuni hii. Kadiri kipato chako kinavyoongezeka ni lazima matumizi yako yabaki vilevile au yaongezeke kwa kiwango kidogo kuliko ongezeko la kipato.
Swali la leo:
Ni kanuni ipi kati ya kanuni hizo 3 umekuwa hauizingatii? Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika hapa chini kwenye sanduku la maoni. Nami nitakurudia ili tupeane ushauri zaidi.
Pia kama una swali au maoni, usisite kuandika hapa chini. Asante sana na karibu katika makala zijazo.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024
5 Replies to “Kanuni 3 Za Fedha Zinazoleta Mafanikio Na Utajiri.”