Jinsi Ya Kutumia Ujuzi Wako Kujiajiri Mtandaoni

Jinsi ya kutumia ujuzi wako wako kujiajiri Mtandaoni

Katika maisha, kila mtu ana ujuzi wake. Ujuzi huu unatokana na kusomea chuoni, kufundishwa nyumbani au mtaani. Hata wewe inawezekana una ujuzi ambao umesomea chuoni au umejifunza mahali fulani. Changamoto kubwa ambayo inajitokeza hapa ni kwa jinsi gani unaweza kutumia ujuzi wako kujiajiri na kutengeneza kipato. Katika makala hii nitakushirikisha jinsi ya kujiajiri mtandaoni na kutengeneza kipato kwa kutumia ujuzi wako.
Katika makala yangu ya njia 10 za kutengeneza pesa mtandaoni nilielezea kwa ufupi njia ambazo unaweza kuzitumia kuweza kujiajiri mtandaoni na kutengeneza kipato. Katika makala hii nitaelezea kwa kina njia moja ya kujiajiri mtandaoni ambayo ni kuanzisha blog. Hapa nitazungumzia jinsi unavyoweza kujiajiri kwa kuanzisha blog ya kitaalamu (niche blog).
Maana ya blog ya kitaalamu (niche blog).
Niche blog au kwa Kiswahili blog ya kitaalamu ni aina ya blog ambayo imejikita katika kufundisha ujuzi wa aina moja. Hapa ina maanisha kuwa, kama wewe una maarifa au ujuzi wa kilimo, basi blog yako itajikita katika kufundisha kilimo tu bila kuchanganya mambo mengine yasiyohusu kilimo. Vivyo hivyo, kwa ujuzi wa aina nyingine kama vile Sheria, Biashara, Elimu, Afya, Mapambo, Mitindo, Ujasiriamali na kadhalika.
Hivyo, kwa kutumia ujuzi au maarifa yoyote uliyonayo, unaweza kuanzisha blog inayotatua changamoto zinazoihusu jamii yako kupitia ujuzi ulionao. Jambo la kuzingatia ni kuwa, unapokuwa umeanzisha niche blog, lenga kundi la watu wanaohitaji ujuzi wako na ujitahidi kuandika makala zinazoelimisha na kutatua matatizo ya kundi hilo. Usichanganye mada. Kama umeamua kuanzisha blog ya kufundisha mapishi au ujasiriamali, usichanganye na mada za siasa. Hii ni kwa sababu, watu watakaokuwa wasomaji wa blog yako ni wale wanaohitaji ujuzi wako na si vinginevyo.
Kwa nini unapaswa kuwa na blog ya ujuzi au utaalamu wako?
Sasa hebu tuangalie ni faida gani utazipata unapokuwa umeanzisha blog ya ujuzi au utaalamu wako.
1. Utapata wasomaji wanaopenda kufuatilia maarifa au ujuzi wako (Loyal readers)
Ukiwa na blog ya kufundisha utaalamu wako, utapata watu wenye changamoto katika jamii wanaohitaji ujuzi wako ili waweze kutatua changamoto zao. Hivyo, watu watakupenda na kukuheshimu kwa sababu unawasaidia kutatua changamoto zao.
2. Utajenga mtandao mkubwa (community) wa watu wenye ujuzi kama wa kwako na wanaopenda kujifunza ujuzi wako.
Kwa kuwa na mtandao mkubwa wa watu wenye ujuzi kama wa kwako, mtaweza kubadilishana maarifa na hivyo kukuza ujuzi wako.
3. Utatambulika katika jamii kuwa wewe ni mtaalamu.
Unapokuwa umeanzisha blog ya utaalamu wako, na ukawa unaandika makala zinazotatua matatizo katika jamii, jamii itakutambua kuwa wewe ni mtu wa kutegemewa.
4. Utakuza jina lako (Brand, Credibility and Profile)
Ukiwa unaandika makala zinazoelezea mada moja kwa muda mrefu, utaifanya blog yako iwe ni sehemu inayoaminika na kuheshimika (trusted source) kwa maarifa unayofundisha. Ukifanya hivyo kwa usahihi, utatambulika kuwa ni mtaalamu uliyebobea kwenye kada unayofundisha.
Faida za kuwa mtaalamu uliyebobea ni nyingi. Mojawapo kubwa ni pale utakapokuwa na bidhaa au huduma unayotaka kuuza. Badala ya kuanza kusaka wateja, utashangaa kuwa watu ndio watakutafuta wewe wakihitaji huduma yako kwa kuwa wanakutambua kuwa wewe ni mtaalamu uliyebobea.
5. Utaweza kuuza bidhaa zako.
Unapokuwa na blog inayoelezea mada au ujuzi wa aina moja, ni rahisi kuuza bidhaa zinazoendana na ujuzi unaofundisha na watu wakanunua. Hii ni kwa sababu, wasomaji wa blog yako watakuwa ni wale wanaopenda na kuhitaji ujuzi wako. Mfano: Ukiwa na Blog ya Ujasiriamali, ni rahisi kuuza vitabu, kozi au bidhaa zinazohusu ujasiriamali. Kadhalika kwa blog zenye ujuzi wa aina nyingine.
6. Ni rahisi kupata watu au makampuni ya kuweka matangazo kwenye blog yako.
Ukiwa na blog yenye mada au ujuzi wa aina moja, ni rahisi kupata watu au makampuni yanayotoa huduma inayofanana na ujuzi wako na wakahitaji kuweka matangazo yao ya biashara. Kwa mfano: Kama blog yako imejikita katika kuelezea mitindo mbalimbali ya nguo, ni rahisi kupata watu wanaohitaji kutangaza bidhaa zao za nguo kwenye blog yako, nao wakakulipa kwa kuweka matangazo yao.
7. Blog yako itaonekana kwa urahisi watu wanapoitafuta Google (Search engine optimization).
Google huwa inatoa kipaumbele kwa blog zinazoelezea mada ya aina moja. Hivyo blog yako itaonekana kwenye ukurasa wa kwanza. Kwa mfano: kama blog yako inahusu ufugaji wa kuku, na mtu akaandika neno ufugaji wa kuku Google, blog yako itaonekana juu kwa sababu, ina makala nyingi za ufugaji wa kuku.
8. Utaweza kuandika makala nyingi.
Unapokuwa unafundisha ujuzi unaoupenda, utakuwa na vitu vingi vya kuandika. Hivyo kila siku utakuwa unapata mawazo na maarifa mapya ya kuandika kwenye blog yako.
9. Blog yako haitapata ushindani mkubwa (Less competition)
Blog za kitaalamu huwa ni chache na huwa zinalenga kundi fulani la watu. Hivyo, unapokuwa unaandika makala zenye mada ya aina moja, utapata faida ya kutokupata ushindani mkubwa mtandaoni.
Ni matumaini yangu kuwa umepata maarifa ya jinsi ya kujiajiri mtandaoni kwa kutumia ujuzi wako. Kama utahitaji kuanzisha blog wewe mwenyewe, nimeelezea kwa kina na hatua kwa hatua jinsi ya kuanzisha blog kwenye makala yangu ya Jinsi ya kuanzisha blog na kutengeneza kipato. Pia kama utahitaji huduma ya kutengenezewa blog, unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba. 0752 081669. Kama una maoni au swali lolote kuhusiana na mada hii, usisite kuweka maoni yako hapa chini. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

One Reply to “Jinsi Ya Kutumia Ujuzi Wako Kujiajiri Mtandaoni”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp