
Moja ya jambo la muhimu sana katika mafanikio yako ya kifedha ni kuwa na bajeti. Watu wengi wamekuwa wakipata pesa nyingi lakini wameshindwa kupiga hatua kwa kuwa huwa wanashindwa kutambua pesa zao huwa zinapotelea wapi. Hata wewe hebu jiulize, ni pesa nyingi kiasi gani zilizowahi kupita mkononi mwako? Halafu tafakari ni mambo gani uliyoyafanya. Katika makala ya leo nitakushirikisha njia rahisi na yenye mafanikio ya jinsi ya kupanga bajeti ya matumizi yako.
Jambo la kuzingatia kabla ya kuanza kupanga bajeti yako: Mkumbuke Mungu kwa kurudisha Zaka na Kutoa Sadaka.
Ili uweze kupata mafanikio na mibaraka, kumbuka kuanza kutenga asilimia 10 ya kipato chako kwa ajili ya Zaka ya Mungu na kiasi fulani kwa ajili ya Sadaka. Baada ya hapo, pesa yako iliyobaki, igawanye kwa kutumia bajeti ambayo nitaielezea kwenye makala hii ya leo. Kumbuka ya kuwa, Mungu ndiye mtoa uhai, afya na mibaraka yote.
Malaki 3:10
Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.
Jinsi ya kupanga bajeti ili uwe na mafanikio.
Kanuni ya 50/30/20.
Kanuni ya 50/30/20 ilitolewa na Senator wa Marekani Elizabeth Warren ambaye aliandika kitabu chake kinachoitwa Ultimate Lifetime: Money Plan. Katika kanuni hii alisema kuwa, unapokuwa umepata kipato chochote, unapaswa kukigawa katika mafungu matatu kama ifuatavyo:
Asilimia 50 : Matumizi ya lazima.
Haya ni matumizi ambayo ni ya lazima katika maisha yako. Matumizi ambayo ni lazima yaendelee katika maisha. Kwa mfano chakula, malazi na matumizi mengine ambayo unaona kabisa lazima yafanyike ili maisha yako yaendelee. Hivyo, chukua pesa yako uliyopata na uzidishe kwa asilimia 50, utapata pesa ambayo unapaswa kuitumia kwenye matumizi yako ya lazima. Pesa ya matumizi yako ya lazima isizidi asilimia 50.
Asilimia 30: Matumizi yasiyo ya lazima.
Haya ni matumizi ambayo siyo ya lazima, lakini unaweza kuyafanya kama unapesa ya kutosha. Ni matumizi ambayo hata kama utaamua kutoyafanya, maisha yako yataendelea. Hivyo, matumizi yako yasiyo ya lazima, yasizidi asilimia 30. Mfano wa matumizi yasiyo ya lazima ni kama vile, kwenda kujiburudisha mwisho wa juma, kununua fasheni mbalimbali za nguo, kutokupitwa na simu za kisasa na kadhalika.
Asilimia 20: Akiba, Uwekezaji na kulipa madeni.
Katika asilimia hii ishirini, utaitumia kwenye kuweka akiba, kuwekeza na kulipa madeni. Unaweza kuongeza hii asilimia 20 kwa kupunguza kiwango cha matumizi yasiyo ya lazima ili uweze kupata pesa nyingi zaidi kwa ajili ya kuwekeza na hivyo kuharakisha mafanikio yako.
Nimatumaini yangu umepata maarifa ya kutosha ambayo yatakusaidia jinsi ya kupanga bajeti ili uweze kuwa na mafanikio. Kama una swali au maoni, usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024
Nashukuru kwa makala nzuri. Natamani kuona mchanganuo wa sisi wafanyakazi mfano kipato Cha tsh 500000 lakitano Kwa mwezi
Asante sana Mr. Mlacha kwa kufuatilia makala hii. Jibu la swali lako ni kama ifuatavyo:
20% ya 500,000 ni 100,000/= Hii ni kwa ajili ya Akiba, uwekezaji na biashara (Hakikisha unaitenga kabla ya matumizi mengine)
50% ya 500,000 ni 250,000/= Hii ni kwa ajili ya matumizi ya lazima kama vile chakula, kodi ya nyumba, kulipia bili ya maji, umeme n.k. Haya ni matumizi ya lazima ambayo usipoyafanya maisha hayawezi kuendelea.
30% ya 500,000 ni 150,000 Hii ni kwa ajili ya matumizi yasiyo ya lazima. Matumizi ambayo hata usipoyafanya, maisha yataendelea. Mfano: Kuwa na simu kali, kwenda kujiburudisha n.k.
Aidha Unaweza kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima na kiasi cha pesa ulichokipunguza ukakiongezea kwenye akiba, biashara na uwekezaji. Aina hii ya bajeti ina matokeo mazuri sana. Mimi ninaitumia na nimeona matokeo yake.
Naomba nipe mfano wa mtu mwenye kipato cha 300000 kwa mwezi. Hapo
Needs = ?
Wants = ?
Investment = ?
Ili nielewe zaidi.
Asante sana Bwana Victor.
Kwa kipato cha 300,000/=, mgawanyo wa bajeti utakuwa kama ifuatavyo:
50% Needs = 150,000/=
30% Wants = 90,000/=
20% Investment= 60,000/=