
Katika somo lililopita la jinsi ya kupata wazo bora la biashara, nilielezea kanuni bora kabisa ya 7/7/7 ambayo ukiitumia inakuwezesha kupata mawazo mbalimbali mbalimbali ambayo yatakusaidia kuanzisha biashara yako ya mtandaoni. Kanuni hiyo ilikuwa na kazi ya kukupatia mawazo mbalimbali ambayo kupitia mawazo hayo uweze kupata wazo moja zuri ambalo utaanzishia biashara yako ya mtandaoni. Katika somo la leo tutaangalia Jinsi ya kugundua biashara unayopaswa kufanya (Discovering your niche).
Jinsi ya kugundua biashara unayopaswa kufanya mtandaoni (Discovering your niche).
Katika somo lililopita nilielezea kanuni ya 7/7/7 ambayo inakusaidia kupata mawazo mbalimbali ambayo yatakuwezesha kupata wazo moja la biashara. Katika kanuni hiyo, inakutaka kuorodhesha matatizo au changamoto 7 ambazo huwa unakabiliana nazo au watu wengine wanakabiliana nazo. Kisha unaorodhesha mambo 7 unayoyapenda (passions) halafu unamalizia na mambo 7 unayoyahofia( fears). Hivyo unakuwa umepata mambo 21 ambayo unaweza kuyatumia kuanzishia biashara mtandaoni. Unaweza kupitia somo hilo ili uweze kujifunza zaidi.
Katika somo la leo tutaangalia jinsi ya kuchagua wazo moja bora kati ya mawazo ishirini na moja ambayo utakuwa umeorodhesha.
Kanuni ya PPP.
Ili uweze kupata wazo bora ambalo utaanzishia biashara yako mtandaoni, tumia kanuni ya PPP au 3P. Kanuni hii inakuwezesha kupima wazo unalotaka kuanzisha biashara yako.Hii ni kanuni ambayo inakuwezesha kupima soko (market map). Kanuni hii ya PPP ni ufupisho wa maneno matatu ya Kingereza ambayo ni P-Place, P-People, na P-Products.
Jambo la kwanza kabisa unapotaka kutumia kanuni hii, unapaswa kuchagua wazo moja ambalo utakuwa umelipenda zaidi kati ya yale mawazo ishirini na moja. Kwa mfano, katika mawazo yangu ambayo niliyaandika kwenye somo lililopita, mimi ninachagua wazo moja ambalo ni Ushauri wa Kibiashara.
Hatua inayofuata sasa ni kutumia kanuni ya PPP kuweza kuangalia kama wazo langu linafaa kuanzishia biashara mtandaoni.
1.P- Place.
Hapa unaangalia sehemu mbalimbali mtandaoni ambazo watu wanafundisha mada unayotaka kufundisha. Hapa utaingia Google na kutafuta ushauri wa Kibiashara. Kwa kutumia Google, utaweza kuona blog mbalimbali ambazo zinafundisha na kutoa ushauri wa kibiashara, majukwaa (forums) mbalimbali zinazofundisha maarifa hayo pamoja na kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii. Kupitia blog, majukwaa mbalimbali na kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii, utaweza kuona kile wanachofundisha na komenti mbalimbali ambazo watu wanauliza.
Kwa kuwepo kwa blog, majukwaa na kurasa mbalimbali zinazofundisha mada unayofundisha, tafsiri yake ni kuwa soko lipo. Hivyo unachotakiwa kuchunguza ni kuangalia mada wanazofundisha. Unaweza kuangalia mada ambazo hawajazitilia mkazo na wewe ukazifundisha. Pia unaweza kuangalia mada ambazo zina mapungufu na wewe ukazifundisha kwa ubora wa hali ya juu.
2.P-People.
Kama nilivyoeleza katika kipengele cha place, hapa unaorodhesha watu wanaomiliki blog, majukwaa na kurasa za mitandao ya kijamii zinazofundisha ujuzi au maarifa ambayo unataka kufundisha. Lengo la kuwa na orodha hiyo ni kuwa, unaweza kuwatumia huko mbeleni katika safari yako ya biashara mtandaoni.
3.P-Products.
Katika kipengele hiki, ingia mtandaoni kupitia Google na uangalie bidhaa na huduma mbalimbali ambazo zinaendana na ujuzi ambao unategemea kufundisha. Unaweza kuangalia vitabu, huduma au kozi mbalimbali ambazo tayari zipo sokoni. Hii itakusaidia kuamua wewe utakuwa unaandaa na kuuza bidhaa za aina gani ambazo zitaendana na ujuzi wako.
Ni matumaini yangu umepata maarifa ya kutosha kukuwezesha kufanikiwa kuanzisha biashara mtandaoni. Ninaomba na wewe sasa uniandikie kwenye sanduku la maoni wazo ambalo unafikiri litakufaa kuanzisha biashara yako ya mtandaoni.
Kama una swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kupitia simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika somo linalofuata.
Masomo yaliyopita.
1. Jinsi kuanzisha biashara mtandaoni: Utangulizi.
2. Biashara inayolipa mtandaoni ni ipi?
3. Jinsi ya kutafuta wazo bora la biashara yako ya mtandaoni.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024
3 Replies to “Jinsi Ya Kugundua Biashara Unayopaswa Kufanya Mtandaoni.”