
Watu wengi wanapotaka kuanzisha blog, hupata shida waanzishe blog kuhusiana na mada ipi. Kama na wewe ni miongoni mwao,nitakupatia hatua rahisi ambazo ukizitumia utaweza kupata mada bora kwa ajili ya blog yako. Katika makala hii nitazungumzia Jinsi ya kuchagua mada (niche) kwa ajili ya blog yako. hebu tuanze kuangalia hatua hizo.
Soma: Njia 9 za kutengeneza kipato kupitia blog
Jinsi ya kuchagua mada(niche) kwa ajili ya blog yako.
1. Chukua karatasi na Orodhesha vitu vyote unavyovipenda.
Nini unapenda kufanya au kuzungumzia?
Orodhesha vitu vyote unavyovipenda kuvifanya au kuvizungumzia kwenye maongezi yako. Haijalishi ni vikubwa au ni vidogo,we viandike tu.
Inawezekana kwenye orodha yako baadhi ya vitu vikawa kwa mfano:
- Biashara ndogondogo
- Soka
- mazoezi
- Kuchati facebook na Instagram.
- Kuogelea
- Kusoma vitabu n.k
Sasa baada ya kuwa umeorodhesha, unapoangalia orodha yako utashangaa kuona kuwa kuna baadhi ya vitu ulivyoorodhesha vinaweza kuwa mada nzuri kwa ajili ya wewe kuanzishia blog yako. Hivyo weka alama ya nyota kwenye vitu unavyoona kwenye orodha yako vinakupendeza zaidi na vinaweza kuwa ni mada za kuanzishia blog ili uje uvirudie baadaye.
2. Fikiria juu ya Blog,magazeti na vitabu unavyopenda kusoma.

Sasa hebu weka pia orodha ya blog,magazeti na vitabu unavyopenda kusoma. Kisha orodhesha mada ambazo huwa unapenda kusoma kwenye vitabu, magazeti au blog hizo. Utashangaa baadhi ya mada ulizoorodhesha zinaweza kuwa ni mada bora za wewe kuanzisha blog yako. Weka alama ya nyota kwenye mada ambazo unaona zinakuvutia ili baadaye uje uzirudie kuziangalia upya.
3. Orodhesha kazi zote ulizowahi kufanya na zile unazoendelea kufanya na uzoefu wako.
Njia nyingine ya kuchagua mada (niche) ni kwa kuangalia ni kazi gani ulizowahi kuzifanya au unaendelea kuzifanya? Ziorodheshe hata kama ni ndogo kiasi gani.Lakini unapendelea vitu gani (hobbies)? Viorodheshe. Inawezekana ukaanzisha blog kuhusiana na ujuzi wako wa kazini au ukachagua kipengele kimoja kati ya majukumu au ujuzi ambao unautumia kazini. Pia unaweza kuanzisha blog kutokana na hobby yako. Hivyo vyote viorodheshe. Baada ya hapo angalia kwenye orodha yako vitu ulivyovipenda zaidi na uviwekee alama ya nyota ili uje kuviangalia zaidi baadae.
4. Orodhesha vitu ulivyowahi kuvikamilisha.
Andika orodha ya vitu ulivyowahi kuvikamilisha katika maisha yako. Kwa mfano;
- Semina ulizowahi kuhudhuria
- Kozi ulizowahi kusoma n.k
Vyote hivi vinaweza kuwa ni vyanzo vya wewe kupata mada ambayo utaitumia kwenye blog yako. Orodhesha ujuzi ulioupata na kwenye hiyo orodha ,weka alama ya nyota kwenye ujuzi ulioupenda zaidi ili baadaye uje kuuangalia zaidi.
5. Angalia mada zenye umaarufu ambazo zitaendelea kuwa maarufu kwa miaka mingi ijayo.

Pia kama bado unapata kikwazo, orodhesha mada ambazo kwa kweli zitaendelea kuwa na uhitaji kwa miaka mingi ijayo na uangalie kipengele kitakachokufaa kwenye blog yako. Mfano wa mada hizo ni:
- Biashara: Hii inajumuisha vipengele kama jinsi ya kuongeza kipato,jinsi ya kuanzisha biashara, jinsi ya kuwekeza,jinsi ya kupunguza matumizi,jinsi ya kuepuka madeni n.k
- Afya:Hii inachukua eneo kubwa sana.Baadhi ya mada zake ni Jinsi ya kupunguza uzito,Afya ya akili,tiba mbadala n.k
- Malezi: Hii inajumuisha malezi ya watoto.
- Ujasiriamali: Hii inajumuisha jinsi ya kujiajiri n.k
- Utengenezaji wa Tovuti: Hii inajumuisha jinsi ya kutumia WordPress n.k
Sasa mada zote ulizozipenda na kuziwekea alama ya nyota unaweza sasa kuangalia ni mada ipi itakufaa.Ili uweze kujua kama mada uliyoichagua itakufaa, unaweza kuipima kwa kutumia maswali yafuatayo:
Maswali 9 ya muhimu unayopaswa kujiuliza unapochagua mada(niche) kwa ajili ya blog yako.
Kabla ya kuchagua mada (niche) yoyote kati ya zile ulizoziwekea nyota jiulize maswali yafuatayo.
Swali #1. Je unaipenda kiasi cha kutosha mada uliyoichagua?

Unaweza kushawishika kuchagua mada kutokana na umaarufu wake.Lakini jambo la msingi kujiuliza ni kuwa ,je unaipenda kiasi cha kutosha mada uliyoichagua? Hii ni kwa sababu mada uliyoichagua utakuwa ukiitumia kwenye blog yako kwa miaka mingi ijayo. Hivyo ukichagua mada ambayo huipendi kiasi cha kutosha,kadri muda unavyokwenda utakosa hamu ya kuendelea kuandika na hivyo blog yako kufa.
Swali #2. Je una maarifa ya kutosha kutokana na mada uliyoichagua?
Kama unataka kujenga blog yenye mafanikio unatakiwa kuandika makala ambazo zitakuwa na msaada mkubwa kwa wasomaji.Ili uweze kuwa unaandika Makala ambazo watu watazipenda na zenye kuelimisha unatakiwa kuwa na maarifa yakutosha kutokana na mada yako. Hii ni kwa sababu wasomaji watakuwa wanakutegemea wewe kuwa ni mtaalamu wa mada husika na hivyo wakati mwingine watahitaji kupata msaada wa ziada. Hivyo hakikisha una uelewa wa kutosha mada uliyoichagua.
Swali #3. Je ukiamua kuuza bidhaa au huduma kutokana na mada uliyoichagua watu watu watakuwa tayari kununua?
Kabla ya kuanzisha blog unatakiwa pia kujiuliza je kuna bidhaa au huduma yoyote ambayo utakuwa unauza kutokana mada uliyoichagua? Kwa mfano: Unahitaji kuanzisha blog kuhusiana na Biashara ndogondogo,
Je ukiuza vitabu,kozi ,bidhaa au huduma inayohusiana na mada yako watu watakuwa tayari kununua?
Hilo pia ni swali unalopaswa kujiuliza kabla ya kuchagua mada hiyo.
Swali #5. Je mada uliyoichagua itaendelea kuhitajiwa na watu kwa miaka mingi ijayo?
Swali jingine la msingi ni kuwa, mada uliyoichagua itaendelea kuhitajiwa na watu kwa miaka mingi ijayo? Kama utachagua mada ambayo itakuwepo kwa muda mfupi halafu ikapitwa na wakati utajikuta kuwa blog yako itakuwa haihitajiki tena.
Swali #6. Je kuna ushindani kiasi kwenye mada uliyoichagua?
Unaweza ukafikiria kuwa mada nzuri ni ile ambayo haina ushindani yaani hakuna blog nyingine zinazotoa mada hiyo. Lakini ukweli ni kuwa ukiona mada uliyoichagua haina ushindani kabisa tafsiri yake ni kuwa inawezekana mada hiyo haihitajiki sana na ndio maana hakuna blog zinazofundisha mada hiyo. Hivyo, chagua mada yenye ushindani wa wastani.
Swali #7. Je unafurahia watu wanapokutambua kuwa wewe ni mtaalam wa mada uliyoichagua?
Ili uweze kufanikiwa kwenye kazi ya blog, ni lazima kuchagua mada (Niche) unayoipenda. Ingawa hutamtangazia kila mtu kuwa wewe ni mwandishi wa blog inayoelezea mada kwa mfano ya malezi ya watoto, lakini ni jambo jema kufurahia mada uliyoichagua na pia kuona fahari watu wanapokutambua kuwa wewe ni mtaalamu wa elimu ya malezi ya watoto. Usichague mada ambayo utaona aibu kujitambulisha kwa watu kuwa wewe ni mtaalamu wa mada hiyo.
Swali#9. Je mada uliyoichagua itakuwa na Makala ambazo zitadumu kwa muda mrefu bila kupoteza thamani yake?
Hapa ninazungumzia Makala ambazo zikisomwa leo,kesho zinakuwa zimepitwa na wakati kwa mfano Makala zinazozungumzia matukio ya siku(News). Siku inapopita Makala uliyoiandika inakuwa haina thamani tena.Hivyo unapochagua mada kwenye blog yako usichague mada ambayo itakuwa na Makala ambazo thamani ya Makala zake zitadumu kwa muda mfupi.Chagua mada ambayo Makala zake zitakuwa na ubora uleule kwa miaka mingi ijayo (evergreen content). Hebu nitoe mfano wa mada ya Ujasiriamali: katika mada hiyo ukawa umeandika Makala ya “JINSI YA KUANZISHA BIASHARA BILA KUWA NA MTAJI WA PESA”. Makala hii hata ikipita miaka 10 itaendelea kuwa na ubora uleule japo kadri muda unavyoenda utakuwa ukiiboresha tu kulingana na mabadiliko ya jamii na teknolojia.
Faida ya kuwa na Makala zenye ubora unaodumu kwa muda mrefu(evergreen content) ni kuwa:
Badala ya kuandika makala mpya mara kwa mara kuvuta wasomaji wa Blog yako, Makala hizi zitakuwezesha kuvuta wasomaji kuja mara kwa mara kwenye blog yako hata kama hujaweka Makala zingine mpya. Hii ni kwa sababu maudhui ya Makala zako yatabaki kuwa na ubora uleule.
Njia 4 ambazo unaweza kuzitumia kujihakikishia kuwa utafanikiwa kwenye mada uliyoichagua kabla ya kuanzisha Blog.

Sasa tayari umeamua kuchagua mada ambayo utaitumia kwenye blog yako. Tutaenda kuangalia majaribio au njia ambazo utazitumia kujihakikishia kuwa utafanikiwa kwenye mada uliyoichagua.
Jaribio #1. Jaribu kufikiria na kuandika vichwa vya habari vya Makala angalau 50 vinavyohusiana na mada uliyoichagua.
Tenga muda wa kama saa moja hivi ukiwa peke yako sehemu tulivu. Chukua kalamu na daftari na jaribu kufikiria vichwa vya habari vya Makala zinazohusiana na mada yako.
Andika vichwa vya habari vingi kadiri unavyoweza . Lengo ni kuandika vichwa vya habari angalau 50.
Kwa mfano: Hebu tuchukulie kuwa umechagua mada ya MALEZI:
Hebu tuanze kufikiria vichwa vya habari vinavyoendana na mada yetu:
- Jinsi ya kulea mtoto akiwa bado tumboni
- Sababu 6 zinazoathiri ukuaji wa mtoto baada ya kuzaliwa
- Jinsi ugomvi kati ya baba na mama unavyoathiri malezi ya watoto
- Jinsi ya kuwafundisha watoto kusoma wakiwa nyumbani.
- ………….
- …………..
- ………….
Kama ukiishiwa vichwa vya habari kwenye hili zoezi kabla ya kufikia vichwa vya habari 50, basi hii ni dalili kuwa inawezekana mada uliyoichagua haitakuwa chaguo sahihi kwako. Hii ni kwa sababu ili blog yako ianze kupata umaarufu na kupata muitikio kutoka kwa wasomaji,unatakiwa uwe umeandike Makala nyingi Zaidi ya 50.
Jaribio #2. Fungua Ukurasa wa Facebook au Group la Facebook linalohusu Mada uliyoichagua.
Njia nyingine na ya moja kwa moja ya kuangalia mada uliyoichagua kama itakufaa ni kuanzisha ukurasa wa Facebook au Group.
Unaweza kuupa ukurasa wako au group lako jina ambalo utalitumia kwenye blog yako.
Anza kuandika Makala na kuziweka kwenye ukurasa wako au group lako. Kama utafurahia kuposti na kuanza kupata wafuasi ambao watakuwa wakikomenti na kulike basi hiyo ni dalili nzuri kuwa utafurahia kuendesha blog kwa mada uliyoichagua.
Jaribio #3. Jaribu kuandika Makala tano zinazoendana na mada yako.
Mwisho, jaribu kuandika Makala tano zinazoendana na mada yako.
Kama utaona kuandika Makala tano ni nyingi au kama utachoka (bored) baada tu ya kuandika Makala moja, basi unapaswa kufikiria upya uchaguzi wako wa mada inawezekana umechagua mada ambayo sio sahihi kwako.
Kwa ufupi: Jinsi gani unaweza kuchagua mada bora kwa ajili ya blog yako?
Hapa ninakupatia vitu vitatu vya kufuata (checklist):
Fikiria mada nyingi iwezekanavyo kabla ya kuchagua mada moja. Kwa kuwa na mada nyingi ulizozifikiria unaweza kupata mada bora Zaidi kutokana na mada ulizozifikiria.
Zifanyie mada zako majaribio kama nilivyokuelekeza katika Makala hii ili kupata mada moja ambayo itakuwa bora kuliko mada zingine.
Kwa kutumia majaribio niliyokuelekeza katika Makala hii utaweza kuchagua mada (niche) bora sana kwa ajili ya blog yako.
Kwa leo niishie hapo. Kama una maoni yoyote kuhusiana na makala hii ya Jinsi ya kuchagua mada(niche) kwa ajili ya blog yako, usisite kudondosha maoni yako hapa chini. Pia kama unahitaji ushauri wowote, wasiliana nami kwa simu/whatsap 0752081669.
Asante na karibu katika makala zijazo.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024
3 Replies to “Jinsi Ya Kuchagua Mada (Niche) Kwa Ajili Ya Blog Yako.”