Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Kuacha Kazi Yako.

Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Kuacha Kazi Yako.

Karibu mpendwa msomaji katika Makala hii. Nimatumaini yangu kuwa unafuatilia Makala hii kwa sababu unahitaji kujifunza jinsi ya kuanzisha Biashara bila kuacha kazi yako au kuathiri muda wako wa kazi au majukumu uliyonayo kwa sasa.

Soma: Njia 10 za kutengeneza pesa mtandaoni.

Katika Makala hii nitazungumzia hatua kwa hatua jinsi unavyoweza kuanzisha biashara yako ya pembeni huku ukiwa unaendelea na kazi zako kama kawaida.

Hebu kwanza nianze kwa kusisitiza hili … Usiache kazi yako mpaka pale utakapokuwa umeanzisha biashara na biashara yako kuwa na mafanikio.

Hapa ninamaanisha kuwa , usiache kazi yako inayokupatia kipato cha kukufanya uishi bila ya kuwa na mbadala wa Biashara nyingine ambayo itakupatia kipato cha kuweza kuendesha maisha yako.

 Hii ndio maana nimeamua kuandika mwongozo huu rahisi ili uweze kukusaidia jinsi ambavyo unaweza kuanzisha biashara yako ya pembeni hata kama ukiwa ni mwajiriwa na ukajiongezea kipato bila kuathiri kazi zako unazofanya.

Mwongozo huu nimeugawanya katika sehemu 10 ambazo ni rahisi tu kuzifuata ili uweze kuanzisha biashara yako ya pembeni wakati huohuo ukiwa unaendelea majukumu yako ya kila siku.

Sasa karibu tuendelee…

Jinsi ya kuanzisha Biashara yako ya pembeni na kujiongezea kipato bila kuathiri muda wako wa kazi: Kwa kufuata hatua hizi 10 rahisi 

Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Kuacha Kazi Yako.
  1. Uwe na Lengo(Wazo) na ujizatiti kutimiza lengo lako
  2. Orodhesha uwezo ulionao na vitu unavyovipenda.
  3. Pima wazo ulilonalo kama linafaa kabla ya kuanza kulifanyia kazi
  4. Fanya kitu cha pekee ambacho kitatofautisha Biashara yako na Biashara zingine.(Kitu gani kitaifanya Biashara yako kuwa ya tofauti)
  5. Weka malengo yako kwa kuyafafanua ili yawe yanayopimika na kutekelezeka (SMART)
  6. Panga tarehe ya kuanza biashara yako rasmi.
  7. Tambua udhaifu ulionao
  8. Fanya tathmini
  9. Weka mstari unaotenganisha kati ya majukumu yako ya kazi na Biashara yako (Usichanganye kazi na Biashara yako)
  10. Usiache kazi kabla ya kufikia kwenye kilele cha mafanikio ya Biashara yako.

Sasa hebu tuanze!

Jinsi ya kuanzisha Biashara yako ya pembeni na kujiongezea kipato bila kuathiri muda wako wa kazi: Kwa kufuata hatua hizi 10 rahisi:

1.Uwe na Lengo(Wazo) na ujizatiti kutimiza lengo lako

Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Kuacha Kazi Yako.

Jambo la kwanza na la msingi ni kujiuliza mwenyewe,je nitaendelea na hali hii ya kutegemea kipato pekee kutoka kwa mwajiri mpaka lini? Swali hili ukilitafakari kwa kina litakusukuma kufanya maamuzi magumu.

Hivyo unapaswa kufikiria ni biashara gani ambayo unaweza kuianzisha na ambayo haitaathiri kazi unayofanya kwa sasa. Kumbuka kama nilivyoanza kwa kusema: … Usiache kazi yako mpaka pale utakapokuwa umeanzisha biashara na biashara yako kuwa na mafanikio.

Jambo la msingi na muhimu unalopaswa kulifahamu na kulikubali ni kuwa, ili uweze kuanzisha biashara unapaswa kujitoa na kufanya kazi kwa bidii kwani utakuwa sasa umeongeza majukumu (majukumu ya mwajiri wako na yale ya Biashara yako).

Sasa je, uko tayari kujitoa kikamilifu ili uweze kutimiza ndoto zako?

Kama jibu lako ni ndio, Sasa chukua kalamu na daftari na uandike orodha ya majukumu na shughuli ulizonazo na muda ambao huwa unautumia kufanya shughuli au majukumu hayo kwa juma.

Wekea alama ya nyota majukumu yote ambayo unahisi hayana umuhimu mkubwa ambayo unaweza kuyapunguza ili uweze kupata muda wa ziada kuweka majukumu mapya ya Biashara yako mpya unayotaka kuianzisha. Lengo ni kupata muda wa ziada wa kutosha kuanzisha na kusimamia biashara yako.

Kumbuka kuwa,kadiri unavyopata muda wa kutosha kwa ajili ya biashara yako, ndivyo matokeo yake utakavyoyaona mapema.

Anza kwa kupunguza maeneo madogomadogo ambayo hayana umuhimu sana kwako ili uweze kuwa na muda wa kutosha. Kwa mfano:

  • Kuangalia filamu
  • Kuchati kwenye mitandao ya kijamii kama vile facebook na Instagram
  • Kucheza magemu
  • Kucheza pulltable n.k

Pia unaweza ukapunguza kidogo muda wa masaa ya kulala.

Ni kweli na inashauriwa kuwa na muda wa kutosha wa kulala ili kuwa na afya njema. Lakini unaweza kupunguza kidogo bila kuathiri afya ya yako. Masaa 6-8 yanatosha kulala na bila kuathiri afya yako. Baada ya kufanya hivyo jali ratiba uliyojiwekea.

Pia angalia muda ambao akili yako inakuwa imetulia na uutumie muda huo kufanya biashara yako.

Baada ya kuwa umepunguza mambo ambayo hayana umuhimu kwenye muda wako ,sasa utakuwa umepata muda wa kutosha kuweza kuutumia kwenye biashara yako. Lengo la kufanya hivi ni kuwa na muda wa kufanya biashara yako lakini pia bila kuathiri majukumu yako ya kazini.

2.Orodhesha uwezo ulionao na vitu unavyovipenda.

Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Kuacha Kazi Yako.

Jiulize maswali haya:

Je ni ujuzi gani unahitajika kwenye Biashara unayotaka kuianzisha? Jambo la pili, je unaipenda kutoka moyoni biashara unayoenda kuianzisha au ni kwa sababu tu unataka kutengeneza pesa ?

Ukianzisha biashara kutokana na kitu unachokipenda, biashara yako itafanikiwa sana.

Baada ya kuwa umepata majibu sasa tumia muda kuorodhesha rasilimali zote pamoja na ujuzi unaohitajika kwenye biashara unayoenda kuianzisha na uangalie katika vitu ulivyoorodhesha ni vitu gani utaweza kuvifanya na vipi ambavyo hautaweza.Kwa kufanya hivyo utagundua maeneo ambayo una uwezo mkubwa na maeneo ambayo una udhaifu na hivyo kukupa mwelekeo wa kitu gani cha kufanya ili uweze kusonga mbele.

Inawezekana katika biashara unayenda kuifanya ikawa inahitaji ujuzi fulani unaopaswa kuwa nao. Kama ni hivyo basi unatakiwa kufanya maamuzi ya :

  • Kusimamisha kwanza mchakato wako wa kuanzisha Biashara hiyo na kutumia muda huo kujifunza ujuzi unaohitajika kwenye Biashara yako.
  • Au kutafuta mtu mwenye ujuzi huo na kumuajiri ili aweze kukusaidia kwenye maeneo ambayo hauna ujuzi huo.

Kuwa mwaminifu kujua ni maeneo gani una uwezo.

  • Ni mambo gani una uwezo wa kuyafanya?
  • Ni mambo gani una uwezo mkubwa wa kuyafanya?
  • Na ni mambo gani yanahitaji maboresho ili uweze kuyafanya vizuri?

Kumbukakama unahitaji kufanikiwa haraka kwenye biashara yako, unapaswa kutumia muda mwingi zaidi kujifunza na kufanya mambo ambayo unayaweza zaidi na kutafuta mtu wa kukusaidia kwenye mambo ambayo una udhaifu.

Lakini pia ,ili uweze kupunguza zaidi gharama za kuanzisha biashara yako utatakiwa ujifunze ujuzi stahiki unaohitajika kwenye Biashara hiyo.

3.Pima wazo ulilonalo kama linafaa kabla ya kuanza kulifanyia kazi

Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Kuacha Kazi Yako.

Sababu kubwa inayosababisha biashara nyingi kufa ni kukosa soko na hii ndio sababu ya kufanya  utafiti wa kutosha kujua kama biashara unayotaka kuianzisha itafanikiwa kwa kuwa na wateja .

Kimsingi unatakiwa kuanzisha Biashara ambayo inalenga kutatua matatizo ya watu. Hivyo lenga kundi dogo la watu ambao unahitaji kutatua changamoto zao.

4.Fanya kitu cha pekee ambacho kitatofautisha Biashara yako na Biashara zingine.(Kitu gani kinaifanya Biashara yako kuwa ya tofauti)

Utofauti wa Biashara ni ile hali ambayo biashara yako inaonekana ina kitu cha ziada ukilinganisha na biashara zingine zinazotoa huduma kama ya kwako.Kwa kingereza inaitwa competitive advantage. Jiulize ni kitu gani cha ziada ambacho utakuwa nacho kwenye Biashara yako ambacho hakipo kwenye Biashara zingine.

Unaweza kuwa tofauti na watu wengine wenye biashara kama yako kwa mfano katika bei,upekee wa jinsi unavyotoa huduma,usambazaji au huduma kwa wateja.

Pia kitu kingine cha tofauti ambacho unaweza kuwa nacho inaweza kuwa ni ujuzi ulionao kwenye huduma unayotoa. Watu wanapenda kuhudumiwa na mtu ambaye amebobea kwenye ujuzi wanaouhitaji na sio mbabaishaji. Hivyo ukiwa na ujuzi wa hali ya juu itakufanya uwe na kitu cha tofauti kwenye biashara yako na hivyo kuweza kushinda ushindani.

5.Weka malengo yako kwa kuyafafanua ili yawe yanayopimika na kutekelezeka (SMART)

Sasa tayari umeshatambua biashara ambayo unaenda kuifanya na jinsi utakavyoifanya kuwa na utofauti na biashara zingine.Sasa ni wakati wa kuweka malengo ya biashara yako. Malengo unayoyaweka ni sharti yawe na sifa hizi:

  • Yanayoeleweka (specific)-Ni lazima yaonyeshe kuwa unataka nini kwenye biashara yako
  •  Yanayopimika (Measurable)-Ni lazima uweke vigezo vya kupima kama malengo yako yamefanikiwa au la.
  • Yanayofikika (attainable)-Lazima uweke malengo ambayo kiuhalisia yanafikika au kutekelezeka.
  • Yawe na uhalisia (Realistic) na
  • Yawe na muda maalumu(Time bound)-Weka muda maalumu wa kufanya tathmini ya malengo uliyojiwekea.

Unaweza kuweka malengo ya siku,juma,mwezi. mwaka n.k

6. Panga tarehe ya kuanza biashara yako rasmi.

Sasa panga ni muda gani unaenda kuanzisha biashara yako.Kumbuka kuwa kupanga haitoshi ,kitu kinachotakiwa kwa sasa ni kuanza utekelezaji wa mipango uliyojiwekea.Kama utaona kuna ugumu unaweza kuomba ushauri kutoka kwa marafiki unaowaamini,familia na washauri wengine.Chuja ushauri unaopewa ili usikukatishe tamaa ya kutimiza malengo yako.

7.Tambua udhaifu ulionao

Tambua maeneo yote ambayo una udhaifu na maeneo yote ambayo una uwezo mkubwa. Katika maeneo ambayo unaona kuwa una udhaifu tafuta watu wenye ujuzi huo wakusaidie ili wewe uweke juhudi kwenye maeneo ambayo una uwezo nayo.

Hapa ninamaanisha kuwa, unatakiwa kuchagua maeneo ambayo unaweza kuyafanya vizuri na yale ambayo huna ujuzi wa kutosha tafuta watu wakusaidie. Kwa mfano,unahitaji kuanzisha blog na wewe una uwezo mkubwa katika kuandika Makala lakini haufahamu jinsi ya kutengeneza Blog,hapa utatakiwa kutafuta mtu ambaye ana ujuzi wa kutengeneza blog wakati huo wewe ukiendelea kuandaa Makala kwa ajili ya blog yako.

8.Fanya tathimini

Lengo lako ni kuwa na bidhaa au huduma ambayo watu wataipenda.

Hivyo sehemu hii ni ya muhimu kufanya tathmini kwenye kila Nyanja ya biashara yako.Fanya hivi kuanzia siku ya kwanza na usiache.

9.Weka mstari unaotenganisha kati ya majukumu yako ya kazi na Biashara yako (Usichanganye kazi na Biashara yako)

Hapa unaweza ukajaribiwa kutegea kazi na muda huo ukautumia kwa ajili ya kuendeleza biashara yako. Lakini kumbuka kuwa wakati unaajiriwa,ulipewa mkataba wenye masharti na ukaweka saini kuwa utakuwa mtiifu kwa mkataba huo.Hivyo ili uweze kufanikiwa katika biashara yako,weka mstari unaotenganisha majukumu ya kazini kwako na biashara yako.Vyote unatakiwa uvipatie vipaumbele sawa. Fanya majukumu ya kazini kwa uaminifu na kwa bidi na pia fanya biashara yako kwa nguvu na maarifa ya kutosha.

10.Usiache kazi kabla ya kufikia kwenye kilele cha mafanikio ya Biashara yako.

Kama nilivyosisitiza mwanzo wa Makala hii, endelea kukuza biashara yako mpaka pale utakapoona umefanikiwa kwa kiasi cha kutosha ndio uwaze kuacha kazi yako.

Kuanza biashara ukiwa kazini ni jambo ambalo ni gumu ukilinganisha na majukumu mengi ambayo utakuwa nayo kazini.Hata hivyo kuna njia nyingi ambazo unaweza kuzitumia ili uweze kuanzisha biashara na kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio huku ukiwa kazini.Fuata hatua hizi nilizokuelezea nawe utafanikiwa kuwa na biashara yako ambayo itakuletea mapato nje ya mshahara wako.

Je uko tayari kuanza biashara yako ukiwa kazini bila kuathiri muda wako wa kazi?

Kwa kufuata kanuni nilizokuelezea hapo juu,unaweza kuanzisha biashara yako bila kuacha kazi unayofanya kwa sasa.Miongoni mwa mifano ya kazi ambazo unaweza kuzifanya ukiwa kazini bila kuathiri muda wako wa kazi nimezielezea kwa undani kwenye Makala yangu ya Njia 10 za kutengeneza pesa kupitia mtandao wa internet bila kuathiri muda wako wa kazi.Kwa ufupi ni hizi hapa:

Anzisha Blog inayohusiana na mada au ujuzi ulionao (Niche Blog).

Tengeneza na uuze application za Simu.

Anzisha duka la mtandaoni na uuze bidhaa kupitia mtandao wa Internet.

Toa huduma kutokana na  ujuzi ulionao mtandaoni.

Fundisha mtandaoni na uuze ujuzi wako(Online coaching)

Andaa kozi mbalimbali kutokana na ujuzi wako na uziuze mtandaoni.

Anzisha Channel ya Youtube.

Andika na uuze vitabu pepe.

Anzisha huduma ya Graphic Design kwa makampuni au wafanya biashara wanaokuzunguka

Kuwa mshauri wa Biashara

Na biashara zingine ambazo unaweza kuzifanya kupitia mtandao wa internet.

Je unahitaji ushauri wangu ni aina gani ya biashara unaweza kuanza nayo?

Anza kwa kuanzisha blog kama hii yangu unayosoma kutokana na ujuzi au maarifa uliyonayo.Ni njia rahisi ya kujiajiri ambayo inahitaji gharama kidogo sana.Halafu biashara zingine utaziongeza na kuzitangaza kupitia blog yako.

Nimatumaini yangu umepata maarifa ya kukusaidia kuanzisha biashara ya pembeni na hivyo kuweza kuwa na kipato cha ziada nje ya mshahara wako. Je una komenti yoyote? Usisite kudondosha komenti yako hapa chini! Pia kwa ushauri wa usisite kuwasiliana nami kwa simu namba 0752081669. Asante na karibu katika makala ijayo.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

4 Replies to “Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Bila Kuacha Kazi Yako.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp