
Karibu mpendwa msomaji katika Makala hii ya leo. Katika Makala hii nitaelezea jambo moja kubwa unalopaswa kulizingatia na kulifanyia kazi ili uweze kufanikiwa katika maisha. Inawezekana umekuwa ukitumia juhudi kubwa katika kazi zako ili uweze kujikwamua kimaisha lakini matokeo yanakuwa hayaonekani. Nikuhakikishie kuwa ukifuatilia Makala hii mwanzo hadi mwisho utakuwa umepata kitu cha msingi sana ambacho kitakusaidia uweze kufanikiwa katika maisha yako. Karibu tuendelee.
Je ulishawahi kujiuliza ni kitu gani kinawatofautisha watu waliofanikiwa sana na wale ambao hawajafanikiwa? Katika Makala hii ya leo ningependa nikushirikishe kitu kimojawapo ambacho kinaweza kukusaidia sana kwenye maisha yako. Kitu hicho ni uwezo wa kupanga malengo na kuyafuatilia.
Watu wengi wanaamka kwenda kazini lakini ukiwauliza baada ya miaka kumi watakuwa akina nani hawawezi kukujibu. Sasa hebu nikushirikishe utafiti uliowahi kufanywa na Chuo Kikuu cha Havard cha nchini Marekani.
Chuo kikuu cha Havard mwaka 1979 kwenye kitengo cha biashara walifanya utafiti. Walikusanya wanafunzi 100 ili waweze kuwafanyia utafiti. Utafiti huo ulikuwa ni wa kuwauliza maswali. Waliwauliza kuwa, wakimaliza shule baada ya miaka kumi watakuwa ni wapi ki-maisha au watakuwa na mafanikio gani? Wanafunzi hao walitoa majibu kama ifuatavyo:
Asilimia 84 ya wanafunzi walikuwa hawajui watakuwa wapi, hivyo hawakuwa na mpango wowote katika maisha yao. Walikuwa wakisoma lakini walikuwa hawajui maisha yao yatakuwaje.
Asilimia 13 ya wanafunzi walikuwa wanajua wanachokitaka lakini hawakuwa na mpango wowote wa jinsi ya kupata kile kitu walichokuwa wanahitaji kwenye maisha yao.
Asilimia 3 ya wanafunzi walisema wanajua wanachokitaka na walikuwa wametengeneza mpango kamili wa jinsi ya kufanikiwa kupata kile walichokuwa wamekusudia kukipata.
Utafiti huo uliendelea baada ya miaka kumi .Baada ya miaka 10 Chuo cha Havard kiliwafuatilia wanafunzi hao ili kiweze kupata matokeo ya utafiti wao. Matokeo yaliyopatikana yalikuwa ni ya kushangaza.
Katika matokeo hayo:
Wale wanafunzi asilimia 13 ambao walisema wanajua wanachokitaka lakini hawakuwa na mpango wowote walikuwa wamefanikiwa mara mbili zaidi ya wale asilimia 84 waliosema hawajui wanataka nini katika maisha yao.
Wale wanafunzi asilimia 3 ambao walisema wanajua wanachokitaka na wametengeneza mpago kamili wa jinsi ya kufanikiwa walikuwa wamefanikiwa mara 10 zaidi ya wale wanafunzi wengine wote.
Utafiti huu ukahitimisha kuwa, unapokuwa na malengo yako na ukayaishi, una uwezo wa kufanikiwa mara 10 zaidi ya wale ambao hawana malengo.
Kuanzia leo usiwe mtu asiyekuwa na malengo. Tumia muda kutafakari na kujiuliza miaka 10 ijayo utakuwa wapi?
Utakuwa na kiwango gani cha elimu.
Utakuwa na cheo gani.
Utakuza biashara yako kwa kiwango gani na kadhalika.
Hivyo, uwezo wa kupanga malengo na kuyaishi ni muhimu sana katika maisha yako. Usiishi kama mtu asiyekuwa na mwelekeo. Weka malengo na upange namna ya kuyafikia. Unapoamka asubuhi hakikisha unapitia malengo yako uliyojiwekea ili usiweze kupoteza muda wako kwa mambo ambayo yako nje ya malengo yako.
Chukua muda kutafakari na kupanga malengo yako unataka kuwa nani na wapi katika maisha. Unaweza kunishirikisha kwa kukomenti hapo chini. Asante sana na karibu katika Makala ijayo.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024