
Brian Tracy, mtaalamu wa masuala ya maendeleo binafsi (self development) aliwahi kusema kuwa, Unaweza kutimiza takriban lengo lolote ulilojiwekea, mradi tu lengo lako liwe wazi na uendelee kwa muda wa kutosha kulifanyia kazi. Kuzingatia mpango wako binafsi wa maendeleo huongeza sifa ulizo nazo ndani yako na hufanya ndoto na matarajio yako kugeuka kuwa ukweli. Uwezo wako hauna kikomo na kuwekeza katika maendeleo yako binafsi ni njia ya kutumia talanta zako nyingi. Katika makala hii nitakushirikisha jinsi ya kuweka mpango wa maendeleo ili uweze kufanikiwa katika maisha yako.
Umuhimu wa Kuwa na Malengo.
Kuweka malengo ya kile unachotaka kufikia na wapi ungependa kwenda kwa muda mfupi au mrefu kunaweza kuboresha maendeleo yako binafsi. Baada ya kusoma karibu kila kitu kilichoandikwa au kusemwa juu ya maendeleo ya binafsi na mafanikio, Brian Tracy alifikia hitimisho kwamba mzizi wa yote mawili ni kiwango chako cha kujiamini. Kujiamini ni jambo muhimu katika kila kitu unachotaka kukikamilisha katika maisha yako.
Watu wengi hawafaulu katika taaluma zao kwa sababu hawatambui maeneo ya maendeleo yao binafsi ambayo yanaweza kuwasaidia kufikia ustadi wa hali ya juu katika maisha yao. Hakuna mbadala wa kufanya kazi kwa bidii. Ikiwa utaweka lengo, weka mpangokazi na uufanyie kazi kila siku, utaona maendeleo ndani ya kazi yako.
Mipaka ipo Akilini Mwako.
Hakuna mipaka ya mafanikio isipokuwa mipaka unajiwekea wewe mwenyewe kwenye mawazo yako. Usichoke kujifunza maisha yako yote. Hata kama una mafanikio ya juu kwenye malengo yako, daima kuna kitu cha kujifunza.
Utakuwa mtu mwenye mafanikio yasiyopimika na utaona maisha yako yote yajayo yanafunguka mbele yako ikiwa unaishi maisha yenye malengo na yenye mwelekeo wa kukua. Kuwa na mpango hukusaidia kupata hali bora ya udhibiti wa maisha yako na kutakufanya uwe tayari kwa lolote litakalokuja.
Maana ya mpango wa maendeleo binafsi.
Unaweza kuwa unafikiria, mpango wa maendeleo binafsi ni nini?
Mpango wa maendeleo binafsi ni mwongozo wa maisha yako na mafanikio yako ya baadaye.
Sababu ya kuwa na mpango wa maendeleo binafsi ni kwamba, kufanya mpango kutakusaidia kufanya maamuzi bora na kujikumbusha mahali unapotaka kwenda. Maandalizi mazuri huongeza uwezekano wa kufaulu na hupunguza hatari ya mambo kwenda kombo. Unapoandika mpango wako wa maendeleo ya binafsi, fikiria kuhusu malengo unayotaka kufikia, njia ambazo unahitajika kuziboresha na kuziendeleza, na hivyo kuwa na mpango ambao utakufanya uwe tayari kukabiliana na kazi muhimu zaidi kwa siku zinazokuja.
Hatua tano Muhimu za Maendeleo Binafsi.
Katika Ukuaji binafsi, kabla ya kujiwekea mpango, unahitajika kutafakari kisha ufuate hatua hizi sita za msingi.
Hatua ya kwanza ni kuandika orodha ya malengo 10 muhimu zaidi ambayo ungependa kuyafikia.
Hatua ya pili ni kuandika ni yapi kati ya hayo malengo 10 ni muhimu zaidi kwako na kwa nini.
Hatua ya tatu ni kuandika ratiba maalum ya kufikia lengo lako.
Hatua ya nne, andika uwezo na udhaifu wako.
Kisha, zingatia kuandika uwezo wako katika maeneo matatu na mapungufu yako matatu na kisha uandike jinsi uwezo wako unavyoweza kukusaidia kufikia lengo hili na jinsi unavyopanga kushinda udhaifu huo. Hii itakusaidia kuweka mpango wa maendeleo binafsi katika vitendo na kutokukata tamaa unapopata changamoto.
Hii inaweza kuwa mambo unayohitajika kuongeza kwenye utaratibu wako wa kila siku pamoja na mambo unayohitaji kuondokana nayo.
Kwa kufanya hivi kutakusaidia kufikia kila lengo haraka.
Na hatimaye, hatua ya tano ni kutathmini maendeleo yako. Andika malengo yale ambayo yamekuwa yakifanya kazi vizuri, yale ambayo umekamilisha, yale ambayo bado unahitajika kuyaboresha, na ni ujuzi gani au maarifa gani umeyapata njiani.
Sasa, ningependa kusikia kutoka kwako. Swali letu la leo; ni nini kinakuzuia kufikia malengo yako? Je, ni ukosefu wa mpango? Acha maoni hapa chini nami nitahakikisha kuwa ninakutafuta ili tushauriane.
Ikiwa umefurahia makala hii na unahisi ilikuwa ni ya thamani sana kwako, usisite kuwashirikisha marafiki zako.
Kama una swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024