
Napoleon Hill alikuwa ni mwandishi wa vitabu vya mafanikio, raia wa Marekani. Vitabu vyake vililenga zaidi kwenye kanuni za mafanikio na kuwa tajiri katika maisha na kifedha. Alianza kazi yake kama mwandishi wa habari kabla ya kuwa mshauri wa rais wa Marekani wa kipindi kile aliyejulikana kwa jina la Franklin D. Roosevelt.
Ni wakati alipofanya mahojiano na Andrew Carnegie ndipo alipopata hamasa ya kuanza kazi yake ya kuhamasisha watu juu ya mafanikio. Alitumia maarifa aliyoyapata kwenye mahojiano hayo kuandika vitabu vya mafanikio katika biashara na kutengeneza kipato. Vitabu vyake vingi vimeendelea kuwa maarufu mpaka sasa kama vile vilivyokuwa kabla ya kifo chake mwaka 1970.
Hatua 10 Za Kuwa Na Mafanikio Na KuwaTajiri.
Kitabu Cha Think and Grow Rich kinaelezea nguvu iliyopo kwenye kuwa na fikra chanya kwenye maisha. Kitabu hiki kinaelezea umuhimu wa kuwa na fikra chanya za mafanikio. Watu waliofanikiwa toka zamani walikuwa na mawazo chanya kuwa watafanikiwa wakiwa na uvumilivu pamoja na elimu ya kile walichokuwa wanafanya. Pia walikuwa wamezingukwa na watu waliokuwa wana mawazo yanayoendana ya mafanikio kwenye kile walichokuwa wanafanya.
Kila mmoja anaweza kushindwa katika malengo aliyojiwekea ya maisha, lakini, kwa wale ambao wataendelea kujaribu bila kukata tamaa watafanikiwa.
Mambo ya msingi ya kujifunza kutoka kwenye kitabu cha Think and grow rich.
1: Mafanikio yanahitaji kuwa na malengo pamoja na mipango iliyoainishwa vizuri.
“Set your mind on a definite goal and observe how quickly the world stands aside to let you pass.” — Napoleon Hill.
Maana yake ni kuwa, jiwekee malengo, hapo ndipo utaona jinsi utakavyowapita wengine kimafanikio kwa haraka.
Jambo la muhimu kabisa katika mafanikio ni kujua nini hasa unachohitaji kufanikiwa. Bila kuwa na malengo yaliyo bayana, hatuwezi kuanza safari ya mafanikio. Hivyo, andika malengo yako kwa lugha rahisi iwezekanavyo. Kama unataka kuwa tajiri, unatakiwa ubainishe ni kiasi gani cha pesa unataka kumiliki utakapokuwa umefikisha umri fulani. Malengo yatakusaidia kufahamu ni kwa kiwango gani unapaswa kuwekeza ili uweze kufikia lengo kuu uliloliweka.
Baada ya kuwa umefahamu hitaji lako kuu na umejiwekea muda wa kuwa umelitimiza, jambo linalofuata ni kuweka mikakati ya hatua kwa hatua jinsi ya kutimiza lengo lako kuu. Baada ya kuwa umeweka hizo hatua, anza kufanyia kazi mara moja bila kukawia.
Kuweka malengo kutakupatia hamasa ya kufanya bidii kwenye kazi zako na hivyo kuweza kufanikiwa.
2: Kuwa na shauku ya kutimiza malengo yako. (Desire is the Starting Point of All Achievement)
Unaweza kupata chochote unachokitafuta katika maisha kama utakuwa na shauku (desire) ya kukipata.
Hii haimaanishi kuwa na shauku tu ya kupata kile unachokitamani. Kwa mfano unatamani kuwa na pesa na hivyo kwa kuwa na shauku tu pesa itashuka kwa muujiza, hapana. Badala yake ni kuwa, unapokuwa na shauku ya kufikia lengo kubwa katika maisha, utahamasika kuweka mipango madhubuti ya kufikia mafanikio.
Hatua zifuatazo zitakusaidia kuweka malengo yako ya kufanikiwa na kuwa tajiri (becoming wealthy):
i. Amua ni kiasi gani cha pesa unahitaji kukipata.
ii. Amua ni kitu gani utatoa au utawekeza ili uweze kupata kiasi cha pesa unachokihitaji.
iii. Weka tarehe ambayo umeamua kuwa utakuwa umepata kiasi hicho cha pesa.
iii. Weka mipango ya hatua kwa hatua ya jinsi utakavyofikia lengo lako. Pia angalia ni kitu gani utaanza kukifanyia kazi sasa bila kuchelewa.
Mambo yote hapo juu yaandike kwa sentensi fupi.
Jambo la mwisho, hakikisha kuwa unasoma sentensi hiyo mara mbili kwa siku.
3: Watu waliofanikiwa huwa wana imani na uwezo wao (successful People Have Faith in Their Abilities)
Imani isiyoyumba ndiyo rasilimali ya muhimu sana na ya ajabu sana kwenye mafanikio yako. Watu walio na imani watafanya kila kitu kwa nguvu, na kwa akili zao zote ili waweze kutimiza malengo yao. Hii ni kwa sababu, hautaweza kutimiza malengo yako kama haujiamini.
Mahatma Gandhi ni mfano mzuri sana wa nguvu ya imani na kujiamini. Gandhi hakuwa na nguvu yoyote ya kifedha au kijeshi. Badala yake alikuwa na imani isiyoyumba kuwa angeweza kuongoza taifa lake la India kupata uhuru. Imani Hii ilimuwezesha kuwashawishi wananchi wenzake kuanza kupigania uhuru wao.
Hata sisi, hatuna tofauti na Gandhi. Ikiwa tutakuwa na imani, ikiwa tutajiamini sisi wenyewe na uwezo tulionao, tutaweza kupata chochote tunachokihitaji.
4: Hauwezi kuwa na imani wakati huohuo ukiwa na hofu na mashaka.
Imani haiwezi kuwepo mahali palipo na hofu. Hivyo, wakati tutakapokuwa tumeshinda hofu zinazotukatisha tamaa, tutakuwa na imani isiyoyumba kutimiza malengo yetu na kupata utajiri.
Kuna aina sita za hofu:
i. Hofu ya umasikini ambayo husababisha kujiona kuwa haufai na kuwa na mashaka.
ii. Hofu ya kukosolewa. Hii ni hofu ambayo humfanya mtu asichukue hatua kwa kuogopa kuwa watu watamdharau na kumkosoa.
iii. Hofu inayosababishwa na hali ya kiafya. Kama mtu afya yake haiko sawa, anaweza kuogopa kuchukua hatua kutimiza malengo yake.
iv. Hofu ya kupoteza marafiki. Wakati mwingine unaweza kuogopa kuchukua hatua kwa kuogopa kupoteza marafiki.
v. Hofu inayotokana na uzee. Umri unavyozidi kwenda kuelekea kwenye uzee uwezo wa kufanya mambo huwa unapungua na kumfanya mtu awe na uoga wa kufanya mambo makubwa ambayo yatabadilisha maisha yake.
vi. Hofu ya kifo. Hofu ya kifo huwa inatufanya tuwaze zaidi kufa badala ya kuwaza ni kwa namna tunaweza kuishi tukiwa na maisha bora.
Mawazo yote ya hofu, hayawezi kukupatia mafanikio ya kifedha. Hivyo, tunapaswa kuepuka hofu ili tuweze kutimiza malengo yetu.
5: Pata elimu ya kitu unachotaka kufanya.
Elimu ni miongoni mwa vitu vya msingi sana katika kufikia malengo yako ya maisha. Kuwa na elimu haimaanishi kuwa na Diploma au Shahada.
Henry Ford ni mfano mzuri wa mtu ambaye hakubahatika kusoma lakini alikuwa na maarifa ya msingi ya kumsaidia kuweza kutimiza malengo yake.
Kuwa na mafanikio haihitaji kuwa na vitu vingi unavyovifahamu, badala yake, unahitajika kuwa kuwa na elimu na na uzoefu sahihi wa kile unachotaka kufanikiwa.
Ni rahisi kuridhika kuwa unafahamu vya kutosha kile unachokifanya katika maisha yako. Lakini, wale ambao wanaendelea kujifunza zaidi na kubobea kwenye ujuzi wa kazi wanazozifanya huwa wanafanikiwa sana. Hivyo, unaweza kujiendeleza zaidi kwa kusoma chuoni au kusoma kozi mtandaoni zinazoendana na kile unachokifanya ili uweze kukifanya kwa ufanisi na hivyo kufanikiwa kwenye maisha yako.
Pia, ili uweze kupata maarifa ya kutosha, mara zote unapaswa kujenga mahusiano na kuwa karibu na watu wenye uzoefu na elimu ya kile unachokifanya.
6: Kuwa na ndoto kubwa na uwe na hisia ya kuwa lazima utafanikiwa.
Kila mtu aliyefanikiwa, alianza kuwa na ndoto. Baada ya kuwa na ndoto, akajenga hisia kuwa lazima atafanikiwa. Hisia hizi zikanasa kwenye ubongo. Hivyo ili uweze kupata mafanikio, ni lazima uwe na ndoto pamoja na na hisia kali za kufanikiwa kwenye ndoto yako. Unapokuwa na hisia za mafanikio, hapo ndipo utapata njia na mipango ya kuwekeza kutimiza ndoto zako.
7: Tambua uwezo wako pamoja na mapungufu yako.
Kama unatambua udhaifu wako, utajipa changamoto ya kuzuia udhaifu wako usiweze kuzuia kutimiza malengo yako. Miongoni mwa mapungufu ambayo watu wengi wanayo ni pamoja na kukosa hamasa ya kufanya mambo (lack of ambition), kughairisha mambo (procrastination) na kuwa na malengo yasiyopimika (vague goals).
Ingawa unaweza kufahamu uwezo wako na udhaifu wako, unaweza kufahamu kwa ufasaha uwezo na mapungufu yako kwa kuandaa maswali ya kukuongoza kama ifuatavyo:
Je, nimetimiza malengo yangu ya mwaka?
Je, huwa ninakuwa na ushirikiano na wenzangu? Na kadhalika.
8: Kuwa na mtizamo chanya.
Unapokuwa ukifanya kazi kutimiza malengo yako, kuwa na mtizamo chanya kuwa utafanikiwa haijalishi utapitia changamoto kubwa kiasi gani. Jenga urafiki na mahusiano na watu walio na mtizamo chanya wa maendeleo kwani ukiwa umezungukwa na watu wenye mtizamo hasi, watakukatisha tamaa.
9: Watu waliofanikiwa ni wavumilivu kwenye changamoto.
Jizatiti kwenye malengo yako.
Watu huwa wanaferi katika malengo yao kutokana na kukosa uvumilivu. Katika malengo yako utapitia kushindwa lakini kumbuka kuwa mvumilivu. Kila unapopata changamoto, ichukulie kuwa ni sehemu ya kujifunza na kukufanya uwe bora zaidi. Watu waliofanikiwa huwa hawatoki nje ya malengo yao haijalishi wanapitia changamoto kubwa kiasi gani.
Jinsi ya kujenga uvumilivu na ustahimilivu kwenye malengo.
Ili uweze kuwa na uvumilivu pamoja na ustahimilivu kwenye kutimiza malengo yako, kanuni hizi zifuatazo zitakusaidia:
i. Andaa lengo katika maisha yako kutokana na kitu unachokipenda (Passion)
ii. Gawa lengo lako kwenye sehemu ndogondogo za utekelezaji na uweke mpango wa kutimiza lengo lako kwa kila sehemu ndogo uliyoiainisha.
iii. Usiruhusu mawazo hasi kuathiri utekelezaji wa malengo yako.
iv. Jenga mahusiano bora na watu wote ambao watakushika mkono katika nyakati ngumu.
10: Jiunge na kundi lenye shauku ya mafanikio ambalo mtabadilishana uzoefu (Mastermind group).
Kutengeneza kipato kunahitaji nguvu. Bila kuwa na nguvu hautaweza kuweka mipango yako katika utendaji. Kundi lako litaundwa na watu wenye shauku ya kufanikiwa na litakuwa na watu wenye ujuzi wa aina mbalimbali ambao mtabadilishana uzoefu na kupeana hamasa ya kuweza kufikia mafanikio. Tumia ujuzi ambao utakuwa unaupata kwenye kundi lako kutimiza malengo yako.
Kwa ufupi, kitabu cha Think And Grow Rich kinaelezea njia rahisi na zilizothibitishwa ambazo zitakusaidia kuwa tajiri. Kanuni hizi zimeelezwa kwa lugha rahisi na pia ni rahisi kuzifuata.
Kuwa na mtizamo chanya na kuweka mipango inayotekelezeka ni njia zitakazokusaidia kufikia malengo yako na kuwa tajiri. Pia unatakiwa kuambatana na watu sahihi ambao watakupa hamasa ya kufanyia kazi malengo yako.
Kanuni hizi ni za msingi, na hivyo jinsi utakavyozitumia itategemea na malengo yako. Hata hivyo, kitabu hiki kinatoa ushauri bora sana kwa mtu yeyote mwenye ndoto kubwa maishani ya kufanikiwa na kuwa tajiri.
Kama una maoni au swali lolote usisite kuandika hapa. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024
Asante Kwa elimu nzuri katika mwangaza kuelekea utajiri nimenufaika sana but nashindwa kuweka malengo ,nanna gani naweza kupanga malengo yqngu?kama Kuna template naweza nikanufaika zaidi,natanguliza shukrani kwenu
Asante sana kwa kufuatilia makala hizi. Tunaweza kuwasiliana ili nikupe msaada zaidi.