Funguo 6 Za Kuwa Kiongozi Bora.

Funguo 6 Za Kuwa Kiongozi Bora.

Uongozi ni mojawapo ya vigezo muhimu sana kwenye mafanikio ya biashara, kazi na mafanikio ya mtu binafsi. Viongozi bora wana uwezo wa kushawishi watu wanaowazunguka kuweza kufanya mambo kwa viwango vya hali ya juu. Katika hali ya kawaida na tafsiri rahisi, uongozi ni uwezo wa kutatua changamoto zilizopo ili kuweza kupata matokeo yaliyokusudiwa.
Watu wengi wanaamini kuwa, viongozi bora ni wa kuzaliwa. Hata hivyo dhana hiyo siyo ya kweli. Kwani, kwa kufanya vitu sahihi na kuchukua hatua sahihi, mtu yeyote anaweza kuboresha uwezo wake wa kuongoza na hivyo kuwa kiongozi bora. Katika makala ya leo, nitakushirikisha funguo 6 za kuwa kiongozi bora.

Funguo 6 za kuwa kiongozi bora.

1.Usijiwekee mipaka.
Jinsi unavyojifikiria ndivyo unavyokuwa. Ukiamini kuwa unaweza basi utaweza. Ukiamini kuwa hauwezi, hautaweza. Akili yako huwa inafanyia kazi kwa usahihi kile tu unachokiamini. Hivyo, ukiamini katika kufanya mambo makubwa, akili yako itafanya hivyohivyo. Hivyo, amini katika uwezo mkubwa ulionao nawe utafanikiwa. Kumbuka kuwa, unawajibika moja kwa moja katika mawazo unayojiwazia na jinsi unavyojiwekea mipaka ya mafanikio makubwa. Hivyo basi, amua kufanya mambo makubwa na uondoe mipaka uliyojiwekea ili uweze kupata mafanikio makubwa katika kazi yako na katika maisha yako kwa ujumla.

2.Acha kuwa na visingizio (Stop making excuses)
Jambo linapotokea ambalo siyo la kawaida, usilichukulie kuwa ni kwa sababu ya uzembe ulioufanya, bali lichukulie kuwa ni sehemu ya majukumu yako ya kawaida na hivyo unawajibika kwa asilimia mia moja kulitatua. Ili uweze kuwa kiongozi bora, ni jambo la muhimu sana kukubali kuwajibika kwa asilimia mia moja kwenye maisha yako mwenyewe, maamuzi yako na uwezo wako. Jambo hili la uwajibikaji kwenye nyanja zote za maisha yako (radical responsibility) litakusaidia kuwa na umiliki wa maisha yako kwa ujumla na kukuondolea visingizio ambavyo vitakufanya usiwajibike.
Acha kulaumu mambo ambayo yako nje ya uwezo wako na tambua kuwa ni jukumu lako kutafuta suluhu ya changamoto zinazojitokeza haijalishi unapitia kipindi gani.

3. Mara zote tafuta fursa mpya za kukufanya uwe bora zaidi.
Viongozi bora huwa hawaridhiki kufanya mambo kwa mazoea. Mara zote huwa wanajifunza kila siku mambo mapya ambayo yatawafanya wawe bora zaidi. Hivyo, ili uwe kiongozi bora, kila siku jifunze mambo mapya kwa kuuliza, kukutana na watu mbalimbali na Kujifunza kupitia kusoma vitabu. Kwa kufanya hivyo, utaweza kufungua fursa mahali ambapo wengine hawazioni na kufanya mambo makubwa mahali ambapo wengine wanaona haiwezekani. Hii ndiyo tofauti iliyopo kati ya kiongozi na wafuasi. Kiongozi huwa anatengeneza njia bali wafuasi husubiri mpaka waone njia imetengenezwa ndiyo wapite.

4. Kubali kushindwa na ujifunze kutokana na makosa.
Kushindwa katika maisha ni jambo lisiloepukika. Viongozi wote bora katika historia walipitia uzoefu wa kushindwa. Wengine walipitia vipindi vigumu vya ukosoaji mkubwa na kukataliwa. Jambo lililowatofautisha na watu wengine ni kuwa, waliweza kushinda changamoto hizo kwa Kujifunza kutokana na kushindwa kwao na na hivyo kuchukua hatua. Viongozi bora huwa wanafahamu ubora wao na mapungufu yao na hivyo hutumia ubora wao na mapungufu yao kama fursa ya kujifunza ili kuwafanya wawe bora zaidi kesho. Hata wewe unaweza kushindwa, lakini kubali kushindwa na utumie makosa yako kama fursa ya kujifunza ili uweze kuwa kiongozi bora.

5. Ongoza kwa kuwa mfano.
Watu huwaheshimu sana viongozi wanaotenda mambo yote wanayoyasema. Kama unataka kuwa kiongozi bora, usitegemee kuwa watu watafanya kitu ambacho wewe kiongozi haukifanyi. Hivyo, watu huwaheshimu viongozi wanaokuwa wa kwanza kufanya vitu ambavyo wanategemea watu wengine wavifanye. Hivyo, ili uwe kiongozi bora, kuwa mfano kwa wale unaowaongoza nawe utaheshimika.

6. Fanya mambo yako kwa ubora na ubunifu.
Viongozi bora pamoja na kuongoza kwa mfano, pia hufanya mambo yao kwa ubora na ubunifu. Maana yake ni kuwa, huwa wanatafuta njia fupi na bora zaidi ya kutatua changamoto. Wana uwezo wa kuona mambo makubwa na kuweka mipango na njia za kuweza kufanikiwa. Huwa wanatafuta njia ya haraka, yenye gharama himilivu na halali ya kufanya mambo lakini kwa ubora uliokusudiwa.

Swali leo.
Ni katika eneo gani unawajibika kwa asilimia mia moja ili uweze kuwa kiongozi bora?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika kwenye sanduku la maoni hapa chini.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp