
Kwa nini unapaswa kuanzisha blog? Kama limekuwa ni swali ambalo umekuwa ukijiuliza kwa muda mrefu, basi nikuhakikishie kuwa, makala hii ni kwa ajili yako. Katika makala hii, nitakushirikisha faida 10 usizozifahamu za kuanzisha blog yako.
Kabla ya kuendelea kwenye faida za kuanzisha blog, hebu kwanza nizungumzie maana ya blog pamoja na aina zake.
Maana ya blog.
Kwa tafsiri rahisi, blog ni aina ya tovuti. Aina hii ya tovuti inakuwa na vitu vifuatavyo:
i. Makala: Blog inakuwa na makala ambazo zinaandikwa mara kwa mara. Kila makala moja inapoandikwa inakuwa juu ya makala ya zamani. Kwa mfano, kama uliandika makala juzi na jana, makala ya juzi itakuwa chini ya makala ya jana. Mfano mzuri wa blog ni hii uliyopo kwa sasa.
ii. Sehemu ya kuweka maoni: Kila makala inapowekwa kwenye blog, kwa chini yake huwa kunakuwa na sehemu ya kuweka maoni. Hivyo, kama msomaji atakuwa amepata swali au maoni yoyote kuhusiana na makala husika, ataweza kuweka maoni yake kwenye sehemu ya kuwekea maoni.
iii. Maktaba: Hii ni sehemu ambayo makala zote za blog zilizowahi kuandikwa huhifadhiwa.
Aina za Blog.
Kuna aina nyingi sana za blog na nitakutajia aina chache tu kama ifuatavyo:
i. Blog binafsi (Personal blog)
Hizi ni blog ambazo huanzishwa na watu binafsi ili kuelezea mambo yao binafsi ya ki-maisha.
ii. Blog za biashara.
Hizi ni blog ambazo huanzishwa na watu au wafanyabiashara ili kutangaza bidhaa au huduma zao na kuweza kuwasiliana na wateja wao.
iii. Blog za kitaalamu.
Hizi ni blog ambazo huanzishwa na watu ambao ni wataalamu wa fani fulani ili kuweza kutoa elimu kutokana na utaalamu wao. Kwa mfano, kuna blog za kilimo, afya, elimu, mapambo, mapishi, mitindo na kadhalika.
iv. Blog za habari.
Hizi ni blog zinazotoa habari na matukio yanayotokea kila siku. Mfano blog ya Milladayo.
v. Blog za Burudani.
Hizi ni blog zinazoandika habari za michezo na burudani. Mfano blog ya Salehe Jembe.
Faida 10 Za kuanzisha Blog.
Kuna faida nyingi sana za wewe kuanzisha blog. Miongoni mwa faida hizo ni hizi zifuatazo:
1. Blog itakujengea ujasiri na kufahamika.
Ukiwa na blog utaweza kufahamina na watu wengi na hivyo kukuza jina lako. Kutokana na kukuza jina lako, utakuwa na followers wengi. Hivyo, ukihitaji kuuza bidhaa au huduma, tayari utakuwa na mtaji wa watu wengi wanaokufahamu.
2. Kupata watembeleaji wengi (Traffic) kwenye bidhaa au huduma unayotoa.
Kama utakuwa unauza bidhaa au unatoa huduma mtandaoni, unapokuwa na blog na ukawa unaandika makala mbalimbali za kuelimisha, utapata watembeleaji wengi kwenye blog yako na hivyo utaweza kuwauzia bidhaa au huduma unayotoa.
3. Kuongeza wigo wa marafiki (Network)
Unapokuwa na blog, utaweza kufahamiana na watu wengi kutokana na makala unazoandika na hivyo kuweza kukuza mtandao wa marafiki.
4. Kuongeza Mauzo (Sales)
Pamoja na kufahamiana na kuongeza mtandao wa marafiki, makala unazoandika zitakufanya uaminike (Trust) na kukujengea heshima (credibility) mambo ambayo ni ya msingi katika kuongeza mauzo ya bidhaa au huduma unayotoa.
5. Kujifunza zaidi.
Ili uweze kuandika makala mara kwa mara, utatakiwa kujifunza zaidi. Hivyo, kwa kuwa na blog, itakufanya uweze kujifunza kila siku mambo mapya kutokana na mada unayoandikia kwenye blog yako.
6. Kuibadilisha jamii kwa kufanya vitu vya tofauti.
Kama una maarifa ambayo ufikiria ukiyatoa kwa jamii yako yataleta mabadiliko, basi, kwa kutumia blog utaweza kuielimisha jamii yako na jamii itakupenda na kukuheshimu.
7. Utaweza kuwasaidia watu.
Kama una ujuzi wowote ambao inawezekana ni wa kujifunza au umesoma chuoni, kwa nini usiwashirikishe watu ujuzi ulionao? Kwa kutumia blog, utaweza kuwashirikisha watu ujuzi wako nao watakupenda na kukuheshimu.
8. Utaweza kutangaza biashara yako.
Kama una bidhaa au huduma yoyote, blog ni sehemu nzuri sana ya kuweza kutangaza biashara yako.
9. Jamii itakutambua kuwa wewe ni mtaalamu (Expart)
Unapokuwa na blog, utaweza kuelimisha jamii ujuzi ulionao. Hivyo, jamii itakueshimu na kukutambua kuwa wewe ni mtaalamu wa fani au ujuzi huo.
10. Utatengeneza pesa.
Unapokuwa na blog na blog yako ikawa na watembeleaji wengi, utaweza kutengeneza pesa. Katika kutengeneza pesa, kuna njia nyingi ambazo unaweza kuzitumia. Njia hizo zimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni:
i. Njia za moja kwa moja (Direct methods)
ii. Njia zisizo za moja kwa moja (Indirect method)
i. Njia za moja kwa moja ni (Direct methods)
Njia za moja kwa moja ni njia ambazo utapata kipato moja kwa moja kutoka kwenye blog yako. Ingawa njia hizi sikupendekezei uzitumie kwenye blog yako kwani ili uweze kupata kipato kupitia njia hizi, ni lazima blog yako iwe na watembeleaji wengi. Mojawapo ya njia hizo ni:
-Kuweka matangazo ya biashara kwenye blog yako (Advertisements)
-Kupata makampuni yatakayodhamini blog yako.
Undani wa njia hizi nimeuelezea kwenye makala yangu ya njia za kutengeneza kipato kupitia blog.
ii. Njia zisizokuwa za moja kwa moja (Indirect methods)
Hizi ndio njia ambazo ninakushauri uzitumie, kwani zitakupatia kipato kikubwa hata kama blog yako itakuwa na watembeleaji wachache. Njia hizo ni pamoja na:
–Kuandika na kuuza vitabu pepe (ebooks) kutokana na makala unazoandika.
–Kuandaa kozi za mtandaoni kutokana na mada unazoandika na kuziuza kwa wasomaji wako.
-Kutoa huduma za kitaalamu za kulipia kwa wasomaji wako.
-Kuuza bidhaa zako zingine kwa wasomaji wa blog yako.
Njia hizi zote, nimezielezea kwa kina kwenye makala yangu ya njia za kutengeneza kipato kupitia blog.
Pia kama unahitaji kujifunza kutengeneza blog yako wewe mwenyewe, unaweza kupitia makala yangu ya jinsi ya kuanzisha blog, ambapo nimeelezea kwa kina na kwa lugha rahisi, jinsi ambavyo utaweza kuanzisha blog yako wewe mwenyewe. Lakini pia kama utahitaji huduma ya kutengenezewa blog, basi unaweza ukawasiliana nami kwa simu no. 0752 081669.
Ni matumaini yangu, kuwa umepata maarifa ya kutosha kuhusiana na faida za kuanzisha blog yako. Kama una swali au maoni, usisite kuandika hapo chini. Pia unaweza kuwasiliana nami moja kwa moja kwa kutumia na. 0752 081669. Asante na karibu tena kwenye makala zijazo.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024
2 Replies to “Faida 10 Usizozijua Za Kuanzisha Blog Yako.”