
Tangu mwaka 2006, wakati Google iliponunua YouTube, jukwaa la video limeendelea kuwa maarufu. Leo hii, sio tu kwamba ni injini ya utafutaji ya pili kwa ukubwa baada ya Google, lakini pia ni tovuti ya tatu inayotembelewa zaidi mtandaoni. Hii imeleta fursa mpya na za kusisimua kwa wamiliki wa biashara ambao wanataka kuwafikia watazamaji na wateja wengi zaidi. Katika makala ya leo nitakushirikisha sifa 6 ambazo chaneli yako ya YouTube lazima iwe nazo ili uweze kufanikiwa.
Sifa 6 Channel Yako ya YouTube Lazima Iwe Nazo Ili Uweze Kufanikiwa.
1.Kuwa na ratiba maalumu ya kuweka video.
Channel ya YouTube yenye mafanikio zaidi, huweka video mpya kila siku au hata mara mbili kwa siku. Kwa aina hii ya kuweka video mara kwa mara, wafuasi wake daima huwa wanakumbushwa juu ya channel hiyo na wanapewa nafasi zaidi ya kuwasiliana na kampuni. Hivyo unahitajika kuwa na ratiba maalumu ya kuweka video mpya kwenye chaneli yako. Ikiwa hauna wakati wa kuandaa video kila siku, basi unahitajika kuweka video mpya angalau mara moja kwa wiki.
2.Jitofautishe.
Ikiwa unataka channel yako iwe na mafanikio, basi unahitajika kufanya kitu cha kipekee ambacho kitakufanya uwe tofauti na wengine. Kwa mfano, ikiwa una channel ya kilimo, kuandaa video zinazofundisha kilimo peke yake haitoshi kukufanya uwe tofauti na wengine. Unaweza kujitofautisha zaidi kwa kubobea kwenye aina fulani ya mazao kwa mfano mbogamboga na matunda. Kwa kufanya hivyo utakuwa umejitofautisha na chaneli zingine.
3.Ubora wa maudhui yako ni muhimu sana katika mafanikio yako kwenye YouTube.
Ikiwa maudhui yako hayana umahiri, watazamaji hawatakuchukulia kwa uzito kuangalia video zako. Hii hasa ni muhimu ikiwa unajaribu kuanzisha akaunti ya YouTube kwa ajili ya biashara yako. Unatakiwa kuhakikisha kuwa vifaa unavyotumia ni vya ubora wa juu, iwe ni simu yako ya mkononi inayoweza kurekodi video za HD na 4K au kamera ya video ya HD yenye gharama nafuu.
4.Jumuisha Bidhaa Zako Katika Video Zako.
Sababu kuu kwa nini biashara nyingi zinageukia YouTube ni kuongeza njia nyingine ya masoko ambayo itasaidia biashara zao kukua. Mojawapo ya njia za msingi za kufanya hivyo ni kwa kutangaza bidhaa zako katika video zako. Tafuta njia ya kufanya bidhaa zako kuwa sehemu muhimu ya maudhui yako ya video.
5.Maudhui yanapaswa kulenga kundi fulani la jamii.
YouTube imekuwa maarufu kimataifa, hivyo unahitajika kuzingatia hadhira gani unayolenga watazame video zako. Ikiwa Kiingereza siyo lugha yako ya asili, usisumbuke, jikite kwenye lugha inayotumika katika biashara yako na jamii unayolenga na hivyo utaweza kufanya vyema sana kwenye jukwaa hilo.
6.Weka burudani kwenye video zako.
Sehemu kubwa ya chaneli za YouTube zilizofanikiwa zimegundua njia ya kuunganisha aina fulani ya burudani katika maudhui yao. Maudhui yoyote unayoandaa kupitia video zako, jitahidi kuchanganya na burudani ili watu wafurahie kuangalia video zako mwanzo hadi mwisho.
Ni matumaini yangu umejifunza maarifa ya kutosha ambayo yatakusaidia kukuza chaneli yako ya YouTube. Kama una maoni au swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante, karibu katika makala zinazofuata.