
Mfumo wetu wa elimu huwa unatufundisha aina mbili za elimu: Aina ya kwanza ni elimu ya kujua kusoma, kuandika na kuhesabu (scholastic education). Hii ni elimu ambayo inakuwezesha kujua jinsi ya kusoma, kuandika na kuhesabu. Aina ya pili ya elimu ni elimu ya ujuzi (professional education). Aina hii ya elimu ndiyo inayozalisha wataalamu mbalimbali kama vile madaktari, walimu, wahandishi na kadhalika. Kuna aina ya tatu ya elimu ambayo haifundishwi darasani, nayo ni elimu ya msingi kuhusu fedha (financial education). Hii ni elimu inayokuwezesha kufahamu jinsi ya kutengeneza kipato, jinsi ya kutumia pesa yako na jinsi ya kuwekeza pesa yako. Katika Makala ya leo nitakushirikisha aina hii ya tatu ya elimu na nitazungumzia jinsi ya kutengeneza kipato endelevu kinachokua kila siku (Passive income).
Jinsi ya kutengeneza kipato endelevu kinachokua kila siku.
Kwanza kabisa, ili uweze kufahamu jinsi ya kutengeneza kipato ambacho kitakuwa kinakuwa kila siku na endelevu, ni lazima nianze kwanza kuelezea aina ya vipato. Watu wote wanaofanya kazi duniani na kupata kipato, vipato vyao vimegawanyika sehemu kuu tatu: aina hizi za vipato ni active income, portfolio income na passive income. Nitaelezea kila aina ya vipato.
Aina za vipato:
1. Active income.
Hii ni aina ya kipato ambayo inakutaka wewe uwe mahali pa kazi, ufanye kazi ndio ulipwe. Hii inajumuisha watu walioajiriwa ambao wanalipwa baada ya kuwa wamefanya kazi. Maana yake ni kuwa, kama hakufanya kazi hawawezi kulipwa. Pia inajumuisha watu waliojiajiri ambao ni lazima waende kwenye maeneo yao ya kazi, wafanye kazi ndio waweze kupata kipato. Kwa lugha rahisi ni kuwa, active income ni aina ya kipato ambayo unalipwa tu pale unapokuwa umefanya kazi. Kama hukufanya kazi huwezi kulipwa.
2. Portfolio income
Hii ni aina ya kipato inayopatikana mtu anapoamua kuwekeza pesa yake kwenye maeneo ambayo itaongezeka thamani kama vile kuwekeza kwenye kununua hisa, kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja na kuwekeza kwenye hatifungani. Kwa ligha rahisi ni kuwa, unawekeza pesa yako kwenye maeneo ambayo baadaye utapata faida.
3. Passive income.
Hii ni aina ya kipato ambayo inapatikana bila ya ulazima wa wewe kuwepo mahali pa kazi. Biashara yako inakuwa inajiendesha yenyewe bila ya wewe kufanya kazi. Kwa mfano: unapokuwa umeamua kuandika kitabu na ukamaliza, basi kitabu hicho utakiuza maisha yako yote. Kazi kubwa utaifanya mwanzoni tu wakati wa kuandika. Lakini baada tu ya kumaliza kuandika kazi yako itakuwa ni kuuza tu. Hivyo kitabu chako kinakuwa ni chanzo cha kukupatia kipato kikubwa na endelevu (passive income). Mfano mwingine ni unapokuwa umeandaa kozi yako na ukaiweka mtandaoni. Kazi yako kubwa itakuwa tu mwanzoni wakati wa kuandaa kozi yako lakini ukishamaliza, basi inakuwa ni chanzo cha kukupatia kipato endelevu bila ya ulazima wa wewe kufanya kazi nyingine ya ziada. Lakini pia unaweza kuandaa video zako za mafunzo na ukaziweka YouTube. Baada ya kuwa umepata wafuasi wa kutosha na video zako zikawa na watazamaji wengi, basi unaweza kutengeneza kipato endelevu (passive income) kwani YouTube itakuwa inakulipa kupitia matangazo yake ambayo itayaweka kwenye video zako.
Kama njia yako ya kutengeneza kipato ni ile ya kwanza (active income) basi unaweza kuifanya lakini uwe na malengo ya kuandaa njia nyingine ambayo itakusaidia kupata kipato endelevu ambacho hakitakulazimu kufanya kazi (passive income). Hii ni kwa sababu, kadiri unavyoendelea kufanya kazi, nguvu zako zinaendelea kupungua hivyo ni muhimu kuwa na njia ya kutengeneza kipato ambayo hakitakulazimu kufanya kazi.
Kwa leo niishie hapo. Ni matumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kutosha ya jinsi ya kutengeneza kipato kinachokua kila siku. Kama una maoni au swali, usisite kuweka maoni yako hapo chini. Pia kwa ushauri wowote usisite kuwasiliana nami moja kwa moja kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu katika Makala zinazokuja.