Kusudi lako kuu maishani ni jambo ambalo unapaswa kulijua na hivyo kupanga malengo pamoja na kufanya shughuli zako kwa kuzingatia kutimiza kusudi lako. Brian Tracy, mtaalamu wa maendeleo binafsi aliwahi kusema kuwa, “Umewekwa kwenye hii dunia ili uweze kutimiza jambo kubwa, zuri na la kushangaza kupitia maisha yako. Kazi yako ni kugundua ni jambo gani hilo na kisha ulifanye kwa moyo wako wote, ili uache urithi kwa vizazi vijavyo.”
Lakini mara nyingi, watu wengi huishi maisha yao yote bila kutumia uwezo wao au kuziishi ndoto zao. Badala ya kuishi kusudi lao la kweli maishani, wanaishi maisha ya kubahatisha, ambayo yanasukumwa na shinikizo, watu wengine, na majukumu ya kila siku ambayo yako mbali sana na kile wanachotaka hasa maishani. Katika makala hii nitakushirikisha Jinsi ya Kutambua Kusudi la Maisha Yako.
Jinsi ya Kutambua Kusudi la Maisha Yako.
Ili uweze kutambua kusudi la maisha yako, jiulize maswali haya manne muhimu kwa uaminifu kadri uwezavyo.
Swali la Kwanza: Malengo Yangu Ya Maisha Ni Yapi?
Unapopita katika maisha, utapitia hatua nyingi tofauti. Ni muhimu kuwa na lengo lililo wazi la kile unachotaka kufanikisha katika kila hatua, na hasa katika kila kipengele cha maisha yako kama vile familia, mahusiano, kazi, uchumi, burudani na kadhalika. Kuwa na uwazi kuhusu kile unachotaka kufanikisha katika maeneo haya kutakuruhusu kupanga maisha yako kwa namna ya kufanikisha malengo hayo. Hii itakusaidia kuweka lengo kubwa na kisha kuligawanya na kuwa hatua ndogo ndogo za kuchukua ili kufanikisha lengo hilo. Hili ni swali la kwanza unalopaswa kulijibu unapokuwa unataka kutambua kusudi la maisha yako.
Swali la Pili: Kwa Nini Nipo Hapa?
Uwezekano wa wewe kuzaliwa ni 1 kati ya trilioni 400. Unapoangalia namba hiyo, ni uwezekano adimu sana, lakini umezaliwa. Uko kwenye sayari hii kwa sababu maalumu na kila mtu ana sababu tofauti. Je, ni kwa ajili ya kutunza familia yako? Je, ni kwa ajili ya kuunda kitu cha ajabu ambacho dunia inakihitaji? Je, umewekwa hapa duniani ili kuanzisha na kukuza biashara? Au ni ili kufurahia kadri uwezavyo kile kilichopo kwenye sayari hii? Ili kujibu swali hili, orodhesha sababu na njia zote unazodhani unahitajiwa kufanya maishani mwako ili kutimiza kusudi la maisha yako.
Swali la Tatu: Ninataka Nini Hasa Maishani?
Sasa kwa kuwa umejua malengo yako na kwa nini uko hapa, hatua inayofuata ni kufafanua kile unachotamani kuwa au kuwa nacho. Kusudi lako linapaswa kuendana na kile unachofurahia kufanya zaidi muda wako mwingi. Haina maana kutumia muda wako wa thamani, nguvu, na juhudi kwa kitu usichokipenda. Ndiyo maana ni muhimu sana kugundua kile unachotaka kufanya maishani na jinsi unavyotakiwa kutumia muda wako ili kubaini kusudi la maisha yako.
Swali la Nne: Ninaenda Wapi na Mafanikio ni Nini Kwangu?
Sasa kwa kuwa una wazo wazi la kile unachotaka maishani na una kusudi lililofafanuliwa vyema, sasa ni wakati wa kuchora njia ya unakoenda. Ili kufanya hivyo, unahitajika kuangalia mbele kwa siku zijazo na kufikiria jinsi unavyofikiri maisha yenye mafanikio yanavyoonekana kwako. Ili kukusaidia kufanya hivyo, fikiria jinsi maisha yako kamili yangekuwa baada ya miaka 3-5. Yatakuwa tofauti vipi na leo? Mara tu unapokuwa na wazo wazi kuhusu maswali haya muhimu, basi ni wakati wa kufanya kazi kwa nguvu ili uweze kutimiza malengo yako.
Unapoanza kufanya kazi kutimiza maono hayo, utagundua polepole hatua unazohitajika kuchukua kuanzia leo ili kujenga maisha ambayo yanakidhi kusudi lako la maisha. Haya ni maswali unayohitajika kujiuliza na hatua unazohitajika kuchukua ili kutengeneza maisha yako kamili. Siyo kazi rahisi, lakini kwa kupitia maswali haya muhimu, utaweza kufafanua kusudi la maisha yako.
Sasa, swali la leo ni hili, ni hatua gani umechukua leo kufafanua kusudi la maisha yako? Acha maoni yako hapa chini, na mimi nitahakikisha ninakufuatilia. Asante kwa kufuatilia makala hii. Ikiwa umefurahia makala hii na unahisi imekuwa na thamani katika kukufundisha kuhusu Jinsi ya Kupata Kusudi la Maisha Yako, usisite kuwashirikisha ndugu na marafiki zako.
Kama una maswali au maoni yoyote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
Ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na malengo. Kujiwekea malengo kunaweza kuwa na uzoefu wenye nguvu wa kubadilisha maisha yako ikiwa utafanya kwa usahihi. Katika makala hii nitakushirikisha kanuni tano za msingi za kujiwekea malengo ambazo ni muhimu kwa mafanikio yako makubwa.
Kanuni ya Kwanza: Ulinganifu
Ili uweze kufanya vizuri zaidi katika maisha yako, malengo yako na maadili yako lazima yaendane. Maadili yako yanawakilisha imani yako ya kina kuhusu kile unachoona kuwa ni chema na chenye manufaa na kile unachoona kuwa ni kibaya kwako. Utendaji wako wa juu na mafanikio yako yatategemea tu pale ambapo malengo yako na maadili yako yapo katika upatanifu kamili.
Kanuni ya Pili: Eneo la Ubora
Kila mtu ana uwezo na ni bora katika kitu fulani, na pengine vitu kadhaa. Unaweza kufikia mafanikio makubwa tu kwa kupata eneo lako la ubora na kisha kuweka moyo wako wote katika kukuza vipaji vyako katika eneo hilo. Kwa lugha nyingine eneo la ubora ni kitu kimoja ambacho una uwezo wa kipekee wa kukifanya kwa ubora. Ni jukumu lako kukibaini kitu hicho, ikiwa bado hujakibaini.
Eneo lako la ubora linaweza kubadilika kadri taaluma yako inavyokua, lakini watu wote waliofanikiwa kwa kweli ni wale ambao wamegundua na kuwekeza nguvu zao zote kwenye maeneo yao ya ubora. Eneo lako la ubora mara zote ni kufanya kile unachokifurahia zaidi na kukifanya vizuri. Hivyo, kanuni ya pili ya kujiwekea malengo ni kwa kutambua eneo lako la ubora.
Kanuni ya Tatu: Kanuni ya Shamba la Almasi
Kanuni ya Shamba la Almasi inatokana na jina la hotuba iliyotolewa na mhubiri aitwaye Russell Conwell. Hotuba hiyo ilipendwa sana.
Katika hotuba hiyo alielezea hadithi ya mkulima mmoja mzee wa kiafrika ambaye alifurahia sana siku moja aliposikia kutoka kwa mfanyabiashara aliyesafiri kwenda Afrika kugundua migodi ya almasi na kuwa tajiri sana. Hivyo na yeye aliamua kuuza shamba lake, kuandaa safari, na kuelekea ndani ya Afrika ili kutafuta almasi kwa lengo la kuwa tajiri mkubwa.
Kwa miaka mingi, alisafiri sehemu kubwa ya bara la Afrika akitafuta almasi. Hatimaye, aliishiwa pesa. Mwishoni kabisa, akiwa peke yake, katika hali ya kukata tamaa, alijitupa baharini na kuzama.
Wakati huo huo, ndani ya shamba alilouza, siku moja mkulima mpya alikuwa akinywesha punda katika kijito kilichokatisha shamba hilo. Alipata jiwe la ajabu lililotoa mwanga kwa namna ya kushangaza. Alilipeleka nyumbani kwake na hakuwa anafahamu lolote kuhusiana na jiwe hilo. Baadaye, mfanyabiashara yule yule alipita kwenye shamba lile na yule mkulima mpya akamwonyesha lile jiwe. Mfanyabiashara alifurahi sana na akauliza kama yule mkulima mzee alikuwa amerudi hatimaye. Hapana, aliambiwa. Mkulima mzee hakuwa ameonekana tena tangu aondoke.
Mfanyabiashara alichukua jiwe hilo na kusema, “Hii ni almasi ya thamani kubwa.” Mkulima mpya alikuwa na shaka, lakini mfanyabiashara alisisitiza na akaomba aonyeshwe wapi alipata almasi hiyo. Wakaenda kwenye shamba ambalo mkulima alikuwa akinywesha punda, na walipozunguka, walipata almasi nyingine, na nyingine, na nyingine. Ikabainika kwamba shamba lote lilikuwa limejaa madini ya almasi. Mkulima mzee alikuwa ameenda Afrika kutafuta almasi bila ya kutazama chini ya miguu yake mwenyewe.
Hadithi hii inafundisha kwamba mkulima mzee hakuweza kutambua kwamba almasi hazionekani kama almasi katika hali yake ya asili. Huonekana kama mawe kwa macho yasiyo na elimu. Almasi inapaswa kukatwa, kupigwa msasa, na kung’arishwa kabla haijawa kama ile inayouzwa kwenye maduka ya vito.
Vivyo hivyo, mashamba yako ya almasi pengine yapo chini ya miguu yako mwenyewe. Lakini mara nyingi yamejificha yanahitaji juhudi kuweza kuyagundua. Mashamba yako ya almasi pengine yapo kwenye vipaji vyako, elimu yako, uzoefu wako, tasnia yako, mji wako, mawasiliano yako na kadhalika. Mashamba yako ya almasi yapo chini ya miguu yako mwenyewe na unachotakiwa kufanya ni kuchukua muda kuyatambua na kisha kuyafanyia kazi.
Theodore Roosevelt aliwahi kusema, “Fanya kile unachoweza, kwa kile ulicho nacho, hapo hapo ulipo.” Huna haja ya kuhamia nchi nyingine au kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yako. Mara nyingi, kile unachokitafuta kiko karibu sana na wewe. Lakini hakionekani kama fursa kwa sababu hujatumia muda wako kuchunguza na kufanyia kazi kwa bidii uwezo ulionao.
Kanuni ya Nne: Uwiano
Kanuni ya uwiano inasema kwamba, unahitaji malengo mbalimbali katika maeneo sita muhimu ya maisha ili uweze kufanya vizuri zaidi. Kama vile gurudumu la gari linavyopaswa kuwa na uwiano ili liweze kuzunguka kwa urahisi, unapaswa kuwa na malengo yenye uwiano ili maisha yako yaweze kwenda vizuri.
Unahitajika kuweka malengo katika maeneo yafuatayo: malengo ya kifamilia malengo ya kimwili kiafya. malengo ya kielimu na maendeleo binafsi (self development). malengo ya kazi na taaluma. malengo ya kifedha na mali. Hatimaye, unahitaji malengo ya kiroho,
Ili kudumisha uwiano mzuri, unahitajika kuwa na malengo mawili au matatu katika kila eneo, jumla ya malengo kumi na mawili hadi kumi na nane. Aina hii ya uwiano itakuwezesha kuwa unafanya kazi kila wakati juu ya kitu muhimu kwako. Unapokuwa haufanyi kazi kwenye ajira yako, unaweza kufuatilia malengo ya kifamilia. Unapokuwa haufanyi kazi juu ya afya ya mwili, unaweza kufanya kazi juu ya maendeleo binafsi na kadhalika.Lengo ni kutokupoteza muda wako kwa kufanya vitu ambavyo havipo kwenye malengo yako.
Kanuni ya Tano: Kusudi Kuu la Maisha
Kanuni ya tano ya kujiwekea malengo ni uamuzi wa kusudi kuu la maisha yako. Kusudi lako kuu ni lengo lako nambari moja, lengo ambalo ni muhimu zaidi kwako kuliko lengo lingine lolote kwa wakati huu. Unaweza kuwa na malengo mbalimbali lakini unaweza kuwa na kusudi kuu moja tu. Kukosa kwa mtu kuchagua lengo au kusudi kuu ni sababu kuu ya kutawanya juhudi, kupoteza muda na kushindwa kupiga hatua.
Jinsi ya kuchagua lengo kuu ni kwa kuchanganua malengo yako yote na kujiuliza, “Ni lengo gani, nikilifikia, litanisaidia zaidi katika kufanikisha malengo yangu mengine yote?”
Kwa kawaida, linaweza kuwa ni lengo la kifedha au kibiashara, lakini wakati mwingine linaweza kuwa lengo ni la afya au mahusiano. Uchaguzi wa kusudi lako kuu ndio mwanzo wa mafanikio yako makubwa. Lengo hili linakuwa ndiyo”dhamira” yako na kanuni ya kupanga shughuli zako zingine zote. Unapokuwa na msisimko au hamasa kuhusu kufanikisha lengo kuu lililo wazi, unaanza kusonga mbele haraka licha ya vikwazo na vizingiti vyote ambavyo utakutana navyo.
Kwa kutumia kanuni hizi tano za kujiwekea malengo, unaweza kufanikisha mambo makubwa na kuwa na mabadiliko ya kweli katika maisha yako. Ulinganifu kati ya malengo na maadili yako, kutambua eneo lako la ubora, kugundua mashamba yako ya almasi, kudumisha uwiano katika malengo yako yote, na kuchagua kusudi lako kuu la maisha, ni mambo muhimu yatakayokupeleka kwenye viwango vya juu vya mafanikio. Kumbuka, fursa yako kubwa inaweza kuwa karibu zaidi kuliko unavyofikiria, na mara nyingi inahitaji kazi ngumu na kujitolea ili uweze kuitambua na kuifanikisha.
Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa yatakayo kusaidia kuwa na kanuni za kujiwekea malengo. Kama una maoni au swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
Mafanikio katika maisha yanatokana na tabia tulizozijenga na ambazo tunaishi nazo kila siku. Katika kusoma kwangu vitabu vya maendeleo binafsi (self development) niligundua kwamba ukiwasoma watu waliofanikiwa, unaanza kufundishwa misingi ya mafanikio. Ukiifuata misingi hii iliyothibitishwa ya mafanikio, na ukafanya kile ambacho wanaume na wanawake waliofanikiwa wamefanya katika historia, nawe pia utafanikiwa. Ugunduzi huu umenipa faida kubwa na ningependa kushiriki na wewe kuhusu baadhi ya misingi niliyogundua katika kusoma kwangu vitabu. Katika makala hii nitakushirikisha tabia kumi za mafanikio kutoka kwa watu waliofanikiwa.
Tabia Kumi za Mafanikio
Sifa hizi kumi ni tabia za kimaadili na hakuna mtu anayezaliwa nazo. Unaweza kujifunza na kuzikuza kwa kuzifanyia mazoezi. Ikiwa utazifanyia mazoezi hadi ziwe tabia yako, hakuna kitu kitakachokuzuia kufanikiwa.
1.Uwazi (Clarity)
Sifa ya kwanza ni uwazi. Uwazi ni sehemu muhimu ya mafanikio. Inamaanisha kuwa na uwazi kwenye malengo yako kwa kutambua hasa kile unachotaka kuwa nacho au kufanya maishani. Watu waliofanikiwa wana uwazi kuhusu wanakoenda na kile wanachotaka kufanikisha. Kwa upande mwingine, watu wasiofanikiwa mara nyingi hawana mwelekeo wowote.
Umuhimu wa Uwazi
Uwazi ni muhimu katika kufanikisha malengo yako. Lazima uwe wazi kuhusu kile unachotaka na unachohitajika kukifanya ili kukipata. Uwe wazi katika mazungumzo yako, vitendo vyako, na maono yako. Uwazi hujenga msingi wa mafanikio.
2.Maamuzi (Decisiveness)
Tabia ya pili ni kuwa na maamuzi thabiti. Uamuzi ni muhimu sana. Watu waliofanikiwa ni wale ambao wanaweza kufanya maamuzi kwa haraka na kwa ujasiri. Hofu ya kufanya makosa mara nyingi inafanya watu wawe na mashaka na wasiweze kufanya maamuzi, na hivyo kushindwa. Kamwe sijawahi kukutana na mtu aliyefanikiwa ambaye hana maamuzi na sijawahi kukutana na mtu aliyeshindwa ambaye ana maamuzi. Kuwa na maamuzi thabiti ni muhimu.
3.Kuwa na Maono (Vision)
Kwa kuongezea, ni muhimu kuwa na maono na ndoto kwa ajili ya maisha yako. Maono yanakupa mwelekeo na kusudi la maisha yako. Watu wote waliofanikiwa wamekuwa na ndoto kubwa ambazo zimewapa motisha ya kufanikisha mambo makubwa. Wote waliofanikiwa na wenye ushawishi mkubwa katika historia walikuwa na ndoto.
4.Kujituma kwa Matokeo
Unapaswa kuelekeza jitihada zako kwenye matokeo, sio shughuli. Watu waliofanikiwa wanazingatia matokeo, wakati wale wasiofanikiwa wanazingatia shughuli. Kwa wale wanaotaka kufikia kilele cha utendaji, ni muhimu kujikita kwenye matokeo na siyo matendo tu. Watu walio na utendaji wa juu wanajikita kwenye matokeo wanayotaka kufanikisha badala ya shughuli zisizo na tija.
Ben Trigo, mtaalamu wa mikakati, alisema kuwa jambo baya zaidi ni kufanya kwa ufanisi kile ambacho hakihitaji kufanywa kabisa. Watu wengi hufanya kazi kwa bidii katika mambo yasiyo na umuhimu wowote kwa mafanikio yao.
Maswali Muhimu
Katika kazi yako, ni muhimu kujiuliza maswali muhimu kama, “Ni matokeo gani yanatarajiwa kutoka kwangu?” na “Kwa nini nipo kwenye orodha ya malipo?” Kujibu maswali haya kutakusaidia kujikita kwenye kazi ambazo zitaleta mafanikio.
5.Nidhamu: Kufanya Kilicho Kigumu na Muhimu
Ni vigumu kufikiria kuwa mtu mwenye mafanikio bila kuwa na nidhamu. Mara nyingi huwa tunachagua kufanya kitu kilicho rahisi na cha kujifurahisha leo badala ya kile kilicho kigumu na muhimu. Hii husababisha mzigo mkubwa baadaye maishani. Uwezo wa kujidhibiti, kuwa na uwazi kuhusu unachotaka, na kujikita kwenye matokeo unayotaka ni muhimu sana kwa mafanikio. Watu waliofanikiwa huwa na nidhamu sana kwenye malengo yao.
6.Kuandika Malengo: Hatua ya Kwanza ya Mafanikio
Kuandika malengo yako kila asubuhi kwa nafsi ya kwanza kana kwamba tayari umeyafanikisha ni muhimu. Ikiwa lengo lako ni kupata milioni 50 kwa mwaka, kila asubuhi andika, “Napata milioni 50 kwa mwaka.” Hii itachukua dakika mbili hadi tano tu.
Kuangalia Maendeleo Yako Kila Jioni
Kila jioni, kabla ya kuangalia televisheni, tumia dakika tano hadi kumi kutathmini maendeleo yako ya siku. Jiulize, “Nimefanya nini kilicho sahihi leo?” na “Ningefanya nini tofauti kama ningekuwa na nafasi ya kuirudia siku hii?” Kujiuliza maswali haya kila siku kwa siku 30 kutaongeza ufanisi wako zaidi ya miezi sita iliyopita. Watu waliofanikiwa huwa wanakuwa na muda wa kutathmini utendaji wao.
Sheria ya Uvutaji: Kuvutia Kile Unachofikiria
Kuandika malengo yako kila siku husaidia kuyaingiza kwenye akili yako ya ndani. Jambo hili linaunda nguvu ya uvutaji inayovutia watu na mazingira yanayohusiana na malengo yako. Hii inaitwa sheria ya uvutaji. Watu wengi wameona kuwa wanapoanza kuzingatia jambo fulani, huwa wanapata fursa za kujifunza na kuendeleza jambo hilo.
7.Ujuzi na Umahiri: Njia ya Mafanikio
Kuwa na ujuzi na umahiri ni muhimu sana kwa mafanikio yako. Watu wote wenye mafanikio walijitolea kuwa bora katika fani zao. Umahiri unahitaji kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa, kuhudhuria semina na kusoma vitabu vinavyohusiana na fani yako.
Sheria ya 80/20
Sheria ya Pareto inasema kwamba, asilimia 20 ya watu hufanya asilimia 80 ya kazi. Hii inaonyesha kuwa watu walio bora zaidi huingiza kipato mara 16 zaidi ya wastani wa watu wengine. Hii ina maanisha kwamba, mafanikio yanatokana na kujitolea kuwa bora zaidi katika kile unachofanya.
Fursa za Kuwa Bora
Ubora hutoa fursa kwa sababu unapokuwa mzuri, unafungua bahari ya fursa mbele yako. Unapokuwa bora, unapata umakini wa watu, na watu wanakutafuta na kukupa majukumu zaidi na fursa zaidi. Watu wanapenda kununua kutoka kwa wauzaji bora katika fani zao.
8.Kujisikia Kufanikiwa
Utafurahia tu kufanya kazi ikiwa unafanya vizuri. Wakati tunapofanya jambo vizuri, linatupa hisia ya kujiheshimu na kujivunia. Tunajisikia washindi. Hivyo, ili uweze kufanikiwa unapaswa kuwa na hisia za ndani za kufanikiwa.
9.Uwezo wa Kuzingatia
Uwezo wa kuzingatia na umakini ni funguo mbili za mafanikio katika maisha. Uwezo wa kuzingatia kwa kujua hasa unachotaka kufanikisha na uwezo unaohitajika ili kufanikiwa ni funguo za mafanikio. Ili uweze kufanikiwa kwenye malengo yako unapaswa kukaa chini na kuangalia kazi zako kwa kutumia sheria ya 80/20. Watu waliofanikiwa huzingatia sana malengo yao.
Jiulize, ni mambo gani ambayo ni asilimia 20 ya mambo yangu yote ambayo nahitajika kuyafanya ambayo yataongeza asilimia 80 ya thamani ya kazi yangu? Na kila wakati fanya kazi kwenye asilimia 20 kwa ubora zaidi. Katika maisha, kamwe hakuna muda wa kufanya kila kitu lakini kuna muda wa kutosha kufanya mambo muhimu. Badala ya kufanya kile kilicho rahisi na cha kufurahisha, ambacho ndio watu wengi hufanya, jiepushe na ufanye mambo umuhimu.
Usimamizi wa Muda
Usimamizi wa muda ni usimamizi wa maisha. Unaweza kufanya chochote unachotaka kwenye maisha yako ikiwa utasimamia muda wako vizuri. Sisi sote tuna masaa 24 sawa kwa siku, na uwezo wa kujidhibiti na uvumilivu wa kuzingatia jambo moja kwa wakati ni sifa ya mafanikio yote.
10.Haraka na Ufanisi
Jenga hisia ya haraka. Hisia ya haraka ni sifa inayomilikiwa na asilimia mbili tu ya watu. Asilimia mbili ya watu hufanya mambo haraka. Katika kitabu kilichoandikwa na Tom Peters cha In Search of Excellence anasema kuwa, kampuni zote bora zimepata sifa hiyo kwa sababu hufanya kazi zao kwa haraka na kwa ufanisi na hivyo kuzipita kampuni zote ambazo hufanya mambo polepole.
Jenga sifa ya kuwa mtu anayefanya mambo haraka. Ikiwa unamiliki kampuni na una wafanyakazi wawili wenye talanta sawa, lakini mmoja ana hisia ya haraka na anafanya mambo kwa kasi, ni yupi utamwongezea majukumu? Ni yupi utampandisha cheo? Ni yupi utamtuma kwenye mafunzo? Watu wengi huendesha maisha yao kwa mwendo wa polepole. Wanajishughulisha tu pale wanapojisikia kufanya hivyo. Lakini watu wote bora, wale wanaofanya vizuri sana, wana hali ya kufanya mambo kwa haraka.
Kuwa na Hisia ya Dharura
Watu wenye mafanikio makubwa wana hisia ya dharura katika kila wanachofanya. Wanajua kuwa muda ni mali na hawapotezi muda wao kwa vitu visivyo na maana. Badala yake, wanajitahidi kukamilisha majukumu yao kwa haraka na kwa ufanisi.
Kukamilisha Kila Kazi Unayoianza
Na hatimaye, kamilisha kila kazi unayoianza. Chukua jukumu na uendelee nalo hadi liwe limekamilika kwa asilimia 100. Hii ni muhimu kwa sababu kazi ambayo haijakamilika inaacha pengo na inaweza kukuvuruga katika majukumu mengine. Kwa hiyo, hakikisha kuwa kazi zote unazoanza unazikamilisha kikamilifu.
Nimatumaini yangu kuwa umenufaika na makala hii ya tabia kumi za mafanikio kutoka kwa watu waliofanikiwa. Kama una swali lolote au maoni usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
Mwaka huu ni wakati muafaka na mzuri wa kuweka maazimio na malengo ambayo yatakusaidia kufanikisha mambo mengi katika maisha yako. Je, unahitaji motisha kidogo kufanikisha malengo hayo? Soma na rudia nukuu hizi za motisha kutoka kwa watu 10 ambao wanajua siri ya kufanikisha mipango mikubwa.
Ndoto Zetu Zote Zinaweza Kutimia Tukipata Ujasiri wa Kuzifuatilia – Walt Disney
Hakuna ndoto ambayo haiwezi kufikiwa, mradi tu uchukue hatua na kwa ujasiri kufuatilia ndoto yako.
Kila Kitu Ulichowahi Kutamani Kiko Upande wa Pili wa Hofu – George Adair
Unahisi wasiwasi kuhusu maazimio yako? Shinda hofu hiyo ili upate unachotaka.
Mafanikio ni Kupata Unachotaka, Furaha ni Kutaka Unachopata – W.P. Kinsella
Mafanikio na furaha haviji pamoja kiotomatiki. Tafuta kile ambacho unataka kweli na kile kitakachokufanya uwe na furaha na kuridhika.
Fikiria Kila Mara Kuhusu Unachotaka, Sio Vitu Unavyoviogopa – Brian Tracy
Usitoe nafasi yoyote ya mawazo kwa vitu unavyoviogopa. Badala yake, zingatia tu kile unachokifanyia kazi.
Mafanikio Hayako Katika Kutokufanya Makosa, Bali Katika Kutojirudia Makosa Mara ya Pili – George Bernard Shaw
Ni sawa kufanya makosa. Jifunze kutokana na makosa yako na songa mbele.
Mahali Pekee Ambapo Mafanikio Yako Kabla ya Kazi ni Katika Kamusi – Vidal Sassoon
Huwezi kutarajia kufanikiwa bila kuweka bidii.
Furaha Sio Kitu Kilichotengenezwa Tayari. Inatokana na Matendo Yako Mwenyewe – Dalai Lama
Tengeneza furaha yako mwenyewe kwa kuweka maazimio ya mwaka mpya na kisha kufanyia kazi kwa nguvu zako zote.
Nashukuru kwa Wale Wote Waliosema Hapana Kwangu. Ni Kwa Sababu yao Nafanya Mwenyewe – Albert Einstein
Kukataliwa ni kugumu, lakini pia kunaweza kuwa kichocheo cha kukutia moyo kufuatilia ndoto zako.
Usikose Ujasiri na Kusitasita Kuhusu Matendo Yako. Maisha Yote ni Jaribio – Ralph Waldo Emerson
Ni sawa kuweka maazimio, kujaribu, kufanya makosa na kuchukua hatua hata kama hujui matokeo yatakuwa nini. Hivyo ndivyo tunavyojifunza, na itakusaidia kukaribia lengo lako.
Jenga Tabia ya Kushukuru Mwaka Huu, na Toa Shukrani kwa Kila Kinachotokea – Brian Tracy
Hakuna kitu kinachopotea. Kila uzoefu ulionao mwaka huu utakuwa kitu unachoweza kukitumia, na ukichukua hatua kila mara, hatimaye utafanikisha lengo lako.
Swali la leo ni: ipi kati ya nukuu hizi inayokugusa zaidi? na kwa nini? Acha maoni yako hapa chini, nami nitahakikisha ninakufuatilia. Asante kwa kufuatilia makala hii ya Nukuu 10 za Kukuongoza Kufanikisha Maazimio Yako. kama una swali au maoni yoyote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
Ili uweze kufanikiwa katika maisha, ni lazima ufahamu jinsi ya kuitumia siku yako vizuri. Kila mtu amepewa sawa siku yenye masaa 24. Tofauti ya watu wenye mafanikio na ambao hawajafanikiwa inatokana na jinsi wanavyotumia masaa ya siku. Unaopanza asubuhi siku yako vizuri, unafungua milango ya mafanikio. Hii ndiyo sababu waswahili wanasema kuwa, nyota njema huonekana asubuhi. Saa chache za kwanza za siku ni muhimu sana kuliko saa nyingine zozote za siku. Mmoja wa wanafikra wakuu alisema kwamba saa ya kwanza ni usukani wa siku. Katika makala ya hii nitakushirikisha ratiba za asubuhi za watu wenye mafanikio.
Umuhimu wa Saa za Asubuhi
Saa za asubuhi, unapamka tu, zinaweka mwelekeo wa siku yako yote, zikiathiri mawazo yako na uzalishaji wako katika masaa yote yanayofuata. Umuhimu wa saa hizi za asubuhi ndio sababu baadhi ya watu wenye mafanikio makubwa duniani huweka kwa umakini taratibu za asubuhi ambazo zinalenga kuwasaidia kuanza siku vizuri na kutumia masaa yanayofuata kwa ufanisi mkubwa.
Jinsi ya Kuanza Siku Vizuri.
1.Panga Siku Yako Usiku Mmoja Kabla.
Ikiwa ungependa kuanza kila siku kwa njia bora zaidi iwezekanavyo, zingatia kutekeleza baadhi ya taratibu hizi zilizothibitishwa za asubuhi kwenye ratiba yako ya asubuhi. Kwanza, panga siku yako usiku mmoja kabla. Kuandaa siku yako usiku mmoja kabla inaweza kuwa si sehemu ya taratibu za asubuhi, lakini ni njia nzuri ya kuanza siku yako vizuri.
Kwa kupanga kile unachotaka kukamilisha usiku kabla, unaweza kuanza kila siku ukiwa na mpango kichwani badala ya kuamka bila kujua unachotaka kufanya. Panga ratiba yako ya asubuhi pamoja na kile unachotaka kufanya. Kisha, amka asubuhi inayofuata na uweke mpango huo kwenye vitendo.
2.Weka Malengo ya Siku Kila Asubuhi
Pili, weka malengo ya siku kila asubuhi. Panga siku yako usiku kabla, lakini weka malengo yako asubuhi. Kwa mfano, unaweza kupanga kufanya kazi kwenye mradi siku nzima. Kisha, asubuhi weka lengo la ni kiasi gani cha mradi huo unataka kukamilisha. Hivyo ndivyo watu wenye mafanikio hufanya.
Kuweka malengo asubuhi ni mkakati mzuri kwa kuwa watu wengi huwa na nia ya kufanikiwa wanapoanza siku yao. Ikiwa utaweka malengo makubwa asubuhi, utahisi kulazimika zaidi na kujituma zaidi kuyatimiza kadri siku inavyoendelea.
3.Epuka Kuangalia Simu Yako au Vifaa Vingine vya Kielektroniki
Tatu, epuka kuangalia simu yako au barua pepe mara tu unapoamka. Hii ni kwa sababu inaweza kuleta usumbufu ambao unaweza kuingilia kati ratiba yako ya asubuhi. Pia unaweza kupata habari za kukatisha tamaa ambazo zinaweza kuua motisha yako wakati ambapo unahitaji kuichochea.
Subiri mpaka ratiba yako ya asubuhi itakapokamilika ndio uangalie simu yako. Julie Morgenstein, mtaalamu wa usimamizi wa muda, aliandika kitabu kinachoitwa Don’t Check Your Email in the Morning. Subiri mpaka saa 11:00 asubuhi na fanya kazi kwa masaa matatu mfululizo kabla ya kuangalia barua pepe zako, kisha fanya kazi tena kwa masaa matatu kabla ya kuziangalia tena, na ziangalie mara mbili au tatu tu kwa siku, na katikati ya wakati huo uzime na uache kuzitazama.
4.Fanya Mazoezi na Kunyosha Mwili Wako.
Nne, fanya mazoezi. Tafiti zimeonyesha kwamba watu wanaofanya mazoezi asubuhi wana uwezekano mkubwa wa kufuata ratiba ya mazoezi kuliko wale wanaofanya mazoezi mchana. Sababu ni kwamba unapamka asubuhi, unakuwa umepumzika na umejaa nishati. Mchana, baada ya siku ndefu ya kazi, unaweza kuwa hauna nishati au hamasa ya kufanya mazoezi.
Kunyoosha na kufanya mazoezi asubuhi pia kunakufanya damu yako izunguke na kukupa mlipuko wa nishati na adrenalin ambayo itakusaidia kuanza siku vizuri.
5.Soma
Tano, soma. Tafiti zinaonyesha kuwa watu wenye mafanikio, mamilionea waliojitengenezea mafanikio wote wanasoma kwa saa moja au zaidi kila asubuhi. Kama vile kufanya mazoezi asubuhi kunavyoufanya mwili wako kuwa tayari, kusoma asubuhi kunaifanya akili yako pia kuwa tayari.
Saa za asubuhi ni wakati mzuri wa kusoma kidogo kabla ya kwenda kazini. Ninapendelea kusoma kitu cha kielimu au cha kuhamasisha au cha kutia moyo ambacho kinanipa hamasa kidogo.
6.Tafakari
Sita, tafakari. Tafakari ni njia bora ya kusafisha akili yako, kuondoa msongo wa mawazo na kusaidia kuzingatia kazi iliyopo. Tumia dakika chache kukaa kimya na kuacha akili yako itulie. Si tu kwamba tafakari ya asubuhi itakusaidia kufurahia faida zote za kiafya zinazohusiana na tafakari, lakini pia itakuruhusu kuanza siku na mwelekeo mpya na safi.
7.Tumia Muda na Familia Yako
Saba, tumia muda na familia yako. Asubuhi inaweza isiwe na muda mwingi wa kutumia na familia yako kabla hawajaondoka, lakini unapaswa kutumia vyema muda unaoupata. Kaa chini na ule kifungua kinywa nao kama hiyo ni chaguo. Ikiwa si chaguo, angalau chukua muda kuzungumza nao kidogo kabla hamjaenda kila mmoja kwenye majukumu yake.
Hakika hakuna motisha bora kwa siku kuliko kutumia muda kidogo na wale unaowapenda zaidi. Zaidi ya yote, itakuwa motisha nzuri kwao pia wanapoanza siku yao.
Kabla sijahitimisha makala hii ya ratiba za asubuhi za watu wenye mafanikio, ningependa kukuachia wazo la kushiriki na marafiki zako. Akili yako ni kama misuli. Kadri unavyoitumia, ndivyo inavyokuwa na nguvu zaidi. Sasa, ningependa kusikia kutoka kwako, swali langu la leo ni, je, unafanya mambo sahihi asubuhi? Acha maoni hapa chini nami nitahakikisha ninakufuatilia.
Ikiwa umeifurahia makala hii na kuhisi ilikuwa ya thamani katika kukufundisha kuhusu taratibu za asubuhi za watu wenye mafanikio, washirikishe na marafiki zako. Pia kama una swali au maoni yoyote usisite kuandika hapa chini. Unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
Tunaishi katika kipindi ambacho kuna fursa na uwezekano zaidi wa wewe kufikia malengo yako zaidi kuliko hapo awali. Kwa kweli, kuna mambo mengi mazuri ambayo unaweza kuyafanya Ili uweze kufanikiwa maishani mwako. Ikiwa wewe ni kama watu wengi leo, umekuwa ukilemewa na mambo mengi ya kufanya kutokana na muda kuwa mdogo sana, unapaswa kutumia muda wako vizuri ili uweze kutimiza malengo yako. Katika makala hii nitakushirikisha jinsi ya kuwa mtu wa vitendo ili uweze kutimiza malengo yako katika maisha.
Jinsi Ya Kuwa Mtu Wa Vitendo.
Kwanza, unahitaji kuchagua. Kuchagua ni muhimu ili kukuza tabia nzuri ya mafanikio. Uwezo wako wa kuchagua kazi yako ya muhimu zaidi kwa kila wakati, ili kuanza kazi hiyo, na kuifanya haraka na kwa ubora huleta mafanikio makubwa kuliko ujuzi mwingine wowote unaoweza kuukuza. Mtu wa kawaida mwenye mazoea ya kufanya kazi muhimu na kuikamilisha kwa haraka atakuwa na mafanikio makubwa kuliko mtu mwenye uwezo mkubwa na akili timamu ambaye anazungumza sana na kupanga mipango mizuri lakini haitekelezi.
Pili, unahitajika kuweka vipaumbele. Mafanikio yako katika maisha yataamuliwa na aina ya tabia ambazo unakuwa umezijenga kwenye maisha yako. Tabia ya kuweka vipaumbele na kuendelea na kazi yako muhimu zaidi ni ujuzi unaopaswa kuuweka kwenye vitendo na kuudumisha.
Kwa hiyo, unaweza kujifunza tabia hii kupitia mazoezi ya kurudia tena na tena hadi inapokuwa imekazwa kwenye akili yako na kuwa sehemu ya kudumu ya tabia yako. Mara tu inapokuwa tabia, inakuwa moja kwa moja na rahisi kufanya. Kupitia usimamizi wa muda, tabia ya kuanza na kukamilisha kazi muhimu ina malipo ya haraka na endelevu.
Umeundwa kiakili na kihisia kwa njia ambayo kukamilika kwa kazi hukupa hisia chanya. Inakufanya uwe na furaha. Inakufanya ujisikie mshindi.
Wakati wowote unapokamilisha kazi kubwa au yenye umuhimu, unahisi kuongezeka kwa nguvu, shauku, na kujistahi. Umuhimu zaidi wa kazi iliyokamilishwa, unakufanya ujihisi furaha, ujasiri zaidi, na nguvu ndani yako. Kukamilika kwa kazi muhimu huchochea kutolewa kwa endorphins kwenye ubongo wako.
Endorphins hizi hukupa kiwango cha juu cha nguvu za asili. Endorphin ambayo inafuatilia kukamilishwa kwa mafanikio kwenye kazi yoyote hukufanya ujisikie chanya zaidi, mwenye utu, mbunifu na mwenye kujiamini.
Kumbuka kuna mambo matatu muhimu unayopaswa kuyafanyia mazoezi ili uweze kuwa mtu wa vitendo na hivyo kufanikiwa kwenye malengo yako. Mambo hayo ni uamuzi, nidhamu, na dhamira.
Kwanza, lazima ufanye uamuzi wa kukuza tabia ya kuwa mtu anayezingatia vitendo.
Pili, kuwa na nidhamu binafsi ili kufanya mazoezi ya kanuni unazojifunza kwa kuzirudia tena na tena hadi iwe ni mazoea yako.
Na tatu, rudisha kila kitu unachofanya kwenye dhamira yako ili iwe ni tabia na kuwa sehemu ya kudumu ya utu wako.
Jione kuwa ni aina ya mtu ambaye anafanya kazi muhimu kwa haraka na kwa kupitia usimamizi mzuri wa wakati. Picha yako ya kiakili ina athari kubwa kwenye tabia yako. Jione kama mtu unayekusudia kuwa hivyo katika siku zijazo.
Taswira yako, jinsi unavyojiona kwa ndani, kwa kiasi kikubwa huamua utendaji wako wa nje. Uboreshaji wote katika maisha yako ya nje huanza na uboreshaji wa picha zako za akili ndani. Una uwezo usio na kikomo wa kujifunza na kukuza ujuzi mpya, tabia, na uwezo.
Unapojizoeza kupitia marudio na mazoezi ya kushinda kuchelewesha na kukamilisha kazi zako muhimu zaidi haraka, utasonga mbele kwenye njia ya haraka katika maisha na taaluma yako. Sasa ningependa kusikia kutoka kwako. Swali langu la leo ni, je, unajionaje? Acha maoni hapa chini na nitahakikisha kukufuata.
Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kukusaidia kuwa mtu wa vitendo. Ikiwa umefurahia makala hii na unahisi kuwa imekuwa ni ya thamani kwako, usisite kuwashirikisha marafiki zako. Pia kama una swali lolote usisite kuandika hapa chini. Unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
Nguvu binafsi ni rasilimali muhimu sana katika kufanikisha malengo yako ya maisha na ya biashara yako. Ni uwezo wa kutumia nguvu zako za ndani, kujiamini, na kuwa na hamasa ili kufikia malengo yako. Kwa kutumia hatua hizi nne, unaweza kujenga nguvu hizi na kufanikisha mambo makubwa maishani mwako. Katika makala ya leo nitakushirikisha hatua nne za kukuza nguvu zako binafsi ili uweze kufanikisha malengo yako.
Hatua Nne Za Kukuza Nguvu Zako binafsi Ili Ufanikiwe.
Hatua ya Kwanza: Kujiamini
Kujiamini ni msingi muhimu wa kujenga nguvu zako binafsi. Imani kwako mwenyewe hukupa ujasiri na uthabiti wa kufuatilia ndoto zako. Ili kujenga kujiamini, anza kwa kutafakari juu ya mafanikio yako na makosa yako yaliyopita. Sherehekea mafanikio yako na jifunze kutokana na makosa yako. Jenga msingi huu mzuri wa kujiamini kisha chukua changamoto kubwa zaidi ambazo zinahitaji kujiamini zaidi.
Hatua ya Pili: Tambua Thamani Yako.
Thamani ni kanuni au viwango vya tabia ambavyo ni vya muhimu kwako. Thamani inaweza kutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine, lakini zinatoa mwelekeo wa kufanya maamuzi maishani. Ili kutambua thamani yako kuu, fikiria juu ya imani, sifa, nguvu, uwezo na uzoefu wa kufanya mambo ulionao. Tambua thamani yako na uitumie kama mwongozo wa kufanya maamuzi katika kutimiza malengo yako.
Hatua ya Tatu: Chukua Hatua kuelekea Malengo Yako.
Kufikia malengo yako inaweza kuwa ni kazi ngumu, lakini unapokuwa umefikia malengo yako inaleta furaha ya ajabu. Chukua hatua ndogo ndogo kuelekea malengo yako. Ni muhimu kuandika malengo yako na kupima maendeleo yako njiani ili kujipa motisha na nguvu. Ili uweze kuchukua hatua kuelekea malengo yako, unapaswa kuwa jasiri, makini na usiyekata tamaa.
Hatua ya Nne: Tengeneza Mtandao wa Msaada
Kuwa na mtandao wa msaada ni muhimu kwa mafanikio na furaha maishani kwa ujumla. Unaweza kupata watu wenye maslahi na malengo yanayofanana na ya kwako kwa njia mbalimbali kama vile: kujiunga na klabu au kuhudhuria matukio ya kijamii. Pia, unaweza kuungana na watu mtandaoni ambao wana malengo kama ya kwako ili muweze kubadilishana uzoefu na kupeana ushauri.
Kwa kufuata hatua hizi nne ambazo ni kujiamini, kutambua thamani yako, kuchukua hatua, na kuunda mtandao wa msaada, unaweza kukuza nguvu zako binafsi zaidi na kufanikisha malengo yako. Kwa nguvu hizi binafsi, chochote kinawezekana.
Sasa swali la leo ni: ni hatua gani kati ya hizi nne utaanza nayo leo? Acha maoni yako hapa chini, nami nitakufuatilia.
Ikiwa umeipenda makala hii na unaona ina thamani kwako, usisite kushiriki na marafiki zako. Kama una swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
Je, kungekuwa na tofauti gani katika maisha yako ikiwa ungekuwa na ujasiri usiotikisika katika uwezo wako wa kufanikiwa katika kila kitu ambacho unakiwaza kwenye akili yako? Msichana mmoja alimwandikia Brian Tracy akimwambia kwamba maisha yake yote yalikuwa yamebadilika kabisa tangu alipomsikia akiuliza swali, “Ni jambo gani kubwa ambalo ungethubutu kulifikiria na kulifanya ikiwa ungejua huwezi kushindwa?” Aliandika kwamba hadi wakati huo hili lilikuwa ni swali ambalo hakuwahi kulifikiria katika maisha yake. Baada ya kusikia swali hilo la Brian Tracy aligundua kuwa jambo kuu lililomtenganisha na matumaini na ndoto zake ni imani katika uwezo wake wa kuzifanikisha.
Wengi wetu tuko hivyo kwa sehemu kubwa ya maisha yetu. Kuna mambo mengi ambayo tunataka kuwa nayo na kuyafanya, lakini tunajizuia. Hatuna uhakika wa kufanikiwa kwa sababu hatuna ujasiri wa kutosha kutoka kwa imani katika mwelekeo wa ndoto zetu.
Hebu fikiria, ingekuwa na tofauti gani katika maisha yako ikiwa ungekuwa na imani isiyotikisika kabisa katika uwezo wako wa kufikia jambo lolote unaloliwaza akilini mwako? Je, ungetaka, kutamani na kutumaini nini? Ungethubutu kuota nini ikiwa unajiamini kwa imani kubwa kiasi kwamba huna hofu ya kushindwa hata kidogo? Jambo kuu ni kuwa mwaminifu kwako mwenyewe, kuwa mwaminifu kwa yaliyo bora zaidi yaliyo ndani yako, na kuishi maisha yako kulingana na maadili na matarajio yako ya juu. Chukua muda kufikiria wewe ni nani na unaamini nini na ni nini muhimu kwako.
Kuwa na ujasiri wa kujikubali jinsi ulivyo, si vile unavyoweza kuwa au jinsi mtu mwingine anavyofikiri unapaswa kuwa. Zingatia kuwa, wewe ni mtu wa thamani sana. Kuwa mwaminifu kwako mwenyewe inamaanisha kujua kile unachotaka na kuwa na mpango wa kukifanikisha. Kujiamini kunakodumu kunatokana na kujua kabisa kwamba unao uwezo wa kutoka hapo ulipo kwenda popote unapotaka kwenda.
Uko nyuma ya gurudumu la maisha yako. Wewe ndiye mbunifu wa hatima yako na bwana wa hatima yako. Tenda kana kwamba haiwezekani kushindwa.
Fanya kana kwamba tayari una kiwango cha juu cha ujasiri na endelea kujiuliza, ni jambo gani kubwa ambalo ningethubutu kulifikiria na kulifanya nikijua siwezi kushindwa? Chochote unachokiwaza kwenye jibu lako, unaweza kukipata ikiwa unajiamini kutoka na kukipokea. Hapa kuna hatua tatu unazoweza kuchukua mara moja ili Kujenga Kujiamini Kusikotetereka.
Kwanza, amua kuchukua hatua kwa imani katika mwelekeo wa ndoto zako. Fanya tu, usiwaze kushindwa.
Pili, jiulize, “ni kitu gani kikubwa ambacho ningethubutu kukiota na kukifanya nikijua siwezi kushindwa?”
Tatu, kuwa mwaminifu kwako mwenyewe, na uanze kuchukua hatua. Usiweke visingizio vingi vya kushindwa.
Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ya jinsi ya kujenga ujasiri usiotetereka ili uweze kufikia mafanikio yako. Ikiwa umefurahia makala hii na unahisi kuwa ilikuwa ya thamani kwako, usisite kuwashirikisha marafiki zako. Kama una swali au maoni usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
Katika maisha, kujitazama nyuma na kutafakari mafanikio uliyoyapata ni jambo muhimu sana. Pia ni vyema kuzingatia changamoto ulizokutana nazo na jinsi zilivyokusaidia kukua. Kitendo cha kufikiria uzoefu wako wa zamani, mafanikio, na mafunzo uliyoyapata, kutaweza kuamua malengo unayotarajia kufikia siku za usoni. Iwe umeweka malengo ya juu zaidi au umelenga kubaki thabiti na malengo yako, unatakiwa kuepuka mambo na tabia fulani ili uweze kufanikiwa. Katika makala hii nitakushirikisha mambo 10 ya kuacha ili ufanikiwe siku za usoni:
Mambo 10 Ya Kuacha Ili Ufanikiwe Siku Za Usoni.
1. Visingizio: Jifunze kuwajibika. Kuwa na malengo na ujikite kufanyia kazi malengo yako bila kuwa na visingizio. Kila kisingizio kinakurudisha nyuma kufikia lengo lako.
2. Kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja: Ingawa inaweza kuonekana kuwa kama suluhisho la ufanisi, kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kunaweza kuharibu malengo yako. Fikiria kufanya kazi moja kwa wakati mmoja.
3.Kusema ndiyo kwa mambo yasiyosaidia malengo yako: Mara nyingine tunajisikia lazima tuseme ndiyo. Lakini kusema ndiyo kwa mambo ambayo hayasaidii malengo yako kunaweza kukurudisha nyuma. Jifunze kusema hapana kwa mambo yasiyo na maana ambayo hayachangii kwenye mafanikio yako.
4. Epuka watu wenye sumu: Kuna wakati utakutana na watu wasio na nia njema na mafanikio yako. Ikiwa hawakusaidii kufikia malengo yako, waache. Kuacha uhusiano na watu wenye mawazo hasi kunaweza kuwa kugumu, lakini kutakusaidia kufanikiwa baadaye.
5. Muda wa kutumia kwenye mitandao ya kijamii: Kwa wastani, mtu hutumia dakika 145 kwa siku, zaidi ya masaa 2 kwenye mitandao ya kijamii. Kudhibiti muda wako kwenye mitandao ya kijamii kunaweza kukuepushia kupoteza muda na badala yake kufanya vitu vingine vyenye tija.
6.Kutothamini kile ulichonacho sasa: Thamini vitu ulivyonavyo sasa. Kudharau vitu ulivyonavyo kunaweza kuzuia kufikia malengo yako. Kuwa na shukrani kwa kila unachokuwa nacho katika maisha yako. Kujifunza kushukuru imegundulika kuwa kunaimarisha mtazamo chanya na afya ya akili kwa ujumla. Hata kama kuna nyakati ambazo hauna furaha, unapothamini mafanikio yako unaongeza motisha ya kupiga hatua zaidi kuelekea kwenye mafanikio yako. Hivyo, unapaswa kuacha tabia hii ili uweze kufanikiwa.
7.Kutafuta idhini kutoka kwa watu wengine. Ikiwa unangoja mtu akuruhusu kufanikiwa, utangoja milele. Usisubiri mtu akwambie unaweza kufanya nini. Badala yake, onyesha uwezo wako. Jitwike jukumu la maisha yako na malengo yako wewe mwenyewe. Jiruhusu kufanikiwa.
8. Uvivu. Kama vile kutoa visingizio, kuchelewesha kazi pia kunazuia kufikia malengo yetu. Badala ya kusubiri kufanya kazi yako hadi dakika ya mwisho, au kuendelea kuahirisha, jichukulie kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii.Tunaona mafanikio tunapochukua hatua na kufanya jambo.
9.Kuamini malengo yako ni makubwa au madogo sana. Malengo yako ni tofauti kabisa na ya mtu mwingine, hivyo unapaswa kuacha kulinganisha malengo. Badala yake, jikite katika jinsi unavyoweza kufikia malengo yako. Usipoteze muda kwa kufikiria sana au kuchambua mambo kama vile ukubwa au udongo wa malengo yako. Anza tu kuyatimiza.
10. Kulinganisha maisha yako na ya wengine. Kama vile malengo yanavyotofautiana na ya mtu mwingine, maisha yako pia ni tofauti kabisa na ya mtu mwingine.
Rais Theodore Roosevelt aliwahi kusema, Kujilinganisha na wengine ni mwizi wa furaha. Tunapojilinganisha na wengine, tunajihisi duni na tusiofaa. Tunapogundua kuwa tunaweza vya kutosha na tuna njia za kufikia malengo yetu, hatutajisikia vibaya kuhusu safari yetu ya mafanikio. Tutagundua kuwa kujilinganisha na wengine kunatuzuia tu kufikia safari yetu.
Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa kuhusu mambo 10 ya kuacha ili ufanikiwe siku za usoni. Kama una swali au maoni usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.
Hofu ni hisia ya asili inayotukumba sisi sote. Inaweza kuwa ni kizuizi kinachotuzuia kufikia uwezo wetu kamili na kutimiza malengo yetu. Lakini, ujasiri siyo ukosefu wa hofu; ni uamuzi wa kuchukua hatua licha ya kuwepo kwa hofu. Katika makala hii nitakushirikisha jinsi ya kushinda hofu ya kufanya maamuzi na hivyo kukuwezesha kuchukua hatua kuelekea mafanikio yako.
Hofu ni nini?
Hofu inaweza kujitokeza kwa namna nyingi, ikiwa ni pamoja na hofu ya kushindwa, hofu ya kukataliwa, au hofu ya yasiyojulikana. Mara nyingi huwa tunashindwa kufanya maamuzi ambayo yangeleta mabadiliko makubwa katika maisha yetu kwa sababu ya hofu. Hivyo, kuelewa chanzo cha hofu yako ni hatua ya kwanza katika kuvuka vizingiti vyake na hivyo kukufanya upate mafanikio makubwa kwenye malengo uliyojiwekea.
Kujenga Ujasiri.
Ujasiri unajengwa kwa kuchukua hatua ndogondogo. Anza na hatua zisizoogopesha sana na endelea kujenga ujasiri wako kadiri unavyokabiliana na changamoto kubwa zaidi. Ili uweze kushinda hofu ni lazima ujifunze kujenga ujasiri katika maisha yako ya kila siku. Zifuatazo ni njia ambazo zitakusaidia kushinda hofu ya kufanya maamuzi na hivyo kujenga ujasiri wa kuchukua hatua muhimu katika mafanikio yako.
Ujasiri wa Kuchukua Hatua: Jinsi Ya Kushinda Hofu Ya Kufanya Maamuzi.
1.Weka Malengo Madogo:
Kama una lengo kubwa unalotaka kulifikia maishani, gawa lengo hilo kwenye malengo madogomadogo ambayo utaweza kuyafikia. Unapoweza kufikia lengo dogo uliloliweka, utakuwa umejenga ujasiri wa kufikia na malengo mengine madogo uliyojiwekea. Hivyo, weka malengo madogomadogo yanayoweza kufikiwa ambayo yatakusaidia kujenga ujasiri wa hatua kwa hatua.
2.Kuwa na Mtazamo Chanya:
Badilisha mawazo hasi na uwe na mawazo chanya yanayohimiza uwezekano wa mafanikio. Usiweke visingizio vya kushindwa. Katika kila jambo unalofanya jipe moyo kwa kujisemea ‘ninaweza’ hata kama watu watakukatisha tamaa.
3.Jiandae Vizuri:
Maandalizi mazuri yanaweza kupunguza hofu na kukupa ujasiri wa kuchukua hatua. Hivyo, unapotaka kufanya jambo lolote, hakikisha umejiandaa vya kutosha. Hii itakusaidia kuondoa hofu ya kushindwa.
Kabiliana na Hofu.
Kukabiliana na hofu kunahitaji muda na uvumilivu. Usijaribu kukimbia au kuepuka hofu yako; badala yake, kabiliana nayo kwa ujasiri na utayari wa kujifunza kutokana na uzoefu.
Kuchukua hatua ni muhimu katika safari ya mafanikio. Hofu itakuwepo, lakini ujasiri wa kuchukua hatua licha ya hofu ndio utakaokuwezesha kuvuka vizingiti na kufikia malengo yako. Kumbuka, kila hatua unayochukua ni ushindi dhidi ya hofu.
Nimatumaini yangu kuwa umenufaika vya kutosha na makala hii ya jinsi ya kushinda hofu ya kufanya maamuzi. Kama una maoni au swali lolote, usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa kupitia simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.