Jinsi Ya Kuandika Na Kuuza Vitabu Pepe.

Mwongozo wa jinsi ya kutengeneza pesa mtandaoni kwa kuandika na kuuza vitabu pepe (ebooks)

Jinsi Ya Kuandika Na Kuuza Kuandika Vitabu Pepe.

Kama unatamani kutengeneza pesa mtandaoni kupitia uandishi wa vitabu, basi nikuhakikishie kuwa upo mahali sahihi. Katika makala hii utajifunza hatua kwa hatua jinsi ya kutengeneza pesa mtandaoni kwa kuandika kitabu chako na kukiuza mtandaoni

Jinsi ya kutengeneza pesa mtandaoni kwa kuandika na kuuza vitabu pepe(ebooks).

Jinsi Ya Kuandika Na Kuuza Kuandika Vitabu Pepe.
  1. Chagua wazo zuri la kitabu chako
  2. Andika dondoo za mtiririko wa kitabu chako
  3. Fikiria urefu wa kitabu chako.
  4. Chagua muundo wa faili la kitabu chako
  5. Tengeneza kava zuri lenye kuvutia la kitabu chako.
  6. Uza kitabu chako kwa jamii inayokuzunguka
  7. Panua mauzo yako kwa kuuza kitabu chako getvalue na amazon.

Ni matumaini yangu kuwa sasa uko tayari kupata maarifa haya ya msingi ili na wewe uanze kutengeneza pesa kwa kuandika vitabu. Sasa karibu tuendelee…

Kimsingi huhitajiki kuwa na watu wengi au followers wengi kuanza kutengeneza pesa kwa kuandika kitabu chako ikiwa kitabu chako kitakuwa kinatatua tatizo fulani la kundi la watu katika jamii. Hivyo basi ukiandika kitabu kinachotatua changamoto mojawapo inayoikabili jamii, kitabu chako kitauzika na utaweza kutengeneza pesa.

Hapa ninazungumzia kama unamiliki blog yako, unaweza kutengeneza pesa na kuwa na kipato kikubwa na endelevu kwa kuuza kitabu chako kwenye blog yako kwa kukitangaza kupitia mitandao ya kijamii mahali ambapo watu uliolenga kuwauzia kitabu chako hutumia muda wao mwingi kuwemo. Huhitajiki kuwa na kundi kubwa la watu ili uweze kuandika kitabu chako na kukiuza.

Sasa kabla hatujazama ndani kabisa kwenye mwongozo huu, ngoja nianze kwanza kwa kujibu maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa mara kwa mara kuhusiana na kuandika vitabu.

Maswali hayo ni haya yafuatayo:

  1. Kwa nini ninapaswa kuandika kitabu?

Wamiliki wengi wa blog huchukua hatua ya juu zaidi kutoka kuandika makala za blog  na hatimaye kuamua kuandika vitabu. Hata wewe kupitia blog yako kama umekuwa ukiandika makala zenye kuelimisha jamii na pia umefanikiwa kuwa na kundi la watu wanaofuatilia makala zako haijalishi ukubwa wa kundi linalokufuatilia, unaweza kuandika kitabu ili kuelezea kwa kina mada unayofundisha ili wasomaji wako waweze kujifunza kwa undani zaidi. Pia kwa kuwa umekuwa ukiandika makala kwa muda mrefu, utakuwa umejifunza watu wako wana changamoto gani na wanahitaji mada zipi ili waweze kutatua changamoto zao, hivyo unaweza kuandika vitabu ili kutoa maarifa kwa undani zaidi kwenye mada ambazo wasomaji wako wanazihitaji kutatua changamoto zao. Kutokana na hali hiyo basi, kuna sababu nyingi sana za wewe kuandika kitabu. Miongoni mwa sababu hizo ni hizi zifuatazo:

  • Vitabu pepe huvutia wasomaji wengi kutembelea blog yako na kukujengea heshima na kukubalika na jamii (authority).

Faida kubwa unayoweza kuipata kwa kuandika kitabu pepe ni kwamba, kitavutia watembeleaji wapya wengi kwenye blog yako. Pia kitakufanya uheshimike na jamii kukuona kuwa wewe ni mtaalamu uliyebobea kwenye  mada unayofundisha (niche). Hata kama umekuwa ukiandika makala ndefu kwenye blog yako, kitabu kitaonyesha kuwa wewe ni mtaalamu wa viwango vya juu kwenye mada unayofundisha.

  • Vitabu pepe vitatoa maarifa ya kina zaidi kwenye mada unayofundika kupitia makala zako: unapokuwa umeandika kitabu pepe, unawasaidia wasomaji wako kupata maarifa ya kina zaidi ambayo usingeweza kuyaweka yote kwenye makala zako za kawaida. Njia nzuri ya kupata wazo zuri la kuandikia kitabu ni kwa kuangalia ni mada gani ambayo wasomaji wako wameipenda zaidi na hivyo kuandika kitabu kinachoelezea kwa kina mada hiyo.
  •  Unaweza kukusanya email za wasomaji wako kwa kuwapatia kitabu cha bure: kukusanya email za wasomaji  ni jambo la muhimu sana kama unamiliki blog na unataka  kutengeneza kipato kupitia blog yako. Unapokuwa umepata watu ambao wamejiunga (subscribe) kwenye blog yako, ni rahisi kuwapa taarifa kila unapokuwa umeweka makala mpya kwenye blog yako. Pia unaweza kuwapa ofa mbalimbali za bidhaa au huduma ambayo utakuwa unaitoa kwenye blog yako kupitia email zao. Njia rahisi ya kupata email za wasomaji wako ni kuwapa kitabu cha bure. Ili mtu aweze kupata kitabu hicho, itamlazimu aweke email yake ili aweze kupakua kitabu chake. Hivyo unapokuwa na email za wasomaji wako ni rahisi kutengeneza kipato kwa kuwauzia huduma unazotoa kwenye blog yako.
  • Je kuandika na kuuza vitabu pepe ni njia nzuri ya kutengeneza kipato?

Kuandika na kuuza vitabu pepe inaweza kuwa ndio njia rahisi kuliko zote ya kutengeneza pesa mtandaoni. Kama unamiliki blog na umeandika makala kadhaa zinazoelimisha jamii, asilimia kubwa ya wasomaji wako watahitaji kujifunza zaidi kile walichokisoma kwenye makala zako, hivyo ukiandika kitabu pepe utawasaidia wasomaji wako kujifunza kwa undani zaidi mada uliyoiandika kwenye blog yako na wakati huo huo ukitengeneza kipato.

  • Ni aina gani ya vitabu pepe ninapaswa kuandika?

Kwa mujibu wa mwongozo huu wa jinsi ya kuandika kitabu pepe, tutajikita kwenye uandishi wa vitabu vya mafunzo. Sitazungumzia kuhusiana na uandishi wa vitabu vya hadithi au riwaya.  Hivyo tutaangalia jinsi ya kuandika vitabu ambavyo vitakuwa vinatatua changamoto fulani kwenye jamii.

Sasa, ni aina gani ya vitabu ambavyo unaweza kuandika? Baadhi ya aina za vitabu ambavyo unaweza kuandika ni hizi zifuatazo:

  • Vitabu vya ‘Jinsi ya…….’: Vitabu vya ‘jinsi ya…’  ni vitabu vizuri sana kuandika. Ni vitabu vinavyotatua changamoto katika jamii. Kumbuka kuwa watu huwa wanaingia mtandaoni kutafuta suluhisho la matatizo yao. Hivyo ukiweza kuandika kitabu kitakachowarahisishia watu kutatua changamoto zao, kitabu chako kitauzika. Mifano ya vitabu hivyo ni:  Jinsi ya kuanzisha biashara mtandaoni, jinsi ya kuanzisha kilimo bora cha ufuta, jinsi ya kupata wateja wengi kwenye biashara yako, n.k.
  •  Vitabu vinavyoboresha maisha ya watu: Vitabu vinavyoboresha maisha ya watu ni aina ya vitabu ambavyo vinalenga kumsaidia mtu kubadilisha mwenendo wake wa maisha ili aweze kufanikiwa katika maisha yake. Mfano wa vitabu hivyo ni:  jinsi ya kufikia malengo yako, jinsi ya kula vizuri ili kujenga afya yako, jinsi ya kuwa na hamasa kwenye kazi zako, jinsi ya kuokoa muda wako n.k.

Kabla hatujaendelea mbele na huu mwongozo wa jinsi ya kuandika kitabu pepe, hapa kuna takwimu chache za kushangaza nilizozipata kuhusiana na vitabu pepe:

Vitabu pepe vinachukua asilimia 19 ya mauzo yote ya vitabu duniani.

Mauzo yote ya vitabu pepe duniani yalifikia zaidi ya dola za kimarekani 16 kwa mwaka 2021.

Sasa hebu tuanze kujifunza jinsi ya kuandika kitabu pepe.

1. Chagua wazo zuri la kitabu chako.

Hatua ya kwanza kabisa kujifunza unapokuwa unahitaji kuandika kitabu ni kuhakikisha kuwa umechagua wazo zuri ambalo sio tu litapendwa na wasomaji wako bali pia litaendana na vitu unavyovipendelea (interest) na malengo yako.

Ili uweze kupata wazo zuri la kitabu chako, hatua zifuatazo zitakusaidia:

  • Ni mawazo gani au mada gani za vitabu hukuvutia zaidi?

Wakati unachagua wazo la kitabu chako, unatakiwa kuangalia mada ambazo wewe mwenyewe zinakuvutia na hivyo unafurahia kuzichimbua na kuingia ndani zaidi.

  • Ni wazo gani moja au mawili ya vitabu ungefurahia kuandika?

Katika makala zako zote ulizowahi kuandika kwenye blog yako, ni mada ipi unayoifurahia zaidi?

Ni mada ipi una ujuzi na uzoefu mkubwa kati ya mada zilizopo kwenye blog yangu?

Ni mada zipi unajihisi una ujasiri wa kuzifundisha kupitia mazungumzo au kuandika?

Hapa kuna njia chache ambazo zitakuwezesha kutambua ni mada ipi ambayo ukiandikia kitabu watu wataipenda:

  1. Angalia kwenye makala ulizowahi kuandika kwenye blog yako na uone makala zilizopata wasomaji wengi na shares nyingi. Hii inamaanisha kuwa makala hizo zilipendwa sana na watu na hivyo unaweza kutumia makala hizo kuandika kitabu pepe.  Pia makala zilizopata comment nyingi inaashiria kuwa makala hizo ziligusa hisia na changamoto za wasomaji wako na hivyo unaweza kutumia makala hizo kuandika kitabu pepe.
  2. Njia nyingine ni kwa kuangalia maswali waliyouliza wasomaji wako pamoja na maoni waliyoandika kwenye makala zako. Kumbuka kuwa, maswali wanayouliza wasomaji wako ni changamoto walizonazo katika maisha, hivyo unaweza kutatua changamoto zao kwa kuandika kitabu pepe.

Kimsingi, wazo zuri la kitabu ni lile ambalo litaendana na kile ambacho watu wanahitaji kujifunza.

Wazo zuri la kitabu ni lazima lifuate kanuni hii:

Kile unachopenda kuandika kioane na kile watu wanachohitaji kujifunza.

Fanya utafiti kuhusiana na ushindani uliopo.

Unapokuwa unataka kuchagua mada utakayoitumia kuandikia kitabu chako, jambo jingine la msingi ni kuangalia ushindani. unaweza kuangalia google ni watu kiasi gani wamekwisha andika vitabu vyenye mada kama ya kwako? Japokuwa hiyo si shida sana kwa lugha ya kiswahili kwani bado waandishi wa vitabu ni wachache na ushindani ni mdogo sana. Hivyo changamkia hiyo fursa.

2. Andika dondoo za mtiririko wa kitabu chako

Hatua inayofuata katika mchakato wa kuandika kitabu pepe ni kufikiria kitabu chako kitakuwa na mtiririko gani kwa ujumla.

Katika hatua hii unatakiwa kufikiria ni mtiririko gani utautumia katika kuandika kitabu chako.

Ingawa kuna aina nyingi za mfumo wa kuandika kitabu pepe, hapa nimekuwekea zoezi ambalo litafanya kazi yako ya uandishi kuwa yenye kueleweka(logical) na rahisi kusomeka.

Anza na kuandika dondoo (outline) za kitabu chako.

Kuanza na dondoo ni jambo la msingi katika uandishi wa aina yoyote. Iwe unaandika makala kwenye blog, kitabu pepe au unaandaa kozi ya mtandaoni, kuwa na dondoo ni jambo la muhimu sana. Katika mwongozo huu nimeelezea kwa kina na hatua kwa hatua jinsi unavyoweza kuandika dondoo za kitabu chako. Ufuatao ni mtiririko wa jinsi unavyotakiwa kuandika dondoo (outline) za kitabu chako:

  • Andika ni vitu gani unataka wasomaji wako wavipate na kuvifanyia kazi maishani baada ya kusoma kitabu chako. Kwa mfano, unataka kuandika kitabu kinachohusu Jinsi ya kuanzisha biashara kwa mtaji mdogo, unaweza kuandaa dondoo kama ifuatavyo:
  • Maana ya biashara
  • Sababu za kuanzisha biashara
  • Aina za biashara
  • Mtaji ni nini
  • Aina za mitaji
  • Aina za biashara zenye mtaji mdogo
  • ………..
  • …………
  • ………… n.k
  • Andika kichwa cha habari kitakachovutia wasomaji wako. Mfano, nimechagua kuandika kichwa cha habari cha kitabu changu kuwa: Jinsi ya kuanzisha biashara kwa mtaji mdogo hapohapo ulipo.
  • Orodhesha maswali yote unayotakiwa kuyajibu kwenye kitabu pepe chako. Hapa unaweza kuorodhesha pembeni maswali ambayo yamekuwa yakiwasumbua sana watu ambayo unahitaji kuyajibu kupitia kitabu chako.  Kwa mfano:
  • ninahitaji kuanzisha biashara lakini sina mtaji, nifanyeje?
  • Ni biashara gani za mtaji mdogo zinazolipa?
  • Nifanye biashara gani?
  • . n. k
  • Pangilia sehemu kuu za kitabu chako. Hapa utapangilia sehemu kuu za kitabu chako kwa kuangalia ni mada ipi ianze, ipi ifuate na ipi utamalizia.
  • Weka takwimu, tafiti na rejea mbalimbali. Unaweza pia kuandaa takwimu, vielelezo na rejea mbalimbali ili kukifanya kitabu chako kuwa bora zaidi.

Fanya marejeo ya dondoo zako na uongeze au kupunguza sehemu unazoona zinahitaji marekebisho.

Anza kuandika kitabu chako.

Faida kubwa ya kuanza kuandika kitabu chako kwa kuandika dondoo ni kwamba, inakupatia picha halisi ya kile unachokwenda kuandika kabla ya kuanza kuandika.

Katika sehemu hii ya mwanzo ya kupangilia jinsi ya kuandika kitabu chako, unaweza kuamua ni mada zipi utaziweka pamoja na mada zipi utaziweka kwenye kitabu kipya kingine utakachoandika hapo baadaye.

Kuandika dondoo pia kunakufanya usitoke nje ya mada unapokuwa unaandika na kukupatia mwelekeo sahihi wa kile unachoandika.

Andika kichwa cha habari kinachovutia wasomaji wako.

Kwa kawaida watu huweza kutathmini ubora wa kitabu kwa kuangalia jalada lake la juu, vivyo hivyo watu watakitathmini kitabu chako kwa kuangalia jina la kitabu chako kabla ya kufungua na kusoma kile ulichoandika.

Hapa kuna mambo machache ya kuzingatia unapokuwa unaandika Jina la kitabu chako:

  • Usiandike kichwa cha habari ambacho kipo kwa ujumla (too general). Hapa ninamaanisha unapokuwa unaandika jina la kitabu chako jizatiti katika kulenga tatizo halisi ambalo kitabu chako kinaenda kutatua.

Kwa mfano, hebu linganisha majina ya vitabu hivi viwili:

Kilimo bora na

Kilimo bora na cha kibiashara cha nyanya.

Ukiangalia majina ya vitabu hivi viwili, unafikiri ni kitabu kipi msomaji akisoma kichwa cha habari tu ataelewa kitabu hicho kinatatua tatizo gani?

Kimsingi kitabu cha pili kinajieleza chenyewe hata kabla hujafungua ndani ya kitabu hicho. Hivyo ninashauri uandike jina la kitabu linalojieleza hata kabla msomaji hajafungua ndani ya kitabu.

  • Chagua jina la kitabu linalovutia wasomaji. Hapa sikuchagulii uandike jina la gani lakini ninachosema jitahidi jina la kitabu chako liwe ni lile linalovuta usikivu wa wasomaji wako.
  • Chagua jina la kitabu ambalo ni rahisi kukumbukwa. Kwa kawaida watu wanapoona kitabu mtandaoni, huwa hawanunui muda huohuo. Huendelea kutafuta mtandaoni vitabu vingine kulingana na mahitaji yao. Baadaye watakapokuwa wamelinganisha vitabu vingi, ndio huchagua miongoni mwa vitabu hivyo kitabu chenye jina linalovutia na ambacho watakuwa wanakikumbuka. Hivyo ukiweka jina ambalo ni rahisi kukumbukwa itakupatia faida ya kitabu chako kuweza kuuzika kwa urahisi mtandaoni.
  • Angalia vitabu vingine ulivyowahi kusoma na ambavyo ulivifurahia sana na ujaribu kujifunza jinsi ambavyo unaweza kuandika jina la kitabu chako. Jifunze jinsi waandishi wengine walivyoandika majina ya vitabu vyao na wewe uweze kupata maarifa ambayo yatakusaidia kupata kichwa cha habari ambacho kitavutia wasomaji wako.

Kumbuka kuwa japokuwa jina la kitabu ni la muhimu sana kwenye uandishi wa kitabu chako, lakini unaweza kulibadilisha kabla ya kumaliza kuchapisha kitabu chako. Hivyo, usitumie muda mwingi sana kuhangaika kupata jina bora la kitabu chako. Unaweza kuendelea kuandika kitabu chako na baadaye ukaweka jina la kitabu chako utakapokuwa umepata jina zuri.

Andika utangulizi unaovutia

Kitu kimoja ambacho kipo kwenye vitabu vyote maarufu ni kuwa na utangulizi unaovuta wasomaji kupata hamu ya kusoma kitabu chote.

Utangulizi ni sehemu fupi kuliko sehemu zingine za kitabu inayoelezea vitu vyote ambavyo vimeelezwa na kufafanuliwa ndani ya kitabu.

Kimsingi, katika utangulizi unatakiwa utengeneze tatizo lililoko katika jamii na ambalo msomaji wako atapata suluhisho la tatizo hilo atakapokuwa amesoma kitabu chako. Kumbuka kuwa, watu huwa wanatafuta maarifa ili waweze kutatua changamoto zao. Hivyo huwa wanatafuta njia sahihi itakayowasaidia kutatua changamoto zao. Hivyo ukiweza kuainisha vizuri tatizo lililopo na jinsi ambavyo msomaji wako ataweza kutatua tatizo lake kupitia kusoma kitabu chako, basi hapo utakuwa umejiweka kwenye nafasi nzuri sana ya kuuza kitabu chako.

Andika Sura za kitabu chako

Kitu kingine kizuri ambacho vitabu vyote vinacho ni kuwepo kwa sura. Sura husaidia kugawanya mawazo mbalimbali yaliyomo ndani ya kitabu chako na kuyapangilia katika mtiririko unaofaa na kusomeka kwa urahisi. Lakini pia kila sura unaweza pia ukaigawa katika sehemu zingine ndogondogo kulingana maarifa unayoelezea ndani ya sura moja.

Mwanzo wa kila sura unatakiwa uanze na utangulizi na baada ya hapo gawanya kichwa cha habari cha sura hiyo kwenye vichwa vya habari vidogovidogo ili kumrahisishia msomaji.

Mwisho wa kitabu chako utatakiwa kumaliza kitabu chako kwa kukazia mada zote ulizokuwa unahitaji msomaji wako azielewe. Pia kumbuka kuwa wakati unaandika utangulizi uliainisha tatizo lililopo katika jamii na jinsi ambavyo msomaji wako angepata suluhisho la tatizo lake kwa kusoma kitabu chako. Hivyo unapokuwa unahitimisha kitabu chako kazia tatizo ulilokuwa unalishughulikia na jinsi ambavyo kitabu chako kimeleta suluhisho.

Pia ainisha pointi za msingi ambazo msomaji wako anapaswa kuondoka nazo na kuzifanyia kazi maishani.

Toa maelezo yaliyonyooka ya namna ambavyo wasomaji wako watachukua hatua kutatua changamoto zao.

3. Fikiria urefu wa kitabu chako na uanze kuandika.

Hapa unatakiwa ufikirie kitabu chako kiwe na kurasa ngapi. Hapa ni wewe mwenyewe utaamua urefu wa kitabu chako kulingana na mada unayoandika.

Badala ya kuweka kiwango cha maneno utakayoandika kwenye kitabu chako, jambo unalopaswa kujiuliza ni maarifa gani ya msingi unayopaswa kuwapa wasomaji wako.

Thamani na ubora wa maarifa utakayotoa kwenye kitabu chako ndiyo yatakayofanya watu waweze kusoma kitabu chako.

4. Chagua aina ya faili utakayoitumia kuhifadhi kitabu chako.

Baada ya kuwa umeandika kitabu chako, unaweza kukiweka katika mfumo wa PDF tayari kwa kuanza kukiuza. Kuna njia nyingi za mifumo ya kuhifadhi kitabu chako kama vile epub n.k lakini PDF ni njia rahisi zaidi.

5. Tengeneza kava zuri la kuvutia la kitabu chako.

Baada ya kuwa umeandika kitabu chako, hatua inayofuata ni kutengeneza kava zuri la kitabu chako. kitabu chenye kava zuri linalovutia huvutia wasomaji kununua na kushare kwa marafiki zao kwenye mitandao ya kijamii.

Chagua maandishi yanayosomeka.

Hapa unatakiwa uchague maandishi (font) yanayosomeka kwa urahisi. Hii itawarahisishia wasomaji wako kuweza kusoma kwa urahisi.

Tumia Sura na kila sura uigawanye kwenye vichwa vya habari na vichwa vidogo vya habari.

Linapokuja suala la kuandika kitu chochote mtandaoni, tafiti zinaonyesha kuwa, watu wengi huwa wanasoma kwa kurashia(skimming). Hivyo hata katika uandishi wako wa kitabu ambacho unategemea kukiuza mtandaoni, jitahidi kukipangilia kwa kugawanya sehemu ndogondogo ndani ya sura za kitabu chako ili kumrahisishia msomaji wako kuelewa kwa urahisi ujumbe uliokusudia aupate.

Kama una blog, kuza brand ya blog yako kwa kuitangaza kupitia kitabu chako.

Kama una blog na umetumia muda mrefu na nguvu nyingi kuikuza, unaweza kutumia kitabu chako kuitangaza.

Hapa unaweza kutumia rangi zilizopo kwenye blog yako ukazitumia kwenye kitabu chako n.k. Kwa kufanya hivyo wasomaji wako watajihisi kuwa kitabu ulichokiandika ni muendelezo wa kina wa kile unachofundisha kwenye blog yako.

Weka picha kitabu chako.

Tumia picha kwenye kitabu chako. unapokuwa unatumia picha kwenye kitabu chako, unakifanya kionekane vizuri na wasomaji wafurahie maarifa uliyowaandalia.

Platfom ya bure unayoweza kuitumia kutengeneza kitabu chako.

Kuandika vitabu au kitabu ni rahisi sana kama utakuwa na vitu sahihi vya kuandikia. Ifuatayo ni platform ya bure kabisa unayoweza kuitumia kuandika kitabu chako. Zipo platform nyingi,  zingine ni za kulipia lakini katika makala hii nitaelezea hii platform ya bure ili uweze kuitumia kuandikia kitabu chako. Baadaye kama utaamua kutumia huduma za kulipia basi ni uamuzi wako. Sasa hebu tuangalie platform hii:

Canva

Canva ni platform nzuri sana unayoweza kuitumia kuandika na kudesign kitabu chako. Canva ina matoleo mawili, moja ni la bure na la pili ni la kulipia. Platform hii itakuwezesha kutengeneza kitabu chako na kukiwekea kava zuri na la kuvutia. Pia canva ina template nyingi na nzuri ambazo unaweza kuzitumia kurahisisha kazi yako. Hapa unachagua template ya kitabu unachokipenda na kazi yako itakuwa ni kuweka maandishi na picha za kitabu chako.

Ninachokipenda zaidi kwenye canva ni kuwa, kila kitu unachokitumia kudesign kitabu chako ni bure. Hata picha nyingi zilizopo ni za bure japokuwa kuna baadhi ya picha ambazo ukitaka kuzitumia kwenye kitabu chako unalipia $ 1 kwa kila picha. Baada ya kuwa umemaliza kuandika kitabu chako canva inakuruhusu kukipakua kwa miundo mbalimbali kama vile PDF n.k.

6. Uza kitabu chako kwa jamii inayokuzunguka

Wapi unapaswa kuanzia kuuza kitabu chako? Jibu zuri ni kwamba, baada ya kuandika vitabu au kitabu kama ni kimoja, uza kitabu chako kwa watu wanaokufahamu. Hii inamaanisha kama una blog, anza kuuza kitabu chako kwa wasomaji wa blog yako waliopenda makala zako. Kama una channel ya Youtube, anza kwa kutangaza na kuuza kitabu chako kupitia channel yako.

Jinsi ya kuuza kitabu chako kwa watu wanaokufahamu.

Kama una blog na umekuwa ukiandika makala nyingi kwa muda mrefu, wasomaji wa makala zako watakuwa ni watu wa kwanza kufurahia kununua na kusoma kitabu chako. Hasa hasa wale waliopenda makala zako na wakajiunga kwa kusubscribe kwa kutumia email zao ili wapate taarifa kila unapoweka makala mpya. Hii ndio sababu watu wanaokufahamu na kupenda kazi yako wanatakiwa kuwa wa kwanza kuwauzia kitabu chako.

Tumia Email kutangaza kitabu chako.

Kama una orodha ya watu waliojiunga kwenye blog yako kwa kusubscribe, unaweza kutangaza kitabu chako kwa kuwatumia email zinazoelezea manufaa ya kununua kitabu chako.

Tangaza kitabu chako kwenye mitandao ya kijamii.

Fungua akaunti kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuelimisha watu juu ya mada mbalimbali zinazowiana na kitabu chako. Hapo utapata wafuasi (followers). Baadaye unaweza kuwaandikia makala ukielezea manufaa ya kitabu chako na namna wanavyoweza kutatua matatizo yao watapokuwa wamesoma kitabu chako.

7.Ongeza mauzo ya kitabu chako kwa kuuza kwenye mtandao wa GetValue na Amazon.

Kufanya mauzo kwa kutumia blog yako ni hatua ya kwanza. Hapo unaweza kuandika vitabu na kuwauzia wasomaji wa blog yako na watu wanaofuatilia makala zako. Hatua nyingine ya kufanya mauzo ni kwa kuuza kitabu chako kwenye mitandao mingine ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kuuzia vitabu. Kwa hapa Tanzania mtandao unaoweza kuuza kitabu chako ni GetValue. Ni bure kabisa kuuza kitabu chako kwenye mtandao huu. Unachotakiwa kufanya ni kujisajiri tu kama muuzaji na baadae unaweka kitabu chako mtandaoni kwa ajili ya mauzo.

Mtandao mwingine ni Amazoni. Huu ni mtandao mkubwa sana au ni soko kubwa sana la mtandaoni lililopo nchini Marekani. Soko hili huwawezesha watu kuuza bidhaa za aina zote mtandaoni. Ili uweze kuuza kitabu chako kupitia Amazon, hatua ya kwanza ni kujisajiri kwenye soko hili na baadaye utaweza kuuza kitabu chako.

Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kutosha yatakayokuwezesha kuanza kuandika vitabu. Kama una swali au maoni yoyote usisite kuandika hapa chini. Asante sana na karibu kwenye makala zinazofuata.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

4 Replies to “Jinsi Ya Kuandika Na Kuuza Vitabu Pepe.”

  1. nimeelewa vizuri asante lakini nina swali je e book inatakiwa baada ya kuandika upate umiliki wowote? yaani kukisajili hati miliki n.k au unaweza kukiuza baada tu ya kumaliza kuandika kikakamilika ?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp