Jinsi Ya Kuandaa Na Kuuza Kozi Za Mtandaoni.

Mwongozo wa jinsi ya kutengeneza kipato kwa kuandaa na kuuza kozi za mtandaoni (online courses)

Jinsi Ya Kuandaa Na Kuuza Kozi Za Mtandaoni.

Karibu mpendwa msomaji wangu ili uweze kujifunza kupitia mwongozo huu wa bure kabisa ambao nimeuandaa kwa ajili yako. Katika mwongozo huu nitazungumzia jinsi ya kutengeneza kipato kwa kuuza kozi za mtandaoni.

Kozi za mtandaoni ni njia nzuri sana ya kuelimisha jamii ujuzi ulionao na wakati huohuo ukiwa unaingiza pesa. Hapa ninazungumzia ujuzi wowote ulionao. Inawezekana ukawa ni ujuzi uliosomea chuoni au ni ujuzi uliojifunza mahali pengine au ni ujuzi unaotokana na kipaji chako. Kumbuka kuwa, kila ujuzi unahitajika katika jamii na hivyo unaweza kubadilisha ujuzi ulionao ukawa chanzo cha kutengeneza kipato. Katika mwongozo huu tutaangalia mambo yafuatayo:

  1. Nini maana ya kozi za mtandaoni?
  2. Kwa nini watu wanapenda kujifunza kupitia kozi za mtandaoni?
  3. Kwa nini kozi za mtandaoni ni njia nzuri ambayo itakunufaisha wewe pamoja na jamii yako?
  4. Vikwazo katika uandaaji wa kozi vinavyotokea mara kwa mara kwa watu wengi.
  5. Jinsi kozi za mtandaoni zinavyofanya kazi.
  6. Ina maana gani tunaposema kuandaa kozi.
  7. Aina za kozi za mtandaoni.
  8. Je, kozi za mtandaoni ni kwa ajili ya kila mtu?
  9. Jinsi ya kutengeneza kozi za mtandaoni.
  10. Jinsi ya kuuza kozi za mtandaoni.
  11. Dondoo zaidi katika kuandaa na kuuza kozi mtandaoni.
  12. Dondoo 26 kutoka kwa waandaaji wa kozi maarufu za mtandaoni.
  13. Makosa 11 ya kuepuka unapoandaa na kuuza kozi za mtandaoni.
  14. Ushauri wa mahali pa kuandalia na kuhifadhi kozi yako ya mtandaoni kwa ajili ya kuuza.   

1. Nini maana ya kozi ya mtandaoni?

Jinsi Ya Kuandaa Na Kuuza Kozi Za Mtandaoni.

Kozi ya mtandaoni ni mazingira ambapo mtu anaweza kuingia na kujifunza maarifa au ujuzi fulani kwa kutumia kifaa chake cha kidigitali kama vile simu janja (smartphone) au computer.

Kozi ya mtandaoni ni njia nzuri sana ya kutoa maarifa au ujuzi ulionao kwa wateja wako wakati huohuo ukijenga jamii kubwa ya watu wanaokutegemea na kukuheshimu (authority) na kutengeneza kipato endelevu (passive income).

Kozi za mtandaoni ni njia nzuri sana ya kufundisha ujuzi ulionao kwa jamii yako wakati huohuo ukiwa unatengeneza kipato. Kwa mujibu wa Stratistics MRC, soko la dunia la kozi za mtandaoni linategemea kukua kutoka  $176.12 billion mwaka 2017 hadi $398.15 billion ifikapo mwaka 2026!

Hili ni soko kubwa sana na linalokua kwa kasi sana hivyo tumia fursa hii kuweza kukuza kipato chako.

2. Kwa nini watu wanapenda kujifunza kupitia kozi za mtandaoni?

Jinsi Ya Kuandaa Na Kuuza Kozi Za Mtandaoni.

Kama wewe ni kama waandaaji wengine wa kozi, unahitaji kuandaa kozi kwa sababu unahitaji kushirikisha wengine ujuzi ulionao. Kwa takwimu za mwaka 2017, asilimia 63 ya waandaaji wa kozi waliandaa kozi kwa ajili ya kushirikisha jamii maarifa na ujuzi waliokuwa nao kama lengo lao kuu la msingi ukilinganisha na asilimia 48 tu ambao waliandaa kozi kwa lengo kuu la kupata pesa.

Lakini hebu niwe mkweli katika hili; faida kubwa ya kuandaa kozi ni kutengeneza mfereji wa kukuingizia kipato bila kutumia nguvu kubwa baada ya kuwa umemalisha kuandaa kozi yako. Kozi yako ya mtandaoni itakupatia kipato endelevu kwa miaka mingi ijayo (passive income) wakati huohuo ukiinufaisha jamii yako kwa kuipatia ujuzi ulionao na hivyo kukufanya uheshimike (authority) katika taaluma au ujuzi wako.

Katika upande wa pili, kwa wanafunzi wanaochukua kozi za mtandaoni, wamependa kozi hizi kwa sababu zifuatazo;

i. Urahisi wa upatikanaji

Kwa kutumia kozi za mtandaoni, huhitajiki kuchukua madaftari na kusafiri mwendo mrefu kwenda shuleni na kuingia kwenye chumba cha darasa kujifunza. Kujifunza kozi mtandaoni ni rahisi sana kwani unahitajika tu kuwa na komputer yako na unaweza kusoma popote ulipo. 

ii. kupata mafunzo kulingana na mahitaji yao

Kuna sehemu nyingi ambazo watu wanaweza kujifunza ujuzi wanaouhitaji kwa kutafuta kwenye google. Lakini unapokuwa umeandaa kozi unawasaidia watu kuweza kupata maarifa yote wanayoyahitaji bila kulazimika kutafuta sehemu mbalimbali sehemu ya maarifa hayo. Hivyo mtu anapokuwa amejiunga kwenye kozi, anapata maarifa yaliyokamili sehemu moja.

.

iii. Gharama nafuu.

Ukilinganisha na aina nyingine za mafunzo, kozi za mtandaoni zina gharama nafuu. Hakuna gharama za usafiri kwani mambo yote mtu anayopaswa kujifunza yamewekwa mtandaoni na anaweza kuyaona mahali popote alipo.

3. Kwa nini kozi za mtandaoni ni njia nzuri ambayo itakunufaisha wewe pamoja na jamii yako?

Jinsi Ya Kuandaa Na Kuuza Kozi Za Mtandaoni.

Kozi za mandaoni huwawezesha wanafunzi kuweza kuzama ndani zaidi kwenye ujuzi wanaojifunza. Kozi iliyoandaliwa vizuri huwa na kila kitu mwanafunzi anachopaswa kukifahamu kulingana na ujuzi anaojifunza.

Kwa upande wako wewe uliyeandaa kozi, faida utakayopata ni kubwa sana. Kama kozi yako umeiandaa vizuri na inawasaidia watu kuweza kutatua changamoto zao, itawafanya watu wakuone kuwa wewe ni mtaalamu uliyebobea kwenye eneo unalofundisha na hivyo kuheshimika katika jamii (authority), unakuwa na watu wengi wanaokufuatilia na kukuamini (followers) wakati huohuo ukiwa unatengeneza kipato kutokana na kuuza kozi yako. Pia unapokuwa umeandaa kozi ya mtandaoni, inakuwezesha kuhudumia watu wengi kwa wakati mmoja na mahali popote duniani.

4. Vikwazo katika uandaaji wa kozi vinavyotokea mara kwa mara kwa watu wengi.

Kimsingi, kama tulivyoona hapo kabla, kabla ya kuandaa kozi jambo la kwanza kabisa kufikiria ni:” ni matatizo gani, changamoto gani au mahitaji gani jamii yangu inayo?” Baada ya hapo jiulize “je italeta maana kama nitaandaa kozi na kuuza kwa jamii yangu ili iwasaidie kutatua changamoto zao?

Kama jibu lako litakuwa ni hapana, basi kuandaa kozi kutakuwa sio chaguo sahihi kwako.

Mawazo hasi matano ambayo huwafanya watu wawe na hofu kuandaa kozi.  

i. “Sina ujuzi wa kutosha kuhusiana na mada ninayotaka kufundisha,” au, “sijasomea mada hiyo.” Ni kweli kuwa huna ujuzi wa kutosha kufundisha mada hiyo au hujui uanze vipi kuandaa kozi hiyo? Hivyo lazima ujue tofauti kati ya dhana hizo mbili. Kama hauna ujuzi wa kutosha, basi unaweza kuboresha kidogo ujuzi wako na ukaanza kuandaa kozi yako. Siyo lazima ubobee sana kwenye mada unayotaka kufundisha. Unachotakiwa kufahamu ni kitu gani unachotaka kufundisha ambacho watu wakijifunza kitawasaidia kutatua changamoto zao.

ii.“kuna watu wengine wanaofundisha mada ninayotaka kufundisha.” Sasa hebu nikuambie hiki kitu ambacho kitakushangaza: kama kuna watu wamefanikiwa kwa kufundisha mada unayotaka kufundisha, basi ujue kuwa soko lipo na hivyo watu wanahitaji ujuzi huo. Hivyo kuna uwezekano mkubwa wa wewe kuboresha kile ambacho watu wengine wanafundisha kwa kuangalia mapungufu waliyonayo washindani wako na hivyo kuweza kuliteka soko.

iii. “sina idadi kubwa ya watu wanaonifuatilia (followers).” Huhitaji kuwa na kundi kubwa la watu wanaokufuatilia kuweza kuandaa kozi na kuiuza mtandaoni. Unachotakiwa ni kulenga kundi dogo tu la watu unaotaka kutatua changamoto zao.

iv. “sina ujuzi wa kutosha wa komputer.” Hiyo ni sawa, nitakuonesha jinsi unavyoweza kuandaa kozi yako hata kama ukiwa huna ujuzi wowote wa komputer.

v. “sijui jinsi ya kutangaza na kuuza kozi yangu.” Hilo ni sawa, niakuelezea jinsi unavyoweza kuitangaza kozi yako na kuiuza mtandaoni.

5. Jinsi kozi za mtandaoni zinavyofanya kazi.

Jinsi Ya Kuandaa Na Kuuza Kozi Za Mtandaoni.

Kozi ya mtandaoni kwa lugha rahisi ni mazingira yaliyoandaliwa kwa ajili ya watu kujifunza maarifa au ujuzi fulani kupitia mtandao wa internet. Kozi nyingi wakati mwingine huwa zinakuwa na jukwaa ambalo wote wanaochukua kozi wanaweza kukutana mtandaoni, kujadili na kutoa maoni kwa pamoja kutokana na maarifa wanayojifunza.

Katika kuandaa kozi unaweza kufundisha kwa kutumia njia mbalimbali kuweza kufikisha ujumbe kama vile maandishi, video au ujumbe kwa njia ya sauti(audio). Pia unaweza kutoa mazoezi ili wanafunzi wa kozi yako waweze kujipima kama wameelewa vizuri somo lako. Kwa upande wako wewe muandaaji wa kozi, utapata faida nyingi zikiwemo kutambulika kama wewe ni mtaalamu uliyebobea, utaongeza jamii inayokuamini na kukufuatilia na wakati huohuo ukitengeneza pesa kwa kuuza kozi yako.

Jambo la msingi kukumbuka ni kuwa, kuandaa na kuuza kozi mtandaoni siyo njia ya kupata utajiri wa haraka kama wa bahatinasibu. Unatakiwa kuwekeza nguvu kubwa katika kuandaa kozi yenye ubora na inayotatua matatizo ya watu halafu pesa utaiona kama matokeo ya kuwekeza nguvu zako. Uzuri ni kuwa baada ya kuwa umeandaa kozi yako na kuiweka mtandaoni, itaendelea kuwa chanzo cha kukuingizia mapato kwa miaka mingi ijayo (passive income).

6. Ina maana gani tunaposema kuandaa kozi.

Sasa hebu tuangalie mambo kadhaa ambayo yakiwepo kwa pamoja yataifanya kozi yako kuwa bora na inayotegemewa kuleta mabadiliko katika jamii yako;

i. KOZI YAKO LAZIMA IJIKITE KATIKA KUTATUA MATATIZO NA KULETA MABADILIKO KATIKA JAMII.

Kuna jambo kubwa na muhimu ambalo kozi yako ili iweze kufanikiwa inapaswa kuwa nalo. Jambo hilo ni uwezo wa kozi yako kutatua tatizo la jamii.

Kozi yako lazima iwe na ‘kwa nini’ au matokeo ambayo yatapatikana baada ya mtu kujifunza na kumaliza kozi yako. Hapa kuna mifano michache ya kozi zinazoleta matokeo (mabadiliko) kwa jamii na zile ambazo hazileti mabadiliko.

KOZI ISIYOLETA MABADILIKO KATIKA JAMII  KOZI INAYOLETA MABADILIKO KATIKA JAMII  
Mfano: Jinsi ya kutengeneza video.  Mfano: Jinsi ya kutengeneza video ili kujipatia kipato kwenye mtandao wa Youtube.  
Mfano: Jinsi ya kutangaza biashara  Mfano: Jinsi ya kutangaza biashara ili kupata wateja wengi kwenye biashara yako yoyote.  

Kama utaweza kuweka kwa usahihi matokeo unayotegemea kuwa kozi yako itayaleta kwa jamii utakuwa katika hatua nzuri sana ya kuandaa kozi ambayo itapendwa na kuuzika kwa watu wengi. Kumbuka kuwa watu huwa wananunua kozi ili kujifunza maarifa au ujuzi utakaowawezesha kutatua matatizo yao.

  • UJUZI (EXPERTIZE)

Baada ya kuwa umeainisha matatizo unayotegemea kutatua kwenye kozi yako hatua inayofuata ni kutoa maarifa na ujuzi wako. Ninaposema ujuzi simaanishi mpaka uwe umesoma Chuo au Chuo Kikuu. Kuwa na ujuzi ni kufahamu maarifa ambayo wengine hawana.

Kuna njia nyingi ambazo unaweza kuzitumia kufikisha ujumbe au ujuzi wako. Miongoni mwa njia hizo ni:

i. Video

ii. Sauti -audio

iii. Maandishi-written materials

iv. Vitu vya kupakua –downloads

Katika aina hizi unaweza kutumia mojawapo au kutumia zote ili kufanya kozi yako iwe nzuri na yenye kuvutia. Baadhi ya sehemu unaweza kutumia video, sehemu zingine maandishi ambayo mtu anaweza kujisomea, sehemu zingine unaweza kuweka material ambayo mtu atapakua na kujifunza Zaidi. Njia hizi zote zitakusaidia kufanya kozi yako kuwa na mvuto.

Ninashauri kutumia njia nyingi za kufikisha ujumbe kwenye kozi yako. Kwa nini? Kwa sababu kila mtu ana aina yake ya kujifunza.

Swali jingine ni ni kuwa, “Niweke material mengi kiasi gani ili kozi yangu iwe na mafanikio?”

Hapa jibu ni fupi tu. Weka material machache, rahisi kueleweka na yaliyopangiliwa vizuri. Lengo la kozi ni kutatua tatizo na sio wingi wa maelezo au urefu wa video.

ii. WEKA RATIBA YA KUWASILIANA NA WANAFUNZI WAKO.

Ingawa kozi nyingi huwa zinaandaliwa na kuwekwa mtandaoni ambapo mtu anajiunga na kujifunza mwenyewe, unaweza pia kuweka ratiba ya masaa fulani ambayo utakuwa umeyatenga kwa ajili ya watu kuwasiliana na wewe ili kupata ushauri zaidi wa kitaalamu.

7. Aina ya kozi za mtandaoni

Sasa hebu tuangalie aina za kozi za mtandaoni ambazo unaweza kuziandaa.

i. Kozi ya bure kupitia barua pepe (Free email Course)

Hii ni kozi ambayo unaweza kuitoa bure kwa waliojisajiri kwenye tovuti yako (subscribers). Hapa unakuwa umeandaa masomo yako ambayo utakuwa unayatuma kwa njia ya barua pepe. Unaweza kufanya kozi yako kuwa ni ya mfululizo wa siku tatu, tano, saba na kadhalika. Kila siku unatuma email moja kwa wasomaji wako waliojisajiri na kila email inakuwa na somo moja.

ii. Kozi ya Bure ya Video (Free Video Course)

Hii ni aina ya kozi ambayo utaandaa video yenye mafunzo na kuiweka kwenye tovuti yako. Hii inahitaji muda kidogo kuiandaa, lakini baada ya kuwa umeiandaa na kuiweka kwenye tovuti yako, itavuta watu wengi kupenda kuwa kwenye tovuti yako.

iii. Kozi fupi ya kulipia (Paid Short Course)

Hapa unaandaa moduli zenye material ambayo utakuwa umeelezea kwa undani ujuzi wako kuliko kwenye kozi fupi ya video ambapo utatoza watu kiasi fulani cha pesa kuweza kujifunza kozi yako.

iv. Kozi ya kulipia ya urefu wa Kati (Paid medium-length course)

Huu ni mkusanyiko wa module nyingi zenye kuelezea kwa undani ujuzi wako.

v. Kozi ndefu ya kulipia (Paid high-end Course)

Kozi ya aina hii Ina mkusanyiko wa aina mbalimbali za mbinu za kufikisha ujumbe ikiwemo na kozi kuunganishwa kwenye kwenye group la Facebook pamoja na kuwa na masaa ya kusikiliza changamoto za wanafunzi na pia kutoa ushauri zaidi wa kitaalamu (coaching).

Kama unavyoona, unaweza ukaanza na kuandaa kozi fupifupi na baadaye kadiri unavyoendelea kuwa na uzoefu ukaendelea na kozi ndefu.

8. Je, mtu yeyote anaweza kuandaa kozi ya mtandaoni?

Jibu ni ndio. Inawezekana kabisa kuandaa kozi Mtandaoni na kutengeneza kipato. Kama unahitaji kuandaa kozi na hujui uanzie wapi, maswali yafuatayo yatakusaidia kupata wazo Bora la kuandaa kozi yako.

i. Ni kitu gani unachopendelea (passion)

Kama una kitu unachokipenda, basi ninaamini utakuwa na mambo mengi ya kuwafundisha wengine. Kwa mfano, unaweza kuwa ni mpenzi wa mapishi, biashara, ubunifu na kadharika. Unaweza kuandaa kozi kufundisha kile unachokipenda na watu wakakulipa.

ii. Una uzoefu gani?

Inawezekana una uzoefu wa kufanya kazi fulani, basi kupitia uzoefu wako unaweza kuandaa kozi ambayo utawashirikisha wengine uzoefu wako na wakakulipa.

iii. Una ujuzi gani?

Inawezekana una ujuzi uliojifunza mtaani au chuoni, ujuzi huo ni mtaji wa kutosha wa wewe kuandaa kozi na kuiuza Mtandaoni.

9. Jinsi ya kutengeneza kozi ya mtandaoni

  1. Lenga kundi la watu unaotegemea kutatua changamoto zao
  2. Fanya utafiti wa kozi yako mtandaoni
  3. Weka kichwa cha habari kinachoelezea jinsi kozi yako inavyoenda kutatua changamoto na kuleta mabadiliko(Transformation)
  4. Anza kufikiria mambo utakayoelezea kwenye kozi yako.
  5. Pangilia mawazo yako katika mtiririko mzuri.
  6. Weka dondoo za kozi yako
  7. Anza kuitangaza kozi yako kabla ya kuanza kuuza.
  8. Jenga mahusiano na wateja wako watarajiwa.
  9. Tengeneza kozi yako
  10. Anza kuuza kozi yako na uanze kupokea mrejesho(feedback)
  11. Boresha kozi yako kulingana na mrejesho unaoendelea kuupata kutoka kwa wateja wako.
  12. Endelea kuuza kozi yako!

Sasa ni muda muafaka wa kuanza kutengeneza kozi yako. Kuna mambo mengi ya kufanya lakini sio kazi ngumu. Ni kazi ambayo utaifanya ukiwa unafurahia kwa sababu utakuwa unafanya kitu unachokipenda kutoka moyoni.

Jambo la kwanza kabisa ambalo unatakiwa kulifikiria ni kichwa cha habari cha kozi yako. Hapa ndio kwenye kiini cha mawazo yako na malengo yako ya kuandaa kozi.

Kama ndio mara ya kwanza kabisa kuandaa kozi na wakati mwingine hujui uandae kozi ya aina gani, zingatia maswali niliyoyaainisha sehemu iliyopita. Hata hivyo nitayarudia ili uweze kupata mtiririko mzuri wa namna bora ya kupata wazo bora la wewe kuandaa kozi.

1. Fikiria ni kitu gani unachokipenda au kupendelea kukifanya (passion)

Kama una kitu unachokipenda, basi ninaamini utakuwa na mambo mengi ya kuwafundisha wengine. Kwa mfano, unaweza kuwa ni mpenzi wa mapishi, biashara, ubunifu na kadharika. Unaweza kuandaa kozi kufundisha kile unachokipenda na watu wakakulipa.

2. Ni uzoefu gani ulionao katika kazi au uliowahi kupitia katika maisha?

Inawezekana una uzoefu wa kufanya kazi fulani, basi kupitia uzoefu wako unaweza kuandaa kozi ambayo utawashirikisha wengine uzoefu wako na wakakulipa.

3. Chunguza vizuri ujuzi ulionao.

Inawezekana una ujuzi uliojifunza mtaani au chuoni, ujuzi huo ni mtaji wa kutosha wa wewe kuandaa kozi na kuiuza Mtandaoni.

Sasa hebu tuanze kuangalia hizi hatua kwa undani zaidi.

Hatua ya 1: Lenga kundi la watu unaotegemea kutatua changamoto zao.

Kabla ya kufikiria mada unayotaka kuiandalia kozi, jambo la kwanza kabisa ni kufikiria ni kundi gani la watu unalotaka kulilenga. Pia unatakiwa kufikiria katika kundi hilo la watu unalotaka kulilenga, unataka kutatua tatizo gani? Kwa mfano, unahitaji kulenga kundi la wanafunzi wahitimu wa vyuo vikuu. Hilo ni kundi la watu. Baada ya kuwa umechagua kundi hilo basi unapaswa kuainisha matatizo waliyonayo na ambayo unataka kutatua kwa kuandaa kozi.

Kama hauna kundi lolote ambalo unafikiria kuuza ujuzi wako, unaweza kupata wazo kwa kutembelea kwenye magrupu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na kuangalia mijadala mbalimbali inayoendeshwa humo au unaweza kutembelea majukwaa (forum) mbalimbali na kuona watu wanauliza maswali gani wanayohitaji msaada. Kwa kutumia maswali yanayoulizwa mara kwa mara au mijadala inayoendelea, unaweza kugundua ni changamoto gani inayowakumba watu na hivyo unaweza kupata wazo la kozi unayopaswa kuandaa

Hatua ya 2: Fanya utafiti wa kozi yako mtandaoni

Baada ya kuwa umechagua kundi unalotaka kulilenga, sasa ni wakati wa kufanyia utafiti kozi yako ni kwa namna gani itatatua changamoto za kundi ulilolilenga. Unaweza kuchunguza mtandaoni kwa kutembelea kwenye magrupu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na kuangalia maswali na mijadala mbalimbali inayoendeshwa humo. Pia unaweza kutembelea majukwaa (forum) mbalimbali kama vile Jamii Forum na majukwaa mbalimbali na kuona watu wanauliza maswali gani wanayohitaji msaada. Kwa kutumia maswali yanayoulizwa mara kwa mara au mijadala inayoendelea, unaweza kugundua ni kwa jinsi gani changamoto hiyo ni kubwa na hivyo ukiandaa kozi utapata watu wengi ambao watakuwa tayari kununua kozi yako.

Angali ushindani uliopo (competition)

Baada ya kuwa umeona changamoto zinazokabili kundi ulilolichagua, unaweza pia kuangalia ni watu kiasi gani wanaofundisha na ni kozi kiasi gani zilizopo mtandaoni zinazotatua changamoto za kundi hilo. Hii itakusaidia kuandaa kozi ambayo itakuwa imejitofautisha na kozi zingine zilizopo mtandaoni.

Hatua ya 3: Weka kichwa cha habari kinacholezea jinsi kozi yako inavyoenda kutatua changamoto za kundi ulilolilenga na kuleta mabadiliko(Transformation)

Katika hatua hii, tunaenda kuandaa kichwa cha habari kinachoenda kutatua changamoto tulizoziona kwenye kundi tulilolichagua. Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wahitimu wa vyuo ni kukosa mitaji ya kuanzisha biashara au kujiajiri. Hivyo unaweza kuandaa kozi inayoweza kutatua tatizo hilo. Mfano: Jinsi ya kuanzisha biashara na kutengeneza kipato bila kuwa na mtaji wa pesa. Unaona! Kozi kama hiyo inaenda kutatua changamoto zao za kukosa mitaji na hivyo kuwawezesha kuanzisha biashara. Ukiandaa kozi inayolenga kundi la watu na inayotatua changamoto zao, hiyo kozi yako itauzika.

 Hatua ya 4: Anza kufikiria mambo utakayoelezea kwenye kozi yako.

Mwanzoni kabisa tulianza kwa kuchagua kundi la watu katika jamii ambalo tunahitaji kulilenga na baadaye tukaangalia changamoto ambazo kundi hilo linapitia. Kisha tuliangalia ni kozi gani tunaweza kuandaa ambayo inaweza kutatua changamoto zao na tukaainisha kichwa cha habari kinachoakisi ni kwa namna gani kozi itatatua changamoto zao. Hatua hii ni rahisi kwani unatakiwa sasa kufikiria ni mambo gani utayaweka kwenye kozi yako. Hapa ninamaanisha ni mada ngapi na ni zipi ambazo utaziweka ili kozi yako iweze kueleweka na kuweza kukamilisha ujuzi ulioukusudia kisha orodhesha mada hizo. Kwa mfano, katika kichwa cha habari cha kozi niliyoitolea mfano hapo awali:

Jinsi ya kuanzisha biashara na kutengeneza kipato bila kuwa na mtaji wa pesa, mada zinazounda kozi hiyo zinaweza kuwa:

  1. Maana ya biashara
  2. Aina za biashara
  3. Mtaji ni nini?
  4. Aina za mitaji
  5.  …………….
  6. ……………..
  7. …………….na kadharika.

Hatua ya 5: Pangilia mawazo yako katika mtiririko mzuri.

Baada ya kuwa umeorodhesha mada ambazo unafikiria zinafaa kuwepo kwenye kozi yako, hatua hii ni rahisi kwani unatakiwa kupangilia mada zako katika mtiririko unaofaa ili mtu anapokuwa anajifunza apate somo lililokamilika. Hapa unaangalia ni mada gani ianze na ipi umalizie ili mwanafunzi aweze kuelewa.

Hatua ya 6: Weka dondoo za kozi yako

Baada ya kuwa umepangilia kozi zako katika mtiririko unaoeleweka, sasa kwa kila mada weka dondoo za mambo muhimu ambayo utafundisha. Hii itakusaidia kutokusahau mambo muhimu katika kila mada. Kwa mfano, Katika kozi tuliyoichagua:

Jinsi ya kuanzisha biashara na kutengeneza kipato bila kuwa na mtaji wa pesa, kwa kila mada unaweza kuiwekea dondoo ya mambo muhimu utakayo zingatia unapokuwa unafundisha mada hiyo. Mfano:

  1. Maana ya biashara
  2. Maana mbalimbali za biashara
  3. Historia ya biashara
  4. ……………………..
  5. …………………….na kadharika
  6. Aina za biashara
  7. ……………………
  8. …………………….na kadharika.

Hatua ya 7: Anza kuitangaza kozi yako kabla ya kuanza kuuza.

Hatua hii ni muhimu sana na unapaswa kuwa makini sana. Watu huwa hawaingii mtandaoni ili kununua kozi. Watu wanaingia mtandaoni ili kupata suluhisho la matatizo yao. Hivyo, hatua ya kwanza unatakiwa kuanza kujenga mahusiano na wateja wako watarajiwa kwa kufundisha bure ujuzi wako na kuwasaidia kutatua matatizo yao. Hapa unaweza kuanzisha blog na kufungua akaunti kwenye mitandao ya kijamii kama vile facebook, youtube, twitter na kadhalika. Weka Makala au rekodi video zinazotatua changamoto za watu. Unapokuwa unafanya hivi unawafanya watu wakuamini kuwa wewe ni mtaalamu na unaweza kuwa msaada kwao katika kutatua changamoto zao. Hivyo watakupenda na kukuamini. Unapokuwa umepata watu wanaopenda makala au video zako, basi unaweza kuanza kuuza ujuzi wako kupitia kozi uliyoiandaa.

Hatua ya 8: Jenga mahusiano na wateja wako watarajiwa.

Hatua ya 8 imejengwa kwenye hatua ya 7 ambayo inahusu jinsi ya kuangaza kozi yako kabla ya kuanza mauzo. Katika hatua ya 7 nilizungumzia namna ya kujenga uaminifu kwa wateja wako kwa kuanzisha blog au youtube channel ili utambulike kwa wateja kuwa wewe kweli ni maalamu wa kile unachofundisha na kuwa unaweza kutatua matatizo ya wateja wako. Hatua hii inahusu jinsi ambavyo unavyoweza kujenga mahusiano na wateja wako watarajiwa. Hapa unatakiwa kujibu komenti za wasomaji wa blog au watazamaji wa channel yako na kujibu maswali yao. Pia kama kuna mtu atahitaji msaada zaidi unaweza kumsaidia. Hii itakufanya upendwe na wasomaji wako na hivyo itakuwa rahisi kwa wewe kuweza kuwauzia kozi yako. Katika hatua hii pia unaweza kufungua group la facebook ambapo utakuwa unatoa msaada kwa wafuasi wako.

Hatua 9: Tengeneza kozi yako

Sasa tunaingia katika hatua ya kuanza kutengeneza kozi yako. Hatua hii sio ngumu kwani utatumia dondoo ambazo utakuwa umezitengeneza katika hatua ya 6. Kazi kubwa ambayo utakuwa unaifanya ni kuandaa masomo kulingana na dondoo hizo. Unaweza kuamua kila dondoo ikawa ni somo linalojitegemea au vyovyote utakavyoona. Lengo ni kuleta mtiririko mzuri kwenye kozi yako. Katika kuandaa kozi yako, ili iwe na ubora na mvuto, jitahidi kuchanganya aina mbalimbali za mbinu za kufundisha kama vile video, maandishi na kadharika. Jitahidi kurekodi video nzuri zenye ubora. Kwa kipindi hiki cha utandawazi hauhitajiki kuwa na kamera ya bei kubwa kuweza kurekodi video nzuri kwani hata kwa kutumia simu janja (smartphone) unaweza kutengeneza video nzuri sana.

Weka bei ya kozi yako

Hatua ya mwisho katika kuandaa kozi ni kufikiria bei ambayo utakuwa unauza kozi yako. Hapa utaangalia thamani ya maarifa unayotoa na bei ambayo unafikiria walengwa wa kozi yako wataweza kununua. Kama kozi yako inatatua matatizo ya wateja wako, watu watakuwa tayari kununua hata kwa bei ya juu. Tumia busara katika kupanga bei ili wateja wako waweze kumudu kununua. usiweke bei a chini sana kwani itashusha thamani ya kozi yako.

 

Hatua ya 10: Anza kuuza kozi yako na uanze kupokea mrejesho(feedback)

Sasa kozi yako tayari imekamilika. Anza kuuza! Unapokuwa unauza hakikisha unafuatilia mrejesho wa wanafunzi wako ili kuona ni kwa jinsi gani wameipokea kozi yako. Hapa utaangalia maoni yote yanayotolewa ili uweze kufahamu ni sehemu gani unapaswa kuboresha zaidi. Maoni yote yanayotolewa hakikisha unayaandika ili uyaweke kwenye utendaji unapokuwa unafanyia maboresho kozi yako.

Hatua ya 11: Boresha kozi yako kulingana na mrejesho unaoendelea kuupata kutoka kwa wateja wako.

Baada ya kuwa umekusanya mrejesho kutoka kwa wateja wako, huu ndio wakati wa kufanyia kazi maoni yote ya wanafunzi wako ili uweze kuboresha kozi. Endelea kuboresha kozi yako kila mara unapopata mrejesho unaokuhitaji kufanya maboresho.

.

Hatua ya 12: Endelea kuuza kozi yako!

Hongera sana kwa kazi nzuri ya kuandaa kozi! Endele kuuza kozi yako lakini kumbuka kuboresha kozi yako mara kwa mara kila unapopata mrejesho unaokuhitaji kufanya maboresho.

10. Jinsi ya kuuza kozi za mtandaoni.

Tayari umekwisha andaa kozi yako na umeshaweka bei ni kiasi gani unaweza kuiuza, swali kubwa linalokuja hapa ni kuwa, ni kwa jinsi gani unaweza kupata wateja wa kununua kozi yako? Kama unahitaji kuwa na wateja wengi na endelevu wa kozi yako, katika sehemu hii nimekuainishia mbinu bora na zinazofanya kazi ambazo unaweza kuzitumia kuweza kupata wateja. Ili uweze kuzifahamu njia hizi vizuri na uweze kuzifanyia kazi, kwanza kabisa unatakiwa kufahamu kwa nini watu huwa wananunua kozi za mtandaoni. Ukifahamu sababu kubwa inayowafanya watu wanunue kozi mtandaoni, utafahamu ni mbinu zipi uzitumie ili kuweza kukidhi haja yao.

Sasa, hebu tuangalie sababu zinazowafanya watu wanunue kozi mtandaoni.

Kanuni 3 unazopaswa kuzifahamu zinazohusu jinsi ya kuuza kozi yako mtandaoni.

  • Kanuni ya 1: Watu huwa hawataki kununua kozi za mtandaoni.
  • Kanuni ya 2: Watu wanapenda mtu anayeaminika na anayewahakikishia ubora wa bidhaa yake.
  • Kanuni ya 3: Watu hununua kozi mtandaoni kwa sababu wanahitaji urahisi wa kupata ujuzi au maarifa yote sehemu moja.

Kuna njia nyingi sana unazoweza kuzitumia kutangaza na kuuza kozi yako mtandaoni zikiwemo kutumia email, kuanzisha blog na kuandika makala kwenye blog yako, kuanzisha youtube channel na kuandaa video mbalimbali kwenye channel yako, kutumia mitandao mingine ya kijamii kama vile facebook na kadhalika. Lakini njia hizi zote ambazo unaweza kuzitumia haziwezi kufanya kazi kama haujafahamu vizuri kanuni za jinsi ya kuuza kozi mtandaoni.

Unaweza kuwa na njia nzuri sana za mauzo, lakini kama hautafahamu kanuni hizi vizuri unaweza kupata hasara ya kutangaza kozi na bila kupata matokeo unayoyakusudia.

Kanuni ya 1: Watu huwa hawataki kununua kozi za mtandaoni.

Watu huwa hawapendi kununua kozi za mtandaoni. Subiri kidogo. Hapa unaweza kushangaa kwa nini ninasema hivyo. Ni kweli kabisa watu huwa hawapendi kununua kozi za mtandaoni. Utanielewa baadaye kidogo. Hebu fikiria, hivi ulishawahi kuchukua simu yako au computer yako na ukasema “leo ninataka kununua kozi ya mtandaoni”. Jibu ni hapana. Watu wanapokuwa wameamua kununua kozi, hawahitaji kozi kama kozi bali wanahitaji kupata matokeo watakayopata baada ya kuwa wamenunua hiyo kozi. Hii ni siri kubwa unayopaswa kuifahamu unapokuwa unahitaji kuuza kitu chochote mtandaoni na nje ya mtandaoni. Watu wanahitaji kutafuta njia rahisi za kutatua matatizo yao na kubadilisha maisha yao. Hivyo, kama kozi unayouza itajipambanua katika kutatua matatizo ya watu, watu watakuwa tayari kununua kozi yako. Hivyo unapokuwa unauza kozi yako mtandaoni, usiuze kozi bali uza suluhisho la changamoto za watu.

Kanuni ya 2: Watu lazima wakuamini kwanza (trust) ndio wanunue kozi yako.

Linapokuja suala la kuuza kozi mtandaoni, ni lazima watu wakupende na kukuamini ndipo watakapofanya maamuzi ya kununua kozi yako. Ili uweze kujenga uaminifu kwa wateja wako watarajiwa, anza kwanza kwa kuwafundisha jinsi ya kutatua changamoto zao. Unaweza kuwa unaandika makala mbalimbali kwenye blog yako au ukawa unarekodi video na kuziweka youtube zinazofundisha maarifa uliyonayo. Hii itasaidia watu kukufahamu na kukuamini kuwa kweli wewe ni mtaalamu wa kile unachowafundisha. Baada ya kuwa umepata watu wanaopenda masomo yako, basi hao ndio watakuwa wateja wako watarajiwa kwani watakuwa wamekwisha jenga uaminifu kwako kuwa unaweza kutatua matatizo yao.

Pia njia nyingine ya kujenga uaminifu kwa wateja wako ni kupitia shuhuda mbalimbali za watu waliosoma kozi yako na ikawasaidia. Swali unaloweza kujiuliza ni kuwa, “kozi yangu ni mpya na bado sijapata wateja, nitapataje hizo shuhuda za kuwaaminisha watu wengine?” Jibu ni rahisi. Unaweza kutoa ofa kwa kutoa bure kozi yako kipindi cha mwanzo na ukawaomba watu uliowapa ofa watoe shuhuda zao ni kwa namna gani wamenufaika na kozi yako. Kwa kufanya hivyo utakuwa umepata shuhuda mbalimbali ambazo zitakusaidia katika kutangaza na kuuza kozi yako kwa watu wengine.

Kanuni ya 3: Watu wananunua kozi za mtandaoni kwa sababu wanahitaji njia rahisi na ya haraka ya kutatua matatizo yao.

Kozi nyingi zilizopo mtandaoni zina maarifa ambayo yanaweza kupatikana bure mahali pengine mtandaoni. Sasa kwa nini watu wanunue maarifa ambayo wanaweza kuyapata mahali pengine mtandaoni tena bure? Watu wananunua kozi mtandaoni kwa sababu wanahitaji maarifa yote wanayoyahitaji katika kutatua changamoto zao yawe sehemu moja na hivyo kuokoa muda wao. Watu hawapendi kuzunguka mtandaoni wakitafuta hapa na pale maarifa wanayoyahitaji. Hivyo, wakipata kozi ambayo inaweza kutatua changamoto zao mara moja watanunua. Hivyo, kama una blog inayofundisha maarifa fulani, unaweza kupangilia makala zako na kuandaa kozi ambayo itawasaidia watu kuokoa muda katika kujifunza ujuzi huo.

11. Baadhi ya njia za kutangaza kozi mtandaoni.

Sasa hebu tuangalie baadhi ya njia unazoweza kuzitumia kutangaza kozi yako mtandaoni.

  • Kwa njia ya barua pepe (email). Kama una blog yako, watu waliojiunga kufuatilia makala zako (subscribers) unaweza kuwa unawatumia barua pepe zenye makala mbalimbali kuhusiana na kile unachofundisha. Kupitia makala hizo unaweza pia kuwafahamisha juu ya ofa ya kozi yako. Jambo unalopaswa kuwa makini nalo kwenye njia hii ni kuwa, tuma barua pepe nyingi za kufundisha na chache ndio ziwe za kutangaza kozi yako. Kwa kawaida watu huwa hawapendi kupokea matangazo mengi ya biashara. Wanapenda mtu aliyetayari kutatua matatizo yao. Hivyo ukituma barua pepe nyingi zenye kufundisha, hata kama ukituma barua pepe chache za kutangaza kozi yako, watu watanunua kwa sababu watakuwa wanakuona wewe kuwa ni msaada kwao.
  • Anzisha channel ya YouTube.ninapendekeza kutumia video zaidi unapokuwa unaandaa kozi kwa sababu ni njia nzuri sana ya kufikisha ujumbe. Pia katika kutangaza kozi yako, njia ya video ni njia nzuri sana kwa sababu inapendwa na wengi. Hivyo, unaweza kuanzisha channel ya youtube na ukawa unaweka video zinazofundisha ujuzi wako na utakapokuwa umepata subscribers, unaweza kuwajulisha kuwa, ili waweze kupata maarifa zaidi basi wajiunge na kozi yako. Katika njia hii pia jizatiti katika kutoa thamani zaidi kuliko kutangaza kozi yako. Kama utakuwa ukitoa video zenye kuelimisha, hata ukiwatangazia watu kuwa una kozi watakuwa tayari kununua kwa sababu watakuwa wanakufahamu vizuri kuwa wewe ni mtaalamu.
  • Tumia watu wengine wakutangazie kozi yako na uwapatie kamisheni (affiliate partnerships). Hii ni njia ambayo unaweza kutoa ofa kwa watu waliojiunga na kozi yako au mtu yeyote kukutangazia kozi yako kwa kushare kwa marafiki zao na kila mtu anayejiunga na kulipia kozi yako unatoa kamisheni kwa aliyemualika.
  • Kwa njia ya mdomo. Hapa unaweza kuwaomba watu waliojiunga na wakaipenda kozi yako kuwashirikisha marafiki zao uzuri wa kozi yako ili waweze kujiunga.
  • Kulipia matangazo (paid advertising). Njia nyingine nzuri sana ni kulipia matangazo facebook na Google. Unapokuwa umelipia tangazo facebook au Google unalifanya tangazo lako lionekane kwa watu wengi zaidi na wale hasa ambao ni walengwa. Nina uzoefu na kutangaza kupitia facebook. Unapokuwa umelipia tangazo facebook, wewe ndio utachagua kuwa tangazo lako lionekane mkoa gani na watu wa aina gani. Hivyo kwa kutumia matangazo ya kulipia yatakuwezesha kupata wateja uliokusudia kwenye kozi yako. 

12. Dondoo 6 kutoka kwa waandaaji maarufu wa kozi za mtandaoni.

1. Usiandae kozi kwa ajili ya kuuza. Andaa kozi kwa kile unachopenda kukifanya na mauzo yatafuata baadaye. – Resit, Master of Project Academy

2. Usiwe na hofu muda wote kuwa ni kwa jinsi gani utauza kozi yako bali muda wote hofu yako iwe ni kwa jinsi gani utaandaa kozi itakayotatua matatizo ya wanafunzi wako na kuwaletea mabadiliko katika maisha yao. David Perálvarez, Club SiliCODE Valley

3. Andaa kozi yenye maarifa ambayo watu hawawezi kuyapata mahali pengine kwa thamani hiyo na kwa ubora huo. Ukiweza kufanya hayo mambo mawili, utauza mpaka uchanganyikiwe. – Dakota Wixom, QuantCourse

4. Acha kuweka sababu nyingi kwamba wewe hauna ujuzi wa kutosha kuweza kufundisha. Jambo unalotakiwa kufanya ni kuweka siku ya mwisho ya kukamilisha kazi yako na ujizatiti kukamilisha kwa muda huo. Usitake mpaka kila kitu kiwe kimekamilika vya kutosha. Huwezi kufanya kitu kikamilike. Lenga kwenye maarifa unayotaka kuwapatia wanafunzi wako na utaendelea kuiboresha kozi yako kadiri inavyohitajika.

– Sarah, User Research Mastery

5. Fanya utafiti kwanza kuona kama kozi unayotaka kuandaa watu wanaihitaji. Usipoteze muda kuandaa kozi kabla ya kujua kama itauzika. Anza kidogo kidogo kwa kuandaa makala kwenye blog ili kuweza kupata wafuasi ambao ndio watakuwa wateja wako wa baadae. Baadaye anzisha kozi yako baada ya watu kuhitaji maarifa zaidi ya kile unachofundisha. – Sarah Crosley, The Creative Boss: Create the Ultimate Opt-In Offer

6. Hakuna kozi ambayo huwa imekamilika kabisa inapokuwa inaanzishwa. Ukitaka kuanzisha kozi iliyokamilika kabisa, hutaanza kwa kuwa kila unapotaka kuitoa utaona ina mapungufu. Anzisha kozi yako na endelea kuiboresha kadiri unavyoendelea kupata mrejesho kutoka kwa wanafunzi wako.– Daniel Milner, Make TV Easy

13. Makosa 9 unayopaswa kuyaepuka unapoandaa na kuuza kozi yako mtandaoni.

Sasa hebu tuangalie makosa ambayo waandaaji wa kozi wanaweza huyafanya mara kwa mara. Nimekuorodheshea makosa haya ili wewe uwe makini usiweze kuangukia kwenye makosa hayo unapokuwa ukiandaa kozi yako.

Kosa la 1: Kuandaa kozi bila kujali mahitaji ya wanafunzi wako walengwa.

Kama nilivyoelezea hapo awali, unatakiwa kuangalia kwanza mahitaji ya wanafunzi wako walengwa kabla ya kuandaa kozi. Unaweza kufahamu mahitaji ya wanafunzi wako kwa kuanzisha blog na kuwa unaweka makala za kufundisha ujuzi wako. Hapo utatambua ni kwa jinsi gani ujuzi wako unahitajika na hivyo kukuwezesha wewe kuandaa kozi.

Kosa la 2: Kutokuuliza mrejesho(feedback)

Kama unahitaji kuboresha kozi yako ni lazima uulize watu waliosoma kozi yako kukupatia mrejesho. Kwa kuzingatia mrejesho utakaokuwa unaupata kutoka kwa wanafunzi wako, utagundua udhaifu wa kozi yako na mahali unapotakiwa kuboresha. Kutokuuliza mrejesho ni kosa kubwa sana.

Kosa la 3: Kutokuboresha maarifa ya kozi yako kuendana na wakati.

Unaweza kuwa uliandaa kozi nzuri sana lakini kadiri siku zinavyoenda, mabadiliko ya teknolojia na utamaduni yakafanya baadhi ya maeneo ya kozi yako kupitwa na wakati. Jambo la muhimu ni kuboresha kozi yako ili iendane na wakati uliopo.

Kosa la 4: Kuchelewa kuweka kozi yako mtandaoni baada ya kukamilisha maandalizi.

Wakati mwingine unaweza kuwa umeandaa kozi na kukamilisha lakini ukawa unachelewa kuiweka mtandaoni ukihofia kuwa inawezekana haina ubora wa kutosha. Hapo unapoteza wakati. Ushauri wangu ni kuwa, ni jambo jema sana kuiweka kozi yako mtandaoni ili watu waanze kusoma na kadiri wanavyokuletea mrejesho utaendelea kuiboresha.  

Kosa la 5: Kutokutangaza vya kutosha kozi.

Baada ya kuwa umeandaa kozi yako na kuiweka mtandaoni, hatua inayofuata ni kuitangaza ili watu waifahamu na wajiunge. Kuna njia nyingi za kutangaza kozi yako kama vile nilivyozielezea hapo awali. Unaweza kutumia matangazo ya facebook, channeli ya youtube, kuandika makala kwenye blog yako na njia nyingine nyingi. Hivyo ni wajibu wako wa msingi kutangaza kozi yako.  

Kosa la 6: Kutokupanga vizuri bei ya kozi yako.  

Hakuna sheria hapa katika kupanga bei. Lakini jambo la kufahamu ni kuwa, ukiweka bei ya juu sana watu wanaweza kushindwa kujiunga. Lakini pia ukiweka bei ya chini sana, watu wataona kuwa kozi yako haina thamani na hivyo wanaweza kuitilia mashaka. Kwa hiyo weka bei ya wastani kulingana na aina ya watu unaowalenga kujiunga na kozi yako.

Kosa la 7: Kuandaa material katika ubora wa hali ya chini.

 Kichwa cha habari cha sehemu hii kinajieleza chenyewe. Kama material ya kozi yako hayana ubora, wanafunzi wako hawatafurahia kozi yako na hivyo utapoteza uaminifu kwa wateja wako na hivyo kupoteza wateja.

Kosa la 8: Kutokuwa na kiwango cha kutosha cha material kwenye kozi yako.

Kozi nzuri ni ile ina uwiano wa material ambayo yatawezesha maarifa kuweza kueleweka kwa wanafunzi. Wapatie wanafunzi wako kiwango kinachotosha tu kwa wao kuweza kuelewa. Usiwapatie material mengi sana kiasi cha kuwafanya wachanganyikiwe badala ya kuelewa. Au usiwapatie material machache sana kiasi cha kuwafanya wasielewe maarifa uliyokusudia wajifunze baada ya kuwa wamechukua kozi yako.  

Kosa la 9: Kutokuzingatia uwezo wako na mapungufu yako.

Je, una uwezo wa kuongea mbele ya kamera vizuri? Tumia uwezo huo kurekodi video nzuri ukiwa unafundisha kozi yako. Je kama hauwezi kuongea mbele ya kamera? Kama hauna uwezo au kipaji cha kusimama na kurekodi video mbele ya kamera, Siyo lazima uonyeshe sura yako unapotaka kurekodi video. Unaweza kurekodi kioo cha computer yako ukiwa unaelezea maarifa yako kwa kutumia software kama vile screen cast, Itop screen recorder na kadharika.

14. Ushauri wa mahali pa kuandalia na kuhifadhi kozi yako ya mtandaoni kwa ajili ya kuuza.    

Kwa kufikia hatua hii utakuwa umejifunza mengi kuhusiana na kutengeneza na kuuza kozi za mtandaoni ninakupongeza kwa kutumia muda wako mwingi kwa kufuatilia mwongozo huu ambao utakuwezesha kutengeneza kozi yako, kuitangaza na kuiuza mtandaoni. Katika hatua hii ya mwisho nitaenda kuelezea ni mahali gani unaweza kuhifadhi kozi yako ili watu waweze kujifunza mtandaoni. Kwa kuanzia unaweza kutumia mtandao wa YouTube kuweza kuandaa kozi yako.

JINSI YA KUFANYA

Andaa video za kozi yako na uziweke youtube. Kisha ziweke kwenye play list kuanzia video ya somo lako la kwanza hadi la mwisho. Kwenye mtandao wa YouTube kuna machaguo ya kuamua video zako zionekane na watu wote (public) au zionekane na watu pekee ambao utawapatia link ya video zako (unlisted). Weka play list ya video za kozi zako unlisted ili zisionekane mahali popote youtube isipokuwa kwa wale tu utakaowatumia link. Baada ya hapo tangaza kozi yako kwa njia nilizoziainisha hapo juu. Kila unapopata mteja na akalipia kozi yako, basi unamtumia link ya playlist ya video zako.

Nikushukuru sana kwa kufuatilia mwongozo huu. Ni matumaini yangu kuwa mwongozo huu utakusaidia kuweza kuanza kuandaa kozi mtandaoni na kukuwezesha kutengeneza kipato.

Kwa ushauri na msaada zaidi, usisite kuwasiliana nami kwa simu namba 0752081669. Asante na karibu kwenye Makala zingine zinazofuata.

Kingi Kigongo
Ungana nae
Latest posts by Kingi Kigongo (see all)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp