
Ili uweze kufanikiwa katika maisha unahitajika kuwa na aina nyingi mbalimbali za elimu na maarifa. Maarifa hayo unapokuwa umejifunza kwa pamoja na kuyafanyia kazi yatakusaidia kutimiza malengo uliyojiwekea. Katika mfumo wetu wa elimu tumekuwa tukijifunza aina mbili tu za elimu ambazo kwa uhalisia hazitoshi kutufanya tufanikiwe kwa viwango vya juu. Aina hizo za elimu ni elimu ya kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu (scholastic education) na elimu inayofundisha ujuzi (professional) education. Aina hizi za elimu ni muhimu lakini bila kuongeza na aina nyingine mbili za elimu ambazo nitakushirikisha katika Makala hii hazitoshi kukufanya uweze kufanikiwa. Hivyo, katika Makala ya leo nitakushirikisha aina nne za elimu unazohitaji ili uweze kufanikiwa.
Zifahamu aina 4 za elimu unazohitaji ili uweze kufanikiwa.
Aina hizi za elimu zimegawanyika katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza ni
1. elimu inayofundishwa darasani.
2. Elimu ambayo haifundishwi darasani.
1. Elimu inayofundiswa darasani.
Katika kundi hili la elimu kuna elimu za aina mbili ambazo ni:
a. Elimu ya kujua kusoma kuandika na kuhesabu (scholastic education).
Hii ni elimu inayokusaidia kufahamu kujua kusoma, kuandika na kuhesabu. Katika elimu hii, mtu anasoma elimu kuondoa ujinga. Hivyo mtu anaposema kuwa amesoma, huwa anamaanisha aina hii ya elimu. Aina hii ya elimu pekee haiwezi kukufanya uweze kufanikiwa.
b. Elimu inayofundisha utaalamu (professional education)
Hii ni elimu inayofundishwa kwenye vyuo mbalimbali. Kazi ya hii elimu ni kufundisha utaalamu kwenye fani mbalimbali. Elimu hii ndiyo inayozalisha wataalamu kama vile madaktari, wahandisi, walimu na kadhalika. Hii ni elimu ambayo inazalisha wataalamu ambao wanaingiza kipato kwa kuuza utaalamu wao. Wanaweza kuwa wameajiriwa au kujiajiri. Hivyo ili waweze kutengeneza kipato, ni lazima wauze utaalamu wao. Aina hii ya elimu itakuwezesha kuwa na kipato cha kati (middle income). Haiwezi kukufanya uweze kufanikiwa kwa kiwango cha juu na kuwa na uhuru wa kifedha. Hii ni kwa sababu haiwezi kukufanya uwe na kipato endelevu (passive income).
2. Elimu ambayo haifundishwi darasani.
Katika kundi hili la elimu kuna aina mbili za elimu ambazo ni:
a. Elimu ya msingi kuhusu fedha (financial education)
Hii ni elimu ya muhimu sana kwani inakufundisha jinsi kutengeneza kipato chako, jinsi ya kutumia kipato chako na ni jinsi gani utawekeza pesa zako ili ziweze kuongezeka thamani na hivyo kukufanya utajirike na kuwa na uhuru wa kifedha (financial freedom), jinsi ya kuweka bajeti na kadhalika. Elimu hii ndiyo inawatofautisha watu matajiri na masikini. Elimu hii haifundishwi darasani. Unaipata kupitia kusoma vitabu mbalimbali. Hivyo wekeza sana kwenye aina hii ya elimu ili uweze kufanikiwa.
b. Elimu ya maendeleo binafsi (self development)
Hii ni elimu inayokusaidia kuweza kutumia vipawa, vipaji na uwezo ulionao ili uweze kufanikiwa. Aina hii ya elimu ni muhimu sana kwani unapofahamu jinsi ya kutumia vipawa na vipaji ulivyonavyo utaweza kufanikiwa kwa viwango vya juu sana. Ndiyo maana kuna watu ambao hawakuwahi kuingia darasani lakini wana mafanikio makubwa sana katika maisha yao. Elimu hii pia unaipata kupitia kusoma vitabu. Hivyo wekeza muda wako kusoma vitabu ili uweze kufanikiwa katika maisha.
Swali la msingi ni hili, je elimu mbili za kwanza sio muhimu?
Jibu ni hapana. Elimu zote ni muhimu, hivyo ili uweze kufanikiwa, kama ukiwa na elimu ya darasani halafu ukaongezea kwenye aina hizi mbili za elimu ambazo hazifundishwi darasani basi mafanikio yako yatakuwa makubwa sana. Hivyo basi kama umebahatika kusoma, basi wekeza pia na kwenye aina hizi mbili za elimu ili uweze kufanikiwa. Lakini pia, kama haukubahatika kusoma, wekeza kwenye aina hizi mbili za elimu ambazo hazifundishwi darasani, utafanikiwa kwani kuna watu ambao hawakubahatika kuingia darasani, lakini kwa sasa ni matajiri wakubwa.
Kwa leo niishie hapo, nimatumaini yangu umepata maarifa ya kutosha ambayo yatakufanya uweze kufanikiwa katika maisha yako. Kama una maoni au swali lolote usisite kuweka maoni yako hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana name moja kwa moja kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu tena katika Makala zinazofuata.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024