
Katika makala zangu zilizopita nilielezea njia mbalimbali za kuanzisha biashara mtandaoni na kutengeneza kipato. Miongoni mwa njia hizo ni kuanzisha na kumiliki channel ya YouTube.Ikiwa umekuwa ukifikiria kuanzisha channel ya YouTube Kwa ajili ya biashara yako na hivyo kutengeneza kipato, kabla ya kuchukua hatua hiyo ni muhimu kujiuliza maswali kadhaa. Katika makala ya leo nitakushirikisha maswali matano muhimu Unayopaswa kujiuliza kabla ya kuanzisha channel ya YouTube ili uweze kupata mafanikio kwenye channel yako.
Maswali 5 Unayopaswa Kujiuliza Kabla ya Kuanzisha Channel Ya YouTube.
1.Kwa nini Unataka Kuanzisha Channel Ya YouTube?
Huenda hili ndilo swali muhimu zaidi unalohitaji kujiuliza kabla ya kuanzisha channel ya YouTube. Je, unahitaji kuanzisha channel ya YouTube kwa ajili ya kupeleka watembeleaji wengi kwenye tovuti ya kampuni yako? Je, unahitaji kuanzisha channel ili kujitangaza watu wafahamu biashara au huduma unayotoa ? Je, una maarifa au ujuzi na hivyo una shauku ya kuwashirikisha watu maarifa yako? Je, unaona kuna tatizo fulani katika jamii na unahisi unaweza kulitatua kupitia kuelimisha kwa kurekodi video? Je, una kipaji fulani na hivyo unahitaji kukionyesha ili watu wakutambue? Hizi zote ni sababu nzuri za kutaka kuanzisha channeli ya YouTube. Hata hivyo, ikiwa unataka kuanzisha channel kwa lengo tu la kutengezeza pesa nyingi, basi unahitaji kufikiria upya kabla ya kufanya uamuzi wako. Kumbuka kuwa kupata pesa kinatakiwa kiwe kipaumbe chako cha mwisho. Kumbuka kuwa, pesa ni matokeo ya kutatua changamoto katika jamii. Hivyo channel yako inapaswa kujikita katika kutatua changamoto fulani katika jamii. Hivyo, ukiweza kutatua changamoto fulani kupitia channel yako, pesa zitakuja tu.
2.Je, nitakuwa ninaweka video zinazotangaza biashara na huduma zangu?
Watu wengi huwa wanaingia YouTube kwa sababu wanataka kuburudishwa, kufahamishwa na kuelimishwa, si kutazama matangazo ya biashara. Ili uweze kuwa na mafanikio kwenye channel ya YouTube ni sharti uwe unatengeneza video zenye manufaa na taarifa zinazoboresha taswira ya kampuni yako bila kutangaza sana. Kuandaa video za ” jinsi ya kufanya”, kunaweza kukusaidia kujenga uaminifu (trust) na kukubalika ( authority) kwa kwa wateja wako na wafuasi wako bila kulazimika kuuza bidhaa kwenye video zako.
3.Je, Nielezeje Video Zangu za YouTube?
Maelezo ya video zako yanapaswa kuwa mafupi na yanapaswa kujumuisha URL ya tovuti ya kampuni yako katika sentensi ya kwanza ya maelezo ili kuwahimiza watazamaji wako kutembelea tovuti yako. Pia hakikisha unajumuisha maneno ya msingi (keywords) kwenye maelezo yako ambayo yanawiana na malengo ya video zako pamoja na channel yako kwa ujumla. Hii itasaidia kuzifanya video zako zionekane kwa urahisi watu wanapozitafuta mtandaoni.
4.Je, Nitayarishe Video Zangu Mimi Mwenyewe?
Unaweza kuchagua kutayarisha video zako wewe mwenyewe au kuajiri mtu au kampuni ya utayarishaji. Hii itategemea ni pesa kiasi ngapi na wakati unaotaka kuwekeza. Ikiwa una rasilimali chache, unaweza kupiga video na smartphone yako au kamera ya HD. Hata hivyo unaporekodi video, unatakiwa kuhakikisha kuwa unapakia video mpya mara kwa mara. Ukiweza kurekodi video mpya na ya kusisimua kila wiki, utaweza kukuza idadi ya watu wanaofuatilia channel yako haraka.
5.Je, Niruhusu Maoni kwenye Video Zangu?
Kuruhusu watu kutoa maoni na kuuliza maswali kwenye video zako za YouTube kutawahimiza kushiriki uzoefu wao na kampuni yako na itaonyesha kuwa uko tayari kupokea maoni yao. Unaweza kufanya maoni yaonyeshwe kiotomatiki, au tu baada ya kuwa umeyaidhinisha.
Kuanzisha Channel ya YouTube kwa ajili ya biashara yako ni njia nzuri ya kukuza brand yako na biashara yako kwa ujumla. Hivyo, kujiuliza maswali haya kabla ya kuanzisha channel yako kunaweza kukuweka kwenye njia ya mafanikio.
Nimatumaini yangu umepata maarifa ya kutosha ambayo yatakusaidia kupata mafanikio unapokuwa umeanzisha channel yako ya YouTube. Kama una maoni au swali lolote usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami moja kwa moja kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu kwenye makala zijazo.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024