
Watu wengi wameshindwa kufanikiwa katika maisha na katika malengo yao sio kwa sababu hawana uwezo au kipaji. Bali ni kwa sababu hawana nidhamu katika maisha yao. Katika makala ya leo nitakushirikisha jinsi ya kujenga nidhamu katika maisha yako ili uweze kufanikiwa.
Maana ya nidhamu.
Nidhamu ni ile hali ya kufanya kitu ambacho ni cha muhimu kwako na kwa muda muafaka bila kujali kama unajisikia au la.
Watu wengi wamezaliwa wakiwa na uwezo mkubwa lakini wameshindwa kufanikiwa katika maisha yao na kuishi wakiwa watu wa kawaida mpaka wanaondoka duniani kwa sababu walishindwa kujenga nidhamu katika maisha yao. Ili uweze kufanikiwa ni lazima ujenge nidhamu katika maisha yako.
Jinsi ya kujenga nidhamu katika maisha ili uweze kufanikiwa.
1. Nidhamu ya muda.
Muda ni rasilimali ya muhimu na ya pekee sana ambayo kila mtu amepewa kwa usawa. Hakuna mtu aliyependelewa akapewa muda mwingi kuliko watu wengine. Hivyo ili uweze kufanikiwa ni lazima ujifunze kuwa na nidhamu ya hali ya juu ya matumizi ya muda. Ili uweze kufanikiwa, hakikisha unaorodhesha Mambo ambayo utayafanya kwenye siku husika siku moja kabla. Pia hakikisha unapoweka orodha hiyo, panga mambo hayo kwa vipaumbele ukianzia na mambo ya muhimu sana kufanyika. Unapokuwa umeamka, anza kufanya mambo muhimu uliyoyaandika. Baada ya kuwa umemaliza kufanya mambo ya muhimu sana yanayochangia mafanikio yako, ndio umalizie mambo ambayo siyo ya muhimu sana.
2. Nidhamu ya fedha
Eneo la pili unalopaswa kulijengea nidhamu ya hali ya juu ni eneo la fedha. Ili uweze kufanikiwa, hakikisha kuwa, kila pesa inayopita kwenye mikono yako inakuwa na udhibiti wa hali ya juu. Katika eneo hili la fedha, fanya mambo yafuatayo ili uweze kuwa na mafanikio:
i. Andaa bajeti yako.
Bajeti ni mwongozo wa mapato yako na jinsi unavyoyatumia. Ni lazima ufahamu kuwa, unapokuwa na pesa na ukawa hauna mwongozo wa jinsi ya kuitumia, pesa yako itatumika kwa mambo yasiyokuwa ya msingi. Watu wengi wameshindwa kufanikiwa Katika suala la kifedha, siyo kwamba hawapati pesa, bali ni kwa sababu hawana bajeti.
ii. Hakikisha kuwa unaweka akiba.
Hakikisha kuwa kila pesa unayopata, unatenga pesa ambayo utaweka akiba. Unaweza kuweka akiba angalau asilimia kumi ya kila kipato chako. Lazima uanze kwa kutenga akiba kwanza kabla ya matumizi mengine.
iii. Epuka mikopo isiyojenga
Mikopo inakuwa na manufaa pale tu itakapotumika kufanya jambo lenye manufaa kwenye kwenye maisha yako. Hakikisha kuwa kama itakulazimu kuchukua mkopo, basi ni lazima uuelekeze kwenye jambo la uzalishaji au kununua kitu ambacho kinaongezeka thamani. Pia unaweza kuchukua mkopo kama tu kuna jambo la dharura kama vile kuokoa maisha.
iv. Fanya uwekezaji wa muda mrefu.
Pesa yako ya akiba unaweza kuiwekeza ili iweze kuongezeka kwa kununua vitu vinavyoongezeka thamani. Hapa unaweza kuiwekeza kwa kununua hisa, hatifungani, kununua shamba au kiwanja. Jambo la msingi hapa ni kuifanya pesa yako iongezeke thamani. Ukiweza kuwekeza pesa yako kwa muda mrefu, utapata matokeo mazuri sana kwani baada ya muda unaweza kuendesha maisha yako kwa ile faida tu inayotokana na uwekezaji wako.
Ni matumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kukusaidia kuweza kujenga nidhamu ili uweze kufanikiwa kupitia makala hii.
Swali la leo.
Ni maeneo gani unahitaji kujenga nidhamu ili uweze kufanikiwa kwenye maisha yako?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika hapa chini Kwenye box la maoni.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024