
Ikiwa umekuwa ukifikiria kuanzisha biashara mtandaoni lakini bado haujafanya utafiti wa biashara Inayolipa mtandaoni, tumia hatua zifuatazo ili kuhakikisha kuwa umechagua biashara yako vizuri na hivyo kuepuka kupoteza muda na pesa zako kwa kujaribu kuanzisha biashara ambayo haitakuwa na faida kwako.
Hatua ya Kwanza: Tambua unapendelea nini.
Ikiwa bado haufahamu kile hasa unachopenda kufanya (passion), hatua ya kwanza kabisa unapaswa ufikirie ni kitu gani hasa ambacho huwa unakipenda kwenye maisha yako. Kama utaanzisha biashara inayohusiana na kitu ambacho hukipendi kuna uwezekano kuwa utaacha biashara hiyo pale ambapo mambo hayataenda vizuri. Lakini kama utaanzisha biashara kutokana na kitu unachokipenda, hautakata tamaa hata kama mambo yatakuwa magumu. Hivyo hatua ya kwanza kabisa ya kutambua biashara Inayolipa mtandaoni ni kujichunguza wewe mwenyewe ni kitu gani huwa unakipenda kwenye maisha yako.
Ili uweze kufanikiwa kwenye hatua hii ya kwanza, chukua karatasi na uorodheshe maeneo kumi ambayo unayapenda sana au ambayo huwa unafurahia kuyafanya. Kama utapata changamoto katika zoezi hili maswali ya mwongozo yafuatayo yatakusaidia:
- Je, huwa unapenda kufanya nini wakati wako wa mapumziko?
- Je, ni magazeti ya aina gani huwa unapenda kusoma? Je! kuna mada yoyote ambayo huwa unapenda kujifunza kwenye magazeti?
- Je, huwa unatumia muda wako mwingi na makundi gani ya watu?
Ukitafakari kwa kina maswali haya utaweza kugundua kitu unachokipenda kwenye maisha yako.
Hatua ya Pili: Tambua Matatizo Unayoweza kutatua.
Baada ya kuwa umeainisha vitu kumi ambavyo unavipenda, basi unaweza kuchagua miongoni mwa vitu hivyo vitu ambavyo unavipenda zaidi. Baada ya kuwa umechagua vitu ambavyo unavipenda zaidi, chunguza uone ni matatizo gani yaliyopo kwenye jamii ambayo unaweza kuyatatua kutokana na vitu ambavyo huwa unapenda kuvifanya. Kumbuka kuwa, kama unataka kuanzisha biashara inayolipa mtandaoni, unatakiwa kutafuta matatizo ambayo jamii yako inakabiliwa nayo na ufikirie ni kwa jinsi gani unaweza kutatua matatizo hayo.
Kama hauna uhakika ni kwa jinsi gani utaweza kutambua matatizo hayo, hapa kuna mambo machache ambayo unaweza kuyafanya ili uweze kutambua matatizo hayo.
- Uliza watu mbalimbali kwenye jamii yako ili uweze kupata maoni yao. Andaa maswali maalumu ambayo ukiwauliza yatakusaidia kugundua matatizo yaliyopo kwenye jamii yako.
- Tembelea majukwaa ya mtandaoni.
Angalia majukwaa ya mtandaoni yanayoendana na vitu unavyovipenda na uangalie mambo mbalimbali wanayojadili na kuulizana maswali. Jaribu kuangalia maswali ambayo yanajirudia mara kwa mara na uangalie namna ambavyo unaweza kutatua maswali hayo. Kumbuka kuwa, maswali yanayoulizwa na watu ndiyo changamoto wanazokabiliana nazo. Hivyo unaweza kutatua changamoto hizi kwa kutoa huduma au kuuza bidhaa mtandaoni.
Hatua ya Tatu: Angalia biashara unayotaka kuanzisha kama ina soko (profitability).
Baada ya kuwa umefikiria biashara ambayo utaifanya, hatua inayofuata katika kuangalia biashara inayolipa mtandaoni ni kuangalia soko lake. Hapa unaweza kuangalia kama group la watu unaolenga kuwauzia bidhaa au huduma yako kama wana uwezo wa kununua bidhaa au kulipia huduma yako. Pia unaweza kuangalia bidhaa au huduma zilizopo tayari mtandaoni. Kama utaona bidhaa zingine kama unazotaka kutengeneza, basi hiyo ni dalili nzuri kuwa soko lipo.
Hatua ya Nne: Jaribu Wazo lako.
Sasa tayari una taarifa kamili kuhusiana na biashara ambayo unatamani kuanza kuifanya mtandaoni. Kitu pekee kilichobaki ni kujaribu wazo lako. Hivyo anza kufanyia kazi wazo lako. Hapa utatakiwa kuwa na tovuti au blog ambayo itakusaidia kuonyesha bidhaa na huduma zako pamoja na kupata watembeleaji kwenye huduma yako.
Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kutosha kukusaidia kutambua biashara inayolipa mtandaoni. Ninaamini kuwa kwa kufuata hatua hizi nne utaweza kuanzisha biashara mtandaoni yenye mafanikio. Kama una swali au maoni usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kupitia simu namba 0752 081669. Asante sana na karibu katika makala zinazofuata.