Jinsi Ya Kutumia Muda Vizuri: Parkinson Law

Jinsi Ya Kutumia Muda Vizuri: Parkinson Law

Kila mmoja amepewa masaa 24 katika siku moja. Lakini, jinsi tunavyotumia masaa tuliyopewa ndiyo itaashiria kiwango cha mafanikio yetu. Watu waliofanikiwa huwa wanatumia vizuri sana masaa ndani ya siku ili waweze kutimiza malengo yao na kufanikiwa katika maisha yao. Sasa, ni kwa jinsi gani watu waliofanikiwa hutumia muda wao? Wengi wao wanafahamu kanuni ya Parkinson na hivyo huwa wanatumia kupanga muda wao. Katika makala ya leo nitakushirikisha jinsi ya kutumia muda wako vizuri.

Kanuni ya Parkinson inasema hivi:
“Work expands to fill the time available for completion.”
Kwa lugha ya kiswahili ni kuwa, kazi huwa inachukua muda wote ulioutenga wa kuikamilisha
.

Hii ina maanisha kuwa, haijalishi ni muda mrefu kiasi gani ulioutenga kwa ajili ya kufanya kazi fulani, kwa muda ulioutenga, kazi yako itakamilika kwa muda huohuo. Kama umetenga muda mfupi, na kazi yako itakamilika ndani ya muda mfupi. Kwa mfano, kama umetenga dakika ishirini za kufanya kazi fulani, utatumia dakika hizo hizo ishirini kukamilisha kazi hiyo. Sasa anza kutumia kanuni ya Parkinson kwa faida kwa kufuata hatua hizi 5.

1.Weka malengo na vipaumbele.
Hatua ya kwanza ya kutumia kanuni ya Parkinson ni kuandika malengo yako na vipaumbele. Elezea kwa nini kazi hii uipe kipaumbele cha kwanza na endelea kuainisha kazi zako zote za siku kwa vipaumbele vyake na kila kazi uipatie muda wa kuikamilisha.

2. Ainisha vikwazo na changamoto ambazo unahisi zinaweza kujitokeza.
Weka orodha ya vikwazo au changamoto ambazo unahisi zinaweza kujitokeza unapokuwa ukitekeleza kazi zako. Hii ni hatua ya muhimu sana, usiiruke. Unapokuwa umefikiria mapema vikwazo au changamoto ambazo zinaweza kujitokeza, utaweza kuziepuka au kuzifanyia kazi mapema hivyo kuokoa muda na kufanya kwa ubora.

3. Weka muda wa kutimiza kila kazi.
Baada ya kukamilisha hatua za mwanzo, basi unatakiwa kugawa muda kwa kila kazi. Kama kazi zako zitakuwa na sehemu ndogondogo, unaweza pia kila kazi ndogo ukaigawia muda wake. Lengo ni kuhakikisha muda wako haupotei. Hii itakusaidia kuwa na picha kamili kuwa kazi zako zote za siku zitatumia muda kiasi gani.

4. Tambua na uondoe vitu vyote ambavyo huwa vinapoteza muda (time wasters)
Hii ni hatua ya muhimu sana ambayo itakusaidia kutunza vizuri muda wako. Unapokuwa umemaliza kazi moja, kuwa makini sana na uepukane na vitu vingine ambavyo vitakuchukulia muda wako ambavyo haviendani na kazi zako. Miongoni mwa vitu hivyo vinaweza kuwa, kujibu barua pepe ambazo hazina umuhimu, kuingia kwenye mitandao ya kijamii, kupoteza muda Whatsapp kwa vitu ambavyo siyo vya msingi na kadhalika.

Katika makala ya leo tumeangalia jinsi ya kutumia muda vizuri ili kuwa na mafanikio. Kwa kutumia kanuni hii ya Parkinson, utaweza kutumia muda wako vizuri na kufanya mambo makubwa ndani ya siku.

Swali la leo:
Tayari umejifunza kuhusu kanuni ya Parkinson, utaitumiaje kutunza muda wako vizuri?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika hapa chini kwenye box la maoni. Pia kama una maoni yoyote au swali, usisite kuandika hapa chini. Asante na karibu kwenye makala zijazo.

Kanuni 3 Za Kuwa Na Maisha Yenye Furaha.

Kanuni 3 Za Kuwa Na Maisha Yenye Furaha

Hivi umeshawahi kupitia kipindi ambacho umekuwa ukijihisi hauna furaha katika maisha yako? Kila kitu unachokifanya unaona kabisa kinakuletea furaha ya muda mfupi tu na baadaye furaha yako inatoweka. Tatizo ni kuwa, umekuwa ukitafuta furaha bila kuwa na kanuni madhubuti ambazo zitakuletea furaha ya kudumu katika maisha yako. Hivyo, ili uweze kuwa na furaha katika maisha yako, unaohitajika kuwa na muda wa kuweka kanuni ambazo zitakuletea furaha katika maisha yako. Katika makala ya leo nitakushirikisha kanuni 3 za kuwa na maisha yenye furaha.

Kanuni 3 za kuwa na maisha yenye furaha.

1.Kuwa mtu mwenye malengo.
Miongoni mwa kanuni ya muhimu sana ya kuwa na maisha yenye furaha ni kuwa mtu mwenye malengo. Ili uweze kuwa na furaha, unahitajika kuweka malengo ambayo yataendana na kusudi la maisha yako na kuyafanyia kazi kila siku. Hii itakupa ramani halisi ya mwelekeo wa maisha yako na jinsi ambavyo utaitumia kila siku kuweza kutimiza malengo yako. Kwa kufanya hivyo utakuwa ukisogelea mafanikio yako na hivyo furaha yako kuongezeka. Kwa kufanyia kazi malengo uliyoyaandika, utajihisi furaha unapokuwa ukipiga hatua kwa kukamilisha lengo moja baada ya lingine kwa siku hiyo. Siku inapokuwa imeisha na ukaangalia nyuma mambo uliyoyatimiza, utajiona mwenye furaha kwani utakuwa unapiga hatua kuelekea kwenye mafanikio yako.

2.Kuwa mtu unayetaka matokeo.
Unapokuwa umeandika malengo yako, utaweza kupima maendeleo yako kwa kuweka vigezo vya mafanikio. Vigezo hivi vitakuwezesha kufahamu mafanikio yako hatua kwa hatua. Utaweza kufahamu ni hatua gani uliyofikia na ni hatua gani zaidi zinahitajika kuweza kufikia matokeo uliyoyakusudia. Unapokuwa unapima hatua za mafanikio yako, utaweza pia kujifunza muda ulioutumia na hivyo kukujengea tabia ya kutunza muda. Kadiri unavyokuwa unapiga hatua kwenye mafanikio uliyojiwekea kwa kutumia vigezo vya mafanikio ulivyoviweka, ndivyo utakavyokuwa na furaha zaidi katika maisha yako.

3.Endelea kuchukua hatua bila kuacha.
Kwa kuwa kuweka malengo ni jambo la muhimu sana ambalo litakupa hamasa ya kufanya kazi, ni muhimu kuendelea kuchukua hatua bila kuacha. Kumbuka, kuwa na malengo yaliyoandikwa bado haitoshi. Unahitajika kuchukua hatua kufanyia kazi malengo yako bila kuacha. Unapokuwa unapiga hatua haijalishi ni kubwa au ni ndogo kiasi gani, furaha yako itaongezeka.

Swali la leo.
Ni kanuni gani kati ya hizi tatu za kuwa na maisha yenye furaha utaanza kuitumia leo?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika kwenye sanduku la maoni hapa chini. Pia kama una swali au maoni yoyote, usisite kuandika hapa chini. Asante na karibu tena katika makala ijayo.

Funguo 6 Za Kuwa Kiongozi Bora.

Funguo 6 Za Kuwa Kiongozi Bora.

Uongozi ni mojawapo ya vigezo muhimu sana kwenye mafanikio ya biashara, kazi na mafanikio ya mtu binafsi. Viongozi bora wana uwezo wa kushawishi watu wanaowazunguka kuweza kufanya mambo kwa viwango vya hali ya juu. Katika hali ya kawaida na tafsiri rahisi, uongozi ni uwezo wa kutatua changamoto zilizopo ili kuweza kupata matokeo yaliyokusudiwa.
Watu wengi wanaamini kuwa, viongozi bora ni wa kuzaliwa. Hata hivyo dhana hiyo siyo ya kweli. Kwani, kwa kufanya vitu sahihi na kuchukua hatua sahihi, mtu yeyote anaweza kuboresha uwezo wake wa kuongoza na hivyo kuwa kiongozi bora. Katika makala ya leo, nitakushirikisha funguo 6 za kuwa kiongozi bora.

Funguo 6 za kuwa kiongozi bora.

1.Usijiwekee mipaka.
Jinsi unavyojifikiria ndivyo unavyokuwa. Ukiamini kuwa unaweza basi utaweza. Ukiamini kuwa hauwezi, hautaweza. Akili yako huwa inafanyia kazi kwa usahihi kile tu unachokiamini. Hivyo, ukiamini katika kufanya mambo makubwa, akili yako itafanya hivyohivyo. Hivyo, amini katika uwezo mkubwa ulionao nawe utafanikiwa. Kumbuka kuwa, unawajibika moja kwa moja katika mawazo unayojiwazia na jinsi unavyojiwekea mipaka ya mafanikio makubwa. Hivyo basi, amua kufanya mambo makubwa na uondoe mipaka uliyojiwekea ili uweze kupata mafanikio makubwa katika kazi yako na katika maisha yako kwa ujumla.

2.Acha kuwa na visingizio (Stop making excuses)
Jambo linapotokea ambalo siyo la kawaida, usilichukulie kuwa ni kwa sababu ya uzembe ulioufanya, bali lichukulie kuwa ni sehemu ya majukumu yako ya kawaida na hivyo unawajibika kwa asilimia mia moja kulitatua. Ili uweze kuwa kiongozi bora, ni jambo la muhimu sana kukubali kuwajibika kwa asilimia mia moja kwenye maisha yako mwenyewe, maamuzi yako na uwezo wako. Jambo hili la uwajibikaji kwenye nyanja zote za maisha yako (radical responsibility) litakusaidia kuwa na umiliki wa maisha yako kwa ujumla na kukuondolea visingizio ambavyo vitakufanya usiwajibike.
Acha kulaumu mambo ambayo yako nje ya uwezo wako na tambua kuwa ni jukumu lako kutafuta suluhu ya changamoto zinazojitokeza haijalishi unapitia kipindi gani.

3. Mara zote tafuta fursa mpya za kukufanya uwe bora zaidi.
Viongozi bora huwa hawaridhiki kufanya mambo kwa mazoea. Mara zote huwa wanajifunza kila siku mambo mapya ambayo yatawafanya wawe bora zaidi. Hivyo, ili uwe kiongozi bora, kila siku jifunze mambo mapya kwa kuuliza, kukutana na watu mbalimbali na Kujifunza kupitia kusoma vitabu. Kwa kufanya hivyo, utaweza kufungua fursa mahali ambapo wengine hawazioni na kufanya mambo makubwa mahali ambapo wengine wanaona haiwezekani. Hii ndiyo tofauti iliyopo kati ya kiongozi na wafuasi. Kiongozi huwa anatengeneza njia bali wafuasi husubiri mpaka waone njia imetengenezwa ndiyo wapite.

4. Kubali kushindwa na ujifunze kutokana na makosa.
Kushindwa katika maisha ni jambo lisiloepukika. Viongozi wote bora katika historia walipitia uzoefu wa kushindwa. Wengine walipitia vipindi vigumu vya ukosoaji mkubwa na kukataliwa. Jambo lililowatofautisha na watu wengine ni kuwa, waliweza kushinda changamoto hizo kwa Kujifunza kutokana na kushindwa kwao na na hivyo kuchukua hatua. Viongozi bora huwa wanafahamu ubora wao na mapungufu yao na hivyo hutumia ubora wao na mapungufu yao kama fursa ya kujifunza ili kuwafanya wawe bora zaidi kesho. Hata wewe unaweza kushindwa, lakini kubali kushindwa na utumie makosa yako kama fursa ya kujifunza ili uweze kuwa kiongozi bora.

5. Ongoza kwa kuwa mfano.
Watu huwaheshimu sana viongozi wanaotenda mambo yote wanayoyasema. Kama unataka kuwa kiongozi bora, usitegemee kuwa watu watafanya kitu ambacho wewe kiongozi haukifanyi. Hivyo, watu huwaheshimu viongozi wanaokuwa wa kwanza kufanya vitu ambavyo wanategemea watu wengine wavifanye. Hivyo, ili uwe kiongozi bora, kuwa mfano kwa wale unaowaongoza nawe utaheshimika.

6. Fanya mambo yako kwa ubora na ubunifu.
Viongozi bora pamoja na kuongoza kwa mfano, pia hufanya mambo yao kwa ubora na ubunifu. Maana yake ni kuwa, huwa wanatafuta njia fupi na bora zaidi ya kutatua changamoto. Wana uwezo wa kuona mambo makubwa na kuweka mipango na njia za kuweza kufanikiwa. Huwa wanatafuta njia ya haraka, yenye gharama himilivu na halali ya kufanya mambo lakini kwa ubora uliokusudiwa.

Swali leo.
Ni katika eneo gani unawajibika kwa asilimia mia moja ili uweze kuwa kiongozi bora?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika kwenye sanduku la maoni hapa chini.

Kuna Tofauti Gani iliyopo kati ya Blog na Tovuti?

Kuna Tofauti Gani iliyopo kati ya Blog na Tovuti?

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza na kushindwa kupambanua tofauti iliyopo kati ya blog na tovuti. Inawezekana hata wewe ni miongoni mwao. Katika makala ya leo nitakushirikisha tofauti iliyopo kati ya blog na tovuti na kipi uchague kama unataka kuanzisha biashara mtandaoni na kutengeneza kipato.

Blog ni nini?
Blog ni tovuti inayowekewa makala mara kwa mara kwa lengo la kuvuta wasomaji na hivyo kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.Katika kila makala kunakuwa na sehemu ambapo msomaji anaweza kuandika maoni yake kuhusiana na makala hiyo au kuuliza swali.

Umekuwa ukisoma blog nyingi bila wewe kujua na hata sasa uko kwenye blog yangu. Inawezekana umewahi kusikia maneno blog na tovuti. Je unajua tofauti yake?
Katika Makala hii tutaangalia maana ya blog, tofauti iliyopo kati ya blog na tovuti na kipi unapaswa kuchagua kati ya blog na tovuti.

Kimsingi blog zote ni tovuti , lakini sio tovuti zote ni blog.

Tofauti iliyopo kati ya Blog na Tovuti.
Kabla hatujaangalia tofauti iliyopo kati ya blog na tovuti, hebu tuangalie kwanza historia fupi ya blog jinsi ilivyoanza mpaka sasa.

Historia fupi ya Blog
Blog zimekuwepo toka miaka ya 1993 na kwa sasa zina miongo miwili na nusu. Japokuwa kumekuwa na mjadala kuwa ni nani hasa mwandishi wa kwanza wa blog, kuna mtu mmoja anaweza kuwa ndiye mwandishi wa kwanza wa blog.

Mwaka 1993 Rob Palmer alianza kufanya kazi kwenye kampuni moja mjini London ambapo alikuwa akiandika makala za robo mwaka za kampuni na kuziweka kwenye tovuti ya kampuni.

Wakati Palmer alipokuwa akiandika makala kwa ajili ya kampuni yake, karibia mwaka mmoja baadaye blog nyingine ilianzishwa na Justin Hall. Blog yake ilikuwa na links na hivyo, watu wengine pamoja na makampuni wakagundua umuhimu wa kuwa na aina hiyo ya tovuti kwa ajili ya kubadilishana taarifa.

Wakati wa kipindi hicho blog zilijulikana kama “online journal” na “online diaries”. Mwaka 1997 mwandishi wa blog Mmarekani Jorn Barger aliziita blog kama “weblog,” ambapo kwa haraka sana zilibadilika jina kutoka “online diaries na online journals “ na kuwa “blog” kama tunavyolitumia leo.

Watengenezaji wa mifumo ya internet (Web developers ) kwa haraka waligundua kuwa watu walipendelea zaidi blog kuliko kitu kingine mtandaoni na hivyo wakaamua kutafuta suluhisho la kuboresha blog.

Mwaka 1998, Open Diary ilianzishwa. Hili lilikuwa ni jukwaa (platform) la watu kuandika makala zao na kubadilishana uzoefu wakati huohuo likiwa na sehemu ya watu kutoa maoni (comments). Platform zingine za blog zilianzishwa zikiwemo LiveJournal, Blogger, Tumblr na Xanga.

Ilipofika mwaka 2003, shughuli za blog zilibadilika kabisa pale ambapo wanachuo wawili walipotengeneza WordPress, mfumo bora kabisa (content management system (CMS)) ambao unachukua karibia mbili ya tatu ya tovuti zote zilizopo kwenye mtandao wa internet duniani leo.

Mwaka 2007, mifumo mingine ya blog (micro-blogging) ilianzishwa. Miongoni mwa mifumo iliyoanzishwa ilikuwa ni Twitter kwa lengo la watu kuandika makala fupifupi zenye maneno kati ya 300-400.

Mwaka 2016, WordPress ilianzisha mfumo kwa ajili ya blog ( .blog domain extension), hali ambayo ilizifanya blog kuendelea kuongeza umaarufu. Kwa sasa kunakadiriwa kuwa na  makala mpya millioni 70 zinazoandikwa na kuwekwa kwenye blog za WordPress kila mwezi.

Kuna tofauti gani kati ya Blog na Tovuti?

Kuna Tofauti Gani iliyopo kati ya Blog na Tovuti?

Tofauti kubwa iliyopo kati ya blog na tovuti ni kuwa, blog inawekewa makala mpya(dynamic) mara kwa mara wakati tovuti haiwekewi makala mpya mara kwa mara (static).

Na kama tulivyoona kabla, blog zote ni tovuti lakini si tovuti zote ni blog.
Tofauti nyingine kubwa ni kuwa tovuti huwa inakuwa na kurasa za msingi kama vile:

Mwanzo au Nyumbani (home),

Huduma zetu (service page) na

Wasiliana Nasi (Contact page).

Pia tovuti inaweza kuwa hata yenye ukurasa mmoja.

Kwa upande mwingine, blog ina kurasa kama zile zilizopo kwenye tovuti pamoja na sehemu ya kuweka makala mbalimbali ambayo kila mara makala mpya huwa zinawekwa.Kila makala huwa na sehemu ambayo wasomaji wanaweza kuuliza maswali au kutoa maoni yao.

Kila unapoweka makala mpya , makala mpya huoneana juu ya makala zingine za zamani. Hivyo wasomaji wako watakuwa wakiona makala mpya kwanza.

Kipi bora, kuwa na Tovuti au Blog?

Kumbuka nilisema hapo awali kuwa tovuti imeundwa na kurasa za msingi tu kwa mfano:

Masaa yako ya kazi,anuani au Menu.

Bidhaa unazouza.

Huduma unazotoa.

Hivyo hata ukurasa mmoja unaweza kutosha kuunda tovuti.

Lakini Blog huwa ina hizo kurasa zote ambazo tovuti inazo pamoja na ukurasa wa kuweka makala mpya (Post page).
Hivyo kama unahitaji kuwa unaweka makala mbalimbali ili kuwasiliana na wateja wako, nakushauri uwe na blog badala ya tovuti.

Blog ni njia nzuri sio tu ya kuwasiliana na wateja wako bali pia kuvutia wateja wapya kuja kwenye biashara au huduma unayotoa.

Kuna tofauti gani kati ya kurasa za msingi na kurasa za Makala (Post pages)?

Kurasa za Makala(Post pages):
1. Huwa zinawekewa makala mara kwa mara.
2. Kila makala huwa na kichwa cha habari na wakati mwingine vichwa vidogo vya habari.
3. Makala huwa zimepangiliwa kulingana na mwezi na mwaka zilipowekwa.
4. Makala huwa zimepangiliwa kulingana na makundi (categories).
5. Kila makala ina sehemu ya kuweka maoni (comments)
6. Kila makala ina jina la mwandishi na tarehe iliyowekwa.
7. Unaweza kuwa na makala zisizokuwa na idadi.

Kurasa za Msingi (pages):
1. Huwa na taarifa za msingi ambazo hazibadiliki mara kwa mara.
2. Taarifa hizi hazionyeshi kuwa ziliwekwa lini.
3. Kurasa hizi zimeandikwa si kwa lengo la kushare taarifa zake kwenye mitandao ya kijamii.
4. Hazina sehemu ya kuweka maoni (comments).
5. Hazina taarifa za mwandishi wala tarehe ya kuandikwa.
Idadi ya kurasa za msingi huwa ni ndogo.

Kurasa za msingi ambazo kila blog na tovuti zinapaswa kuwa nazo.
Hata kama blog yako ni kwa ajili tu ya kuandika makala mbalimbali, kurasa hizi zifuatazo unapaswa kuwa nazo.

1.Sisi Ni Nani (About page)
Ukurasa wa Sisi Ni Nani (The About Us Page) hutumika kuelezea kuwa Blog yako au Tovuti yako inahusika na nini.
Ukurasa huu unasaidia kuwaelezea watembeleaji wa blog au tovuti yako huduma unayotoa na hivyo kuwawezesha kufanya maamuzi kama huduma unayoitoa wanaihitaji au la. Katika ukurasa huu unaweza pia kuelezea kampuni yako, malengo na njozi za kampuni yako kuhusiana na huduma unayotoa.
Kama wewe ni mwandishi wa blog, unaweza kutumia ukurasa huu kuweka link za mitandao yako ya kijamii, kuwaomba wasomaji wako waungane na wewe (follow) kwenye mitandao ya kijamii, kuwasimulia wasifu wako kwa ufupi na kuwaelekeza makala muhumu kwao kuzisoma.

2. Wasiliana Nasi (Contact page)
Huu ni ukurasa ambao unaweza kuweka form ambayo watu wataweza kuwasiliana na wewe na kupata huduma unayoitoa.Pia unaweza kutumia ukurasa huu kuuza bidhaa au huduma unayotoa. Hii ni sehemu ambapo utaweka anuani yako ya barua pepe (email), Anuani yako na namba ya simu. Uwe ni mwandishi wa blog au mfanyabiashara ,unatakiwa kuweka mawasiliano yako wazi kupitia ukurasa huu ili watu waweze kukupata kwa urahisi.

3. Privacy policy page
Unapaswa kuwaambia watembeleaji wa blog yako kuwa unakusanya taarifa zao kwa mfano, email au hata kupitia kifaa cha Google Analytics ambacho huwa kinatoa takwimu za watembeleaji wa blog yako.

4. Vigezo na masharti (Terms of Service)
Ukurasa huu ni wa muhimu kama unauza bidhaa kwenye blog yako au unatangaza bidhaa za makampuni mengine kwa kulipwa gawio (commission). Ukurasa huu unaelezea jinsi ambavyo mteja pamoja na wewe mtoa huduma haki zenu zinalindwa kwenye biashara hiyo.

Hizi ndio kurasa nne ambazo kila tovuti inapaswa kuwa nazo.
Pamoja na kuwa na kurasa hizi, ninasisitiza tena kwa nguvu zote kuwa na blog kwenye tovuti yako.

Kwanini kila Tovuti inapaswa kuwa na Blog?

Kuna Tofauti Gani iliyopo kati ya Blog na Tovuti?


Kama tovuti yako imetengenezwa kwa kutumia  WordPress au platform zingine, inawezekana kabisa kuweka blog kwenye tovuti yako!
Hii ni kwa sababu: Unapokuwa na blog kwenye tovuti yako unakuwa na uwezo wa kuvutia watembeleaji wengi kwenye tovuti yako. Hii ni kwa sababu, kwenye blog utaweza kuandika makala nyingi zenye kuelimisha na hivyo kujenga mahusiano na wateja wako. Pia unapoandika makala nyingi kupitia blog, tovuti yako itaonekana zaidi watu wanapoitafuta kwenye Google na hivyo utapata watembeleaji wengi.

Kwa nini Unapaswa kuanzisha blog (Badala ya Tovuti)?
Tovuti ni nzuri kwa watu ambao tayari wana biashara na hivyo wanahitaji tu kutangaza biashara zao. Lakini hata na wao pia wanaweza kuweka blog kwenye tovuti zao ili wapate mahali ambapo watakuwa wakiandika makala mbalimbali na hivyo kuzifanya tovuti zao ziweze kuonekana kwa urahisi kwenye Google search engine.
Tovuti sio nzuri kwa mtu ambaye ndio anaanza na hana bidhaa yoyote wala huduma anayotoa.

Kwa mfano, kama wewe una duka la nguo, unaweza kuanzisha tovuti badala ya blog. Unaweza kuweka kurasa ambazo utawaelezea wateja wako huduma unazotoa, muda wa kazi , mawasiliano yako n.k.

Hata hivyo, kama huna bidhaa au huduma yoyote unayotoa, unaweza kuanzisha blog ukielimisha watu kutokana na ujuzi ulionao na baadaye utakapokuwa umepata wasomaji wengi wanaofuatilia blog yako ndio unaweza kuamua kuuza bidhaa au huduma kutokana na kile unachofundisha.

Jinsi Blog ilivyo na njia nyingi za kutengeneza pesa kuliko Tovuti.
Sasa hebu tulinganishe jinsi blog ilivyo na njia nyingi za kutengeneza pesa kuliko Tovuti.
Kama una tovuti (Isiyo kuwa na blog) una njia chache tu ambazo unaweza kuzitumia kutengeneza kipato kupitia tovuti yako.
Njia moja iliyozoeleka ni ile ya kuuza bidhaa au huduma kutoka kwa wateja ambao tayari unao. Pia wateja wengine wanaweza kukupata kwa kukutafuta kwenye search engine kama vile Google, kwa wewe kulipia matangazo Google au kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram n.k.

Kwa upande wa Blog, kuna njia nyingi sana za kutengeneza kipato. Uzuri wa blog ni kuwa unakuwa unatengeneza kipato huku ukielimisha jamii na kukuza jina (Brand) ya blog yako na wewe mwenyewe. Miongoni mwa njia hizo ni hizi zifuatazo:
1. Kuuza huduma mbalimbali unazotoa
2. Kutangaza na Kuuza bidhaa za makampuni mbalimbali kwa lengo la kupata gawio (commissions)
3. Kuuza bidhaa mbalimbali (Physical and Digital products)

1.Kuuza huduma mbalimbali unazotoa.
Kupitia makala ambazo utakuwa unaziandika na kuelimisha jamii, watu watakuamini na kukuona kuwa wewe ni mtaalamu wa mada unayofundisha ambaye unaweza kutatua changamoto zao. Hivyo unaweza kutoa huduma mbalimbali kwa malipo kutokana na utaalamu ulionao.

2.Kutangaza na Kuuza bidhaa za makampuni mbalimbali kwa lengo la kupata gawio (commissions)
Njia nyingine unayoweza kuitumia kujipatia kipato kwenye blog yako ni ile ya kutangaza na kuuza bidhaa za makampuni mbalimbali kwa lengo la kupata gawio (commissions) . Njia hii inajulikana kwa kiingereza kama Affiliate marketing. Kuna makampuni mengi yanayotoa huduma hii ambayo unaweza kujiunga na wakakupa link ambayo utaiweka kwenye blog yako. Kila msomaji atakayebofya link hiyo ataelekezwa kwenye tovuti ya kampuni husika ambapo kuna bidhaa au huduma inayouzwa. Iwapo mteja atanunua bidhaa au huduma hiyo, wewe unapata gawio. Miongoni mwa makampuni yaliyo na program hii ni amazon, Aliexpress na kwa Tanzania kuna getvalue n.k

3.Kuuza bidhaa mbalimbali (Physical and Digital products)
Kuuza bidhaa pia ni njia unayoweza kuitumia kujipatia kipato kupitia blog yako. Unaweza kuuza bidhaa zinazoshikika (Physical Products) au bidhaa pepe (Digital products).
Bidhaa pepe (Digital products) ni rahisi sana kutengeneza kwani unaweza kukusanya makala ambazo umekuwa ukiandika na kuziweka kwenye vitabu na ukauza vitabu pepe (ebooks) . Pia unaweza kutumia makala ulizoandika kuandaa kozi na kuiuza kwenye blog yako.

Kwa ufupi:
Katika Makala hii tumeangalia tofauti ya blog na tovuti . Swali langu kwako ni kuwa baada ya kusoma Makala hii, utachagua kipi kati ya blog na tovuti?
Je una biashara na unataka iwafikie watu wengi zaidi au unahitaji kujiajiri kupitia mtandao wa internet kwa kutoa maarifa yako kwa jamii huku ukijipatia kipato?
Vyovyote vile kati ya mambo hayo mawili Blog itakuwezesha kuyatimiza kikamilifu.
Je una maoni yoyote? Usisite kudondosha maoni yako hapa chini.

Njia 5 Za Kujenga Uwezo Wa Kujiamini.

Njia 5 Za Kujenga Uwezo Wa Kujiamini

Katika maisha siyo jambo jepesi kujiamini ikiwa umepitia changamoto zilizokuumiza na hivyo kukukatisha tamaa. Unapokuwa umejenga uwezo wa Kujiamini, utaweza kutatua changamoto zinazokukabili na hivyo kufanikiwa katika malengo uliyojiwekea na katika maisha yako kwa ujumla. Kwa kuwa kujiamini ni jambo la muhimu sana katika kufikia mafanikio yako, katika makala ya leo nitakushirikisha njia 5 za kujenga uwezo wa kujiamini.
Njia 5 za kujenga uwezo wa kujiamini.

  1. Jifunze kujisamehe.
    Jambo la kwanza unapojenga uwezo wako wa kujiamini ni kujifunza kujisamehe. Tambua kuwa wewe ni binadamu na hivyo haujakamilika. Hivyo, jifunze kujisamehe kwa changamoto ambazo umewahi kuzipitia na ujifunze kujisemea maneno chanya. Jizoeze kujisemea kuwa pamoja na changamoto unazopitia, unafanya kadiri ya uwezo wako wote kuweza kutatua changamoto zinazokukabili.
  2. Jipe nafasi.

Unapokuwa umejisamehe, jipe nafasi ya kusema hapana kwa mambo ambayo hutaki kuyafanya, kwa mambo yote ambayo yanakukosesha furaha na kwa mambo yote ambayo yanakufanya ukate tamaa na hivyo kukuondolea nguvu na hamasa ya kufanya kazi ili kutimiza malengo yako. Hii itasaidia akili yako kuwaza vitu vipya na kuleta ubunifu mpya ambao utakusaidia kusonga mbele kwenye malengo yako. Jipe nafasi ya kufurahia na marafiki zako katika michezo mbalimbali unayoipenda. Kwa kufanya hivyo utaongeza uwezo wako wa kujiamini.

3. Weka malengo na uyafuatilie.
Hatua inayofuata ni kuweka malengo na kuanza kuyafanyia kazi. Kwa kila lengo utakalokuwa unatimiza, litakujengea uwezo wa kujiamini zaidi na zaidi na kukupa hamasa ya kuendelea kufanyia kazi malengo mengine. Hivyo, unapokuwa umetimiza malengo makubwa, utaongeza uwezo wako wa kujiamini.

4. Wekeza zaidi kwenye uwezo ulionao na ufanyie kazi mapungufu yako.
Kila mmoja ana uwezo katika mambo fulani na mapungufu katika mambo mengine. Hakuna mwanadamu aliyekamilika. Hivyo, njia nyingine ya kuongeza uwezo wako wa kujiamini ni kukuza uwezo wako na kufanyia kazi mapungufu yako. Utashangaa kuona kuwa, kadiri unavyowekeza zaidi kwenye uwezo ulionao, utaongeza uwezo wako wa kujiamini. Pia uwezo wako wa kujiamini utaongeza pale utakapoanza kufanya vizuri kwenye vitu ambavyo vilikuwa ni changamoto kwako. Unapofanyia kazi mapungufu yako, utaona kuwa uwezo wako wa kujiamini ukiongezeka.

5. Furahia mafanikio yako.
Katika hatua za kujenga uwezo wa kujiamini, usisahau kujipongeza kwa mambo yote ambayo umefanikiwa kuyatimiza. Kwa kufanya hivyo, utaongeza uwezo wako wa kujiamini kwani, utaona mambo uliyoyafanya na ukafanikiwa kuyakamilisha. Jipongeze na ufurahie mafanikio yako haijalishi ni makubwa au ni madogo kiasi gani kwani yataongeza uwezo wako wa kujiamini.
Kujiamini kwenye uwezo ulionao ni njia ya pekee na yenye nguvu sana itakayokuwezesha kufanya mambo makubwa katika maisha yako.
Hivyo basi, kwa kufuata hizi njia 5 zitakusaidia kujenga uwezo wako wa kujiamini na hivyo kufanya mambo makubwa katika maisha yako.
Swali la leo:
Ni mafanikio gani makubwa katika malengo yako utayafurahia ili kuongeza uwezo wako wa kujiamini?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika kwenye sanduku la maoni hapa chini.

Kwanini Unapaswa Kuanza Kuweka malengo?

Kwanini unayopaswa kuanza kuweka malengo?

Watu wengi huwa wanatamani sana kupata mafanikio katika maisha na kazi zao. Kama vile mbegu, huwa wanafanya kile wanachotakiwa kufanya ili waweze kupata mafanikio wanayoyatamani. Lakini, kitu ambacho huwa kinapungua ni udongo ambao utasababisha mbegu iote na kukua. Udongo huo ni malengo. Hivyo, ili uweze kufanikiwa katika kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla, unahitajika kuweka malengo. Unatakiwa utenge muda, uyaandike kwa ufasaha na namna ambavyo utayatekeleza. Katika makala hii, nitakushirikisha sababu tano za wewe kuanza kuweka malengo.
Sababu 5 za wewe kuanza kuweka malengo.
1. Malengo yanakupa mwelekeo (focus)
Mojawapo ya kitu cha msingi sana katika mafanikio ni kutambua unahitaji nini katika maisha yako. Hivyo, ukiwa na malengo na umeyaandika, yatakusaidia kufanya kazi kwa bidii ukiwa umelenga kile tu unachohitaji katika maisha yako. Hivyo kuweka malengo kutakusaidia usipoteze muda wako kwa mambo ambayo siyo ya muhimu kwenye maisha yako.
2. Malengo yatakusaidia kupima maendeleo yako.
Unapokuwa umeweka malengo, yatakusaidia kuweza kupima mafanikio kwenye kila hatua unayopitia kwenye maisha yako. Unapokuwa umekamilisha lengo moja utaweza kuona ni kwa kiwango gani umeweza kufanikiwa na hivyo kukupatia hamasa ya kuendelea mbele zaidi kutimiza malengo mengine. Kama haujaweka malengo, hautaweza kufahamu chochote kwa sababu hautakuwa na kitu cha kupima mafanikio yako. Hautafahamu umefikia wapi na umekwama wapi kuelekea kwenye mafanikio yako.
3. Malengo yatakupatia hamasa (Motivation)
Unapokuwa umeweka malengo, yatakupatia hamasa ya kufanya kazi kwa bidi zote ili uweze kuyatimiza. Aina hii ya hamasa ni ya muhimu sana kwani hata kama utapata changamoto, kwa kuwa una malengo, utakuwa na nguvu ya kupambana kufikia mafanikio uliyoyakusudia. Kumbuka kuwa, unapokuwa una malengo, utaona thamani halisi ya kile unachokifanya na hivyo hautakata tamaa.
4. Malengo yatakusaidia kutokughairisha mambo (procrastination)
Kila mtu huwa anapitia changamoto ya kughairisha mambo kwenye maisha yake. Tabia hii inachangia sana watu wengi kushindwa kufanikiwa kwenye maisha yao. Hivyo, unapokuwa umeweka malengo, utaweza kukabiliana na changamoto hii kwa sababu utakuwa unafahamu kwa ufasaha nini unahitaji kwenye maisha yako na hatua muhimu za kuchukua ili uweze kufikia malengo yako.
5. Malengo yatakuwezesha kufanikiwa.
Moja ya kitu cha msingi sana unapokuwa umeweka malengo ni kuwa, yatakusukuma kutumia nguvu zako zote kuweza kufikia maisha unayoyatamani. Hivyo, kutokana na malengo, utaweza kuchukua hatua za msingi kwenye maisha yako bila kupoteza nguvu na muda wako kwenye mambo ambayo hayachangii kwenye mafanikio yako.
Hivyo basi, kama umekuwa ukipambana sana kupata mafanikio kwenye maisha yako, jambo la kwanza unalotakiwa kufanya ni kuangalia kama umeweka malengo. Hivyo, katika makala hii nimeelezea kwa kina faida tano ambazo utazipata utakapokuwa umeweka malengo katika maisha yako.
Swali la leo:
Ni lengo gani kubwa uliloliweka kwa mwaka huu?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuweka maoni yako kwenye sanduku la maoni hapa chini.

Tabia 6 Za Watu Waliofanikiwa.

Tabia 6 Za Watu Waliofanikiwa

Aristotle aliwahi kusema maneno yafuatayo:
“95% of everything you do is the result of your habit.”
Kwa tafsiri ya kiswahili maana yake ni kuwa, asilimia 95 ya kila kitu unachokifanya inatokana na tabia yako.
Hapa inamaanisha kuwa, ukitaka kuwa na mafanikio ni lazima ujenge tabia za mafanikio. Fanya vitu vinavyochangia kwenye mafanikio yako na ujitahidi kuvifanyia mazoezi mpaka vigeuke kuwa ndiyo tabia yako na ujizuie kufanya vitu ambavyo havina mchango wowote kwenye mafanikio yako. Katika makala ya leo nitakushirikisha tabia 6 za watu waliofanikiwa.
Ninawezaje kujenga tabia?
Tabia yoyote iwe nzuri au mbaya inajengwa kwa kurudiarudia (repetition). Hivyo kama unahitaji kujenga tabia njema za mafaniko ni sharti uwe tayari kuzirudiarudia kila siku. Baada ya muda utazoea kuzifanya na hivyo zitabadilika na kuwa ndiyo tabia yako. Katika makala hii tutaangalia tabia za watu waliofanikiwa.
Tabia 6 za watu waliofanikiwa.
1. Wanaweka malengo ya siku (daily goal setting)
Watu waliofanikiwa huwa wanaweka malengo ya siku. Hivyo ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na tabia ya kuweka malengo yako ya siku. Unapoenda kulala, hakikisha umeweka malengo yako ya siku inayofuata. Unapoamka unapaswa kufanya kazi zako kwa bidii ili uweze kutimiza malengo ya siku uliyojiwekea. Umuhimu wa kuweka malengo ya siku ni kuwa, unapoweka malengo na unayafikiria muda wote, utaweza kuyatimiza kwani utakuwa na hamasa ya kuyatimiza. Hivyo, watu waliofanikiwa huwa wanafikiria juu ya malengo yao muda wote.
2. Huwa ni watu wanaolenga kupata matokeo (result oriented)
Watu waliofanikiwa huwa wanafikiria kiwango cha matokeo watakayopata kwenye malengo waliyojiwekea. Hivyo, ili uweze kufanikiwa, kuweka malengo pekee haitoshi, ni lazima uwe na kipimo kitakachokusaidia kuona kama malengo yako yamefanikiwa au la. Kwa mfano, umeweka lengo la kusoma kitabu kila siku. Hili ni lengo ambalo liko kwa ujumla sana. Ili uweze kupima matokeo ni sharti lengo lako uliweke katika mfumo huu: Nitakuwa nikisoma kurasa 10 za kitabu kila siku. Hivyo, hata katika malengo yako mengine hakikisha unakuwa mtu wa kupima matokeo. Je, ni orodha ya mambo gani uliyoiweka leo? Weka vipaumbele vya mambo yako na vipimo vitakavyokusaidia kuangalia mafanikio.
3. Wanajali sana mahitaji ya watu (people oriented)
Watu waliofanikiwa huwa wanajali sana ni kwa jinsi gani wanaweza kusaidia watu wengine kutatua changamoto zao. Hivyo ili uweze kufanikiwa ni lazima ufikirie unawezaje kutatua changamoto za watu. Iwe kwenye kazi yako au biashara yako, jambo la kwanza kufikiria ni kuwa, biashara yangu au kazi yangu inatatua changamoto gani katika jamii. Kama ni kwenye kazi yako, jali sana watu unaowahudumia. Kama ni kwenye biashara yako, wajali wateja wako kwa kuwapa huduma bora. Jali changamoto za watu na uzitatue nawe utafanikiwa sana kwenye kazi au biashara yako.
4. Wanajali sana afya zao.
Watu waliofanikiwa huwa wanajali sana afya zao. Hii ni kwa sababu wanafahamu kuwa mafanikio yao yanategemea sana kama afya zao zitakuwa bora. Hivyo, ili uweze kufanikiwa, ni lazima mwili wako uwe na afya njema. Jali afya yako kwa kula vizuri, kufanya mazoezi pamoja na kupumzika.
5. Huwa ni waminifu
Waswahili wanasema kuwa, uaminifu ni mtaji. Watu wote waliofanikiwa ni waminifu kwenye kazi zao. Hivyo, ili uweze kufanikiwa, unapaswa kuwa mwaminifu kwenye maisha yako. Unapokuwa mwaminifu kwenye maisha yako, utavuta fursa nyingi sana kuja kwako. Kupitia uaminifu wako, utavutia watu kukupatia mtaji, kazi, masoko na fursa nyingine nyingi.
6. Huwa na nidhamu binafsi (self-discipline)
Nidhamu ndio msingi wa mafanikio yote katika maisha. Maana ya nidhamu ni:
Uwezo wa wewe mwenyewe kufanya kile unachotakiwa kufanya katika muda muafaka bila kujali unajisikia kufanya au la.
Watu waliofanikiwa huwa na nidhamu kubwa sana kwenye maisha yao. Hata wewe ili uweze kufanikiwa, hakikisha unakuwa na nidhamu kwenye maisha yako. Unapokuwa umeweka malengo, hakikisha kuwa unakuwa na nidhamu ya kuyakamilisha kwa muda muafaka. Kwa kufanya hivyo, utafanikiwa sana.
Swali la leo.
Je, ni tabia zipi za mafanikio ambazo unazijenga kwa sasa?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika kwenye sanduku la maoni hapa chini.

Jinsi Ya Kujenga Nidhamu ili Ufanikiwe Maishani.

Jinsi Ya Kujenga Nidhamu ili Ufanikiwe Maishani.

Watu wengi wameshindwa kufanikiwa katika maisha na katika malengo yao sio kwa sababu hawana uwezo au kipaji. Bali ni kwa sababu hawana nidhamu katika maisha yao. Katika makala ya leo nitakushirikisha jinsi ya kujenga nidhamu katika maisha yako ili uweze kufanikiwa.
Maana ya nidhamu.
Nidhamu ni ile hali ya kufanya kitu ambacho ni cha muhimu kwako na kwa muda muafaka bila kujali kama unajisikia au la.
Watu wengi wamezaliwa wakiwa na uwezo mkubwa lakini wameshindwa kufanikiwa katika maisha yao na kuishi wakiwa watu wa kawaida mpaka wanaondoka duniani kwa sababu walishindwa kujenga nidhamu katika maisha yao. Ili uweze kufanikiwa ni lazima ujenge nidhamu katika maisha yako.
Jinsi ya kujenga nidhamu katika maisha ili uweze kufanikiwa.
1. Nidhamu ya muda.
Muda ni rasilimali ya muhimu na ya pekee sana ambayo kila mtu amepewa kwa usawa. Hakuna mtu aliyependelewa akapewa muda mwingi kuliko watu wengine. Hivyo ili uweze kufanikiwa ni lazima ujifunze kuwa na nidhamu ya hali ya juu ya matumizi ya muda. Ili uweze kufanikiwa, hakikisha unaorodhesha Mambo ambayo utayafanya kwenye siku husika siku moja kabla. Pia hakikisha unapoweka orodha hiyo, panga mambo hayo kwa vipaumbele ukianzia na mambo ya muhimu sana kufanyika. Unapokuwa umeamka, anza kufanya mambo muhimu uliyoyaandika. Baada ya kuwa umemaliza kufanya mambo ya muhimu sana yanayochangia mafanikio yako, ndio umalizie mambo ambayo siyo ya muhimu sana.
2. Nidhamu ya fedha
Eneo la pili unalopaswa kulijengea nidhamu ya hali ya juu ni eneo la fedha. Ili uweze kufanikiwa, hakikisha kuwa, kila pesa inayopita kwenye mikono yako inakuwa na udhibiti wa hali ya juu. Katika eneo hili la fedha, fanya mambo yafuatayo ili uweze kuwa na mafanikio:
i. Andaa bajeti yako.
Bajeti ni mwongozo wa mapato yako na jinsi unavyoyatumia. Ni lazima ufahamu kuwa, unapokuwa na pesa na ukawa hauna mwongozo wa jinsi ya kuitumia, pesa yako itatumika kwa mambo yasiyokuwa ya msingi. Watu wengi wameshindwa kufanikiwa Katika suala la kifedha, siyo kwamba hawapati pesa, bali ni kwa sababu hawana bajeti.
ii. Hakikisha kuwa unaweka akiba.
Hakikisha kuwa kila pesa unayopata, unatenga pesa ambayo utaweka akiba. Unaweza kuweka akiba angalau asilimia kumi ya kila kipato chako. Lazima uanze kwa kutenga akiba kwanza kabla ya matumizi mengine.
iii. Epuka mikopo isiyojenga
Mikopo inakuwa na manufaa pale tu itakapotumika kufanya jambo lenye manufaa kwenye kwenye maisha yako. Hakikisha kuwa kama itakulazimu kuchukua mkopo, basi ni lazima uuelekeze kwenye jambo la uzalishaji au kununua kitu ambacho kinaongezeka thamani. Pia unaweza kuchukua mkopo kama tu kuna jambo la dharura kama vile kuokoa maisha.
iv. Fanya uwekezaji wa muda mrefu.
Pesa yako ya akiba unaweza kuiwekeza ili iweze kuongezeka kwa kununua vitu vinavyoongezeka thamani. Hapa unaweza kuiwekeza kwa kununua hisa, hatifungani, kununua shamba au kiwanja. Jambo la msingi hapa ni kuifanya pesa yako iongezeke thamani. Ukiweza kuwekeza pesa yako kwa muda mrefu, utapata matokeo mazuri sana kwani baada ya muda unaweza kuendesha maisha yako kwa ile faida tu inayotokana na uwekezaji wako.
Ni matumaini yangu kuwa umepata maarifa ya kukusaidia kuweza kujenga nidhamu ili uweze kufanikiwa kupitia makala hii.
Swali la leo.
Ni maeneo gani unahitaji kujenga nidhamu ili uweze kufanikiwa kwenye maisha yako?
Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika hapa chini Kwenye box la maoni.

Unapimaje Mafanikio Ya Kweli Katika Maisha Yako?

Unapimaje Mafanikio Ya Kweli Katika Maisha Yako?

Mafanikio ni neno ambalo linafahamika na kuzoeleka sana katika jamii yetu, lakini maana yake hasa ni nini? Ni kwa namna gani unaweza kupima mafanikio katika maisha? Je, mafanikio kuwa na utajiri, mamlaka na cheo, au kuna jambo jingine zaidi ya hayo?
Katika makala ya leo, nitaelezea maana ya mafanikio na kudadavua ni kwa jinsi gani unaweza kupima mafanikio ya kweli kwenye maisha yako. Nitaelezea vigezo vya ndani na vya nje ambayo vinachangia mafanikio na ni kwa jinsi gani unaweza kuvitumia kupima mafanikio yako.

Mafanikio ni nini?

Mafanikio yanaweza kutafsiriwa kama kufikia malengo au ndoto za maisha yako. Ni jinsi unavyoweza kutumia uwezo ulio ndani yako (your potential) kuweza kuishi maisha ya furaha na uliyoyakusudia (fulfilling and meaningful life). Kimsingi, mafanikio siyo tu kufikia malengo uliyojiwekea, lakini pia ni kufikia viwango vya maisha ya furaha (fulfilling life).

Mafanikio yanaweza kuwa na maana tofauti kwa watu tofauti pia, hii ndiyo sababu ni lazima kuwa makini kusema “mtu fulani amefanikiwa”. Jambo la msingi hapa ni kuwa, kama unahisi kuwa umefanikiwa, ni lazima uwe na furaha ya maisha baada ya kufikia malengo uliyojiwekea.

Umuhimu wa kupima mafanikio.

Kupima mafanikio ni jambo la muhimu sana. Linakuwezesha kufahamu wapi ulipo na hivyo kukupatia hamasa (motivation) ya kuendelea mbele kufikia malengo uliyojiwekea. Bila kupima mafanikio, unaweza kupoteza mwelekeo wa malengo yako. Kupima mafanikio pia kunakuwezesha pia kufurahia malengo uliyoyafikia, kujifunza kutokana na makosa na kufanya maboresho yanayohitajika.
Katika makala hii pia nitaelezea jinsi ya kupima mafanikio yako kwa kuwianisha vigezo vya ndani (internal factors) na vya nje (external factors).

Vigezo vya ndani (Internal Factors ) vya kupima mafanikio ya kweli

Unapimaje Mafanikio Ya Kweli Katika Maisha Yako?

Vigezo vya ndani ni mambo katika maisha yako ambayo yako ndani ya uwezo wako. Vigezo vya ndani ni hivi vifuatavyo:

1. Kuwa na furaha katika maisha yako (Happiness And Fulfillment)

Miongoni mwa vigezo vya muhimu sana vya kuzingatia unapopima mafanikio ni kuangalia kama una furaha ya maisha. Kigezo hiki kinajumuisha:

i. Kufanya kitu au kazi unayoipenda (passion).

ii. Kuwa na mahusiano bora (positive relationship).

iii. Kujua kusudi la maisha yako (Your life purpose) na kufanya vitu vinavyochangia kutimiza kusudi la maisha yako. Sasa hebu tuangalie kila kipengele kwa undani.

i. Kufanya kitu au kazi unayoipenda (passion)

Kufanya kitu kinachoendana na passion yako inamaanisha kufanya kazi unayoipenda na hivyo kufurahia kazi yako, haijalishi unalipwa mshahara kiasi gani au unapata kipato kiasi gani. Inamaanisha kuwa, unaamka kila siku na kuwa na shauku ya kazi yako. Unapokuwa unafanya kazi ambayo ni passion yako, kazi inabadilika kuwa siyo kazi bali inakuwa ni kitu unachokifurahia.

ii. Kuwa na mahusiano bora (positive relationship)

Kuwa na mahusiano bora ni jambo la muhimu sana ili kuwa na furaha katika maisha. Hii inajumuisha mahusiano bora na familia yako, marafiki zako na jamii yako. Ili kuimarisha mahusiano hayo, tenga muda wa kuwa na familia yako, marafiki zako na jamii yako.

iii. Kujua kusudi la maisha yako (Your life Purpose) na kufanya vitu vinavyochangia kutimiza kusudi la maisha yako.

Kufanya jambo linaloendana na kusudi la maisha yako inachangia kufanya uwe na furaha. Inakupatia hamasa na hivyo kukuwezesha kutotoka nje ya malengo yako.

2. Maendeleo binafsi (Personal Growth)

Kigezo cha pili cha ndani cha kuangalia unapopima mafanikio ya kweli ni maendeleo binafsi (personal growth). Katika kuangalia maendeleo binafsi katika maisha inajumuisha
i. kuweka na kutimiza malengo (setting and achieving clear, measurable goals),
ii. kujifunza kutokana na na makosa ( learning from your mistakes) na
iii. Kujitambua (self-awareness and self-improvement).

i. Kuweka na kutimiza malengo (setting and achieving clear, measurable goals)

Ni jambo la muhimu sana kuweka malengo kwa sababu ndiyo yanayokupatia ramani ya maisha yako. Unapofahamu wapi unakwenda, Inakupatia hamasa ya kufanya kazi kwa bidii na bila kutoka nje ya ramani. Pia inakuwezesha kupima mafanikio kwa kila hatua ndogo unayopiga kuelekea kwenye kutimiza malengo yako makubwa ya maisha.

ii. Kujifunza kutokana na makosa (Learning from your mistakes)

Kujifunza kutokana na makosa ni sehemu nyingine ya muhimu sana kwenye maendeleo yako binafsi (Personal growth). Unapokuwa umefanya makosa, chukulia makosa hayo kuwa ni fursa kwako kwa ajili ya kujifunza, kupata uzoefu na kuboresha pale ambapo ulikuwa na udhaifu. Kwa kuangalia makosa uliyoyafanya, itakusaidia kutokurudia makosa hayo na hivyo kukuwezesha kufanikiwa kwenye kazi zako.

iii. Kujitambua (Self-awareness and self-improvement)

Hili ni jambo la msingi sana kwenye maendeleo yako (Personal growth). Maana ya kujitambua ni kufahamu ubora wako (your strengths) na madhaifu yako (your weaknesses) na kuchukua hatua ya kuboresha mapungufu yako ili uwe mtu bora zaidi na hivyo kuweza kutimiza malengo yako katika ubora wa hali ya juu.

3. Afya ya kimwili na kiakili (Mental And Physical Health)

Kuwa na afya bora kimwili na kiakili ni kigezo cha muhimu sana cha ndani kinachopima mafanikio yako. Hii inajumuisha kufanya kila kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wako kuweza:
i. Kuboresha afya yako ya mwili.
ii. Kuhimili misongo (stress) na changamoto (challenges) za maisha.
iii. Kuweka uwiano mzuri wa kazi na maisha yako (good work -life balance).

i. Kuboresha afya yako ya mwili.

Hii inajumuisha kula mlo kamili (healthy diet), kufanya mazoezi na kupata usingizi wa kutosha. Unapokuwa na afya bora, mwili wako unakuwa na nguvu ya kuweza kutimiza malengo yako ya maisha na hivyo kuchangia kwenye mafanikio yako.

ii. Kuhimili misongo na changamoto (Coping with stress and challenges).

Hili ni jambo la muhimu sana kwenye afya yako ya mwili na akili. Maisha yamejaa milima na mabonde, hivyo ni muhimu kuweza Kuhimili changamoto na misongo inayojitokeza kwenye maisha yako.

iii. Kuweka uwiano mzuri wa kazi na maisha yako (good work -life balance)

Kuweka uwiano mzuri kati ya kazi zako na maisha yako mengine ni jambo la muhimu sana. Hii itakuwezesha kufanikiwa kwenye kazi zako wakati huohuo ukiwa na muda mzuri wa kufurahia na familia yako, marafiki zako na jamii yako kwa ujumla.

Vigezo vya nje (External Factors ) vya kupima mafanikio ya kweli.

Unapimaje Mafanikio Ya Kweli Katika Maisha Yako?

Pamoja na vigezo vya ndani nikivyoelezea hapo juu, pia kuna vigezo vya nje vinavyotumika kupima mafanikio yako. Vigezo hivyo ni hivi vifuatavyo:

1. Utajiri au kuwa na uchumi imara (Financial Stability And Wealth)

Kigezo cha kwanza kabisa cha nje ni kuwa tajiri au kuwa na uchumi imara. Watu wenye pesa nyingi, nyumba nzuri au gari huwa wanaonekana kuwa wamefanikiwa. Watu hawa huwa wamefanya kazi kwa bidii kuweza kutimiza malengo yao. Hivyo, ili uweze kuwa na uhuru wa kifedha, ni lazima uzingatie mambo yafuatayo:
i. Kuepukana na madeni
ii. Kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa muda mrefu.

i. Kuepukana na madeni.

Ili uweze kuepukana na madeni, ni sharti ujifunze kuweka bajeti. Kwa kufanya hivyo, utaweza kutumia kipato chako bila kuingia kwenye madeni na kubakiza kiasi cha pesa ambacho utaweka akiba, kuwekeza na kuwa na uchumi imara.

ii. Kuweka akiba na kufanya uwekezaji wa muda mrefu.

Kigezo hiki, kina uhusiano wa moja Kwa moja na kigezo cha kwanza. Kama utaweza kuishi chini ya kipato chako, utapata pesa ya ziada ambayo utaiwekeza kwenye biashara, kununua hisa, hati fungani na kadhalika. Unapoiwekeza pesa yako, itaongezeka na hivyo kufanya uwe na mafanikio kwenye maisha yako. Jambo la msingi hapa ni kuwekeza pesa yako mahali ambapo itaongezeka thamani.

2. Kufanikiwa kwenye kazi kipaji au taaluma Yako (Professional Accomplishments)

Kigezo kingine cha kupima mafanikio ya nje ni kufanikiwa kwenye taaluma, kipaji au kazi yako. Hii inajumuisha kufikia malengo uliyojiwekea. Kufanya mambo makubwa kwenye kazi yako ambayo yataleta mchango chanya kwenye eneo lako la kazi.

3. Kuwa na mchango kwenye jamii yako (Contribution To Society)

Kigezo cha mwisho kwenye kupima mafanikio yako ni kwa kuangalia ni mchango gani unaotoa kwenye jamii yako. Jamii yako lazima ihisi uwepo wako. Taaluma yako, kipaji chako au kazi yako ni lazima itatue matatizo yaliyopo kwenye jamii yako. Kwa kufanya hivyo, jamii itakupenda na kukuheshimu kwa sababu utakuwa unasaidia kutatua changamoto zinazoikabili.
Mafanikio ya kweli ni lazima yawe na uwiano wa vigezo vya ndani na vya nje.
Hivyo, ili uweze kuhitimisha kuwa na mafanikio ya kweli ni lazima kuwe na uwiano kati ya vigezo vya ndani na vya nje.

Swali la leo.

Katika maisha yako, unafikiri ni vigezo gani vya mafanikio haujavifikia na unatamani kuvifanyia kazi ili uweze kuwa na mafanikio ya kweli?

Ninatamani sana unishirikishe kwa kuandika hapa chini kwenye box la maoni.

error

Enjoy this blog? Please spread the word :)

Follow by Email
WhatsApp