
Kila mmoja anahitaji kufanikiwa katika malengo aliyojipangia. Hata wewe ninaamini una malengo ambayo umeyaweka kwa mwaka huu Ili uweze kuyakamilisha. Malengo ambayo yatakutoa kutoka hatua moja kwenda nyingine. Watu wengi wamekuwa wakiweka malengo makubwa katika maisha yao lakini wameshindwa kupata matokeo waliyokusudia. Kuna sababu nyingi zinazochangia kushindwa kufikia malengo uliyojipangia. Katika makala ya leo nitakushirikisha sababu 6 usizozijua zinazozuia mafanikio kwenye malengo yako.
Sababu 6 usizozijua zinazozuia mafanikio kwenye malengo yako.
1. Kuwa na malengo mengi bila Kuweka vipaumbele.
Miongoni mwa sababu zinazozuia mafanikio kwenye malengo yako, sababu ya kwanza kabisa ni kuwa na malengo mengi bila kuweka vipaumbele. Unapokuwa na malengo mengi, siyo rahisi kupata matokeo makubwa. Hii ni kwa sababu, kila lengo unaloliweka litahitaji rasilimali ya muda, nguvu, pesa na kadhalika. Kwa hivyo, unapokuwa na malengo mengi utajikuta kuwa unatawanya rasilimali zako kidogo kidogo kwenye kila lengo na hivyo utapata matokeo madogo kwenye kila lengo. Hivyo, ili uweze kupata matokeo makubwa ni sharti uwe na malengo machache na uwekeze rasilimali za kutosha kwenye malengo hayo. Kama una malengo mengi ni sharti uwe na vipaumbele uanze na malengo yapi kisha utakapofanikiwa uhamie malengo mengine. Unaweza kugawanya malengo yako katika sehemu tatu: malengo ya muda mfupi, malengo ya muda wa kati na malengo ya muda mrefu.
2. Kutofanya jambo linalochangia malengo Yako Kila siku.
Unapokuwa umeweka malengo yako, kwa mfano malengo ya mwaka, gawa malengo hayo sehemu ndogo ndogo ili upate malengo madogo ya kufanya kwa mwezi, juma na siku. Hii itakusaidia kuwa na kitu cha kufanya kila siku kinachochangia malengo yako. Kwa kufanya hivyo utajikuta unatimiza malengo yako hata kama yalikuwa ni makubwa kiasi gani.
3. Kutokujenga tabia ambazo zitakuwezesha kufanikisha malengo yako.
Unapokuwa umeweka lengo, ni lazima ujenge tabia ambazo zitakusaidia kuweza kutimiza lengo hilo. Kwa mfano: umeweka lengo la kuandika kitabu mwaka huu. Hapa ni lazima ujenge tabia mpya ambazo inawezekana haukuwa nazo. Mfano wa tabia hizi ni kama vile kujisomea vitabu, kuandika na kadhalika. Hivyo, kila lengo utakaloliweka litahitaji tabia fulani ambazo lazima uzijenge ili uweze kufanikiwa.
4. Kushindwa kuwekeza kwenye maarifa na ujuzi unaohitajika.
Katika kila lengo utakaloliweka, utahitajika kupata ujuzi na maarifa ambayo yatakusaidia kufanikisha lengo lako. Maarifa hayo unaweza kuyapata kwa watu,kupitia kusoma vitabu,kuhudhuria semina au kusoma chuoni. Hivyo ili uweze kufanikiwa, ni lazima uwekeze ujuzi utakaohitajika kutimiza lengo lako.
5. Kushindwa kuwa na nidhamu binafsi (self discipline)
Kuwa na nidhamu binafsi ni kuwa na uwezo wa kujitawala na kuwajibika. Hapa ni lazima uhakikishe mambo uliyoyapanga unayatimiza kwa muda muafaka. Ni lazima uwe na ratiba ya kutimiza malengo yako na uisimamie. Watu wengi huwa wanaweka malengo mazuri lakini huwa wanakosa nidhamu binafsi ya kuhakikisha malengo waliyoyaweka yanatimia kwa muda muafaka.
6. Kuwa na tabia ya kughairisha mambo
Hii ni sababu nyingine inayowafanya watu wasiweze kuchukua hatua kutimiza malengo yako. Huwa wanasubiri mpaka wawe na kitu fulani ndio waanze. Tabia hii inachelewesha sana mafanikio. Unapokuwa umeweka malengo, usisubiri mpaka uwe umekamilika. Anza na ulichonacho na milango itafunguka mara tu utakapokuwa umeamua kuanza.
Kwa leo niishie hapo. Nimatumaini yangu kuwa umepata maarifa ambayo yamekusaidia kufahamu sababu 6 usizozijua zinazozuia mafanikio yako. Kama una swali au maoni yoyote, usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba 0752 081669. Asante na karibu katika makala zijazo.