
Katika Maisha, ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na uwezo wa kuchangamkia fursa zinazokuja mbele yako. Watu waliofanikiwa ni wale waliotumia kwa usahihi fursa ambazo walizipata. Ninapozungumzia fursa, ninamaanisha jambo lolote ambalo ukilipata litakufanya ufanikiwe Katika maisha. Mfano wa fursa ni kama vile kupata ajira, kupata mtaji wa biashara, kupata wateja kwenye biashara yako na kadhalika. Kimsingi, fursa hazitafutwi bali zinavutiwa. Kuna tabia ambazo mtu akiwa nazo zinamfanya aweze kuvutia fursa nyingi kwake. Lakini pia kuna tabia ambazo ukiwa nazo zinafukuza fursa. Unabaki unalalamika tu kuwa huna bahati ya mafanikio, kumbe mafanikio umeyazuia kutokana na tabia ulizonazo. Katika makala ya leo nitakushirikisha tabia nane zinazozuia fursa za Mafanikio kwenye maisha yako.
Tabia 8 zinazozuia fursa za Mafanikio kwenye maisha yako.
- Mawazo hasi (negative thought)
Mawazo hasi ni tabia inayoweza kuzuia fursa za Mafanikio. Mtu mwenye mawazo hasi ni mtu ambaye haamini kuwa anaweza kufanikiwa. Haamini kuwa vitu vinawezekana. Hawezi kuthubutu kufanya jambo ambalo linaweza kumletea Mafanikio. Hivyo, ukiwa na mawazo hasi watu watashindwa kukushirikisha fursa ambazo zingeweza kukufaa Katika maisha yako wakijua kuwa utazitilia mashaka na hivyo hautathubutu kuzifanyia kazi. - Malalamiko au kutoa lawama.
Malalamiko ni tabia nyingine ambayo inaweza kuzuia fursa za Mafanikio kwenye maisha yako. Mtu mwenye malalamiko ni mtu ambaye haridhiki na chochote atakachopata. Ni mtu ambaye analalamikia watu changamoto alizonazo badala ya kutafuta njia ya kuzitatua. Kimsingi, watu hawapendi mtu mwenye kulalamika muda wote kwani huwa wanahisi kuwa analalamika Ili awatwike matatizo yake. Mtu mwenye malalamiko hata kama akipata fursa, hataridhika bali ataitafutia kasoro na kulalamika. Hivyo ukiwa mtu mlalamishi, watu hawatakushirikisha fursa, kwani wanafahamu kuwa hautaridhika nayo. - Kutokujali muda na kutokuwa na ratiba
Kutokujali muda ni tabia nyingine ambayo inaweza kuzuia fursa za mafanikio kwenye maisha yako. Watu wanajali sana muda, hivyo wakiona kuwa wewe haujali muda, watakukwepa na hawatakushirikisha fursa. Jitahidi kujali sana muda Kwa kuwa na ratiba Katika maisha yako. Usikubali muda Wako kupotea bila sababu ya msingi kwani muda ni rasilimali ambayo ikipotea hauwezi kuirudisha. - Kutokuwa mwaminifu
Kuna msemo wa kiswahili unaosema ‘uaminifu ni mtaji’. Ukiwa mwaminifu Katika mambo Yako yote, watu watakuamini na watatamani kufanya na wewe kazi. Kama umeajiriwa fanya kazi zako Kwa uaminifu, watu watakupenda na utapata fursa nyingine nyingi kupitia uaminifu Wako. Kama umejiajiri, kuwa mwaminifu kwenye kazi unazoletewa. Zifanye Kwa ubora wa hali ya juu, watu watakupenda na utapata fursa nyingi zaidi. Hivyo, kutokuwa mwaminifu ni tabia inayoweza kuzuia fursa za Mafanikio kwenye maisha yako. - Kudharau mwanzo mdogo
Watu wengi wameshindwa kuanzisha biashara au kazi zao Kwa kuhofia kuanzia na mwanzo mdogo. Ili uweze kufanikiwa. Kubali kuanzia chini Ili upate msingi wa kukupeleka kwenye mafanikio unayoyahitaji. Ukianzia chini na ukafanya Kwa uaminifu, unajiwekea nafasi ya kupata fursa kubwa zaidi. - Kushindwa kujifunza kwa haraka
Katika Dunia ya leo mambo yanabadilika Kwa haraka sana. Hii ni kuanzia mfumo wa maisha, jinsi tunavyofanya kazi, jinsi tunavyofanya biashara na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hivyo Ili uweze kuendana na mabadiliko haya, unapaswa kuwa mwepesi kujifunza. Ukishindwa kujifunza kwa haraka utaachwa nyuma na utakosa fursa za mafanikio kwenye maisha yako. Kama unafanya biashara, jifunze Kila siku Ili uboreshe biashara yako. Kama unafanya kazi usiache kuboresha ujuzi Wako ili uweze kutoa huduma Bora zaidi. Kumbuka kuwa unapotoa huduma bora, unajiweka kwenye nafasi ya kupata fursa nyingi zaidi za mafanikio. - Kujifanya mjuaji
Ujuaji ni tabia mbaya sana inayoweza kukukosesha fursa. Mtu mjuaji ni mtu ambaye anahisi kuwa anajua Kila kitu hivyo hahitaji kujifunza zaidi. Ni mtu ambaye hashauriki. Watu hawapendi mtu mjuaji hivyo hawawezi kumshirikisha fursa kwani wanajua kuwa ataharibu. - Kuwa na hasira za haraka Mtu mwenye hasira za haraka ni mtu asiyetabirika. Anaweza kukasirika muda wote akafanya maamuzi ya ajabu ambayo yanaweza kuleta hasira kubwa kazini au kwenye biashara. Hivyo, ukiwa na hasira za haraka, watu watashindwa kukushirikisha fursa ambazo zingeweza kukufaa Katika maisha yako. Ni matumaini yangu kuwa umepata maarifa ambayo yatakusaidia kwenye safari yako ya mafanikio. Kama una swali au maoni yoyote kuhusiana na mada hii usisite kuandika hapa chini. Pia unaweza kuwasiliana name moja kwa moja kwa simu namba 0752081669. Asante na karibu kwenye makala ijayo.