
Katika maisha kila mmoja wetu anahitaji kufanikiwa. Lakini katika mafanikio kuna kanuni ambazo kila ambaye anahitaji kufanikiwa anapaswa kuzifahamu na kuzifanyia kazi. Na ndio maana katika maisha kuna watu waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa japokuwa wote wanawekeza juhudi kubwa kutafuta maisha. Hivyo kuna moja ambalo watu waliofanikiwa huwa wanalifanya na hivyo kuwatofautisha na watu wengine ambao hawafanikiwi. Katika Makala hii, tutaangalia jambo kubwa au uamuzi mkubwa ambao kila aliyefanikiwa alifanya.
Tunapozungumzia mafanikio ni pana sana. Kwa mujibu wa Makala hii, mafanikio ni ile hali ya kufikia viwango ulivyojiwekea kwenye maisha yako. Viwango hivyo vinaweza kuwa: Kuwa na elimu kubwa, kuwa na biashara kubwa, Kuwa na kazi nzuri, Kukuza kipaji chako na kadharika. Hivyo katika Makala hii nitajikita kuelezea ni uamuzi gani mkubwa ambao kila aliyefanikiwa alifanya.
Sasa, nianze na tabia ambayo watu wengi ambao hawajafanikiwa wanayo. Tabia mojawapo ambayo watu ambao wameshindwa kufanikiwa wanayo ni tabia ya kurukaruka. Maana yake ni kuwa watu wengi wanafanya vitu ambavyo kwa asilimia 100 hawajaamua kufanya. Au kwa lugha nyingine ni kuwa, wanafanya vitu kwa kujaribu.
Kwenye maisha, kama hautaweka nguvu zako, akili zako na mawazo yako kwenye jambo unalotaka kufanya kwa asilimia mia moja, kamwe hautaweza kufanikiwa. Ndio maana watu wengi walioingia kwenye biashara walifeli, kwa sababu hawakuingia wazima wazima bali waliingia mguu mmoja ndani mwingine nje. Hivyo wakaweka nguvu kidogo hapo na pale kidogo. Hivyo wakashindwa kupata matokeo makubwa. Watu wa namna hiyo unakuta leo anafanya biashara hii, kesho anaona mwingine anafanya biashara nyingine na wao wanafuata. Hawawekezi nguvu zao sehemu moja.
Sasa ngoja nikusimulie habari hii itakupatia jambo la kujifunza.
Miaka mingi iliyopita kulikuwa na Kamanda mmoja wa kikosi cha Hispania cha Kijeshi aliyekuwa anaitwa Hernan Cortes. Mwaka 1519 alipewa kazi ya kwenda kuvamia kisiwa kimoja nchini Mexico kilichoitwa Berecluse na akapewa wanajeshi 500 na meli 11. Walipofika pale Kisiwani akaagiza wanajeshi wote washuke pamoja na wale mabaharia. Waliposhuka akaagiza meli zote zichomwe moto. Walipochoma moto na moshi ulipoanza kupanda juu, akawaita wale wanajeshi na wale mabaharia akawauliza, mnaona nini? Wakasema tunaona meli zetu zinaungua. Akasema, safi sana. Akawaambia, tuna chaguzi mbili tu zilizobaki hapa, tushinde vita au tushindwe vita tuangamie wote hapa. Hakuna njia mbadala tofauti na hizo.
Matokeo yake yalikuwaje?
Walikuwa wanajeshi wachache sana lakini vita walishinda. Kwa nini? Ni kwa sababu waliamua kwa asilimia mia moja kufanya kile kitu walichokuwa wanakifanya.
Jambo la kujifunza ni hili, ili uweze kufanikiwa kwenye jambo lolote, usiseme ninajaribu. Sema ninafanya. Chochote unachoamua kufanya, jitoe kwa nguvu zako zote na utaona matokeo makubwa. Kuanzia leo, usiseme najaribu jaribu, bali sema nafanya. Na ukiamua kufanya, CHOMA MELI ZAKO ZOTE na utashinda.