
Kabla ya kujenga biashara yenye mafanikio, jambo la kwanza kabisa tunapaswa kwanza kuelewa ni nini kinafanya biashara kufanikiwa. Katika somo la hili la pili nitakushirikisha jinsi ya kutambua Biashara inayolipa mtandaoni. Somo hili litaweka msingi wa masomo yangu mengine yanayofuata katika mfululizo wa masomo haya ya Jinsi ya kuanzisha biashara mtandaoni.
Biashara inayolipa mtandaoni na yenye mafanikio ni ipi?
Kuna biashara za aina nyingi mtandaoni na nje ya mtandao. Kuna nyingine zimefanikiwa na nyingine hazijafanikiwa. Hivyo, kabla ya kuanzisha biashara yoyote mtandaoni ni lazima utambue ni biashara gani itakulipa na kukuletea mafanikio.
Kimsingi, biashara inayolipa na yenye mafanikio sana ni biashara ambayo imejikita katika kutatua tatizo fulani katika jamii. Hivyo, biashara zote zilizofanikiwa hutatua matatizo au changamoto zilizopo katika jamii.
Katika somo linalofuata ambapo tutaangalia Jinsi ya kutafuta wazo bora la biashara yako ya mtandaoni, nataka na wewe pia ufikiria ni matatizo gani makubwa yaliyopo kwenye jamii na ni kwa jinsi gani unaweza kuyatatua. Hiyo ndiyo siri kubwa iliyopo kwenye biashara zote zilizofanikiwa.
Watu wote wanaoanzisha na kufanikiwa kwenye biashara zao wanatatua changamoto au matatizo yaliyopo kwenye jamii fulani na wanafanya hivyo kwa njia tofauti kama ifuatavyo:
1.Kuuza bidhaa.
Watu waliofanikiwa kwenye biashara, wengine huuza bidhaa ambazo zinawasaidia watu kutatua matatizo yao. Hivyo, kama utaamua kuuza bidhaa mtandaoni ni lazima kwanza ufahamu unalenga watu wenye matatizo gani.
2.Kutoa huduma.
Watu wengine wamefanikiwa kwenye biashara ya mtandaoni kwa kujikita katika kutoa huduma inayolenga kutatua tatizo fulani katika jamii. Mfano: huduma za ushauri wa kifedha, huduma za ushauri wa kiafya, huduma za ushauri wa kisaikolojia na huduma zingine nyingi.
3.Kufundisha ujuzi au utaalamu.
Wengine wamefanikiwa kwenye biashara za mtandaoni kwa kujikita kufundisha ujuzi au utaalamu wao waliojifunza chuoni au mtaani. Ujuzi ambao unahitajika ili kutatua tatizo fulani katika jamii.
4.Kutoa habari.
Watu wengine wamefanikiwa mtandaoni kwa kutoa habari ambazo jamii inazitafuta. Watu wanakuwa na tatizo la kukosa taarifa sahihi, hivyo wao wanatatua changamoto hiyo kwa kuwapatia taarifa sahihi.
Hivyo, kuna aina tofauti nyingi za biashara huko nje, lakini kimsingi zote zinasuluhisha au kutatua tatizo fulani. Kupitia kutatua matatizo yaliyopo kwenye jamii, biashara hizo pia hutengeneza pesa.
Jambo la msingi kabla ya kuchagua biashara ya kufanya: Kuwa na shauku (Passion).
Inawezekana ukawa una biashara inayolipa kama nilivyoeleza hapo juu, lakini kama biashara hiyo hauipendi au hauna shauku (passion), mafanikio yako yatakuwa magumu sana. Jambo la msingi hapa ni kuchagua biashara unayoipenda. Lazima kuwe na shauku mahali fulani. Kama ni kwenye kitu, soko ambalo unaingia, au kwa madhumuni ya kweli ya kuwahudumia watu.
Kuna wajasiriamali wengi ambao wamefanikiwa kwa nje.Kwa mfano, wana wafanyakazi wengi, wana wateja wengi, wanapata pesa nyingi, lakini kwa kweli hawafurahii kile wanachofanya tena. Hawana shauku tena, bila shaka biashara za aina hiyo huwa zinakufa. Hivyo hatutaki hilo litokee. Katika mfululizo wa masomo haya, nitakushirikisha jinsi ya kuwa na biashara inayolipa mtandaoni na ambayo utakuwa unapenda kuifanya na hivyo kukupatia furaha katika maisha yako.
Katika somo linalofuata tutaangalia somo linalohusu Jinsi ya kutafuta wazo bora la biashara yako ya mtandaoni.
Kama una swali au maoni usisite kuandika hapa chini. Asante sana na karibu katika somo linalofuata.
Masomo yaliyopita:
1. Jinsi kuanzisha biashara mtandaoni: 1. Utangulizi.
- Mbinu Tatu Rahisi Za Mafanikio Zinazopuuzwa. - August 9, 2024
- Jinsi Ya Kugundua Kusudi La Maisha Yako - August 7, 2024
- Kanuni za Kujiwekea Malengo - August 5, 2024
3 Replies to “2. Biashara Inayolipa Mtandaoni Ni Ipi?”